Consigliere
JF-Expert Member
- Sep 9, 2010
- 12,037
- 24,595
Mkuu Malcom Lumumba umemaliza kila kitu, binafsi sikuwahi kuafiki Rwanda, na Burundi kujiunga EAC pia siafiki hili la Congo DRC kujiunga EAC, lakini sababu ulizozitoa zimenifundisha vitu vingi sana na the moment namaliza kuisoma nukta ya mwisho tayari kichwa changu kilishajenga Action Plan.Mkuu Red Giant nilitoa ahadi ya kurudi na sasa nimerudi na nitachangia kidogo juu ya hii mada ambayo ni muhimu kabisa. Nitatoa maoni kama Mwanasiasa, pia nitatoa maoni kama Mwansheria. Naomba niende moja kwa moja kwenye mada:
Congo DRC isitengwe bali isiruhusiwe kuingia kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwasababu itaongeza changamoto ambazo tayari EAC inazo na imeshindwa kuzimaliza kwa muda mrefu. Changamoto kubwa ni hii ifuatayo hapa chini:
Mosi, nchi wanachama wa EAC wanakumbwa na matatizo ya kisiasa ndani ya nchi zao ambayo kwa namna moja au nyingine yameugharimu huu ukanda muda na rasilimali nyingi ambazo zingewekezwa katika kufanya mambo ya msingi.
Uganda mpaka leo wanapigana na waasi wa Lord's Resistance Army wa Bwana Joseph Konyi. Upande wa pili kuna sintofahamu kubwa sana kwenye siasa zake za ndani na hatufahamu nini kitatokea nchini humo baada ya Raisi Museveni kutoka. Tunaweza kuhisi kwamba Uganda iko salama lakini kumbuka tangu nchi hiyo inapata uhuru hakujawahi kuwa na Raisi ambaye hatatoka kwa vimbwanga na kusababisha kuchafukwa kwa hali ya kisiasa nchini humo kuanzia Mutesa hadi Obote.
Rwanda nayo mpaka sasa iko kwenye vita isiyoisha na makundi ya waasi wa Kihutu ambao wako Congo DRC na duniani kote. Hivi karibuni siasa ya Rwanda imegubikwa na kiza kikali baada ya kusemekana kwamba kuna Watutsi ambao waliwahi kuwa ndani ya Serikali ya Raisi Paul Kagame wameunda mtandao mkubwa wa kutaka kumpindua. Rwanda kama nchi inaenda vizuri kwasasa lakini bado kuna sintofahamu kubwa kama Uganda ambako mpaka leo hawana uhakika na Smooth Transition of Power after the fall of their strongmen.
Burundi mpaka sasa unafahamu nini kimekuwa kinaendelea tokea mwaka 2015, na bado nako kuna sintofahamu kubwa sana na Serikali ya Raisi Nkurunzinza iko nje-ndani.
Tanzania na Kenya hazijatofautiani sana. Zimefanikiwa sana kwenye suala la Smooth Transition of Power hivyo kufanikiwa kukwepa sintofahamu nyingi za kisiasa ambazo zimewakuta mataifa ya jirani. Japo upande wa pili bado Kenya ina changamoto kubwa za kiusalama ambazo zimemfanya apoteze rasilimalu nyingi sana kule Somalia akipambana na kikundi cha Al Shabab huku Tanzania ikiwa inapita kwenye kipindi kigumu kisiasa ambacho pia kinaweza kuzaa sintofahamu kubwa sana huko mbeleni kama siasa yake itaendelea kwenye njia hii.
Ninachotaka kusema kwenye hoja hii ni hiki hapa: EAC iliundwa kama Jumuiya ya kiuchumi na siyo ya kisiasa. Haya ya siasa kama kuunda shirikisho ni malengo ya baadae sana (Future Objectives) ambayo hayatakiwi kuwa kwenye ajenda yoyote kwenye kipindi hiki.
Lengo kuu na ajenda ya sasa (Main and Primary Objective) inabidi iwe ni Uchumi kupitia soko la pamoja na sarafu moja. Kama tukifanikiwa kujenga uchumi wa pamoja basi ndiyo mambo ya siasa yaanze kuingia kwenye ajenda za vikao vyetu. Sasa machafuko ya kisiasa huwa yanatutoa kwenye mstari maana hutulazimisha kuacha kufanya mambo ya kiuchumi na kujiingiza kwenye siasa, kitu ambacho siyo lengo letu kama EAC.
Tokea EAC iundwe tumekuwa tukitatua matatizo ya kisiasa yanayogharimu rasilimali nyingi kuliko kufanya mambo muhimu: Tunalazimika kufanya hivyo kwasababu ni majirani zetu lakini haswa kwasababu ni wanajumuiya wenzetu. Tulianza na Kenya mwaka 2007-2008: Kenya na Alshabaab 2012:Tukaja Rwanda na Tanzania mwaka 2013: Burundi mwaka 2015: Uganda na Rwanda 2019. Sasa tukiileta DRC na ilivyo na matatizo lukuki basi fahamu kwamba tutabeba na changamoto zao kuanzia uchaguzi hadi waasi wa Kagame na Museveni.
Pili, Congo DRC kama nchi imeshaigharimu SADC ambayo ilijiunga mwaka 1997 punde tu baada ya kumtoa Mobutu Sese Seko madarakani. SADC ilijikuta inatumia muda mwingi sana kushughulika na CONGO DRC badala ya kujikita kufanya mambo ya msingi. Ikumbukwe Mzee Kabila alivutana sana na viongozi wenzake wa SADC pale alipotaka wamsaidie kupambana kwenye The Congo War lakini wakawa wanasuasua. Wakina Quett Masire wanataka kumsuluhisha yeye Kabila anasusia vikao. Unadhani nchi kama hii ikijiunga na EAC na ikapatwa na tatizo tutakwepa kweli kuhusika ???
Tatu, wengi tunatamani Congo DRC ijiunge EAC kwasababu ya rasilimali zake. Basi kama itijiunga na EAC itageuzwa rasmi kuwa kichaka cha mashindano ya wizi wa rasilimali zake baina ya nchi wanachama wa EAC. Mfano hai tu, Umoja wa Mataifa (UN) waliwahi kutoa taarifa ya uchunguzi kwamba kipindi cha Vita ya Congo Zimbabwe ilipewa na serikali ya Laurent Kabila malipo ya dola za Kimarekani Bilioni 5 ambazo zimetoka kwenye mali mbalimbali za watu wa Congo DRC. Haya malipo yalienda sambamba na mikataba ya madini ambayo Zimbabwe na Angola waliipata kwa kumsaidia Kabila.
Upande mwingine inasemekana mataifa ya nje yaliua zaidi ya tembo 12,000 kwenye mbuga ya Garamba. Umoja wa Mataifa uliilaani Rwanda na Uganda kwa kuiba maelfu ya rasilimali za watu wa Congo DRC kwa kisingizio cha kupigana na waasi.
Sasa hii ilikuwa miaka ya 1999-2003, unadhani DRC ikijiunga rasmi na EAC Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda watakaa tu kuziangalia zile rasilimali ??? Utatokea mvutano mkubwa sana baina yetu kuanzia kwenye uchaguzi wa DRC maana kila nchi mwanachama atataka aweke kwenye serikali mtu ambaye atakuwa na ushawishi mkubwa sana kwake: Rwanda na Uganda walishawahi kupigana kisa kutaka rasilimali za Congo DRC, sasa DRC ijiunge na EAC hapo waongezeka Tanzania na Kenya unadhani kuna utulivu hapo ???
Mfano mwingine ,angalia kilichotokea Burundi 2015 baina ya Tanzania na Rwanda kutaka kujenga ushawishi kwa serikali ya Bujumbura. Sasa piga picha Burundi alikuwa hana utajiri wowote ule, unadhani Congo mwenye utajiri atatuacha salama ???
Sisi Tanzania tuna utajiri mkubwa ambao Mungu ametupa na itakuwa ni ujinga kama tutaka Congo DRC iinge EAC kwasababu ya utajiri wake. Japo kimkakati (Strategically)ni jambo sahihi, lakini tatizo linakuja kwamba pale ambapo hatuna mpango maalumu na nini tutafanya na Congo DRC baada ya kuwa karibu na sisi. Hivyo tuiache tu na tusitafute matatizo yasiyo na ulazima wowote ule: Pia tusichume dhambi with this Imperialistic Mindset....
