Nawaomba sana Ccm (ambao vyombo vya dola viko chini yao), wajue kwamba idadi kubwa ya Watanzania wa sasa ni vijana. Kwa kawaida, vijana ni watu ambao katika kutenda jambo lolote wana jazba nyingi kuliko utulivu. Ukichanganya hali hii na athari za corona zilizofanya biashara nyingi zidorore, na pia ukweli kwamba zaidi ya 90% ya vijana waliomaliza masomo hawana ajira, vijana wengi sana wana msongo wa mawazo (stress).
Kwa sababu hiyo, wale ambao ni mashabiki wa upinzani, hawawezi kukubali kabisa kwamba Mbowe anaweza kuwa na tuhuma za kweli za ugaidi kama ambavyo vyombo vya usalama vinavyosema. Bado wanakumbuka jinsi Mdude Nyagali alivyofungwa kwa kesi ya kubambikwa hadi alipoachiwa juzi juzi tu. Kwa hivyo kuna uwezekano mkubwa sana kwamba wataona kwamba hata hizo tuhuma dhidi ya Mbowe bila shaka ni za kubambikiza tu. Kwa stress walizonazo, hao vijana mashabiki wa upinzani watakuwa wameundiwa chuki kubwa sana mioyoni mwao.
Jambo moja ambalo pia linawafanya watu wengi waamini kwamba kukamatwa kwa Mbowe ni moja ya matukio ya Ccm kuonea wapinzani (hasa Chadema) ni ukweli kwamba viongozi wa Chadema walikamatwa wakati huo huo Mbowe alipokamatwa kwa kosa la kutaka kwenda kufanya kongamano la kudai katiba mpya. Wangekuwa wamekamatiwa kwenye ukumbi tungesema wamekiuka amri ya kuzuia mikutano kwa sababu ya corona. Lakini walikamatiwa hotelini. Nashindwa kuelewa hao waliowakamatia hoteli watathibitisha vipi mahakamani kwamba waliokamatwa kweli walikuwa na mpango wa kukutana ilhali hawakuwa wamefika ukumbini.
Kwa mawazo yangu, naamini matendo ya kuwakamata wapinzani kwa mtindo huo yanachochea chuki kubwa ndani ya mioyo ya wapinzani. Naomba wana Ccm mtambue kwamba chuki ikishapandwa ndani ya mioyo ya watu, inakuwa vigumu sana kuiondoa. Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalitokana na chuki zilizokuwa "zimejikusanya" ndani ya mioyo ya watu kwa muda mrefu. Kwa sababu tu Tanzania imekuwa nchi yenye amani kwa muda mrefu,.haina maana amani hiyo haiwezi ikapotea ghafla kwa sababu ya chuki zilizo ndani ya mioyo ya watu. Halafu, tukumbuke kwamba kule Soweto Afrika Kusini, watoto wadogo wa shule za msingi waliamua "liwalo na liwe" wakaanza kupambana na askari wa makaburu wenye mabunduki, mabomu na mbwa bila kujali kwamba wenzao walikuwa wanauawa wao wakiona. Kwa hivyo tusidhani ya kuwa hata hapa Tanzania hali kama hiyo haiwezi ikatokea kama vijana wengi wanaona wanaonewa kwa sababu tu ni wapinzani.
Nawaombeni sana, sana, vyombo vya ulinzi. Mnapofanya kazi zenu, msizifanye kwa namna ambayo itawafanya mwonekane mnaonea watu. Kama mlikuwa mmeshapata habari za tuhuma dhidi ya Mbowe kabla hajaenda Mwanza, basi mngemkamata kabla hajaenda huko. Kama mlipata hizo habari baada ya kujua anajipanga kuingia kwenye kongamano la katiba, mngemwacha amalize kongamano ndipo mumkamate. Hapo ingeonekana wazi kwamba kosa alilokamatwa nalo sio la kudai katiba mpya. Nawaomba mtambue kwamba mnasababisha nchi yetu ionekane katika "picha mbaya" kwa Watanzania wengi na mataifa ya nje (wakiwemo wafadhili na wahisani wetu).