SIMULIZI: THE LOST BOYS (25)
MTUNZI: FRANK MASAI
MAWASILIANO: 0752353039
****ILIPOISHIA*****
Hali hiyo haikumfanya Hans kujichukulia paja na kuanza kulitafuna kwa uchu. Hapo hapo na Junior aliinuka toka kwenye kitanda chake cha chini na kwenda kujichukulia kilichopo kwenye sinia lile la Hans.
“Nimekitolea jasho hiki.Kupambana na wale wahudumu hadi kukipata wadhani jambo dogo lile.”Junior aliongea huku akishika mgongo wa kuku na kuanza ku-usosomola.
“Fred vipi kaka,mboa hivyo?.”Suarez alimuuliza Fred baada ya kumuona hana la kuongea bali kushikwa na kigugumizi.
“Chakula chetu,mimi na Eve.”Fred aliongea huku machozi kama yanataka kumtoka.
“Sasa nyie mliacha chakula chote hiki,nyie vipi?Na bahati yenu vinywaji hamkununua.”Hans hakuwa nyuma kuongea japo alikuwa anabugia tambi kwenye kinywa chake.
Fred hakuvumilia hali ile. Yaani kuaibika, ka-aibika, chakula kimelipiwa bila kuliwa. Halafu mbaya zaidi wanao-kila ndio hao waliomuaibisha. Haikuwezekana kukubalika kwenye kichwa cha Fred.
SASA ENDELEA...
Hali hiyo ya kutovumilia,ilimfanya Fred akwapue lile sinia kwenye vidole vilivyokuwa vinaendela kufakamia ule msosi wa ghari,aliougharamia mpenzi wake kwaajili yake.
“Pumbavu zenu,sasa ole wake boya asogee.”Fred aliongea huku anaelekea pembeni na sinia lile la chakula kwa lengo la kukila peke yake.
“Mwanangu na sisi tumeweka chakula chetu humo,kwani chenu kilikuwa kingi hivyo.”Junior aliongea huku akimfata Fred kule ukutani alipoenda.
“Nitakumwagia hizi tambi,kuku na haya makachumbali usoni na hutonifanya kitu,nisogelee sasa.”Baba Paroko aligeuka gaidi kwelikweli.
Junior ilibidi harudi nyuma hasa alipofikiria muwasho wa ile kachumbali mdomoni,sasa anaambiwa atamwagiwa usoni.
Fred akawa m-babe mule ndani. Akachukua paja moja la kuku na kumrushia Suarez,naye Suarez akalidaka na kulitia mdomoni kwake.
Fred akageukia ukutani na wakati huohuo akawapa wakina Hans mgongo na kuwafanya waone ile suruali ilivyokuwa imeharibika.Kicheko kikaanza kwa kasi ya ajabu lakini Fred hakujali zaidi ya kuendelea kula huku akicheza taratibu na kukata kiuno kwa mbali. Hasira zikamuisha kihivyo maana angeendelea kuwa na hasira hizo,ingekuwa hasara kwake. Cha msingi aliona bora asahau,lakini si kwamba alisahau kabisa.
*****
Kesho yake waliamka wenye furaha kama jana yake usiku kulikuwa hakujatokea kitu. Walikuwa ni watu wenye amani kupitiliza huku ikionekana wazi hakuna kisasi baina yao.
Lakini ajuaye moyo wa mwanadamu una nini,ni yeye mwenyewe binadamu pamoja na MUNGU wake.
Moyo wa Fred ulikuwa haujafurahia kabisa kile kitendo alichofanyiwa na Hans. Pia alikuwa kampatia sana hasira Junior kwa kuwa mshirika wa Hans. Hayo yote aliyaweka moyoni na kuyapangia mkakati kabambe wa kuyalipa.
Bila wale jamaa zake kujua yaliyo-moyoni mwake.Fred alionesha mwenye amani na furaha kila wakati huku akiwa mstari wa mbele kukumbushia kilichomtokea jana.
****
Siku nne mbele toka siku ya tukio la Fred,ilikuwa ni zamu ya Junior kukutana na Eve. Fred alifahamu hilo,hivyo akaanza kutafuta njia za kulipa kisasi kwa alichofanyiwa na wale rafiki zake.
