TET: 60% Watoto wenye changamoto ya kufaulu darasani wana tatizo la uoni hafifu

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,808
11,973
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imetoa ripoti baada ya kupokea maoni ya wadau kupitia mikutano mikubwa mitatu iliyofanyika Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar kuhusu Mapitio Makubwa ya 6 ya Mitaala ya Elimu ya Tanzania

TET imesema imekusanya maoni kupitia vikao vilivyofanywa na makundi mbalimbali yakiwemo Baraza la Watoto Tanzania, viongozi wa dini, umoja wa wakuu wa shule za Msingi na umoja wa wakuu wa shule za sekondari. Pia, maoni mengine yalipokelewa kwa kutumia namba ya simu, barua pepe, sanduku la barua, kiunganishi kwenye tovuti ya TET, dodoso na hojaji.

IMG-20220809-WA0007.jpg


Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth A. Komba ameyasema hayo leo 09 Agosti 2022 Mkoani Dar Es Salaam wakati alipokuwa anatoa Taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Taasisi ya elimu Tanzania (TET) na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa Waandishi wa Habari.

Amesema Kamati ya Kitaifa ya Mitaala iliyoteuliwa na waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mh. Prof Adolf Mkenda (MB.), inaendelea kukutana na makundi mbalimbali ya wadau.

“Siku za hivi karibuni tunatarajia kukutana na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Kwa kupitia mkutano huu ninawaomba wadau na wananchi kwa ujumla waendelee kutoa maoni yao kupitia barua pepe maoniyawadau@tie.go.tz na namba ya simu 0735 041169,” anasema Dkt. Komba

TET: 60% Watoto wenye changamoto darasani wana tatizo la uoni hafifu

Imebainika kuwa 60% ya Watoto wenye changamoto ya kujifunza wana matatizo ya kutoona vizuri, hali inayosababisha wengi wao kuhitimu elimu yao ya Msingi wakiwa hawana uelewa mzuri wa kusoma na kuandika.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth A. Komba amesema utafiti huo uliokamilika mwaka 2020 uliopewa jina la ‘Kuona Ni Kujifunza’ umewafanya waandae Moduli za kuwawezesha Walimu wote kubaini watoto wenye changamoto hiyo na kuwapa mstaada stahiki wakati wa ufundishaji.

“Utafiti huo ulifanyika Arusha na Kilimanjaro, tumebaini Walimu wengi hawana ufahamu na mbinu za kuwaendeleza Wanafunzi wenye changamoto hiyo,” – Dkt. Komba.

==================

TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA TAASISI YA ELIMU TANZANIA (TET) NA MWELEKEO WA UTEKELEZAJI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023 ILIYOTOLEWA NA MKURUGENZI MKUU DKT. ANETH A. KOMBA KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
TAREHE: 9 AGOSTI 2022

 Mkurugenzi Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali -
Idara ya Habari- Maelezo;
 Waandishi wa habari;
 Mabibi na Mabwana;
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania...

Ndugu Wanahabari; wali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia kukutana siku ya leo tukiwa wazima wa afya njema. Pili, napenda kuwakaribisha wote katika mkutano huu muhimu na wanahabari wenye lengo la kuhabarisha Umma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za TET na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023. Tatu, ninawashukuru sana wanahabari wote mlioitikia wito wetu, TET inatambua kuwa ninyi ni daraja muhimu baina yetu, wadau wa elimu pamoja na wananchi kwa ujumla. Nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza sana kwa kazi nzuri mnayofanya katika kuhabarisha umma wa Tanzania.

Ndugu Wanahabari;
Taasisi ya Elimu Tanzania ni Taasisi ya umma iliyo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 13 ya Mwaka 1975 (Sura ya
142 Marejeo ya 2002). Kwa mujibu wa sheria hiyo, majukumu ya taasisi yamejumuishwa katika makundi manne yafuatayo:
(i) Kubuni, kuandaa na kuboresha mitaala ya Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu (Astashahada na Stashahada).
(ii) Kuandaa vifaa saidizi vya kutekeleza mitaala kama vile vitabu vya kiada, viongozi vya mwalimu, miongozo mbalimbali ya kufundishia na moduli. Kazi hii pia inahusisha kusimamia taratibu za uidhinishwaji wa vitabu vya ziada.
(iii) Kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wasimamizi wa utekelezaji wa mitaala (wathibiti ubora, maafisa elimu wa mikoa, wilaya na kata) ili kuwawezesha kutekeleza mitaala kadiri ya matarajio.
(iv) Kufanya utafiti na kutoa ushauri elekezi kwa serikali na wadau wengine wa elimu juu ya mitaala na maswala mengine yanayohusiana na ubora wa elimu.

