Titus Amigu: Maneno uchawi au mchawi kwa dhana za Kiafrika hayastahili kuwamo kwenye Biblia

EP cosmetics

JF-Expert Member
Oct 18, 2015
2,469
3,839
Nimekataa uwapo wa uchawi na wachawi kati yetu. Tulionao ni wababaishaji na watu tunaowatuhumu kwa kuwasengenyasengenya tu. Wachawi kiukweli hawapo na bado ninawatafuta. Ninataka wajitokeze na nimesema kama kuna anayewajua awataje, atuitie au atuoneshe

Nisikilizeni vijana na wasomaji wangu. Ni hivi, kwenye Biblia hakuna hata mahali pamoja palipoandikwa kwa Kiswahili neno “Mchawi” au “Uchawi” kwa mastahili. Biblia za Kiswahili zimetutumbukizia maneno hayo pasipo simile.

Maneno hayo yaliyotumbukia humo hayabebi maana na dhana halisi ya kilichosemwa katika lugha asilia za Kiebrania au Kigiriki. Dhana ya Kiafrika juu ya uchawi na wachawi haiingii kwenye Biblia hata kidogo.

Nina hoja. Nadhani mnaweza kukubaliana nami kwamba katika makabila yetu dhana au fasili ya uchawi si nyepesi. Ni dhana mtambuka.

Dhana au fasili yetu ya wachawi ni ya watu wenye nguvu za ajabu za kufanyia mambo ya ajabu kama tunavyosema wenyewe, labda kuruka angani kwa nyungo, fisi, mbweha, pembe au mikeka, kunyesha mvua hata kiangazi, kupiga radi wapendavyo, kuingia majumbani mwa watu kwa kupitia milango na hata madirisha yaliyofungwa, kuroga tokea mbali, kutazama na kudhuru watu kwa macho au kauli, kuwabadili watu wakawa labda mainzi, nyoka au ngedere na kadhalika. Orodha ni ndefu mno. Kwa lugha yenu vijana, “orodha ni ndefu kishenzi!”

Ndipo kwetu sisi “wachawi” ni watu wenye uwezo wa kuwatoa wafu makaburini na kuwala nyama maiti, wenye uwezo wa kufanya mikutano usiku pasipo watu wengine kuwaona, watu wenye kuwatengeneza na kuwatunza watu kama misukule, watu wenye uwezo wa kuroga wengine kutoka mbali, watu wasioweza kuonekana wanapofanya shughuli zao, watu wenye kutembea usiku uchi wa mnyama, watu wanaoweza wakawatazama watu kwa macho ya aina yake wakadhurika vibaya, watu wanaoweza kuwasemea wenzao maneno ya laana au mikosi wakadhurika na kadhalika.

Naomba maweza mengine muyaongezee wenyewe maana, bila mashaka, kwenu dhana hii ipo nanyi, kama humwamini wenyewe, walau mmesikia habari zake.

Aghalabu, mnajua jinsi tunavyodhuriana katika jamii zetu, kujichonganisha, kupoteza muda na pesa nyingi, kwa shughuli za jamaa kushikana na kwenda kunyoana kwa waganga wa kienyeji, watu kuwaalika akina Lambalamba na kusafisha vijiji vyao, watoto kuwatuhumu na kuwaua wazazi wao, wanavijiji kubomoleana nyumba au kuchomeana moto wakifukuzana kwa ukatili mkubwa.

Watu kuwaua vikongwe na wazee, watu kuwafukuzia watuhumiwa wao kwenye vijiji vya wachawi, watu kuwapiga na kuwachomea wengine nyumba moto au kuwaharibia mazao na mali zao wakidaiwa kuzuia mvua, timu zetu za michezo kutumia pesa nyingi kulipia mabenchi ya ufundi yaani waganga wa kienyeji.

Wachezaji wetu kupewa masharti magumu au kulazwa makaburini kabla ya mechi, watu kuzindika nyumba zao kwa hirizi, watu kuwaua au kuwadhuru albino wakitafuta viungo vyao wapate vyeo na utajiri, watu kutafuta mifupa na mafuvu ya binadamu kwa ajili ya kuboreshea biashara au ajira zao, akina mama kuuawa kwa sababu ya sehemu zao za siri, watu kunyofolewa macho, ndimi na masikio, watu kutafuta, kuchukua na kuvaa hiziri na kadhalika.

Sina mashaka, haya yote mnayajua, imani na vitendo vilivyoipa Tanzania nafasi ya kwanza Afrika katika kuamini uchawi, kwa kadiri ya utafiti wa mwaka 2009 wa PEW Research Centre ya Washington D.C, Marekani.

Lakini habari ngeni kwenu nyote ni hii kwamba Biblia haina dhana hiyo, hata chembe na hakuna panapostahili kutokea neno uchawi au mchawi ndani yake. Maneno hayo yanatokea isivyostahili.

Msishtuke. Ndipo hapo hapo ninapojaribu kulitangaza jambo hili pasipo kusadikika. Wengi wananishangaa sana, lakini si kitu nimeunda jeshi la mtu mmoja! Kumbe, nguvu ya hoja yangu ni lugha asilia zilizotumika kuandikia Biblia. Nawahakikishieni nyote kwamba dhana yetu ya uchawi na wachawi haimo kwenye Biblia maana maneno yote asilia yaliyotumika humo hayana maana zetu.

Msinibishe. Nendeni kwenye lugha asilia Kiebrania (Agano la Kale) na Kigiriki (Agano Jipya). Biblia katika lugha zake asilia hazina maneno yenye maana zetu. Ndiyo maana nakataa kwa nguvu na kwa kujiamini kabisa.

Tafsiri za Kiswahili na Kiingereza zinatupotosha. Kwa bahati njema baadhi ya watafsiri wa nakala za Kiingereza wamejitahidi sana ama kuepuka au kutumia kiusahihi maneno: 'witchcraft', 'sorcery' na 'magic'. Katika Kiswahili tuna maksi ya karibu sefuri.

Tusiandikie mate, wino ungalipo. Hebu tuthubutu kujitengea muda siku fulani tujisomee na kutafakari kwa utulivu sehemu zifuatazo: Mwa 41:8.21, 1Sam 28:7, Kut 7:11.22, 8:7.18.19, 9:11, Law 19:26, Kum 18:10-11, Isa 3:3, 47:9.12, Dan 1:20, 2:2.10.27, Nah 3:4, Mdo 13:6.8, 19:19, Gal 5:20 na Ufu 22:15. Hizi ndizo sehemu maarufu kwa maneno uchawi, mchawi au wachawi. Zatupasa kuzichambua kwa makini. Maneno yametumika kwa kupwaya mno.

Nawahakikishieni tena kwamba tukizitalii sehemu hizi katika lugha zake asilia, hatutapata maana ya wachawi katika dhana ya Kiafrika isipokuwa mojawapo ya maana hizi: mabingwa wa kutumia visivyo utaalamu mbalimbali, wachanganya madawa, wacheza mazingaombwe, watu wenye kuwatinga wenzao kwa utaalamu, wataalamu wa nyota, watabiri, wapiga ramili, waona maono, watu wanaotafuta ushauri wa wafu au mapepo, watafsiri ndoto na kadhalika. Maana hizi ndizo zilipaswa kuchaguliwa vyema na waliotutafsiria Biblia katika Kiswahili zamani zile.

Kumbe, wote waliotajwa hivyo, kwenye Biblia, kwa Wayahudi, walikuwa wataalamu waliokuwa wanajulikana na watu na utaalamu wao uliwekwa kwenye vitabu vyenye kusomeka bayana (rej. Mdo 19:19).

Ndipo, basi, tusidanganyike tukachukua dhana yetu ya uchawi ya Kiafrika tukaiingiza kwenye Biblia takatifu. Tutakuwa waongo na wakufi wa weledi. Narudia na kusisitiza kwamba katika Biblia hicho kinachotafsiriwa kama “uchawi” kilikuwa aina ya elimu au utaalamu.

Ndiyo maana kulikuwa na vitabu vyake kama nilivyosema sasa hivi (rej. Mdo 19:19) na watu wenye elimu hiyo walikuwa wakijulikana na wengine. Wataalamu wenyewe hawakumwonea mtu yoyote haya na wala hawakujificha. Ndiyo maana waliwahi kuitwa na Farao wakatokea barazani (Kut 7:11) na waliwahi kuitwa na mfalme Nebukadneza huko Babiloni wakajumuika na wataalamu wengine (rej. Dan 2:2). Hali kadhalika tazama jinsi Simeoni “mcheza mazingaombwe” alivyokuwa anajulikana na watu (rej. Mdo 13:6.8).

Tusemeje? Wale waliokuwa wanachuana na Musa wakati ule wa mapigo, hawastahili kuitwa wachawi kwa kadiri ya dhana yetu, isipokuwa “maprofesa wa mazingaombwe” maana wakati ule kulikuwa na shule ya kufundishia uchezaji mazingaombwe kule Misri.

Ndiyo maana, kama maprofesa wenye elimu yenye kikomo, walishindwa kufanyiza vituko vya mapigo kadhaa. Mwanzoni mwa shughuli zake za kufanyiza miujiza, Yesu alidhaniwa kuwa amesomea katika chuo cha namna hiyo. Kwa ushuhuda, rejea maana ya watu wa Nazareti walivyojikwaa kwake katika Mk 6:1-6. Kifupi, katika tukio hilo la Nazareti, watu wa kijiji chake walikuwa wakihoji Yesu alipataje ada ya kusomea mazingaombwe wakati familia yake ilikuwa na kipato cha maseremala tu.

Hali kadhalika, wale waliokuwa wanaitwa na Mfalme Nekabudneza wamtafsirie ndoto yake wanastahili kutafsiriwa kama “makuhani watafsiri mambo” na siyo wachawi kwa kadiri ya dhana yetu. Soma vyema Dan 1:20 na 2:2.

Naendelea kukujuza. Usichoke kusoma. Kama wataalamu, watu tunaowasoma katika Biblia zetu za Kiswahili kama wachawi, walikuwa wanajulikana na watu. Nimesema wala hawakujificha. Zaidi ya hayo, kama wataalamu hawakuwa peke yao.

Ndiyo maana wakati wa matatizo walipokuwa wanaitwa wasaidie walikuwa hawaitwi peke yao isipokuwa pamoja na wataalamu wengine, kama vile, waganga, wenye hekima, mamajusi (tukitaka wanajimu), Wakaldayo (yaani watu wenye akili sana) na kadhalika (rejea tena Kut 7:11 na Dan 2:2).

Kinyume chake, huku kwetu tunasema sema tu majumbani au vijiweni mwetu. Tuseme tunasengenya tu. Huku kwetu nani anawajua “wachawi” wetu na nani anaweza kutuitia “wachawi” hao? Wako wapi? Nani anawajua? Hayupo Kwa nini hayupo anayewajua? Kwa sababu dhana yetu ya uchawi na wachawi ni tofauti kabisa na ile ya Biblia.

Katika Biblia unazungumziwa utaalamu sisi tunazungumzia uovu.
Biblia za Kiswahili zinatupotosha kama “Hatujiongezi”. Dhiki ya tafsiri imetufikisha pabaya pasipo kukusudia. Ndugu zanguni au rafiki zangu, maneno yaliyokosewa kutafsiriwa vizuri katika Biblia zetu za Kiswahili hata tukawa na maneno uchawi na mchawi ndanimwe ni haya: katika Kebrania 'artam' na 'artamim', 'oobh' na 'baelath oobh'.

Neno artam lilistahili kutafsiriwa kama kuhani mfasili mambo, au mtafsiri wa ndoto au kuhani msomaji mambo. Baelath oobh maana yake ni mwona maono au mtu anayetafsiri mambo kwa kuwasiliana na wafu.

Katika Kigiriki ni “farmakeia” na “farmakos”, “mageia” na “magos”. Kwa upande wake maneno “farmakeia” lilistahili kutafsiriwa kama “utaalamu wa uchanganyaji madawa” na hivyo “farmakos” kuwa “mchanganya madawa”. Neno “farmakeia” ndilo lililozaa neno la Kiingereza “pharmacy” neno tunalotumia sisi na kuliweka katika Kiswahili kama “sehemu ya dawa” au “duka la madawa”. Mnanielewa vizuri? Mnaona hapo? Mbona hatuiti “PHARMACY” “duka la uchawi”? Na mbona hatumwiti anayehusika na “pharmacy” mchawi?

Mintarafu neno “mageia” linalozaa neno “magic” lilistahili kutafsiriwa “utumiaji wa mbinu au elimu fulani kupata matokeo fulani”, kwa mfano kutumia ujuzi fulani, dawa fulani, maneno fulani, matamshi au formula fulani. Na mwenye kutumia mbinu hizo ndiye anayeitwa “magos”.

Ndipo hapa walipoingia wale wataalamu wa kusoma nyota kutoka mashariki (rejea sikukuu ya Epifania au Tokeo la Bwana). Wataalamu hawa wanaitwa kwa Kiingereza “magi” au “astrologers” nasi Waswahili tunawaita mamajusi au watu wenye hekima na siyo wachawi.

Ndipo hapa Waingereza walipojitengenezea istilahi za “black magic” kama utaalamu wa kudhuru watu na “white magic” kama utaalamu wa kufanya maajabu bila kudhuru watu, yaani mazingaombwe ya kawaida.

