SoC03 Uchumi wa Buluu Uimarishwe ili Kuboresha Uchumi na Ajira kwa Vijana Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
242
615
Utangulizi
Uchumi wa Buluu ni nini?
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (“World Bank”), Uchumi wa Buluu ni “Matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa ajili ya ukuaji wa uchumi, kuboresha shughuli za kujipati kipato, na ajira, huku afya ya mfumo wa ikolojia ukihifadhiwa”.

Kwa mujibu wa Kamisheni ya Ulaya, Uchumi wa Buluu ni “Shughuli zote za kiuchumi zinazohusiana na bahari na fukwe. Inashusisha sekta mbalimbali zilizopo na zile zinazojitokeza”.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, hivi karibuni alifafanua Uchumi wa Buluu kama Uchumi unaojumuisha sekta mbalimbali za kiuchumi pamoja na sera zake ambazo kwa pamoja huamua kama matumizi ya rasilimali za bahari ni endelevu.

Kwa muktadha wa Makala hii, ninatafsiri Uchumi wa Buluu kama “Shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali zinazohusiana na bahari, maziwa, mabwawa, mito pamoja na fukwe zake zinazozingatia uhifadhi wa afya ya ikolojia”.

Uchumi wa Buluu Unaimarishwa Upande wa Tanzania Visiwani (Zanzibar)

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zanzibar, Lengo Kuu la Wizara hii ni kusimamia utekelezaji wa kasi na endelevu wa fursa zilizopo na vipaumbele vyake vya uchumi unaotegemea rasilmali za bahari au Uchumi wa Buluu ili kuijenga Zanzibar mpya yenye uchumi wa kisasa. Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia matumizi na usimamizi endelevu wa bahari na ukanda wa pwani pamoja na kusimamia, kuratibu na kuimarisha fursa za uwezeshaji na uwekezaji katika sekta za uvuvi, mazao ya baharini, kilimo cha mwani na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ilianzishwa rasmi na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza La Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi mwezi Novemba 2020.

Kitendo cha Zanzibar kuunda Wizara maalum ya Uchumi wa Buluu, kinaonyesha dhamira ya serikali ya Zanzibar kuifanya sekta hii kuwa nguzo imara na muhimu ya Uchumi.

Uchumi wa Buluu uimarishwe Tanzania Bara
Tanzania Bara ina kilomita zaidi ya 800 za bahari (Bahari ya Hindi), ikijumuisha mikoa mitano, ambayo ni Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Tanga; ina ziwa Victoria ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani, ambalo ni chanzo cha mto Nile, linalounganisha Tanzania na Uganda na Kenya; Ziwa Tanganyika, ziwa refu la maji yasiyokuwa ya chumvi, linalounganisha Tanzania na Kongo (DRC), Burundi, na Zambia; Ziwa Nyasa, nalo ni kubwa linalounganisha Tanzania na Malawi na Msumbiji. Kuna maziwa mengine nchini Tanzania na mito kama itakavyoonyeshwa kwenye ramani hapa chini.

Kilelezo Na. 1: Ramani ya Tanzania ikionyesha Bahari, Maziwa na Mito

Maziwa na Mito TZ.png

Chanzo: Google: Maziwa na Mito Tanzania

Fursa za Kiuchumi na Ajira

  • Bahari: Kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinazoajiri watu wengi, ambazo ni: usafiri na usafirishaji, uvuvi, utalii, kilimo cha mikoko na mwani na kadhalika.
  • Maziwa: Katika maziwa makubwa, shughuli zote zilizotajwa hapo juu zinafanyika.
  • Mabwawa: Shughuli za uvuvi, uzalishaji wa nishati ya umeme – kama Bwawa la Mtera, Bwawa la Nyumba ya Mungu, na sasa Bwawa la Mwalimu Nyerere (Mto Rufiji), ambapo shughuli za kitalii zinaweza kufanyika.
  • Mito: Shughuli za umwagiliaji mashamba, uvuvi, na kulisha maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.
Maeneo haya yakiendelezwa vizuri, yatakuwa na mchango mkubwa sana katika mapato ya nchi na ajira kwa watu wengi, hasa vijana.

Changamoto za Uchumi wa Buluu
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, changamoto muhimu ya Uchumi wa Buluu ni kuelewa namna nzuri ya kusimamia vipengele vingi endelevu vya bahari, kuanzia uvuvi endelevu mpaka afya ya ikolojia ya bahari, kuanzia uvuvi endelevu mpaka afya ya ikolojia kuzuia uchafuzi. Pili, Uchumi wa buluu unatupa changamoto ya kutambua kwamba usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari utahitaji ushirikiano kutoka nje ya mipaka na sekta mbalimbali kupitia aina za mashirikiano, na katika kiwango ambacho hakijafikiwa hapo awali.

Umoja wa Mataifa umebaini kuwa Uchumi wa buluu utasaidia kufikia lengo namba 14 la maendeleo endelevu, ambalo ni “Maisha chini ya Bahari”

Kilelezo Na. 2: Wanawake Mwaloni Kigoma, Tanzania Wakikausha Samaki Juani.
Uvuvi wa Samaki Kigoma.png

Chanzo: FAO/Luis Tato

Mapendekezo

Serikali ianzishe kitengo au kamisheni maalum kwa lengo la kuendeleza maeneo yote ya maji, ambayo ni bahari na fukwe zake, maziwa na fukwe zake, mabwawa na mito; kuinua uvuvi, usafiri/usafirishaji, kilimo cha mikoko na mwani, utalii, uzalishaji wa umeme na shughuli nyingine zinazohusiana na Uchumi wa buluu. Hii itachochea uwekezaji wa ndani na nje katika maeneo yaliyopo na maeneo mapya. Katika maeneo haya, serikali inaweza kuwezesha wananchi kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kwa ajili ya kuchakata mazao yanayotokana na maji, mfano: Samaki, chumvi, na kadhalika.

Serikali isimamie vizuri na kulinda vyazo hivi vya Uchumi wa buluu dhidi ya uharibifu wowote, mfano: uvuvi haramu, ufugaji holela, matumizi mabaya ya vyanzo vya maji, ukataji miti holela, na uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Hitimisho
Uchumi wa Buluu ukitiliwa mkazo na serikali pamoja na wadau wengine, Uchumi wa nchi utaboreka, na ajira kwa vijana zitaongezeka, huku afya ya ikolojia ikihifadhiwa.

Marejeo
Ferdinand Omondi, BBC Swahili (Novemba 26, 2018), “Blue Economy”: Namna ya Kufaidika na Rasilimali Bahari ya Mikoko katika Uimarishaji Biashara na Mazingira.

Uchumi wa Bluu - The Ocean Foundation

https://www.un.org/regularprocess/sites/www.un.org.regularprocess/files/rok_part_2.pdf
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom