SoC04 Uboreshaji wa Huduma za Posta ili Kuwezesha Biashara Mtandao (Electronic Commerce) Kuendana na Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia

Tanzania Tuitakayo competition threads

tamsana

JF-Expert Member
Jan 13, 2012
3,299
7,216
A: Utangulizi:
Tanzania imefanikiwa kupata fursa ya kuwa mwenyeji wa Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (Pan African Postal Union - PAPU) jijini Arusha, ambapo hatua hii inategemewa kuchagiza maendeleo ya huduma za posta nchini na barani Afrika kwa ujumla. Katika maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayotawaliwa na Uchumi wa kidijitali (digital economy), sekta ya posta inasimama kama mwezeshaji au muhimili muhimu katika kuimarisha uchumi wa kidijitali kupitia maendeleo ya biashara mtandao (electronic commerce). Shirika la Posta Tanzania (Tanzania Postal Corporation) linabeba mchango mkubwa katika kuwezesha biashara mtandao nchini na duniani kwa ujumla. Kwa kutumia faida hiyo, pamoja na kutambua mwelekeo wa ulimwengu kiteknolojia, tunaweza kupanga njia au mifumo mizuri ya utoaji wa huduma za posta kufikia kiwango cha juu cha mchango wa huduma za posta katika biashara ya kidijitali.

Sekta ya posta nchini imekuwa muhimili muhimu katika miundombinu ya mawasiliano na maendeleo ya biashara. Kasi ya ukuaji wa maendeleo ya sayansi na teknolojia hususan maendeleo ya uchumi wa kidijitali katika biashara mtandao linachagizwa na uwepo wa huduma za posta. Kwa kutambua mabadiliko haya, ni muhimu taifa kutumia kwa kiasi kikubwa na kuboresha huduma za posta zilizopo ili ziendane na maendeleo ya teknolojia kwa lengo la kuchochea biashara mtandao na hatimaye kuimarisha ukuaji wa kiuchumi katika kuchangia Pato la Taifa (GDP).

B: Hali ya Sasa ya Huduma za Posta za Tanzania:
Miundombinu ya huduma za posta Tanzania inajumuisha mtandao wa ofisi za posta, huduma za haraka (Express Mail Service - EMS), na vituo vya usafirishaji (transport and distribution centers) vilivyosambaa nchini. Ingawa Shirika la Posta limejitahidi kukabiliana na maendeleo ya kiteknolojia kwa kiwango fulani, bado kuna changamoto mbalimbali kama vile kutokuwa na miundombinu ya kidijitali ya kutosha, upatikanaji wa huduma za posta katika maeneo ya vijijini, na ushindani kutoka kwa watoa huduma wa makampuni binafsi. Licha ya changamoto hizo, sekta ya posta inaendelea kuchukua jukumu muhimu katika kurahisisha mawasiliano, huduma za kifedha, na usafirishaji wa vifurushi..

C: Mchango wa Huduma za Posta kwenye Biashara Mtandao:
Ripoti za Shirikisho la Posta Ulimwenguni zinathibitisha mchango mkubwa wa huduma za posta kwenye uchumi wa dunia, na mchango moja kwa moja na usio wa moja kwa moja ukiwa 7% ya Pato la Taifa la Dunia. Katika muktadha wa biashara ya mtandao, huduma za posta ni muhimili muhimu (enabler) kwa kutoa usafirishaji wa vifurushi na mizigo kutoka kwa muuzaji hadi kwa mteja, kuanzisha majukwaa ya biashara mtandao (digital trade platforms), na kurahisisha biashara za mpakani. Kwa kuwa biashara mtandao inaendelea kupanuka kimataifa, kuna uwezekano mkubwa kwa huduma za posta nchini kuchukua jukumu muhimu katika kukuza ukuaji huo.

