Ugonjwa wa COVID-19 uwe somo kwa nchi za Afrika kuboresha Mifumo ya Afya na Miundombinu ya Afya

Yoyo Zhou

Member
Jun 16, 2020
72
110
Hali ya mifumo ya afya katika nchi nyingi za Afrika limekuwa ni suala lenye msukosuko mkubwa. Miundombinu ya afya katika nchi nyingi za Afrika haitoshelezi mahitaji ya raia na kuepeleka vifo ambavyo vinaweza kuzuiliwa

Ujio wa ugonjwa wa Covid-19 umepelekea viongozi wengi wa Afrika wataharuki wakijua ukali wa ugonjwa huu. Ingawa hadi sasa kwa Afrika makali yanaonekana siyo makubwa sana ikilinganishwa na mabara mengine, lakini bado ugonjwa huu thakili unaendelea kuchukua roho za watu katika Afrika.

Hata hivyo nchi za Afrika hazitakiwi kutulia na kuridhika kwani maambukizi haya yanaendelea kuongezeka kila siku. Kituo cha Kuzuia na Kukinga Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) Hivi karibuni kiliripoti idadi ya watu waliothibitishwa kuwa na COVID-19 katika Afrika imefikia 306,567 huku kukiwa na vifo 8,115.

Janga hili limefanya vituo vya afya vya nchi zilizoendelea kuelemewa, na wataalamu walitabiri kwamba kwa Afrika mifumo yake ya afya itaelemewa zaidi kutoka na udhaifu wake. Tukitolea mfano mdogo tu, mashine za kupumulia ambazo ni muhimu katika kudhibiti Covid-19, kwa baadhi ya nchi za Afrika hiki bado kinaonekana ni kifaa cha kifahari, watu wenye uwezo wao ndio wanamudu kukitumia pale wanapokumbwa na magonjwa yanayohitaji kutumia kifaa hicho.

Imezoeleka kwa viongozi wengi wa Afrika pamoja na matajiri, pale wanapopatwa magonjwa mbalimbali, kimbilio lao ni kupata matibabu katika hospitali za nje ya nchi, badala ya kuwekeza katika nchi zao. Lakini baada ya kuibuka kwa ugonjwa huu, sasa watu wote si matajiri wala viongozi wanalazimika kutibiwa katika nchi zao baada ya nchi mbalimbali kutangaza zuio la usafiri, kufunga nchi na kuhudumia wagonjwa wao wa ndani badala ya kupokea wagonjwa kutoka nchi za nje. Hivyo serikali nyingi za Afrika zimeanza kuzinduka kwenye usingizi mzito na kuanza kufanya juhudi za kuandaa miundombinu ya afya pamoja na kurekebisha mifumo yao ya afya ili kuweza kukabiliana vizuri na janga hili.

Kwa Tanzania, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu hivi karibu alisema kuwapo kwa virusi vya corona nchini humo, kumeleta fursa ya kuboresha huduma za afya katika vituo mbalimbali vya afya.

Baada ya kuzuka kwa janga la corona, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, sekta ya afya imekuwa ikiangaliwa kwa jicho la umakini zaidi. Watu wengi walijitolea kuchangia vifaa na vifaa tiba ambavyo vimesaidia kuimarisha huduma za afya na kuokoa maisha kwa wagonjwa mahututi.

Mbali na michango inayotolewa na watu lakini serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imejitutumua na kujenga maabara ya kisasa ya uchunguzi wa magonjwa ya binadamu ya kuambukiza iliyogharimu Shilingi Bilioni 9 katika Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro.

Waswahili wanasema shilingi ina pande mbili, yaani kuna upande mzuri na mbaya. Ni sawa na huu ugonjwa wa Covid-19, kwani umeleta madhara makubwa kabisa katika uchumi wa nchi mbalimbali na kuzorotesha afya za watu, lakini kwa upande wa pili umekuja na kutoa somo hasa kwa nchi ambazo ziliipa mgongo mifumo yao ya afya na miundombinu ya afya.

Ni wakati sasa kwa viongozi wa Afrika kuhakikisha wananchi wote wawe matajiri au masikini, wawe viongozi au wasiwe viongozi, wote wanatibiwa ndani ya nchi. Katika hotuba yake ya kuvunja bunge la Muungano wa Tanzania, Rais John Magufuli alisema kwa sasa Tanzania idadi ya rufaa za kwenda kutibiwa nchi za nje zimepungua kwa asilimia 95 baada ya kuboresha sekta ya afya. Hata wagonjwa kutoka mataifa jirani sasa pia wanakwenda Tanzania kutibiwa hasa wagonjwa wa moyo.

Hivyo basi hakuna kisichowezekana, na penye nia pana njia. Ugonjwa wa Covid-19, tusiuchukulie kuwa ni tatizo bali tuone ni kama changamoto ambayo tunaweza kuikabili na kupambana nayo.
 
Back
Top Bottom