Daaah! Ebwanaeee Sikuwahi kuwaza kitu kama hiki Komrade. Lakini kwa kutambua nakuthamini hisia zako ngoja nijaribu mkuu! Ila kwakuwa itakuwa ni habari ya kweli basi kuna baadhi ya majina ya mahali na ya wahusika sitaweza kuyataja kwa usalama wangu na wao pia....
◆Nilizaliwa uamishoni takribani miaka thelathini na kitu iliyopita mkoani Arusha. Asili yangu ikiwa moja ya makabila hodari nchini Tanzania. Katika malezi na makuzi nilifanikiwa kuwa na mdogo wangu wakuzaliwa wakike. Pia hatukuwa sisi wenyewe tu kama watoto wa baba na mama mmoja bali tulikuwa na ndugu zetu wengine kadhaa wakiume na wakike ambao baba yetu aliweza kuwazaa kwa mama wengine ambao sisi tuliwaita dada na kaka zetu. Maisha yalikuwa mazuri sana enzi hizo na ilikuwa kama ndio fashion ya kipindi hicho. Baba yetu alikuwa na pesa nyingi ambapo wakati wote sisi hatukuwa na mahitaji yakumshinda hata kidogo. Alihakikisha watoto wake hatupati shida yoyote kwani ni sisi wawili tu ndo tulikuwa tunaishi na baba yetu. Wale ndugu zetu wengine walikuwa wakiishi na mama zao huko walipo. Ila pamoja na upendo mwingi kwa baba yetu hatukuwa tukiishi na mama yetu mzazi bali tulikuwa tunaishi na mama zetu wadogo ambao kwa lugha ya leo tunawaita Mama wa Kambo. Kwetu sisi haikutusumbua kwakuwa kwanza tulikuwa wadogo sana na pia baba alikuwa anafedha hivyo hata kuteswa ilikuwa ni ngumu. Baba yetu alikuwa mkali sana na mkorofi na alikuwa mywapombe lakini si mlevi. Wakati fulani anaetoka safari kalewa hata kama iwe saa ngapi lazima tuamshwe tulenae chakula atuulize maswali ya shule sasa ikitokea tumekosea daaah tunapigwa vibaya mnoo. Hajali ni usiku au ni mchana na hachagui chakukupigia iwe mwiko,mkanda wa suruali,makofi yeye twende kazi hii ilinifanya mnyonge sana hasa ninapokuwa kweli nimekosea. Kuna wakati alishawahi kunipiga mpaka nikashindwa kukaa na hata kwenda shule sababu ya maumivu

lakini hii yote pia ilichangiwa na mama yetu mdogo yule mama namkumbuka vizuri sana hakuwa hana hata chembe ya huruma kwa baba yangu naamini alimpendea fedha tu na wala si kitu kingine.
Nikiwa darasa la nne na mdogo wangu akiwa la pili au la kwanza hivi tulifunga shule na likizo yetu ikabidi tuchukuliwe na huyo mama yetu mdogo mpaka kijijini kwao mkoa mwingine kabisa. Tulikaa kule kwa upendo kabisa na baba yetu alikuwa akitutembelea mara moja moja. Familia yao mama yetu mdogo nao walikuwa vizuri tu baadhi ya ndugu zake mmoja alikuwa akifanyakazi benki,mwingine alikuwa mfanyabiashara na mwingine alikuwa ameolewa nje ya nchi ila mtoto wake wa kike alikuwa pale kijijini na kijana wao wa mwisho alikuwa akisoma sekondari....
Baba wa familia hiyo alikuwa mkusanya ushuru katika kampuni moja ya mabasi. Ila huyu mjukuu wao wa kike alionekana ni malaika pale ndani sisi tulikuwa si kitu wala si chochote ila bado tuliheshimu na kutii vyote. Baada ya kukaa kwa muda huko ikabidi twende shule tu kwani zamani hizo hakukuwa na sheria zuizi sana tena kwa shule za msingi hakukuwa na tatizo. Hivyo kiujumla maisha yalikuwa salama tu.
◆Siku moja sikumbuki nilikosa kosa gani jamani ila nakumbuka mama yangu mdogo alinipiga sana na akanambia ngoja baba yako anakuja kesho na lazima nitamwambia. Nilijihisi marehemu wa muda. Nilikaa migombani chini ya mkahawa mmoja nikawaza nakuwazua nikiona vile jinsi kesho nitakavyokuja kupigwa na babangu sijui nitakuwaje Mungu wangu. Maana huyu mamangu mdogo alikuwa akisema jambo kwa baba aisee hauna bahati maana baba hatakuacha na kama ikitokea amekuacha jua umewekwa kiporo.