Ndugu Wanahabari;
Kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 TET, iliendelea kufanya mapitio makubwa ya Mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu. Kazi hii inafanyika ikiwa ni kutekeleza moja ya majukumu ya msingi ya TET ambapo maboresho ya mitaala hufanyika kila baada ya mzunguko mmoja wa ngazi fulani ya elimu kukamilika au panapokuwa na mahitaji ya jamii, mabadiliko ya sayansi, teknolojia, siasa na uchumi. Vilevile, mabadiliko haya, ni maelekezo ya Rais wa Awamu ya Sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza mara nyingi katika hotuba zake haja ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuboresha mitaala inayotumika ili iweze kuendana na mahitaji ya aina ya wahitimu wanaohitajika katika karne hii.

Katika maagizo yake, Mheshimiwa Rais amesisitiza kuwa Mitaala yetu lazima iwajengee wahitimu ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na kutumia vema fursa zinazopatikana nchini; hususani kwa kujiajiri, kuajiriwa au kumudu maisha yao ya kila siku pale wanapohitimu mafunzo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono haya. Hivyo, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia TET, sasa inafanya mapitio makubwa ya sita ya mitaala tangu Tanzania ipate uhuru.

Ndugu Wanahabari;
Katika kutekeleza jukumu hili serikali ilitoa jumla ya shilingi 1,427,030,000. Fedha hii imetumika kukusanya maoni ya wadau, kuchakata data na kuandaa rasimu za mitaala ya ngazi zinazopendekezwa. Katika kukusanya maoni, jumla ya wadau 103,210 wamefikiwa. Awali, TET ilipokea maoni ya wadau kupitia mikutano mikubwa mitatu iliyofanyika Dar es Salaam, Dodoma na
Zanzibar. Aidha, TET ilikusanya maoni kupitia vikao vilivyofanywa na makundi mbalimbali yakiwemo Baraza la Watoto Tanzania, viongozi wa dini, umoja wa wakuu wa shule za Msingi na umoja wa wakuu wa shule za sekondari. Pia, maoni mengine yalipokelewa kwa kutumia namba ya simu, barua pepe, sanduku la barua, kiunganishi kwenye tovuti ya TET, dodoso na hojaji.

Kwa ujumla wadau waliofikiwa ni pamoja na viongozi wa serikali, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wahitimu wa vyuo vikuu, walimu, wazazi, wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu, mashirika yasiyo ya kiserikali, walimu wakuu wa shule za msingi, walimu wakuu wa shule za sekondari, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, maafisa elimu wa mikoa na wilaya, wahadhiri na wakufunzi, waajiri, wamiliki wa shule zisizo za serikali, wajumbe wa bodi za shule na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Maoni yaliyokusanywa yamechakatwa na taarifa ya maoni ya wadau imeandikwa. Taarifa hii ndio iliyotumika kuandaa rasimu za mitaala iliyopendekezwa. Rasimu hizi pia zinahusisha rasimu za mitaala rekebifu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika fani za ulemavu wa akili, kutoona, uziwi, uziwikutoona na usonji.

Hatua inayofuata kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 ni kuwashirikisha wadau kuhusu rasimu za mitaala zilizopendekezwa na kuendelea na hatua ya kuandaa vifaa vingine vya utekelezaji wa mitaala ikiwemo mihtasari pamoja na kutoa mafunzo ya walimu na wasimamizi wengine wa utekelezaji wa mitaala.
Kwa Mwaka wa Fedha 2022/23, serikali imetenga jumla ya shilingi 1,769,340,000.00 kwa kazi hii inayotarajiwa kukamilika Disemba, 2022.

Ninaomba nisisitize kuwa katika kufanya kazi ya mapitio ya mitaala zoezi la kukusanya maoni kutoka kwa wadau ni endelevu. Taasisi ikishirikiana na Kamati ya Kitaifa ya Mitaala iliyoteuliwa na waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mh. Prof Adolf Mkenda (MB.), inaendelea kukutana na makundi mbalimbali ya wadau na katika siku za hivi karibuni tunataraji kukutana na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kwa kupitia mkutano huu ninawaomba wadau na wananchi kwa ujumla waendelee kutoa maoni yao kupitia barua pepe maoniyawadau@tie.go.tz na namba ya simu 0735 041169.

