ARSENAL ya England imepewa kibarua kigumu na nafasi nyingine ya ama kulipa kisasi dhidi ya mabingwa wa Hispania na mabingwa wa Ulaya mwaka jana, Barcelona katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kinyume chake itaiaga mapema michuano hiyo.
Katika ratiba iliyopangwa jana na Shirikisho la Soka Ulaya, (Uefa) mjini Nyon, Uswisi, Arsenal imekutanishwa tena na miamba hao wa Hispania ambao waliwabwaga kwa mabao 2-1 kwenye fainali ya 2006 mjini Paris, Ufaransa ambako kipa Jens Lehmann alitolewa kwa kadi nyekundu.
Mwaka jana, Barca ndiyo iliyoitoa Arsenal kwenye michuano hiyo, hatua ya robo fainali kwa mabao 4-0 katika mchezo wa marudiano uliofanyika Uwanja wa Nou Camp.
Katika mchezo huo, mshambuliaji ambaye Arsenal hawataweza kumsahau ni Lionel Messi ambaye alikuwa mwiba mkali kwa vijana hao wa Arsene Wenger.
Kulingana na ratiba hiyo, Arsenal iliyomaliza ya pili Kundi H itaanzia nyumbani, Emirates, London kati ya Februari 15 / 16 au wiki moja baadaye, Februari 22au 23 .
Mechi za marudiano ambazo zitaamua ni timu zipi nane zitacheza robo fainali mwezi Aprili zitachezwa Machi 8/9 na 15/16, huku Uefa ikiwa imezipanga timu hizo kwa mfumo ambao unaziepusha timu za nchi moja kukutana katika hatua hiyo .
Katika ratiba hiyo, mchuano mwingine mkali na mgumu utakuwa baina ya Inter Milan, bingwa mtetezi wa michuano hiyo dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani.
Timu hizo zilikutana katika mchezo wa fainali msimu uliopita ambako Inter iliilaza Bayern kwa mabao 2-0 ya Diego Milito katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid, Jumamosi Mei 22 mwaka huu.
Mchezo mwingine ambao utakuwa kivutio kikubwa ni baina ya Lyon ya Ufaransa na Real Madrid, ambazo zilikutana pia mwaka 2009 na Madrid wakatupwa nje.
Wawakilishi wengine wa England, Tottenham Hotspur ambao msimu huu wamefuzu kwa mara ya kwanza lakini wakaoonyesha maajabu makubwa, wamekutanishwa na wakongwe AC Milan kutoka Italia.
Nao vinara wa Ligi Kuu England, Manchester United wamepangwa dhidi ya Olympique Marseille ya Ufaransa.
Chelsea, ambayo msimu huu imekuwa haitabiriki imepangwa dhidi ya timu ngeni katika michuano hiyo, FC Copenhagen ya Denmark. Copenhagen ndiyo zaidi itakuwa na kibarua cha kusaka nafasi ya kucheza robo fainali kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo ya Ulaya.
Mechi nyingine itakuwa baina ya AS Roma ya Italia dhidi ya Shakhtar Donestsk ya Ukraine, zikikamilisha ratiba hiyo ambayo inashirikisha timu 16.
Nao Valencia kutoka Hispania watakuwa kibaruani dhidi ya Schalke 04 kutoka Ujerumani.
Akizungumza baada ya kupangwa kwa makundi hayo jana, kipa wa Arsenal, Lukasz Fabianski ambaye msimu huu amekuwa akicheza badala ya Manuel Almunia alisema kuwa kupangwa dhidi ya Barca ndicho kitu ambacho kila mmoja wao alikihitaji.
"Utakuwa mchezo mgumu, lakini hatuwezi kuifikiria sana Barcelona.
"Si kama ilivyokuwa msimu uliopita, lakini tutacheza nao kwa kumbukumbu ya kilichotokea. Timu hizo zinafahamiana.
"Lakini, hatuwaogopi . Tunajiamini, tutawamudu."
Kocha wa Spurs, Harry Redknapp ameeleza kuwa anarejea San Siro akifahamu kuwa AC Milan ni timu ngumu.
"Tuliwafunga Inter Milan msimu huu uwanjani hapo, sasa tunajiandaa kuikabili AC Milan. Itakuwa mechi ngumu. Lakini, ningepewa nafasi ya kuchagua, ningeichagua AC Milan.
"Wanaongoza Ligi Kuu (Serie A), lakini tusubiri mchezo mgumu. Ninausubiri kwa hamu."