Kwa vyovyote, watu wanaoujua lugha asilia za Biblia hawawezi kuingia katika wepesi wa kutafsiri maneno “artam”, “artamim”, “oobh”, “baelath oobh”, “farmakeia”, “farmakos”, “mageia” na “magos” kama “uchawi” au “mchawi” kwa dhana za Kiafrika.

Katika mstari huo huo, tusiwe watu wepesi wa kuchukulia na watumiaji Biblia wanaotusonga siku kwa siku kwa kudai wanajua Biblia. Imani yetu ni ya gharama, jamani. Hivi, tujitahidi sana tusimruhusu mtu yeyote aliyepitisha macho juu juu kwenye Biblia atupotoshe baada ya yeye mwenyewe kupotoshwa na Kiswahili kilichomletea maneno “uchawi” na “wachawi” bila tafakari.

Nitaeleza na ninaeleza sasa hivi. Ni hivi, tunachozugwa sisi na Biblia zetu za Kiswahili tukaelewa ni “uchawi” ulikuwa ni utaalamu au kazi. Utaalamu huo ulikuwa ukitumika kwa ngazi mbalimbali. Aidha, kadiri ya Biblia, utaalamu (au kazi hiyo) unajulikana kwa majina mengi vile vile. Katika ngazi ya juu wanasimama “mamajusi” na katika ngazi ya chini wanasimama wanaoitwa “wadanganyifu”. Msihangaike, tutawafahamu hivi punde.

Nimesema katika ngazi ya juu kabisa wanasimama “mamajusi’, yaani “wataalamu wa mambo ya nyota” au “watu wenye hekima”. Hawa ndio waliotajwa katika Mathayo 2 na katika Danieli 1 na 2. Katika kitabu cha Danieli wataalamu hawa huitwa vile vile Walkadayo, yaani watu kutoka Kaldea ambako enzi zile kuliaminika kuwako watu wenye akili sana.

Ndiyo kisa, Danieli alipoonekana kuwa mtaalamu sana aliwekwa kuwa mkuu wa wataalamu wa Babiloni (Kiswahili chetu kikinyoosha husema “mkuu wa wachawi” tu). Danieli alifanywa mkuu wa wataalamu (“wachawi” kwa Kiswahili chetu rahisi) kwa sababu “roho ya miungu watakatifu, mwanga na elimu na hekima, kama hekima ya miungu, vilionekana ndani yake”. Kwa ushuhuda soma vizuri Dan 5:11.29.

Basi, kama mmenielewa vizuri, sasa tunazungumzia utaalamu na siyo uchawi kwa dhana yetu ya Kiafrika. Nimeshadokeza. Katika ngazi ya chini ya utaalamu huo walikuwa “wadanganyifu” au “matapeli” waliokuwa wanacheza kwa viinimacho vyao kama wacheza mazingaombwe wanavyofanya leo hii kati yetu. Juu ya wadanganyifu hao Paulo anaandika, “Watu waovu na wadanganyifu wanaendelea kuwa wabaya, wakidanganya wengine, na wao wenyewe wakidanganywa” (2 Tim 3:13).

Katikati ya ngazi hizo mbili, yaani katikati ya mamajusi na wadanganyifu (matapeli) walikuwa watu waliobabaisha wenzao kwa pilikapilika za ulozi, kupiga ramli, kupandisha mapepo na waganga waliokuwa wakijitafutia nguvu za pekee kwa kutamka maneno, kutumia majani na mizizi na madawa mbalimbali. Basi, hivi ndivyo isemavyo Biblia.

Natumaini tupo bado pamoja. Hadi hapa nimeshazinyooshea kidole Biblia za Kiswahili kwa kutokutuletea tafsiri muafaka. Lakini tuwasamehe watafsiri wake. Labda mnaweza kuniliuza, limetokeaje jambo hilo? Nisikilizeni tena. Miaka ile ya 1937, kule Zanzibar, Wazungu waliposimamia zoezi la kutafsiri Biblia katika Kiswahili, hawakuketi na kujaribu kutuletea dhana halisi ya maneno “artam”, “artamim”, “oobh”, “baelath oobh”, “farmakeia”, “farmakos”, “mageia” na “magos”. Ndipo kwa kunyoosha mambo wao na wasaidizi wao wakawa wanapachika neno “uchawi” au “mchawi” popote pale pasipo simile.