Ndugu Wanahabari;
Kuhusu kazi ya kuandika vitabu, viongozi vya mwalimu na vifaa vingine vya kutekeleza mitaala, mpaka sasa TET imekamilisha kazi ya kuandika, kuchapa na kusambaza vitabu vya kiada na kiongozi cha mwalimu kwa masomo yote kwa Ngazi ya Awali na Msingi kwa shule zinazotumia Kingereza na Kiswahili kama lugha za kufundishia pamoja na vitabu vya hadithi. Jumla ya nakala 28,469,667 za vitabu vya kiada na hadithi zimekwisha sambazwa kwa uwiano wa 1:2, yaani kitabu kimoja wanafunzi wawili.

Na katika kila Mwaka wa Fedha serikali imeweka mpango endelevu wa kufanya uchapaji wa kujazia kwa vitabu vilivyochakaa au kupotea.

Kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu TET imechapa na kusambaza jumla ya nakala 180,852 ya vitabu vya Breli kwa ajili ya wanafunzi wasioona Darasa la I-VII. Vitabu hivi vimegawanywa kwa uwiano wa vitabu vitatu mwanafunzi mmoja. Vilevile, TET imechapa na kusambaza jumla ya nakala 155,562 ya vitabu vya maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu kuanzia Darasa la I-VII. Vitabu hivi vimegawiwa kwa uwiano wa 1:1, yaani kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.

Vitabu vyote vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu vimechapwa katika viwanda vya TET vya Press A na B. Naomba nichukue fursa hii kuishukuru na kuipongeza serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia hitaji hili na kuhakikisha kuwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapata haki yao ya msingi ya kupata elimu wakiwa na vitabu vya kiada kama ilivyo kwa wanafunzi wasio na mahitaji maalumu.

Ndugu Wanahabari;
Uwekezaji wa serikali katika kazi ya uandishi, uchapaji na usambazaji wa vitabu vya kiada kwa Ngazi ya Elimu ya Awali na Msingi pamoja na vya hadithi kwa wanafunzi wasio na mahitaji maalumu kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 ni jumla ya shilingi 42,370,613,340.00. Kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 serikali ilitoa jumla ya shilingi 2,189,683,466.00 Kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 TET inaendelea kufanya uchapaji wa vitabu kwa shule zenye upungufu kwa Ngazi ya Elimu ya Awali na Msingi Darasa la I-VII kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wale wasio na mahitaji maalumu. Upungufu wa vitabu
husababishwa na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi, kupotea au kuchakaa kwa vitabu, kwa kuwa katika hali ya kawaida uhai wa vitabu shuleni ni miaka minne.

Ndugu Wanahabari;
Kwa upande wa Sekondari, TET imeandika, kuchapa na kusambaza vitabu vya masomo mbalimbali ikiwemo masomo ya: Physics, Chemistry, Kiswahili, English, French, Geography, History, Biology, Mathematics, Agriculture, Home Economics, Music na Fine Arts kwa Kidato cha 1-6. Jumla ya nakala 7,641,534 zimekwisha chapwa na kusambazwa. Katika eneo hili serikali imewekeza jumla ya shilingi 43,799,090,664.00 ambazo zimewezesha kuandika, kuchapa na kusambaza vitabu kwa uwiano wa 1:3 (kitabu kimoja wanafunzi watatu).

Vilevile, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 TET iliweza kubadilisha vitabu vya Elimu ya Sekondari kuwa katika maandishi ya Breli na yaliyokuzwa kwa ajili ya wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu. TET, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilipokea shilingi 707,000,000.00 ambazo ni sehemu ya fedha za mradi wa mapambano ya athari za UVIKO-19 zilizotumika kuchapa Vitabu vya Kiada vya Breli 9,100 vyenye jumla ya juzuu 32,140 na Vitabu vya Michoro Mguso vyenye jumla ya juzuu 20,400 kwa ajili ya wanafunzi wasioona na vitabu vya kiada vya

Maandishi yaliyokuzwa 60,283 kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu Kidato cha 1-4. Vitabu hivi vimekwisha kusambazwa kwa uwiano wa 3:1 yaani vitabu vitatu kwa kila mwanafunzi kwa wanafunzi wasioona na uwiano wa 1:1 yaani kitabu kimoja kwa mwanafunzi kwa wanafunzi wenye uoni hafifu.

Kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 TET, inaendelea kukamilisha kazi ya usambazaji wa vitabu vya masomo mbalimbali Ngazi ya Sekondari na kukamilisha uandishi wa vitabu vya masomo yote ya Ufundi Kidato cha I-IV na vya masomo ya Additional Mathematics, Theatre Arts, Music, Computer Science, Commerce, Food and Human Nutrition, Textile and Garment Construction, Arabic, General Studies na Book Keeping Kidato cha 1-VI pamoja na kuvibadilisha vitabu hivi kuwa katika maandishi ya Breli na yaliyokuzwa.

Katika kazi hii serikali imetenga jumla ya shilingi 4,238,569,340.00 kuwezesha uandishi na uchapaji wa vitabu vya kiada vya masomo haya kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu Kidato cha 1-4.

Ndugu Wanahabari; amoja na kuandaa nakala ngumu za vitabu, TET inatambua na kuzingatia umuhimu wa matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.

Hivyo, vitabu vyote vimewekwa katika Maktaba Mtandao inayopatikana katika tovuti ya www.tie.go.tz. Kuingia katika tovuti hii kwa mtumiaji mwenye barua pepe ya gmail, ataitumia barua pepe yake kuingia na kuweza kutumia machapisho yote yanayopatikana katika maktaba. Kwa mtumiaji asiyekuwa na barua pepe ya gmail atapaswa kujisajili bure kwa kutumia barua pepe anayotumia. Maktaba hii ina machapisho yote ya kiada na imepakiwa pia machapisho mbalimbali ya ziada yanayoweza kupatikana kwa wanafunzi wanaoona na wasioona.

Kwa wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu Maktaba Mtandao imefanywa kuwa rafiki kwao kuwawezesha kusoma sawa na wasiokuwa na changamoto ya uoni kwa kutumia vifaa saidizi.

Maktaba Mtandao inapatikana bure. TET kwa kushirikiana na UNICEF- Tanzania, imeingia makubaliano na kampuni ya simu ya Airtel yanayoruhusu watumiaji wa Maktaba Mtandao kutumia bure maktaba bila kuwa na kifurushi cha internet.

TET inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni mengine ya simu. Ninaomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Airtel na kuwaomba makampuni mengine ya simu kusaidia katika eneo hili. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwa sasa, Maktaba Mtandao inatembelewa na wastani wa wasomaji 400-500 kwa siku.

Ninawashukuru sana watumiaji wa maktaba hii na ninawaalika wanafunzi na walimu kutumia maktaba mtandao hii katika ufundishaji na ujifunzaji.

Ndugu Wanahabari; wa upande wa mafunzo ya walimu kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 serikali ilitoa shilingi 1,243,400,000 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa walimu, wathibiti ubora wa shule ambao jukumu lao kubwa ni kufuatilia utekelezaji wa mitaala na wasimamizi wengine wa utekelezaji wa mitaala. Kwa kutumia fedha hizi, TET iliweza kutoa mafunzo kazini kwa jumla ya walimu 4,627 wa Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari.

Mchanganuo wa walimu hawa ni: Walimu 200 wa Elimu ya Awali, 2,770 wa Elimu ya Msingi, 927 wa masomo ya Kilimo, Ufundi, Biashara na Sayansi Kimu na 730 wa masomo ya Sayansi na Hisabati Ngazi ya Sekondari Kidato cha 1-4. Walimu hawa wamepatiwa mafunzo ya utekelezaji wa mtaala unaozingatia ujenzi wa umahiri.

Aidha, jumla ya wasimamizi 1200 wa utekelezaji wa mitaala walipatiwa mafunzo wakiwemo wathibiti ubora wa shule, Maafisa Elimu Wilaya na Kata.

Kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 TET, inatarajia kuendelea kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wasimamizi wengine wa utekelezaji wa mitaala ambapo jumla ya shilingi 1,400,000,000 zimetengwa na zimelenga kuwafikia jumla ya walimu na wasimamizi wa utekelezaji wa mitaala 8,500.