D: Mikakati ya kuwezesha Puduma za Posta katika Biashara Mtandao:
1. Kuboresha miundombinu ya Kidijitali:
  • Shirika la Posta kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali ili kuimarisha uwezo utoaji wa huduma zake ikiwemo kufuatilia (tracking) mzingo/kifurushi kuanzia kwa muuzaji hadi kwa mteja;​
  • Kuanzisha na kutangamanisha majukwaa ya biashara mtandao na mifumo ya kidijitali ya huduma za posta pamoja na kuboresha malipo ya kidijitali ili kurahisisha miamala mtandaoni na kupanua wigo wa masoko;​
  • Kuboresha mifumo ya anwani kielektroniki ili kuongeza ufanisi wa utoaji na usahihi wa anwani; na​
  • Kutumia ofsi za huduma za posta zilizopo kama sehemu za kukusanyia na kupokelea mizigo na vifurushi.​
2. Kurahisisha Biashara za Mpakani:
  • Kuimarisha ushirikiano na nchi jirani na mashirika ya kikanda ili kuhawilisha (harmonize) taratibu za forodha, sheria, na kurahisisha uondoaji wa mizigo/vifurushi mpakani kidijitali; na​
  • Kuanzisha vituo vya biashara vya kidijitali mpakani pamoja na vituo vya huduma za posta vya usafirishaji mipakani ili kuharakisha upitishaji wa mizigo na kupunguza muda wa usafirishaji.​
3. Kukuza Biashara za Kati na Ndogo (SMEs):
  • kutoa motisha na programu za kusaidia wafanyabiashara wadogo (Micro, Small and Medium Enterprises – MSMEs) kutumia huduma za posta kwa kupanua biashara mtandao, ikiwa ni pamoja na viwango nafuu vya, msaada wa upatikanaji wa masoko, na upatikanaji wa mitaji; na​
  • Kuimarisha ushirikiano kati ya MSMEs na Shirika la Posta ili kuimarisha usambazaji wa bidhaa nchini na kwenda nje ya nchi.​
4. Kutumia Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika:
  • Kutumia uwepo wa makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika kushiriki katika kuboresha sera, kupata uzoefu, na mipango ya kujenga uwezo wa Shirika la Posta nchini; na​
  • Kutengeneza mfumo wa pamoja wa huduma za posta Afrika ili kuimarisha biashara ndani ya Afrika na dunia kwa ujumla kwa kuzingatia uwepo wa fursa za bishara kupitia Eneo Huru la Biashara Afrika (African Continental Free Trade Area – AfCFTA).​
E: Hitimisho:
Mabadiliko ya huduma za posta Tanzania kwa kiasi kikubwa yatasaidia kuongezwa kasi ya biashara mtandao ndani ya nchi, Afrika na dunia kwa ujumla. Biashara mtandao ni endelevu kwani hubadilika kadiri teknolojia inavyo kua. Mambo ya muhimu ya kuanza nayo ni pamoja na kuweka mikakati Madhubuti inayolenga matumizi ya mifumo ya kidijitali, kujenga uwezo watumiaji wa mifumo hiyo, kurahisisha biashara za mpakani, kusaidia wafanyabiashara wadogo, na kutumia fursa ya uwepo wa Umoja wa Posta Afrika katika kuitumia Tanzania kama kitovu cha ukuaji wa huduma za posta. Tanzania inaweza kutumia uwezo kamili wa sekta ya posta ili kuendesha ukuaji wa kiuchumi na ustawi wa biashara mtandao na hatimaye kuongeza mchango katika pato la taifa.​
 
Madhubuti inayolenga matumizi ya mifumo ya kidijitali, kujenga uwezo watumiaji wa mifumo hiyo, kurahisisha biashara za mpakani, kusaidia wafanyabiashara wadogo, na kutumia fursa ya uwepo wa Umoja wa Posta Afrika katika kuitumia Tanzania kama kitovu cha ukuaji wa huduma za posta.
Uliyoyaongea ni sahihi kabisa.

Posta, kwa kuwa kwake na vituo nchi nzima, kila kijimji kina kituo cha posta kunaiweka katika nafasi ya kimkakati kuwa kitovu cha biashara na usambazaji wa vifurushi.

Mara kadhaa nimepokea vifurushi toka nje vya bidhaa.

Tena posta wanalo duka la mtandaoni ambalo sijajua limefikia wapi?
Screenshot_20240504-112923_Chrome.jpg

Naungana na mtoa mada kutoa rai, kuwepo usmakini kusimamia huduma kama hizi. Nasema hivi kwa sababu ipo siku nilihitaji kusafirisha kikopo cha mafuta haya;
Screenshot_20240504-112540_Chrome.jpg

kupitia posta walinikatalia, walitoa sababu kuwa mafuta yakimwagikia barua itakuwaje? Ilinibidi kurudi kutumia njia za basi ambazo waliwahi kusema(wao mamlaka ya posta) hawaruhusiwi kusafirisha vifurushi bila kibali maalumu. Lakini ndiko ilikowezekana.

Tunahitaji mashirika ya kiserikali, yakiona kama hivyo ipo bidhaa hawajaiwekea utaratibu. Basi wanaboresha ili kuwahudumia wateja wapya. Sema serikalini kuna ile, 'wateja waje wasije mshahara wangu upo palepale' inaathiri utendaji. Bonus za anayeenda zaidi ya kiwango zipo sasa sijui tatzo n nn? Uwajibikaji?

Njia ya posta ndiyo ingewezesha sio tu duka lake lakini platform zote zinazouza kidijitali nchi nzima hata kabla hatujafika Afrika na dunia nzima. Ahsante sana mtoa mada kutukumbusha kuwa miundombinu tunayo ifanye tu kazi zake. Itimize wajibu wake.
 
Back
Top Bottom