HII NDIO TAARIFA YA GAZETI LA KULIKONI TOLEO LA LEO KUHUSU UTAJIRI TATA WA ROSTAM AZIZ:
MJADALA kuhusu utajiri tata alionao mbunge wa Igunga, Rostam Aziz sasa umevuka mipaka kufuatia jarida la kimataifa liitwalo 'Africa Intelligence' kuhoji biashara lilizoziita kuwa ni za kizani zinazoendeshwa na mbunge huyo, huku likisema kuwa biashara za mwanasiasa huyo ambaye pia ni mfanyabiashara zinaacha maswali mengi kuliko majibu.
Katika toleo lake la hivi karibuni, jarida hilo ambalo pia linapatikana kwenye mtandao wa 'internet' linabainisha kuwa utata kuhusu biashara za Rostam unachagizwa na jina lake kutoonekana katika kampuni hata zile anazozimiliki.
"Mfanyabiashara Rostam Aziz, ambaye ni mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala ambaye pia aliwahi kudhaniwa na Bunge kuhusika katika tuhuma kadhaa za ufisadi, pia ni mwanzishaji wa kampuni mahiri," inasomeka sehemu ya makala kuhusu Rostam katika jarida hilo na kumwelezea kuwa ni "mfanyabiashara asiyeeleweka".
"Wakati anapoanzisha (Rostam) kampuni mpya mara nyingi hucheza na majina. Licha ya kuwa mmiliki wa kampuni kadhaa, ambazo baadhi yake zina anwani na/au namba za simu zinazofanana, jina lake hutokea katika kampuni moja tu iitwayo 'African Trade Development (T) Ltd (ATDL)."
Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo katika ofisi za Wakala wa Usajili wa Leseni za Makampuni (Brela) kuhusu kampuni hiyo, yeye ameorodheshwa kama mmoja wa wakurugenzi wa ATDL lakini kwa jina la Rostam Sakarri, linaelezea jarida la Africa Intelligence.
"Katika kampuni nyingine zote wakurugenzi wake pia wana majina yanayoshabihiana na jina la Rostam kwa namna moja au nyingine ambayo ni kama; Rostom A. Sakarr, Rustom Aziz Sakarr, Rustam Sakarri and Rustam Sakaari," inafafanua makala hiyo.
Jarida hilo limeendelea kubainisha kwamba katika orodha ya wanahisa wa kampuni nyingine Rostam huonekana kujificha katika kivuli cha majina yenye asili ya Iran kama vile Chakaar na Mehrab.
Jina la Rostam Aziz halijitokezi kabisa katika nyaraka za Brela hata walau kwa nusu ya kampuni ambazo zinapaswa kuwa chini ya umiliki wake kama vile Africa Tanneries Limited, Tanzania Leather Industries Limited, Wembere Hunting Safari Limited, Tanzania Packages Manufacturer Limited na hata ile inayofahamika sana inamilikiwa na yeye ya Caspian Construction Limited.
"Rostam Aziz alitangaza hadharani kwamba ameinunua kampuni ya Habari Corporation ambayo inachapisha magazeti kadhaa na inayoendesha chuo cha mafunzo ya uandishi wa habari cha MAMET," lilisema Africa Intelligence, na kuongeza ; "Hata hivyo jina lake halionekani katika orodha ya wanahisa wa kampuni ya Isenegeja ambayo kimsingi ndiyo ilinunua kampuni hiyo ambayo baadaye ilibatizwa jina la New Habari (2006) Limited kwa ajili ya kuendelea na uchapishaji wa magazeti ambayo anaimiliki hadi sasa. Mambo ya kustaajabisha kweli!"
Jarida hilo linalochapishwa Paris nchini Ufaransa linasema mbunge huyo ambaye alikuwa mtunza hazina wa CCM Taifa "Sasa anawachanganya vichwa vigogo wa Chama cha Mapinduzi".
"Baadhi ya vigogo serikalini wanahisi kwamba Rostam alikuwa na mpango wa kuuza hisa zake katika kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ili kupata fedha zitakazotumika katika mapambano ya uchaguzi mkuu wa 2010," linasema jarida hilo.
Utafiti uliofanywa na KULIKONI siku chache zilizopita, tuhuma zinazomwandama mfanyabiashara huyo hivi sasa zinaonekana kuharibu sifa ya chama tawala hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Mbali na kuwa mbunge wa jimbo la Igunga mkoani Tabora, Rostam pia ni mjumbe katika Kamati Kuu ya CCM.
Hivi sasa ni dhahiri kwamba umaarufu wa mwanasiasa huyo umekuwa ukipungua mbele ya vigogo wa chama chake cha CCM ambao kimsingi wanaamini kuwa atakuwa mzigo katika chama hicho.
Baadhi ya makada waandamizi ndani ya CCM wanabainisha kuwa wakati vigogo watatu wa kisiasa waliangushwa kufuatia kutajwa kuhusika katika kashfa ya ununuzi wa mitambo tata ya Richmond, Rostam pia alipaswa kuchukuliwa hatua kwani naye ni mmoja wa wahusika wakuu wa kashfa hiyo.
Taarifa ya Richmond ilisababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri wengine wawili ambao ni Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.
Hata hivyo pamoja na kwamba alitajwa katika taarifa hiyo, Rostam bado anaendelea kushikilia nafasi nyeti katika chama chake licha ya maazimio yaliyopitishwa na Bunge kwamba wahusika wote waliotajwa waondolewe katika nafasi zao za chama na serikalini.