Labda sijaeleweka. Nitawaelewesha kwa mifano. Mfano wa kwanza ni huu wa mtafsiri wa maandishi fulani ambaye atatumia neno “pombe” kutafsiri maneno kadha wa kadha: divai, bia, whisky, gongo, mbege, ulanzi, tembo, uraka, komoni, chibuku, kangara, wanzuki, gundi ya seremala, “ketamine”, dawa ya panya na chochote chenye nguvu ya kumlewesha mtu.

Ataweza kufanya hivyo lakini hatakuwa sahihi kwa maana divai ni tofauti na komoni, mbege ni tofauti na ulanzi, gongo ni tofauti na wanzuki, gundi ya seremala ni tofauti na whisky, “ketamine” ni tofauti na dawa ya panya na kadhalika. Hapo itabidi msomaji awe na akili ya kujiongeza. La sivyo, atasema vyote hivyo ni sawa tu kwa vile vimetafsiriwa vyote kwa neno moja “pombe”.

Natoa mfano mwingine. Ni kama mtu anavyopaswa kuwa na akili ya kujiongeza anaposoma misemo kama hii: “Baada ya kufanya vibaya katika Ligi Kuu, timu ya Majimaji inamtafuta mchawi”, “Kaka yangu alikuwa mchawi wa hesabu”, “Newton alikuwa mchawi wa sayansi”, “Pele alikuwa mchawi wa kabumbu”, “Maradona alikuwa mchawi wa chenga”, “Bibi Kalembwani alikuwa ananyoa wachawi Mahenge”, “akina Lambalamba wapo Dodoma kuwashika wachawi” na kadhalika. Ikiwa msomaji husika ataelewa misemo hiyo yote sawa, basi yeye atakuwa amefeli medani ya lugha.

Kwa hiyo, ni tafsiri kumbakumba ya Zanzibar iliyotuingiza katika kadhia ya kuwa na maneno “uchawi” na “mchawi” isivyojuzu kwenye Biblia ya Kiswahili. Maneno mengine yanayopaswa kuwekwa sawa kitaalamu kabisa na pengine kufutwa kabisa ni: YEHOVA, JINI na UZINZI. Siku moja nitawafafanulieni kwa jinsi gani maneno haya yanasikitisha kuonekana katika Biblia zetu za Kiswahili.

Kumbe, natamatisha somo langu, kwa kusisitiza kunena kwamba katika sehemu mbalimbali tunapoona Kiswahili kimetunyooshea tafsiri kwa maneno “uchawi” au “wachawi” ni tafsri ya maneno “kuona maono”, au “kucheza mazingaombwe” au “kuchanganya madawa” au “kutumia ujuzi kutafsiri mambo” na kadhalika.

Kwa mantiki hii, ndugu zanguni, tukirudi kwenye lugha asilia za Biblia, yaani Kiebrania na Kigiriki tutakuwa na fikra mbadala. La sivyo, tutaendelea kukaidiana juu ya dhana yetu ya uchawi, tukiamini Biblia ipo upande wetu.

Haya shime hatujachelewa kuingia kwenye mabadiliko haya ya fikra kwa njia ya lugha asilia za Biblia. Ndiyo, Kiswahili ndiyo hicho, lakini kuna sehemu na maneno ya Biblia fulani fulani ambapo lazima “tujiongeze”.
Leo nimekuhadithieni maneno “uchawi” na “mchawi”. Nimesema hayakustahili kuingizwa katika Biblia kama yalivyoingizwa. Yamekosewa. Matokeo yake, yanawapotosha na kuwatia ubishi watu wengi.

Hali kadhalika, nimedokeza kwamba kuna maneno mengine ya mkasa wa aina hiyo hiyo, hususan maneno YEHOVA na JINI. Ni mambo ya kuelimishana na wala tusione haya kuulizana tunapokwama kuielewa Biblia maana elimu haina mwisho na kusoma sana siyo mwisho wa ujinga.

Yule afisa Mwitheopia aliposhindwa kuelewa maneno ya Nabii Isaya aliyokuwa anayasoma, hakuona haya kujieleza kwa Filipo akisema, “Nitawezaje kuelewa bila mtu kuniongoza?” (Mdo 8:31). Filipo alijitolea kumwelewesha naye akaelewa. Natumaini njia ya afisa yule inaweza kuwa njia yetu pia. Tusione haya kuulizana mambo ya Biblia. Karibuni wote!

Credit: Padre Titus Amigu.
 
Padre Amigu kichwa kimejaa madini kiasi wengine wanamuona kama hafikiri sawasawa! Lakini ni mwalimu bingwa wa maandiko.

