Kuishi kwa kutegemea au kuvizia uteuzi ni moja ya changamoto kubwa kwa baadhi ya watu. Huondoa umakini, hugeuza mtu kuwa zezeta, na wakati mwingine humfanya mtu aonekane kama kichaa-ni suala la kisaikilojia zaidi. Ukisoma andishi lote la huyu anayejiita mtaalamu wa commmucation ni rahisi kuona kuwa ni andishi lenye msukumo wa matamanio fulani, na hapa bila shaka ni matamanio ya uteuzi. Anadhani, kwa kuwa andishi lake hili jepesi linamhusu Lissu basi wakubwa wanaweza kumfikiria. Wakimfikiria, kupitia andishi hili, nao watakuwa na matatizo!
Hisia katika matukio ya kijinai haijawahi kuwa ujinga, na wala haijawahi kuwa tatizo kisheria. Ukitaka kufahamu hilo ni rahisi sana. Ukienda polisi kuripoti kuvunjiwa nyumba yako na watu wanaodhaniwa kuwa wezi miongoni mwa maswali muhimu sana ambalo polisi watakuuliza ni je, nani unahisi kuwa amefanya tukio hilo? Hivyo, mpaka hatua hii sio IMMA wala TLS (TL) ambao wana hatia ya kuwahisi polisi katika tukio hili. Kama Nape alionyeshwa bastola mchana kweupe, Roma alitendewa alichotendewa na ikatangazwa kuwa baada ya siku fulani atapatikana na leo anatuambia kuwa "anaenda Zimbabwe", basi hakuna tatizo kwa TLS ya Tundu Lisu kuwa na hisia ya uhusika wa polisi au dola.
Huyu "mjanja mjanja" wa mjini anadai kuwa tamko la TLS linafanana na tamko la CUF. Nini hoja yake hapa? Analazimisha hoja kwamba uwepo wa TL TLS kama Rais unaigeuza TLS kuwa taasisi inayofanya mambo yake katika mwelekeo wa kisiasa za upinzani. Huu ni mtazamo wa awali kabisa wa serikali pamoja na chama chake cha CCM. Wengi wanafahamu kwamba hoja hii ilitumiwa sana kujaribu kumkwamisha TL kuwa Rais wa TLS lakini kilichotokea ni historia iliyoacha maumivu kwa genge la watu wavizia makombo ambao wanashangilia hata matukio yanayovunja haki za raia. Kuna watu wamejitoa mhanga kuunga mkono uvunjwaji wa Katiba na manyanyaso mengine yote ili waweze kudaka makombo yanayotoka kwa wasigina Katiba. Huyu ni miongoni mwao.
Kwani kuna tatizo gani vilio vya taasisi dhidi ya tukio lililofanywa IMMA vikifanana (hata kama kweli vinafanana)? Lakini muhimu zaidi, kwanini "mjanja mjanja" huyu wa mjini kama kweli alitaka kuonyesha mfanano wa statement ya CUF na ya TLS kwenye tukio hili hakuweka kwenye andishi lake hizo paragraph anazodai zimefanana ili kuimarisha hoja yake. Unajua kwanini hakufanya hivyo? -anajua wasomaji wengi ni wavivu hawawezi kuchukua muda kuchunguza taarifa hizo mbili, bali watachukulia alichokiandika yeye ndicho sahihi.
Huyu mvizia makombo anawahoji mawakili ni kwanini walikaa kimya wakati akina marehemu Mwakyusa walipouawa, lakini leo wanataka wagome kutokana na kulipuliwa kwa ofisi za IMMA? Hapa ndipo unaweza kuona zaidi uzwazwa wa "mtaalamu" huyu wa "communication". Sijui kiwango cha elimu yake kwenye eneo hili la communication analojinasibisha nalo, lakini angalau ni wazi kwamba hata mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa mass communication anaweza kujua pengine kwanini TLS ya wakati ule ilikuwa kimya wakati akina Mwakyusa wakiuawa lakini TLS hii ya kipindi cha "mabadiliko yanayozungumzwa sana na chama chake cha CCM" ime react mara tu ofisi za mawakili za IMMA zilipolipuliwa. Anatumia approach ya kizwazwa kujaribu kuwachanganya mawakili! Maneno kama haya yangezungumwa na watu kama mbunge Msukuma, isingekuwa na tatizo lakini sio mtu anayejitambulisha kama msomi.
Huyu "mjanja mjanja wa mjini" anadhihirisha weupe wake upstairs na matamanio yake ya uteuzi anavyoandika haya, hebu msome vizuri- "Hivi mnajua IMMA advocate ni kampuni "inayotajwa" KUCHOTA mabilioni ya fedha za EPA kupitia kampuni ya DEEP GREEN kiasi cha *BIlioni 8* zilichotwa, mnajua hilo? kama hamjui nendeni Brella kisha mkasome anuani za Kampuni ya *DEEP GREEN,* kisha mtangaze *MGOMO.*
Hivi mnajua huyu Rais wenu Lissu akiwa Bungeni mwaka 2012 Aliitaja kampuni ya IMMA advocate kuwa ilizitetea kampuni za TanGold na Deep green microfinances *KUCHOTA* pesa za EPA, halafu Leo HAWAHAWA imma advocate ndio wanaomtetea Lissu katika kesi zake?
Hivi mnajua maana ya vita ya *KIUCHUMI,* adui yako anaweza kutumia *MKEO, WATOTO* na hata Ndugu zako ili mradi *APATE USHINDI.*
Mwisho, Nawapenda sana *WANASHERIA,* mana najua mchango wao katika taifa la Tanzania, nawathamini sana Wanasheria wamaotanguliza *UZALENDO* kwa taifa Lao pamoja na changamoto tunazopitia kama taifa Changa, Nawapenda Wanasheria wanaosem *KWELI* kwa maslahi ya taifa Lao na Sio *MATUMBO* yao. "
Hicho alichokimalizia nimeona kimesambazwa sana mitandaoni baada ya press conference ya TLS (TL) kufuatia kulipuliwa kwa ofisi za IMMA, sasa mvizia makombo huyo atujibu maswali yafuatayo:
1. Kwa kuwa mpaka sasa hakuna mahakama yoyote iliyowatia hatiani IMMA kuhusika kuchota hizo bilioni 8, na kwa kuwa hakuna mahali popote panapoelezwa kuwa mawakili wa IMMA wamepoteza haki ya uanachama wao TLS, kwanini mvizia makombo unataka mawakili wasishiriki pamoja kulaani walichofanyiwa IMMA?
2. Tangu mwaka 2012 Tundu Lissu kama mbunge alipoitaja bungeni IMMA kuwa ilizitetea kampuni za Tangold na Deep Green serikali inayoongozwa na CCM chama chako unachokitumia sasa kuvizia uteuzi, ilichukua hatua gani?
3. Unafahamu kuwa mawakili unaowakumbusha leo habari za IMMA kutajwa bungeni, wanafahamu pia kuwa mwenyekiti wako wa CCM, ambaye leo unavizia akupe uteuzi, naye alitajwa kwenye kashfa nyingi tu zilizoigharimu serikali, ikiwemo kuuza, kujigawia/kugawia ndugu na 'rafiki' nyumba za serikali; kununua kivuko kibovu na anaendelea kuhusishwa na mengine mengi?
Mtaalamu yeyote wa mawasiliano (mwenye uelewa) hawezi kuwa negative kwenye suala la mgomo wa siku mbili wenye lengo tu la mawakili kuonyesha solidarity katika kulaani tukio kama hilo lililofanywa dhidi ya IMMA bila kujali limefanywa na nani. Lakini kwa kuwa wakati wote watu kama huyu mvizia makombo wanawaza teuzi na makombo mengine, kila jambo hata ambalo ni haki kwa wengine, ili mradi linaonyesha udhaifu wa serikali kwa namna moja au nyingine, wanaligeuza fursa ya kupiga kelele ili mteuzi awasikie!