TMA: Mvua za El-Nino kuendelea hadi Aprili 2024

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema bado kuna viashiria vya uwepo wa El-Nino hadi Aprili mwaka huu.

El-nino ni mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la kati la Kitropiki kwenye Bahari ya Pasifiki.

Mwaka jana, TMA ilieleza kuwepo kwa El-Nino katika kipindi cha mvua za msimu wa vuli zilizotarajiwa kuanza Oktoba hadi Desemba.

Mvua zimeendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali nchini hadi sasa, TMA ikizitaja kuwa ni za nje ya msimu ambazo zimechangiwa na unyevunyevu kutoka magharibi ya misitu ya Congo, pia kuendelea kwa viashiria vya El-Nino.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Januari 30, 2024 Meneja wa Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla amesema viashiria vya El-Nino bado vipo hadi Aprili.

“Viashiria vyake bado vipo, ingawa nguvu yake si kubwa kama ilivyokuwa awali, mwanzo ilionyesha kilele chake ni Desemba au Januari, lakini viashiria bado vipo hadi Aprili,” amesema.

Akizungumzia wingi wa mvua katika maeneo mbalimbali nchini, amesema unasababishwa na migandamizo midogo ya hewa iliyoko mashariki mwa Kisiwa cha Madagascar.

“Hii migandamizo imekuwa na mchango mkubwa kwenye kuvuta upepo wenye unyevunyevu kutoka magharibi ya misitu ya Congo kuja maeneo mengi ya nchi.

“Kuwepo kwa migandamizo hii kwa takribani wiki tatu na kuimarika kwa ukanda wa mvua kumesababisha uwepo wa mvua hizi, ingawa inaonyesha Februari mosi na pili, 2024 migandamizo hii itakwenda kusini mwa ncha ya Bara la Afrika, hivyo hata mvua zitaanza kupungua,” amesema.

Akizungumzia athari kwa wakulima, amesema maeneo ambayo mvua inanyesha kwa wingi, kiwango cha unyevunyevu kwenye udongo huongezeka.

“Unyevunyevu ukipitiliza unaweza kuathiri mazao ambayo hayaendani na maji mengi, ni vema wakulima wachukue ushauri kutoka kwa maofisa ugani,” amesema.

Amesema katikati ya Februari, 2024 watatoa utabiri wa mvua za masika zinazotarajiwa kuanza Machi hadi Mei na kutoa mwelekeo wake.

Jana Januari 29, 2024, TMA ilitoa angalizo la uwepo wa hali mbaya ya hewa kwenye mikoa ya Morogoro, Lindi, Iringa, Mtwara, Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma kwa siku tano kuanzia leo Januari 30, 2024, ikiwataka watu wachukue tahadhari.

Angalizo hilo limetolewa tayari, baadhi ya mikoa kama vile Dar es Salaam na Morogoro ikishuhudia madhara makubwa ya miundombinu ya barabara, madaraja na nyumba yaliyotokana na mvua.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom