Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, ambacho jina lake linahifadhiwa, bifu la wawili hao limefikia mahala ambapo watu hao hawasalimiani wala kutazamana usoni.
Habari zinasema kuwa waheshimiwa hao mwishoni mwa wiki iliyopita, walipanda ndege moja wakitokea Mwanza hadi Dar es Salaam huku wakiwa wamenuniana.
Tangu walipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, kila mmoja alionekana kumkwepa mwenzake, alisema mtoa habari huyo ambaye alisafiri ndege moja na waheshimiwa hao.
Chanzo hicho kiliendelea kudai kuwa wakiwa ndani ya ndege hiyo kila mmoja alionekana bize na simu yake ya kiganjani, jambo lililozua maswali kwa watu waliowafahamu wabunge hao ndani ya ndege hiyo.
Mara baada ya kupata taarifa hiyo, mwandishi wetu alimpigia simu Shibuda, alipomuuliza kuhusu madai ya kutozungumza na mbunge mwenzake, kabla ya kutoa jibu alicheka.
Baada ya muda, alisema kuwa Chenge ni ndugu yake na alimfahamisha mwandishi wetu kuwa, akiona ndugu wanagombana, yeye achukue jembe akalime.
Unasikia bwana mwandishi, ndugu wanapogombana, wewe chukua jembe ukalime, alisema Mheshimiwa Shibuda.
Alipoulizwa sababu hasa ya yeye na mbunge mwenzake kununiana, wakati wanatoka katika mkoa mmoja wa Shinyanga, Shibuda alisema kuwa hajui na kwamba hadi sasa anafanya utafiti ili kujua sababu.
Hadi sasa nafanya utafiti, nikipata jibu la utafiti wangu nitazungumza, kwani yeye Chenge kasemaje? Aliuliza Shibuda huku akicheka.
Naye Chenge ambaye siku za hivi karibuni alipachikwa jina la Mzee wa Vijisenti, alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Simu hiyo, ilipigwa mara kwa mara na hadi tukwenda mitamboni ilikuwa haina majibu.
Kama ilivyokuwa kauli ya Shibuda kuwa anafanya utafiti, nasi tunafanya uchunguzi ili kujua sababu hasa ya waheshimiwa hao kununiana, tukibaini ukweli tutaweka mambo hadharani - Mhariri.