Mambo mengine waamini wachanga utawavuruga! Wanazuoni na wafasiri washindane wenyewe huko.

Ndiyo maana wenzetu Waislamu waliona maandiko yao yabakie kwenye lugha asilia ili kuwe na maana ile ile iliyokusudiwa.

Sent from my SM-A315F using JamiiForums mobile app
 
Hii ndio tofauti ya mtu aliyepitia majiundo ya Falsafa na Teolojia, huwezi kulinganisha na shee (sic), mitume na manabii wa mchongo. Fr. Amigo ni tunda la Kanisa kwelikweli.
Mtume Petro alikuwa hajasoma hajui kusoma wala kuandika lakini ndie alikuwa papa wa kwanza wa kanisa

Huyo father Amigu na falsafa yake na midigrii kibao ya falsafa na theolojia kaishia upadri tu
 
Padre Amigu kichwa kimejaa madini kiasi wengine wanamuona kama hafikiri sawasawa! Lakini ni mwalimu bingwa wa maandiko...
Lakini ilikuwa ni muhimu na mafaa zaidi kufasiri ili kurahisisha uinjilishaji.

Makosa machache kama haya hayakwepeki kwenye kazi ya binadamu.

Otherwise, tungekaririshana kama wale wenzetu, kitu ambacho siyo sahihi kwa mtazamo wangu.
 
Asante mwalimu wangu Kwa madini , ila duu ulikuwa unatubana kwenye Kona za maloweka
 
Lakini ilikuwa ni muhimu na mafaa zaidi kufasiri ili kurahisisha uinjilishaji.

Makosa machache kama haya hayakwepeki kwenye kazi ya binadamu.

Otherwise, tungekaririshana kama wale wenzetu, kitu ambacho siyo sahihi kwa mtazamo wangu.
Padre Amigu kichwa kimejaa madini kiasi wengine wanamuona kama hafikiri sawasawa! Lakini ni mwalimu bingwa wa maandiko...
Ipo mbona ishakuwa tayari muda inaitwa, BIBLIA YA KIAFRIKA kwa Kiswahili. Na huyu Amigu ni moja ya waandishi wakuu na muandaaji wa hiyo BIBLIA YA KIAFRIKA ameplay part kubwa sana huyo mzee mpaka kukamilika kwake.

Ni biblia moja nzuri sana imerekebisha makosa mengi ya tafrisiri za zamani na kuyafafanua vizuri. Matumiz ya Maneno kama uchawi, uzinzi, uasharati nk.
Weakman
 
Hii ndio tofauti ya mtu aliyepitia majiundo ya Falsafa na Teolojia, huwezi kulinganisha na shee (sic), mitume na manabii wa mchongo. Fr. Amigo ni tunda la Kanisa kwelikweli.
Mkatiliki mie. Namsikiliza sana Fr. Titus sawa ni mtauhidi mzuri kwa maana ya fani hiyo ndani ya Kanisa Katoliki. Anaelewa lugha mama ya Maandiko Matakatifu. Lakini asisahau kuwa hata Afrika au uswahilini zipo taaluma zote hizo kama za mamajusi, waongea na wafu, mazingaombwe, nk na kuna shule za kujifunza hayo kwa namna rasmi (formal) na isiyo rasmi (informal).

Kusema kwamba hayo mambo yanayoitwa uchawi kwenye Biblia ilikuwa taaluma lakini katika mazingira ya uswahili sio taaluma sio kweli.

Wachawi walikuwepo kwenye biblia na uchawi wao sio less evil ukilinganisha na uchawi kwa dhana ya Kiswahili. Wale wachawi wa Misri hawakubadili fimbo zao kuwa nyoka kwa kutumia ujuzi wa kisayansi ya binadamu, walitumia nguvu ya kipepo. Hayo hufanyika pia katika dhana ya uchawi ya Kiswahili.

Ambacho Pd. Amigu na wengine hukosea sana ni kutokuamini uwepo wa wachawi na uhalisia wao. Wengi wa hawa wanatheologia wasomi hufikiri ni ujinga kusema nimelogwa. Ulozi upo na hayo yote ni kazi za shetani katika madaraja mbalimbali.
 
Mkatiliki mie. Namsikiliza sana Fr. Titus sawa ni mtauhidi mzuri kwa maana ya fani hiyo ndani ya Kanisa Katoliki. Anaelewa lugha mama ya Maandiko Matakatifu. Lakini asisahau kuwa hata Afrika au uswahilini zipo taaluma zote hizo kama za mamajusi, waongea na wafu, mazingaombwe, nk na kuna shule za kujifunza hayo kwa namna rasmi (formal) na isiyo rasmi (informal).