Baada ya muda mrefu kukaa pale chini ya mkahawa nikapata wazo rahisi sana nikajiuliza hivi sumu si inaua? Sasa kwanini usubiri uje uuliwe na baba yako si bora unywe sumu! Oooh Yes! Nikapata mwanga sasa nini chakufanya. Haraka nikaamka nikaelekea stoo ambayo ilikuwa imejengwa shambani kwa ajili ya kuhifadhi nafaka na mashine ndogondogo za kilimo. Niliingia ndani nakuanza kutafuta dawa ambayo ingenisababishia kifo ili tu nisikutwe. Baada ya kutafuta sana nilipata mfuko ukiwa na dawa ya bluu sikujua ni dawa gani lakini mi niliona tayari nimeshapata ninachokitafuta.
Ilikuwa kama saa 12:45 jioni nilienda kuoga ili nisijekutafutwa. Baada ya kumaliza kuoga nilirudi stoo kwenda kunywa ile dawa (Blue Copper). Kwakuwa ilikuwa ni ya unga nifanya kulamba. Niliilamba yakutosha halafu nikarudi ndani nikijua sitachukua muda mrefu nitakuwa nimeshakufa. Nilikuta chakula mezani nikala haraka haraka kisha nikaenda kulala. Ilikuwa imekaribia saa mbili usiku nilipoanza kutapika. Niliulizwa umekula nini nikasema sijala kitu ila matapishi ni ya rangi ya bluu. Sikukumbuka chochote hadi kesho yake nilipojikuta naruhusiwa kuondoka kurudishwa nyumbani. Mungu wangu sijafa!! Mbona ndo kama nimejiwashia moto tena moto wa mafuta ya petrol!! Nitamwambia nini baba yangu anielewe?? Isitoshe mama jana alisema leo ndio atakuja? Hapo ndio unasikia unatamani ardhi ipasuke utumbukie ndani usikutwe. Nikaomba sala zote nikalia moyoni kwa uchungu sana nikasema haya yote nahisi yasingelitokea kama mama angelikuwepo.

Nilichoka akili na mwili huku wasiwasi ukiwa mkubwa sana. Kila nikitafakari ujio wa baba yangu nilichanganyikiwa. Ilipofika usiku na sikumuona baba amani ilirejea kidogo kwani wakati huo magari ya kufika huko kijijini mwisho ilikuwa ni saa 1 jioni. Sasa ikabidi niamue jambo moja kuliko kukutwa na kujitafutia kifo au kilema cha maisha bora nitoroke nyumbani niende kusikojulikana. Asubuhi na mapema niliwahi kuamka nikavaa nguo zangu kawaida kisha nikaondoka. Nikaenda kupanda basi kuelekea mjini. Bahati nzuri watoto hatukuwa tukitozwa nauli hivyo nilifanikiwa kusafiri bure. Nilifika mjini mchana njaa inauma ila kwakuwa nimeshatoka kwenye eneo la mashaka na wasiwasi nilihisi kushiba kila wakati. Ilikuwa siku ngumu sana kwangu kuisha siku hiyo kwani nilizoea kupata kila kitu kwakuletewa na wazazi. Nilijitahidi kuficha aiba yangu na ya watoto wengine pale stendi lakini haikuweza kufichika kwani pamoja na kujifananisha na watoto wa mitaani lakini sikufanania kabisa. Usiku ule nilikaa mahali nikalia kwauchungu sana nikiwaza nitakula nini, nitalala wapi, na kwanini niko hapa!!! Machozi na kilio kilizidi ambapo nikutwa na baadhi ya watu nikilia, waliniuliza kwanini niliwajibu kwamba kuna vijana wamenipiga. Hivyo niliachwa pale. Baridi ilikuwa kali usiku nikiwa nimejikunyata pembezoni mwa mizigo ya abiria wakati wote kukiwa na kelele za magari na watu pia nikajikuta nalala. Nilishtushwa na konda aliekuwa anapakia mizigo saa kumi na mbili kasoro akinitaka niamke ili achukue mizigo. Unaitwa nani? Unaenda wapi? Wazazi wako wako wapi? Ni maswali ambayo wakati wote kila alieniona asubuhi ile aliniuliza wakati huo mimi sikutaka kabisa kuulizwa maswali hayo. Asubuhi kulipambazuka na safari ya mtoto wa mtaani (Chokoraa) ikaanzia hapo.....