Suala la usafi katika maeneo yetu linatakiwa kusimamiwa na kila mtu.
Nimesimama nje ya jengo la Posta ya zamani. Ni kituo cha mabasi yafanyayo safari za Posta (baharini) na Mwenge kupitia barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Saa niliyo nayo inaniashiria kuwa ni saa sita urobo adhuhuri.
Kushoto kwangu, kijana fulani anakula ndizi. Hatua tatu kutoka pale tulipo, kuna chombo cha kutupia taka. Humo hutupwa vitu visivyofaa kwa matumizi, aghalabu kwa sababu ya kwisha muda wake, uchakavu au ubovu.
Kijana huyu baada ya kula ndizi, anatupa ganda (la ndizi) kando. Namwuliza: Mbona hutupii pale penye chombo cha takataka? Ananiangalia kwa kedi kabla ya kunijibu: Wapo walioajiriwa kufanya kazi hiyo, kisha anasogea mbali, bila shaka kukwepa maswali mengine kutoka kwangu.
Huyu ni miongoni mwa Watanzania kadhaa wenye tabia hiyo. Hawathamini sio usafi wa mazingira tu bali hata maeneo wanayoishi. Majumba yao yamezingirwa na majani na taka kila pembe. Ikinya mvua kidogo tu hata kuingia majumbani mwao huwa kero. Mitaro ya maji imejazwa mifuko ya nailoni na taka za kila aina, bila kuzibuliwa na kufanyiwa usafi.
Ukibahatika kuingia katika nyua za majumba mengi jijini Dar es Salaam, utapata kinyaa na mzubao wa aina yake. Vyombo vichafu vimezagaa ovyo kwenye karo huku nzi wakigombea masalia ya vyakula.
Vyoo vinatisha kwani vimejaa pomoni na mumo humo ndimo watu wanamoogea!
Hali katika masoko yetu ndio hatari zaidi. Uchafu unashindana na bidhaa za vyakula, hasa matunda. Kuna wakati mtu hudhani hata taka (uchafu) za sokoni nazo zinauzwa, ndio maana hazizolewi kwa wakati muafaka. Je, ni kutokana na hali hiyo ndio sababu hata wauzaji wanakuwa wachafu?
Au ni ule usemi kwamba ukienda Rumi fanya kama wafanyavyo Warumi? Mola tuzindue, tusaidie, tuelimishe.
Kama ilivyo katika majumba na mazingira yake, ndivyo pia ilivyo katika barabara za mitaani. Katika kila watu 10 ni mmoja au wawili tu wanaozingatia usafi. Ingawa karibu maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam yamewekwa mapipa ya kutupia taka, watu 8 kati ya kumi hawana habari nayo.
Chochote kisichohitajika maganda ya matunda, chupa za maji, mifuko ya nailoni, vipande vya magazeti, pakiti za sigara na vichungi vyake hutupwa popote.
Baadhi ya kampuni za watu binafsi zimepewa zabuni za kufagia na kuzoa taka maeneo mbalimbali ya jiji. Ingawa kwa kiasi fulani akina mama huonekana kufagia barabarani kuanzia asubuhi mpaka jioni, ni kama wanatwanga maji kwenye kinu. Mule mule wanamofagia, hatua mbili nyuma yao wanapita wachafuzi na kutupa taka!
Masikini wa Mungu akina mama hao hawana hata vifaa vya kazi. Hawapewi mabuti ya mpira (gum boots), glovu za mikono, vichuja hewa vya kufunika pua, kofia za kujikinga jua na vumbi, n.k. Kila mfagizi hutumia vifaa kadiri alivyojaliwa kuwa navyo.
Wanaume wanaopakia taka kwenye magari ya kuzolea na kumwaga majalalani (dampo) hawana nafuu. Hawa wanatia huruma zaidi. Vifaa vyote wasivyopewa akina mama wafagizi, nao pia hawapewi. Ukiwaona juu ya magari yaliyosheheni taka, ni vigumu kutofautisha kati ya taka na binadamu. Wenyewe wamechafuka na kuwa kama taka zenyewe. Ee Mwenyezi Mungu wanusuru waja wako.
Katika nchi za wenzetu (Uzunguni) hao wanaofanya kazi za uchafu ndio wanaolipwa vizuri huku wakichunguzwa afya zao mara kwa mara. Hapa kwetu wanafanyiwa hivyo? Ukiwaangalia sura, afya na mavazi yao utapata jibu ila mimi nachelea kuhukumu ili nisije kuhukumiwa kwa hukumu ileile
Magari ya kuzolea taka, yenyewe yanastahili kabisa kuitwa takataka. Kusema kweli yangestahili kuachwa kule kule majalalani. Tena hata magari hayo kufika jalalani ni muhali. Kwa hakika asilimia 90 ya magari hayo, yamechoka na hayastahili kuwamo barabarani.
Inanipa shida kuamini kuwa yalikaguliwa kabla ya kupewa leseni ya kufanya kazi hiyo ngumu na nyeti. Mara kadhaa huonekana yameharibikia barabarani na kuwa kero kwa magari mengine.
Mambo mawili yatakujulisha kama gari la taka limepita au la. Kwanza ni uvundo (sisemi harufu, kwani harufu yaweza kuwa nzuri au mbaya ila uvundo ni uvundo tu); na pili ni taka zinazomwagika kuanzia pale zinakozolewa mpaka zinakotupwa. Kumwagika kwa taka ni magari hayo kutokuwa na nyavu za kufunikia au kama zipo, ni ushahidi tu kwani huwa mbovu mno.
Humo majalalani, hukosi kuona watu wakichakura chakura kutafuta riziki. Kuna watu kadhaa wanaoishi kwa riziki za majalalani. Usibishe, huko ndiko kufa kufaana! Wazoaji huwa na vigunia vyao vya kuwekea vitu vya thamani na vile wanavyoona kutokuwa na thamani, huwa na thamani kwa wale wanaoshinda majalalani kusubiri riziki yao. Vyote hivyo hurejeshwa tena jijini kuuzwa na kutumiwa!
Inashangaza kusikia baadhi ya watu wakiilaumu serikali kwa kushindwa kufanya usafi kwenye maeneo yao. Serikali itafanya mangapi? Hata kutufyekea majani yanayozunguka nyumba zetu? Ifagie mabaraza na nyua zetu? Upuuzi mtupu!
Nadhani uchafu uliokithiri katika jiji la Dar es Salaam ndio uliomfanya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kufanya ziara isiyo rasmi katika maeneo mbalimbali ya jiji. Amejionea jinsi wakazi wake wanavyokumbatia uchafu na kuutaka uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam kuidhibiti hali hiyo.
Tukirudi nyuma, bila shaka kuna sheria ndogo ndogo za miji zinazohusu usafi wa mazingira. Katika hali ya kawaida, kila mwenye nyumba anahitajiwa kutunza usafi wa mazingira na nyumba zao. Kadhalika kuna sheria inayokataza kutupa taka barabarani, vingenevyo ni faini au kifungo.
Ni wakati muafaka kuzirejea sheria hizo ili kulifanya jiji la Dar es Salaam liwe na hadhi inayostahili kwani ni kioo cha Tanzania.
http://www.ippmedia.com/?item=15032007news