Kusema kwamba hayo mambo yanayoitwa uchawi kwenye Biblia ilikuwa taaluma lakini katika mazingira ya uswahili sio taaluma sio kweli.

Wachawi walikuwepo kwenye biblia na uchawi wao sio less evil ukilinganisha na uchawi kwa dhana ya Kiswahili. Wale wachawi wa Misri hawakubadili fimbo zao kuwa nyoka kwa kutumia ujuzi wa kisayansi ya binadamu, walitumia nguvu ya kipepo. Hayo hufanyika pia katika dhana ya uchawi ya Kiswahili.

Ambacho Pd. Amigu na wengine hukosea sana ni kutokuamini uwepo wa wachawi na uhalisia wao. Wengi wa hawa wanatheologia wasomi hufikiri ni ujinga kusema nimelogwa. Ulozi upo na hayo yote ni kazi za shetani katika madaraja mbalimbali.
Rudia kumsoma.
 
Yuko sahihi,hayo ni maneno ya Wazungu kuchafua Mila zetu..

Tunahitaji dini zetu za Kiafrika sio hizo dini zao za Mashoga.
 
Ipo mbona ishakuwa tayari muda inaitwa, BIBLIA YA KIAFRIKA kwa Kiswahili. Na huyu Amigu ni moja ya waandishi wakuu na muandaaji wa hiyo BIBLIA YA KIAFRIKA ameplay part kubwa sana huyo mzee mpaka kukamilika kwake.

Ni biblia moja nzuri sana imerekebisha makosa mengi ya tafrisiri za zamani na kuyafafanua vizuri. Matumiz ya Maneno kama uchawi, uzinzi, uasharati nk.
Weakman
Katika Biblia yenye makosa mengi na makubwa ni hiyo Biblia ya Kiafrika waliyotafsiri hao akina Padri Amigu
Iko chini ya kiwango ambacho hata mjinga ambaye hajasoma falsafa au theolojia aweza ipinga waziwazi


Kuanzia msitari wa kwanza kabisa wa Biblilia ambao ni wa kitabu cha Mwanzo 1:1 yaani Genesis 1:1

Bibliia ya King James version na Biblia za zamani huo mstari unasomeka hivi "In the begining God created heavens and Earth"

Hiyo tafsiri ya African Bible ya Akina Padri Amigu na kundi lake inasomeka hivi "At first God made Heavens and Earth '
Sasa mimi mfuasi wa mitume na manabii nichambue upotofu wa akina Padri Amigu.kwenye hiyo Biblia yao ya African Bible kwenye huo mstari tu

Biblia za zamani zilitumia neno.God Created heavens and Earth akina Amigu wakatafsiri God made Heavens and Earth

Tofauti iko wapi mtu aweza ulizs.Tofauti
Creating means making something out of Nothing.Kuwa Mungu aliiumba dunia bila kutumia mali ghafi yeyote toka popote.alitamka tu iwepo mbingu ikawepo akatamka iwepo dunia ikawepo hakukuwa na utengeneza dunia na Mbingu kama vile Mungu aliingia kwenye karakana akakusanya materials na kuanza kuchonga mbingu na dunia ndio maana Biblia zilizotangulia zilitambua ukuu wa Mungu wa ku create vitu out of nothing

Twende hiyo Tafsiri ya hiyo Biblia ya African Bible waliyotafsiri Akina Amigu inasema God made heavens and Earth.Tunaelewa wote maana ya Made.Kitu ukiambiwa made ni kuwa kuna materials zimetumika kukitengeneza ndio kikawa hivyo kilivyo hakikuibuka tu yaani hakikuwa created

Sasa tuje kwa nini waliamua huo mstari kutumia God made badala ya God Created?

Hilo kundi lililotafsiri hiyo Biblia la Akina Amigu ni wana theolojia na falsafa wasioamini mambo ya miujiza kabisa
Ndio maana walipofikia kutafsiri palipoandikwa God Created wakasema haiwezekani akaitoa mbingu na dunia into existence bila kutumia materials kutengeneza hiyo dunia na mbingu futa hilo neno Created weka made!!!