NINI KIFANYIKE KUHUSU CONGO DRC???
Hapa nitatoa maoni kama mwanasiasa:
Mosi, EAC ijikite kwenye kuimarisha taasisi zake yenyewe (Consolidation and Amalgmation of it's Institutions) na siyo kujitanua (Enlargement of the bloc) kwa kutafuta au kuruhusu wanachama wapya.
EAC imeiga vitu vingi kutoka European Union (EU) ambayo zamani ilikuwa ni European Economic Community (EEC) lakini haifanyi vizuri kama ambavyo EEC ilifanya. Umoja wa Ulaya ulianza kama Umoja wa Uchumi (Economic Union) na siyo Umoja wa Kisiasa (Political Union), lakini baadae ndiyo ukafika hapa ulipo. Ulipitia hatua
Ulianza kutengeneza kitu kinachoitwa The European Coal and Steel Community mwaka 1951 ambayo ilikuwa ni taasisi iliyoundwa kwa lengo la kuhakikisha makaa ya mawe na chuka vinasimamiwa na Chombo/Taasisi moja ya kimataifa inayojitegemea ili kuzuia mvutano baina ya nchi kubwa kama Ujerumani na Ufaransa ambao ulipelekea kutokea vita ya kwanza na ya pili ya dunia.
Aliyesuka huu mpango anaitwa Jean Monet ambaye alisema ili tuweze kujenga umoja imara ni lazima tuhakikishe mataifa yenye nguvu na rasilimali nyingi ya Ujerumani na Ufaransa yanaungwanishwa kiuchumi kiasi kwamba nchi yeyote haiwezi kufikiria kwenda vitani na mwenzake. Kweli walifanikiwa sana maana mkataba huu ulisainiwa na mataifa sita (Ujerumani Magharibi, Ufaransa, Italia, Ubelgiji na Luxembourg) hata yale ambayo yalikuwa hayana rasilimali kama Ubelgiji na Luxembourg walinufaika.
Mwaka 1957 wakasaini mkata wa kuunda taasisi nyingine iitwayo The European Atomic Energy Community ambayo kazi yake ilikuwa kuzimamia uzalisha wa nishati ya nyuklia Ulaya ili kuwasaidia wanachama kupunguza utegemezi kwenye mafuta, pia kuuza nishati ya akiba kwa mataifa yasiyo wanachama. Hili nalo walifanikiwa sana.
Mwaka 1957 wakatengeneza sasa Umoja wa Uchumi wa Ulaya ambao leo ndiyo Umoja wa Ulaya. Lakini hawakuwa na haraka na hili liliwezekana kwasababu wao walikuwa na hali nzuri ya kisiasa nchini mwao. Mwaka 1967 taasisi za European Economic Community, European Steel and Coal Community na European Atomic Energy Community ziliungwanishwa kuwa chombo kimoja. Biashara baina ya wanachama ilikuwa kwa asilima 28.4%.
Hawakukimbilia kujitanua bali walijijenga kwanza wao kiuchumi na kisiasa kabla ya kuhakikisha wanayakaribisha mataifa mengine kama Uingereza mwaka 1973. Japo wanafanya vizuri lakini bado wana matatizo sana, Raisi wa Ufaransa Charles De Gaulle miaka ya 1969 hakupenda Uingereza ijiunge na EEC kwasababu alisema italeta matatizo kwenye jumuiya hivyo alipinga sana hadi anafariki.
Uingereza aliruhusiwa kujiunga baada ya De Gaulle kufariki. Lakini mbali na yote yale siasa za Uingereza zimeutikisa Umoja wa Ulaya kama ambavyo De Gaulle alionya. Sasa Uingereza taifa lililoendelea sana kuliko Congo DRC matatizo yake ya ndani yamevuruga Umoja wa Ulaya unadhani ni busara kuleta tena mgeni ???