Ndugu Wanahabari; li kupunguza gharama za utoaji wa mafunzo kazini na kuhakikisha kuwa mafunzo ya walimu yanakuwa endelevu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanzisha Mpango Endelevu wa Kutoa Mafunzo kwa Walimu Kazini (MEWAKA).

Mafunzo haya yatatolewa kwa njia za Jumuiya za Kujifunza (JzK), njia ya kujisomea binafsi, ana kwa ana, na mtandaoni. MEWAKA imepangwa kufanyika shuleni na kwenye Vituo vya Walimu.

Katika mpango huu, jukumu la TET ni kuandaa moduli mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya walimu na kutoa mafunzo kwa wawezeshaji rika. Moduli hizo zitawawezesha walimu kupata maarifa na ujuzi wakiwa kazini kwa kutumia JzK.

Ili kurahisisha upatikananji wa mafunzo haya TET imeandaa mfumo wa kidigitali wa kufundishia na kujifunzia unaojulikana kama Learning Management System (LMS).

Mfumo huu umepakiwa moduli mbalimbali na unapatikana kupitia tovuti ya www.tcpd.tie.go.tz. Kuingia katika Mfumo huu mtumiaji atapaswa kujisajili ili kufungua akaunti kwa kutumia namba ya simu ambapo atapewa nywila atakayoitumia kila anapotaka kuingia kwenye mfumo. Kupitia mfumo huu, walimu zaidi ya 48,000 wamejisajili na wanatumia mfumo.

Ndugu Wanahabari; uhusu utafiti, kwa Mwaka huu wa Fedha 2021/222022/23, TET inafanya tafiti kuu mbili:
(i) TET inashirikiana na Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Aghakani, Aga Khan Foundation (AKF) na EdTech Hub kufanya utafiti wenye lengo la kubainisha teknolojia ya TEHAMA iliyo nafuu, sahihi na endelevu itakayofaa kutumika katika kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini ili kuboresha matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya Elimu ya Msingi kwa shule zilizoko vijijini. Utafiti huu unafadhiliwa na wadau wa maendeleo na utagharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania 850,000,000.

(ii) Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Western Norway of Applied Sciences imekamilisha utafiti unaojulikana kama Kuona ni Kujifunza.

Matokeo ya utafiti huu yamepelekea uhitaji wa kuandaa moduli kwa ajili ya kutolea mafunzo kazini kwa walimu ili kuongeza umahiri wao katika kuwabaini, kuwachunguza na kutoa afua stahiki kwa wanafunzi wenye changamoto za uoni katika kujifunza kuanzia Elimu ya Awali hadi sekondari. Jumla ya Tsh. 82,642,545 zimetengwa kwa ajili ya kuandaa moduli hizi.

Ndugu Wanahabari; wa niaba ya Baraza, Menejimenti na watumishi wa
TET, napenda nimalizie kwa kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya TET.

Hakika Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa kila mtoto wa kitanzania anapata elimu bora na bila ada.

Vilevile, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inayoongozwa na Mhe. Prof. Adolf Mkenda (MB.), Naibu Waziri QS Mhe. Omary Juma Kipanga, Katibu Mkuu Dkt. Francis Michael, Manaibu Katibu wakuu Prof. James Mdoe na Prof. Carolyne Nombo pamoja na viongozi wote wa Wizara kwa usimamizi, miongozo, na ushauri unaotuwezesha kutekeleza vyema majukumu ya TET.

Ndugu Wanahabari:
Ni matumaini yangu kuwa mmepata uelewa mpana wa majukumu ya TET. Nimalizie kwa kusema kuwa TET inatekeleza majukumu yake kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano wa kipindi cha mwaka 2018/19 hadi mwaka 2023/24.

Vilevile, utekelezaji wa majukumu ya TET unazingatia sheria anzilishi ya taasisi hii, mipango
mbalimbali ya maendeleo ya nchi, Sera ya Elimu, dira ya elimu, nyaraka na miongozo mbalimbali inayotolewa na serikali.

Kwa mara nyingine tena ninawashukuru sana wanahabari wote kwa kuendelea kushirikiana na TET. Na sasa ninawakaribisha kwa maswali.

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA! Mungu Ibariki Tanzania
 

Attachments

  • MTAALA (B5) Jan 2019.pdf
    465.9 KB · Views: 7
Back
Top Bottom