Tutafikia Estado Novo bila udikteta...Sehemu ya 1

Mwita Maranya

JF-Expert Member
Jul 1, 2008
10,564
7,973
Asalam aleikum "wananzengo". Ni siku nyingi sana sijashiriki mijadala hapa JF lakini nimekuwa msomaji zaidi. Kutokana na mihemko ya kisiasa inayoendelea hapa nchini upotoshaji umekuwa ni mkubwa sana na watanzania wengine bila kutafakari wamekuwa wakilipuka na kufuata mizuka ya viongozi bila kutafakari athari za mihemko na mizuka hiyo.

Hivi karibuni baadhi ya vijana wa mtaa Lumumba wamekuwa wakijitahidi sana kuutetea ''uvunjifu wa katiba na sheria" unaofanywa na mwenyekiti wa ccm Taifa kwa kumfananisha na Waziri Mkuu na dikteta wa zamani wa Ureno. Hapa nimeona ni vizuri kuwashirikisha mawazo makini na mbadala kama yalivyoandikwa na kijana machachari Ben Saanane akimjibu mwandishi na Mhariri wa gazeti la raiamwema.

JUNE 23, 2016
Na Ben Saanane

HATUHITAJI udikteta kufikia Estado Novo, tunahitaji kilicho bora zaidi. Tunahitaji Katiba Mpya na bora zaidi. Naandika kujibu makala ya mwanahabari na mchambuzi mahiri Godfrey Dilunga ya gazeti hili toleo namba 462, yenye kichwa cha habari “Tunahitaji udikteta kufikia Estado Novo”

Katika makala hiyo rejea yake ilimhusu Antonio de Oliveira Salazar, Waziri Mkuu wa 100 wa Ureno aliyesimamia kile kile ambacho Wareno wanaita Estado Novo yaani ujenzi wa taifa jipya. Mwandishi anajenga hoja yake kwa kuusifia mtindo wa Salazar kutupilia mbali mfumo wa demokrasia ambayo mwandishi anaita kuwa “demokrasia isiyo na tija” na kuunga mkono udikteta wenye kuibua matokeo ya jumla yenye manufaa kwa wananchi wote.
Ametetea hoja yake kuwa Rais wa Awamu ya Tano John Pombe Magufuli anakabiliwa na mazingira hayo hivyo anapaswa kuitupilia mbali demokrasia anayoita “isiyo na tija” ili akumbatie udikteta. Eti hiyo ndio njia nzuri ya kujenga taifa jipya.

Katika Karne hii iliyostaarabika yaani karne ya 21 hakuna njia ya kujenga taifa jipya kwa kutumia udikteta. Haya mambo yaliwezekana kipindi hicho alipotawala waziri mkuu huyo kabla na baada tu ya vita ya pili ya dunia 1932-1968. Ni mbinu za karne iliyopita kipindi ambacho ilikua rahisi kuvumilia na kuendekeza udikteta na hata ukoloni. Ni kipindi ambacho hata taifa la waziri mkuu huyo lilijengwa kwa unyonyaji na uporaji wa raslimali za makoloni. Tanzania inahitaji mfumo thabiti wa kitaasisi ili nchi iweze kupiga hatua. Tunahitaji Katiba Mpya ambayo itatoa mwongozo bora kati ya watawala na watawaliwa. Rasimu ya Tume ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba ilikua na kila jiwe, tofali na vyote vilivyohitajika kujenga taifa jipya.
Rasimu ilitoa mwelekeo sahihi wa maadili ya kiuongozi, mgawanyo sahihi wa rasilimali za nchi, mgawanyo sahihi wa madaraka, nguzo za dola kama Utawala (Executive), Bunge (Legislature) na Mahakama (Judiciary).

Tanzania haiwezi kurudi nyuma hadi karne iliyopita na kukumbatia udikteta kwa kisingizio cha jaribio la kujenga Tanzania mpya kwa gharama ya demokrasia na utawala bora. Idd Amin wa Uganda aliingia madarakani na miezi ya mwanzo alishangiliwa na wananchi aliposema anataka kujenga uchumi na kuijenga Uganda kuwa taifa jipya kwanza ndipo aruhusu demokrasia. Kilichotokea kila mtu anajua. Nchi inayofuata msingi wa demokrasia ni lazima Bunge lifanye kazi yake ya kuisimamia serikali kama chombo cha uwakilishi wa wananchi katika kujadili na kuhoji juu ya uamuzi wa kisera na kisheria unaoamua mustakabali wao na taifa lao.

Ni lazima kuheshimu uhuru wa Mahakama na pia mgawanyo sahihi wa madaraka kati ya Bunge, Utawala na Mahakama. Ni lazima wananchi wapewe haki ya kutoa maoni yao kikatiba. Na katika hili kuna uhuru wa vyombo vya habari katika kusema na kuikosoa serikali pamoja na kutoa uhuru kwa asasi za kiraia. Utawala wa kidikteta hauruhusu kukosolewa, hauruhusu Bunge kuwepo au kama lipo hautaliruhusu kuwa na meno katika kuisimamia na kuiwajibisha serikali bali utataka kulidhibiti hata ikiwezekana kupandikiza spika anayewajibika kwa utawala na pia kamati zenye nguvu kama zile za PAC na LAAC zitafinyangwa katika namna ambayo hazitafurukuta.

Utawala wa aina hii unapenda kusifiwa tu na mara nyingi hufifisha taasisi za uwajibikaji hata kama utakua unadai kuwa unapambana na rushwa na kurejesha uwajibikaji. Ni rahisi kukutana na vituko vinavyokinzana na wanahohubiri. Unahubiri kupambana na rushwa lakini wakati huo huo hautaki kuipa nguvu ya kutosha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wala hutaki kuipa meno Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na kuifanya kuwa yenye nguvu kisheria au kuwa huru. Haya ndiyo yanayojiri katika utawala wa awamu ya tano. Rasimu ya Katiba Mpya ilikua na tiba za mambo yote haya.

Historia inaonesha kwamba sehemu yenye demokrasia uchumi hukua na hali hiyo huwa nzuri zaidi hasa kwa nchi zinazofuata uchumi wa soko na ambapo mataifa yanategemea diplomasia ya uchumi katika uhusiano wao na mataifa, mashirika ya kimataifa na wafanyabiashara binafsi.
Utawala wa kiimla hautabiriki hata kidogo na katika dunia ya leo wawekezaji wanahitaji kuwekeza kwenye nchi ambazo sera na sheria zinazoongoza nchi zinatabirika na sio kuwekeza fedha sehemu ambako utawala hauna dira, bali unategemea na uamuzi binafsi wa kiongozi wa nchi ambaye anaweza kuamka asubuhi na kuamua mali zote zitaifishwe au akaanzisha vita na wafanyabiashara.

Itaendelea...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom