Tundu Lissu: Jeshi la Polisi linaendeshwa Kikoloni ndio maana wanafikiria kupiga na kuonea watu

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu amesema muundo wa jeshi la polisi unapaswa ufumuliwe na sheria ya kuanzishwa kwake irekebishwe ili lilinde raia na haki zao.

Lissu alitoa kauli hiyo juzi nyumbani kwake Tegeta, jijini Dar es Salaam, katika mahojiano maalumu na Mwananchi, ambapo alisema mabadiliko ya viongozi wa jeshi hilo yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan hayakidhi matarajio ya wananchi.

Alisema muundo uliopo hivi sasa ni wa kikoloni, ndiyo maana baadhi ya polisi wanafikiria zaidi kudhibiti, kupiga na kufanya uonevu kwa kujiona wana mamlaka hayo kisheria.

Hata hivyo, juzi Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Tume ya kuangalia namna ya kuboresha Haki Jinai itakayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, akisaidiana na sekretarieti itakayokuwa chini ya Balozi Ombeni Sefue.

Katika uzinduzi huo, Rais Samia alisema mifumo ya Haki Jinai nchini imevurugika kwa sababu ya kupuuza maadili na si kutokuwapo kwa mifumo ya maadili.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Lissu, aliyerejea nchini wiki iliyopita akitokea Ubelgiji alikokimbilia kwa kuhofia usalama wake baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu wa 2020, alisema yeye ni miongoni mwa waathirika wa utendaji usiofaa wa polisi.

Alitolea mfano tukio la kushambuliwa kwake lililotokea Septemba 7, 2017 alipopigwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana alipokuwa akitokea kuhudhuria vikao vya Bunge akiwa katika nyumba za makazi ya viongozi Area C, ambapo mpaka sasa hakuna aliyekamatwa wala uchunguzi uliofanyika.

“Tatizo halikuwa IGP Sirro, amekuja IGP Wambura mambo ni yaleyale, kila kukicha polisi wanabambikia kesi, kupora, kuua, kudhulumu na kujeruhiwa. Hawa wakuu wanaochaguliwa wamelelewa na kukuzwa katika muundo na mfumo unaowapa nguvu ya kufanya hivyo wanavyofanya,” alisema.Lissu alisema Chadema wamepitia madhila lukuki yaliyosababishwa na polisi ambao wanawaza kutumia nguvu na kudhibiti mikutano yao na shughuli mbalimbali badala ya kuangalia namna watakavyotimiza wajibu wao kwa kuzingatia haki.

Lissu alisema polisi wanapaswa kuwa watoa huduma kwa raia na haki zao kama wafanyavyo wenzao wa nchi zilizoendelea, ikiwamo Ubelgiji alikokuwa akiishi tangu mwaka 2018 alikokwenda kwa ajili ya matibabu.

“Kule Ubelgiji polisi wanalinda raia na haki zao, mtu unaweza kwenda kwenye baa ukanywa halafu ukawapigia simu polisi kuwa huwezi kuendesha gari kwenda kwako, nao wakaja kukuchukua na kukupeleka ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea, nasi tujifunze,” alisema.


Uenyekiti Chadema

Kuhusu kutaka kuwania uenyekiti ndani ya Chadema, Lissu alisema hajawahi kuwaza wala kuwa na ndoto ya nafasi hiyo, lakini kumekuwa na watu wanaomhusisha kwa lengo la kutengeneza mtafaruku ndani ya chama.

Alisema watu wanaleta chokochoko ili afarakane na Mwenyekiti Freeman Mbowe na wapoteze nguvu za kudai Katiba mpya itakayowakomboa wananchi na madhila mbalimbali wanayopitia hivi sasa.

“Mimi sijawahi kusema popote kuwa nataka uenyekiti, watu wananisemea kwa lengo la kutuchonganisha ndani ya chama, si wasubiri niseme mwenyewe, hata wadhifa nilionao sikuutaka, nilikuwa Ubelgiji wenzangu waliniambia wanaona nafaa kwa nafasi hiyo, nami nikakubali,” alisema.

Mwanasiasa huyo ambaye katika uchaguzi wa chama hicho uliofanyika 2019 alihusishwa na kuwania nafasi hiyo, alisema Chadema kinazidi kuimarika kila kukicha na kuwatisha watawala wanaofanya hila kiparaganyike.

“Siwazi urais, ubunge wala uenyekiti Chadema, kipaumbele changu ni Katiba...Katiba...Katiba,” alisema.


Katiba ndani ya miaka mitatu

Kuhusu Katiba mpya, Lissu alisema anaamini inaweza kupatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Alifafanua kuwa maandalizi ya Katiba yanaweza kufanyika ndani ya mwaka mmoja na baadaye zikaendelea hatua nyingine.

Kuhusu suala la Katiba, Rais Samia, ameahidi kuunda kamati maalumu itayokuwa na jukumu la kuangalia namna bora ya kuukwamua mchakato wa kupata Katiba mpya.

Januari 3 wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa nchini Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema Serikali yake imedhamiria kuukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba mpya kwa namna watakavyokubaliana kwa siku za usoni.

Katika mahojiano na Mwananchi, Lissu alisema mchakato huo ulikwama mwaka 2014 baada ya kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa, lakini kwa kuwa hakukuwa na maridhiano wakati huo, haifai kuendeleza mchakato huo kuanzia kwenye Katiba Inayopendekezwa.

Alisema anapendekeza mchakato wa Katiba mpya uanzie kwenye rasimu ya pili ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, hata hivyo alibainisha kwamba itahitaji kufanyiwa marekebisho kwa sababu miaka 10 imepita sasa.

Alisema kuendelea na Katiba Inayopendekezwa maana yake ni kwamba Katiba itakayopatikana haitakuwa na tofauti na Katiba ya sasa kwa misingi na maudhui. “Huo unapaswa kuwa fundisho kubwa kwetu kuhusiana na suala zima la urais na madaraka ya Rais. Miongoni mwa mambo yanayopaswa kurekebishwa kwenye rasimu ya Warioba ni masuala yanayohusiana na mamlaka ya Rais,” alisema.

Lissu alisema rasimu ya Warioba haijampunguzia Rais madaraka, lakini imeweka utaratibu wa kudhibiti mamlaka yake. Alisisitiza kwamba hiyo haitoshi, Rais anatakiwa kupunguziwa madaraka aliyonayo.

“Kimsingi Rais anatakiwa apunguziwe madaraka, siyo yadhibitiwe kwa sababu kuna uzoefu mkubwa wa nchi nyingine zenye mfumo kama wa kwetu, kwamba haiwezekani kumdhibiti Rais, hata Marekani, kwa sababu Rais ni mtu mwenye nguvu mno,” alisema Lissu.

Mtaalamu huyo wa sheria alieleza kwamba mamlaka ya Rais yatakayopunguzwa yatakwenda kwenye taasisi nyingine na kuwarudia wananchi. Alisema taasisi zote zimekuwa ombaomba kwa Rais kwa sababu hawana mamlaka na kivuli cha Rais kiko kila mahali.

Alisema Katiba mpya inaweka utaratibu wa kubadilisha taasisi, lakini alisema kilichopo kwenye akili za watu kwa sasa ni Uchaguzi Mkuu wa 2025, hivyo kuna haja ya kufanya mabadiliko ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Lissu alisisitiza kwamba haihitaji muda mrefu wa kuunda Tume ya uchaguzi ambayo ina makamishna saba au zaidi na kuiwezesha Tume kupata watumishi wake kuanzia ngazi ya juu hadi chini.

MWANANCHI
 
Screenshot_20230120-225240_WhatsApp.jpg
 
Katiba na Tume Huru ya Uchaguzi ndo legacy Mama Samia ataiacha akumbukwe vizazi na vizazi.
 
Lissu akili hana yeye kutwa kuwalamba wakoloni anapata wapi nguvu za kuwasema?

Akiwa ulaya wazungu wazuri akiwa tanzania wazungu wabaya

Ovyo sana hl
 
Lissu akili hana yeye kutwa kuwalamba wakoloni anapata wapi nguvu za kuwasema?

Akiwa ulaya wazungu wazuri akiwa tanzania wazungu wabaya

Ovyo sana hl
Wewe usiyeovyo mbona hukutoa mapendezo yako.
 
Lissu akili hana yeye kutwa kuwalamba wakoloni anapata wapi nguvu za kuwasema?

Akiwa ulaya wazungu wazuri akiwa tanzania wazungu wabaya

Ovyo sana hl
Bila hao wazungu kuja africa hata chupi ungekuwa huijui madafaka
 
Back
Top Bottom