Hapa hoja yangu ni hii: Kichwa na Moyo wa EAC ni Kenya na Tanzania wala siyo rasilimali za Congo DRC. Kama tunataka EAC imara basi ni lazima tuhakikishe Kenya na Tanzania zinaelewana na kuzungumza lugha moja. Maana binafsi naamini ushawishi wa Kenya na Tanzania wakiwa wanaongea lugha moja ni hatari kuliko mlipuko wa bomu la kiatomiki na hakuna taifa la Afrika linaweza kuwashinda. Raisi Kwame Nkhuruma alilifahamu vizuri hili suala ndiyo maana alipinga sana EAC isiwe nchi moja.
Kenya na Tanzania wakiungana basi lazima Uganda, Rwanda na Burundi watafuata tu. Kenya na Tanzania zina Uchumi mkubwa, ushawishi mkubwa sana kikanda na kimataifa, zimekaa pazuri sana kijiografia, zina rasilimali nyingi na zina watu wengi wanaozungumza lugha moja. Wakenya na Watanzania hawapatani kwasababu wamefanana mno tabia, fanya uchunguzi utaligundua hili.
Mtifuano wa kiuchumi na kihistoria baina ya Kenya na Tanzania ndiyo unavuruga EAC. Tunafanyiana hujuma badala ya kuunganisha nguvu za kitaasisi ili tujikwamue hapa tulipo. Hujuma kwenye kilimo, hujuma kwenye bandari na hujuma kwenye viwanda bila kufahamu kwamba Afrika Mashariki yote tunaweza kuwa Mamlaka moja ya Bandari ambayo ingetusaidia sana.
AU tungeweza kuanzisha Joint Venture Agreement kupitia Special Purpose Vehicle kwenye kuratibu biashara ya Usafiri wa anga. AU tukaunganisha nguvu kwenye tafiti za Uchimbaji wa mafuta na gesi mbona tungefika mbali sana tu. Wazungu walitwangana ndiyo wakapata akili kwamba kumbe tunaweza kushirikiana bila mabomu na vifaru.
Lakini sisi tunataka kushindana kisa kulipizana visasi vya ugomvi wa Mzee Kenyatta na Mzee Nyerere. Leo hii kwa mitandao ya kibiashara ambayo Kenya na Tanzania tunayo kupitia nguvu za diplomasia za nchi zetu kama tukishirikiana sauti yetu itafika hadi mwisho wa dunia. Nashangaa kwanini hatulioni hili. Binafsi Kenya and Tanzania is a key, ndiyo maana hata Rwanda, Burundi na Uganda walipovutana hakikutokea kitu sana lakini Kenyatta na Jakaya wakivutana lazima EAC iyumbe. Hujiulizi kwanini ???
Pili, na mwisho kabisa natoa ushauri kama mwanasheria sasa. Congo DRC asiwe mwanachama ila aidha apewe nafasi ya mtazamaji (Observer Status) kwanza ndani ya EAC huku akijifunza mwenendo mzima wa EAC. Sambamba na hilo EAC tunaweza kusaini mkataba maalumu wa Congo DRC (Sui Generis Treaty) ambao utampa nafasi ya kipekee kunufaika kiuchumi bila kuwa mwanachama. Anaweza akaandaliwa vipengele (Extracts Clause with Limitations ) kutoka mikataba mbalimbali (Protocols) ambayo EAC ameshasaini. Anaweza kufanya kama ambavyo Uingereza na Umoja wa Ulaya walifanya miaka ya 1960's- 1970's au ambavyo wanataka kufanya baada ya Brexit.
Tujijenge kwanza sisi ndiyo turuhusu waliovurugwa kama Congo DRC wajiunge.
Uliyoyaongea naona yanafanyika kinyume yakionyesha tabia halisi za kiafrika ni kama tunataka kuanzia pale wenzetu walipofikia yaani kwenye success point za wenzetu badala ya kurudi chini na kutengeneza njia zetu.
Pia, kwa kudhani wingi wa rasilimali ndiyo huleta nguvu na mshikamano wenye tija tunakosea sana, kwetu Congo DRC anaweza akawa ni fursa nzuri kuliko mwana jumuia mzuri, tunaangalia zaidi rasilimali na rangi yake hatujiulizi rasilimali za Kenya na Tanzania zimeinufaisha vipi Jumuiya.
Kwa mchanganuo ulioutoa EAC inaweza ikajulikana zaidi kama EAVC (East Africa Violence Community)