Ndio maana Padre Amigu pia haamini kuwa uchawi upo!!! Ndio maana maneno yote ongelea uchawi wakayoondoa kwenye hiyo.African Bible yao waliyotafsiri

Nimetolea mfano wa huo mstari mmoja kifupi hiyo Biblia imejaa makosa mengi mno yasiyoendana na utendaji wa.Mungu ni ya watu wasioamini miujiza ya Mungu.wala uwezo wake au maajabu ya mashetani na malaika waliasi mbinguni na uchawi wao walioleta Duniani
 
Kuwa msomi wa Biblia hakumaanishi unaijua biblia au maandiko thus pana madhehebu mengi haya yametokana na viongozi wao au waanzilishi wao kutoyajua maandiko.
Padri Titus inamchanganya kutofautisha taaluma ya uchawi, usomaji nyota, uganga, waonaji, nk.
Unaposema nguvu za giza, uchawi ni kijinukta tu katika jumla ya nguvu zote za giza au uwezo usioonekana.

UCHAWI NI NINI
ni nguvu hasi iliyojificha yenye kudhuru mwili, mali, wanyama nk. Mchawi amebase kwenye kudhuru au kuharibu,
Uchawi ni mpana pana aina za uchawi,makundi na vyama vya kichawi.mfano black magic, red magic,white magic,nk.


MGANGA anafanya vyote kudhuru na kuponya kutegemea na matakwa ya mteja, mganga ni mfanyabiashara pesa YAKO ndio uamuru mganga afanye nini. Hata ukitaka kusomea uganga ni lazima usomee uchawi kwanza ukifuzu uchawi ndipo unaanza kozi ya pili ya uganga. Kipo Chuo unasoma uchawi miaka mitano then uganga miaka miwili so mda wa kozi yote ni miaka 7 unakuwa umefuzu.

MAGICIAN mazingaombwe huyu ni mchawi yeye utumia uchawi kufanya miujiza kwenye maonyeaho kwa malipo ya kiingilio, ufanya visivyoonekana kwa macho ya kawaida kwa msaada wa nguvu za mapepo au majini ambayo uwafunika macho watazamaji wasione mchakato mzima jinsi mazingaombwe yanayofanyika.

MAMA JUSI ,WASOMA NYOTA,WANAJIMU ,Wazee wa falaki hawa ni wataalamu wa elimu ya nyota Wana elimu ya kusoma mpangilio wa nyota, mwezi na jua KWA kuhusisha na maisha ya wanadamu.

WATABIRI WAONAJI hawa ni watu wenye uwezo wa kutambua mambo yaliyojificha yasiyoonwa kwa macho ya kawaida wenye kutambua mambo yatakayotea, nk hapa Wanahusika viumbe vya roho mfano majini, malaika, nk.
 
Mkatiliki mie. Namsikiliza sana Fr. Titus sawa ni mtauhidi mzuri kwa maana ya fani hiyo ndani ya Kanisa Katoliki. Anaelewa lugha mama ya Maandiko Matakatifu. Lakini asisahau kuwa hata Afrika au uswahilini zipo taaluma zote hizo kama za mamajusi, waongea na wafu, mazingaombwe, nk na kuna shule za kujifunza hayo kwa namna rasmi (formal) na isiyo rasmi (informal).

Kusema kwamba hayo mambo yanayoitwa uchawi kwenye Biblia ilikuwa taaluma lakini katika mazingira ya uswahili sio taaluma sio kweli.

Wachawi walikuwepo kwenye biblia na uchawi wao sio less evil ukilinganisha na uchawi kwa dhana ya Kiswahili. Wale wachawi wa Misri hawakubadili fimbo zao kuwa nyoka kwa kutumia ujuzi wa kisayansi ya binadamu, walitumia nguvu ya kipepo. Hayo hufanyika pia katika dhana ya uchawi ya Kiswahili.

Ambacho Pd. Amigu na wengine hukosea sana ni kutokuamini uwepo wa wachawi na uhalisia wao. Wengi wa hawa wanatheologia wasomi hufikiri ni ujinga kusema nimelogwa. Ulozi upo na hayo yote ni kazi za shetani katika madaraja mbalimbali.
Uko sahihi
 
Hoja ya padre ni ngumu kueleweka.
Kwake uchawi na mchawi anaelewa nini
 

Attachments

  • Screenshot_20230323_114941.jpg
    Screenshot_20230323_114941.jpg
    99.4 KB · Views: 16
  • Screenshot_20230323_115057.jpg
    Screenshot_20230323_115057.jpg
    105 KB · Views: 14
Padri jinga hili, usikute lenyewe ndio CHAWI HASWA.

Ukiona mtu anapinga uchawi ujue ndio CHAWI LENYEWE.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom