Leo hii nimechukua zaidi ya masaa manne kuwasikiliza viongozi wastaafu, maprofesa na wadau mbali mbali katika mdahalo uloandaliwa na TLS.
Hakika nimejifunza mengi na yanilazimu kuwashukuru sana Mzee wetu Jaji Warioba, Profesa Shivji, Mwanasheria kutoka Kenya, Profesa Tibaijika, viongozi wa vyama vya Siasa na taasisi nyinginezo hususani TLS wenyewe. Wote kwa ujumla wao wamezungumzia mambo muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.
Pamoja na yote yale wameniachia maswali magumu zaidi nimekaa na kujiuliza hivi tatizo hasa lipo wapi? Na tumefika hapa kwa sababu gani?
Kubwa zaidi lilojitokeza kwangu linatokana na hotuba ya Profesa Shivji alipozungumzia Misingi mikuu ya Demokrasia akifafanua juu ya pande mbili yaani upande Wananchi na upande wa Utawala. Na kilichojitokeza wazi kwangu ni Kupotea thamani na heshima ya UTU wetu. UTU ndio kiashiria cha ujenzi na usimamizi wa Uhuru na Usalama.
Taifa letu limepoteza UTU kiasi kwamba Utawala hauthamini wala kuheshimu Wananchi na Wananchi hawawathamini wala kuheshimu Viongozi wake. Haiishi hapo, tumefikia kiasi kwamba Utawala hauheshimu viongozi wenzao na Wananchi hawathamini wala kuheshimu Wananchi wenzao.
Na katika hali hii, Uhuru na Usalama wa wananchi upo hatarini kama ilivyo kwa viongozi wenyewe hawaaminiani wala hawaheshimiani isipokuwa kwa yule mwenye nguvu ya utawala na fedha, hii ndio Tanzania ya leo (status quo)
Swali linakuja tumefikaje hapa? Naamini kila mtu ana mtazamo wake lakini binafsi yangu akili yangu inanambia yote haya yametokana utovu wa nidhamu katika miiko na maadili ya UTU wetu kwa kuiga mifumo ya kigeni ambayo ilidhalilisha mila na tamaduni zetu kama ni misingi ya kale (primitive) ilopitwa na wakati.
Mifumo ya Demokrasia tuloichukua ndio chanzo cha kuharibika kwa misingi ya Demokrasia kupitia mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1984 na 1992 upande wa Jamhuri pia Uandishi wa Katiba ya Zanzibar mwaka 1984 na mabadiliko yalofuatia mwaka 2002. Isipokuwa nitaacha pembeni Katiba ya Zanzibar, hii inahitaji mada nyingine tofauti kabisa.
Najua hoja yangu inahitaji mjadala mpana zaidi lakini niseme kwamba mabadiliko haya ndio mwanzo wa matatizo yote yanayofuatia katika miongo tofauti ya Kiutawala kufikia leo hii.
Katika makosa makubwa yalofanyika ni kuondolewa kwa Miiko na Maadili ya Viongozi hivyo kupoteza Sifa zinazotakiwa za viongozi wetu Kitaifa. Kwa nafasi walizokuwa nazo viongozi serikalini, Wabunge na hata majaji wakaanza kumiliki utajiri pasi kuulizwa wamepataje mali na utajiri huo, hii njia panda ndio ikawa mwanzo wa mmomonyoko wa maadili na chachu ya rushwa kuzaliwa.
Jambo la pili lilikuwa ujio mfumo wa Vyama Vingi ambavyo havikuzingatia misingi ya Demokrasia ( Uhuru, Utu na Usalama) bali ilikuwa ni tiketi ya jicho la Uheshimiwa na kuingia Ikulu kutawala (mfumo wa Vyama vingi). Vyama vingi ndivyo viloweka nadharia ya kina nani watakuwa Waheshimiwa kati ya Wananchi wote na hii ikazaa tamaa ya utukufu wa nyadhifa hizo. Hakuna Chama hata kimoja kinachosimamia itikadi na Sera zake wakati wote ila kulingana na fursa zinazojitokeza.
Katika mukhtadha huo tulipoteza Siasa safi za vyama Kiitakadi, hasada ikachukua nafasi baina ya vyama vya Siasa, viongozi kwa viongozi, Wananchi na vyama pinzani na kibaya zaidi rushwa na upendeleo vikatumiwa kama zana katika teuzi toka chaguzi za ndani ya Vyama vya Kisiasa hadi Viongozi wa Kitaifa – Yakaibuka makundi ya timu za Wana, hasada ikazaa Chuki na Uadui matokeo yake UZALENDO kwa Taifa letu UKAPUKUTIKA.
Kwa hiyo tukiacha hoja ya Katiba Mpya pembeni, sisi Watanzania tuna wivu na chuki za kuhasimiana wenyewe kwa sababu ya fursa za madaraka na utajiri zimeletwa kupitia vyama vingi.
Viongozi waliopo madarakani hujiona wapo katika nafasi adimu sana ya Utajiri wa hadhi na mali na wanajua kuna macho ya wivu dhidi yao hata kama wanayofanya nia njema ama kinyume cha misingi ya demokrasia, bado utachikiwa tu. Siasa zetu zimekuwa ni za Ukinzani ambazo kiitikadi hazifanani kabisa na Upinzani kwa nia, dhamira na malengo ya Demokrasia.
Tujiulize wenyewe mpaka hapa tumefika ni viongozi wangapi wameuawa kwa ajali, risasi au sumu na hakuna watu walotiwa hatiani wala kuchukuliwa hatua. Nini hasa sababu za viongozi hao kuuawa? Bila shaka ni kunatokana na UADUI wa kisiasa walojenga dhidi ya kiongozi ama viongozi wengine iwe kwa nia safi au mbaya.
Wivu na Chuki sii lazima vitumike kwa wale washindani tu bali inaweza toka chini kwa wale wanaotaka kufika pale kiongozi alipofika ama kiongozi kulinda maslahi yake dhidi ya wale wanaotaka nafasi yake.
Kwa hiyo tunapozungumzia leo Maombolezi, Maridhiano na sijui Katiba Mpya ni muhimu kwanza sisi wenyewe tukubali mapungufu yetu kimaadili ili TUBADILIKE - Heshima ya Utu wetu na Uzalendo kwa Taifa ni utamaduni ulopitwa na wakati.
Hatuwezi fanya maombolezi ambayo baadhi yetu hawaoni umuhimu wala sababu. Hatuwezi fanya Maridhiano kwa kuwekeana masharti yasiyojali Utu wetu na Uzalendo kwa Taifa hili bali maslahi ya mtu au chama.
Mwisho hatuwezi kuwa na Katiba mpya inayotokana na maoni ya Wananchi wenye wivu, chuki na uadui isipokuwa Katiba lazima iwe ni mwongozo wa Wananchi hao bila kujali tofauti zao - Katiba ni ya Wananchi iheshimiwe na wote.
Maasalaam