Aliangaika sana na mwisho wake aliona ni bora aende kwa wagumu kuomba msaada kwani Junior alionekana ni mtu makini sana kwenye mambo yake.
Haikuwa rahisi kwa Junior kuacha nguo zake hovyo,wala kabati lake. Kifupi alizidisha umakini hasa kila alipofikiria tukio lililomtokea Fred. Sasa Alfred aliamua kuomba msaada kwa Wagumu,walewale aliowahi kuwaabisha walipofika chuoni kwa mara ya kwanza. Ndio walewale wakina Moi Shabala,Kamanda wao Ban Diho na Sunday Magembe.
“Kwa hiyo mkuu unatakaje sasa.”Kamanda wa Wagumu,Ban Diho alimuuliza Fred baada ya Fred kutoa mkasa mzima ulimkuta.
“Nataka boya naye aibike mbele ya mtoto kama mimi nilivyoaibika.”Fred aliongea kwa hamasa juu ya nia yake
“Basi usijali. Cha msingi taarifa umetupa,sisi tutapiga kazi kama kawaida ila yapasa uache kitu hapa,hatupigi kazi bila mshiko,si wajua sisi makamanda.”Ban aliongea kwa makini huku akimwangalia usoni Fred aliyewafuata chumbani kwao.
“Hilo usijali,nyie niambieni kiasi mnachotaka.”Fred alizidi kujiingiza kwenye dhamira yake ya kisasi.
Kwa kuwa wale jamaa walikuwa na kisasi na lile kundi la akina Hans,waliamua kuutumia mwanya huo kulipa walichowahi kufanyiwa.
“Hapo utaacha elfu hamsini mwanangu.”Ban alimjibu Fred na kumuacha kinywa wazi.
“Kaka mbona kitu kidogo sana lakini umekaza hivyo. Au unaenda kuua? Sitaki mauaji,nataka aibike tu!.”Fred alishindwa kuzuia hisia zake juu ya ile bei aliyotajiwa na Ban.
“Hafi mtu hapa jembe langu. Tunataka kukufanyia kazi ya uhakika. We mwenyewe si wacheki makamanda tupo wangapi? Huyo dogo ataaibika mpaka mwenyewe utakuja na kutuongeza elfu hamsini nyingine. Ila kwa sasa,sisi tunataka hiyo fifte halafu kazi nzima tutaifanya wenyewe hadi iishe.”Ban alizidi kumvuta Fred ili amuingize kitanzini kwa ile hela aliyomtajia kama gharama.
“Fanyeni elfu thelathini basi,hiyo hamsini mimi sina.”Fred alibembeleza jambo kana kwamba anachotaka kufanya ni sheria iliyoruhusiwa na tume yakutunga sheria hapa nchini.
“Kama utataka kwa bei hiyo,itabidi na wewe uwemo kwenye mchakato huo. Sisi tutakutafutia kila kitendea kazi,halafu utakamilisha kazi hiyo we mwenyewe.Unasemaje.”Ban alikuwa mkavu na mwenye msisitizo wakati anaongea hayo.
“Mazee,mimi yamenishinda na ndio maana nimekuj kwenu. Nisaidieni bwana.”Fred alizidi kubembeleza huku shingo yake kaiweka upande kuwasilisha bembelezo lile.
“Sikiliza kamanda Fred,sisi tutakupigia kazi ya maana ambayo hutatambulika kama ni wewe bali yule Hans. Na kama Junior atamshuku yule,ni lazima atataka kulipa kisasi. Sasa wewe ndiye utatuletea mteja huyo. Na yeye tutampa bei kama yako,na kama yawezekana tutaipandisha juu iwe kama elfu sabini au laki moja. Wewe ndio utakuwa unamsukuma ili alipe kiasi hicho,tena ikibidi mkopeshe kiasi kilichozidi.
Akitulipa,sisi tunakata elfu hamsini yetu,kile kilichozidi tunakupa wewe kama shukrani ya kutuletea mteja. Hapo vipi kamanda.”Safari hii aliongea Moi Shabala kibiashara zaidi.
“Hapo haina noma. Basi nipeni nusu saa kwanza nikafanye mambo benki.”Fred aliomba ruhusa na kutoka chumbani kwa akina Ban akiwa ameridhika na maamuzi yake juu ya kulipa kisasi kwa Junior.
*****
Alienda benki na kufanya muhamala wa fedha kwa kiasi cha shilingi elfu sabini. Elfu ishirini aliweka pembeni na elfu hamsini akaiweka mahala kwingine. Hapo tayari akawa amekamilisha kazi iliyompeleka benki na akawa tayari kwa ajili ya kuingia vitani,vita ya kijinga kabisa kuwahi kutokea katika maisha ya mwanadamu wa leo.
Baada ya dakika zisizopungua arobaini,Fred alikuwa chumbai kwa akina Ban akifanya makabidhiano ya fedha zile alizoenda kuzichomoa benki.
“Mzigo ndio huo hapa wazee. Nataka kazi ifanyike bila mimi kujulikana, na pia nataka siku ya tukio na mimi mnitaarifu ili niwepo eneo hilo nione kitakachotokea.”Fred alikuwa anatoa kiasi cha fedha huku anaongea hayo.
“Hamna shaka hata kidogo. Deal done.”Ban alikamilisha maongezi huku akikabidhi noti tano nyekundu,fedha halali kwa malipo nchini Tanzania kwa Sunday Magembe aliyekuwa katoa tabasamu la pongezi kwa kamanda wao,Ban.
“Basi fresh. Mambo yote ni kesho. Dogo ndio anaenda kukutana manzi. Fanyeni yenu kama kawa.”Fred aliweka hitimisho juu ya maongezi yale na kutoka nje chumba kile akiwa na uhakika wa kazi yake kufanyika bila zengwe wala kokoro.
Ama hakika alipania kufanya kisasi,kitendo cha kutoa kiasi kile cha fedha kwa ajili ya kumuaibisha mwenzako,ni kitendo cha kijasiri sana kupata kutokea kwenye dunia ya sasa,dunia iliyojaa vituko kila kona ya pembe zake. Yote yanabaki kuwa siri yake,hakuna aliyepaswa kujua kama analipa kisasi zaidi ya wale aliyowapa kazi ile.
*****
Huku nyuma baada ya Fred kuondoka,Ban alipanga jeshi lake kwa ajili yakutimiza kazi waliyokuwa wamekabidhiwa na Fred,kazi ya kuhakikisha Junior anaaibika mbele ya umati wa watu.
“Umeona maboya hayo? Sasa ni muda wa wao kuaibika,walidhani tumesahau ya siku zile? Sasa hapa ni kuwafanya waaibike bila sisi kugundulika. Yaani tunacheza chezo huku tunawapakazia wao. Tunakula hela,na bado tunawaabisha. Huo ndio mpango.”Aliongea kamanda mkuu wa chumba kile,Ban Diho.
“Hapo kamanda umecheza kama Pele. Naikumbuka sana ile siku tuliyotembea uchi. Mi kidogo nihame na chuo,ila nikajikaza kiume tu.”Moi Shabala naye aliongezea chachandu juu ya maongezi yale.
“Na hapo lazima ziwamwagike haswaa,si walijidai manunda. Sasa wamekutana na manunda square.”Ban aliongea kwa chuki iliyokuwa wazi kabisa.
“Ndio maana yake. Watajua wenyewe wakipigana,wakikatana mapanga,wakitishiana bastola na hata wakichinjana. Cha msingi sisi tupange jinsi ya kumwaibisha huyo dogo ili akome.”Mdomo wa Sunday nao haukuwa nyuma kudhibitisha kuwa yupo ndani ya wenzake na hawezi kuwatosa.
“Hapa watasanda tu!.Sisi ndio maji,ukishindwa kwa kutunawa,utatugida tu.”Ban alimaliza tambo zilizokuwa zinaendelea chumbani mule na sasa alikuwa kajiweka wima kwa jili ya kuanza kazi ya kuupanga mkakati uliokuwa umewatinga mbele yao.