TARURA kuondoa vikwanzo mtandao wa barabara za Wilaya

JUMA JUMA

JF-Expert Member
Jan 5, 2013
666
835
TARURA KUONDOA VIKWANZO MTANDAO WA BARABARA ZA WILAYA

Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umesema maeneo ya kipaumbele kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni Kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za Wilaya ili angalau ziweze kupitika misimu yote.

Hayo yamesemwa na mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff Agosti 24,2023 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa TARURA kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mhandisi Seff amesema asilimia 71.48 ya mtandao wa barabara za Wilaya ni za udongo na zinaathirika sana wakati wa misimu ya mvua na kusababisha maeneo mengi kuharibika/kutopitika.

“Changamoto hiyo ya maeneo mengi kuharibika/kutopitika wakati wa misimu ya mvua inadhoofisha ukuaji wa sekta ya kilimo, inapandisha gharama za usafiri na usafirishaji na pia kutofikika kwa huduma za kijamii na kiuchumi (Shule, vituo vya Afya, masoko na ajira)”,

Aidha, Amesema Katika mwaka wa fedha 2022/23 Wakala iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 838,158,970,993 kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara za Wilaya, kati ya fedha hizo Shilingi 776,628,938,748 ni fedha za ndani na Shilingi 61,530,032,245.58 ni fedha za nje.

Hata hivyo Mhandisi Seff ameendelea kutaja vipaumbe ni pamoja na Kuzitunza Barabara zilizo katika Hali Nzuri na Hali ya Wastani kubaki katika hali hiyo ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika.

“Kupandisha hadhi (upgrading) barabara za udongo kuwa za Changarawe/Lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii, Mipango ya muda mrefu ya Kitaifa na Kimataifa, ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika majiji, manispaa na miji,”

Hata hivyo amesema Matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi (kwa mfano mawe) katika ujenzi na matengenezo ya barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira.

“Utekelezaji wa kazi za ujenzi na matengenezo kwa mwaka wa fedha 2022/23 umefikia asilimia 85 hadi kufikia mwezi Juni 2023 ambapo jumla ya Shilingi bilioni 743.405 zilipokelewa sawa na asilimia 89 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 598.81 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 144.593 ni fedha za nje,”

Mbali na hayo amesema Kupitia fedha za ndani, jumla ya kilomita 22,523.51 zimefanyiwa matengenezo (utunzaji wa barabara), ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilomita 249.74, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe kilomita 9,761.01, Ujenzi wa madaraja na makalavati 463 pamoja na ujenzi wa mifereji ya kuondoa maji barabarani kilomita 64.47.

“Kupitia fedha za nje kulikuwa na miradi minne (4) inayoendelea na utekelezaji ambayo ni Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Mradi wa Uboreshaji wa Barabara vijijini na fursa za kiuchumi na kijamii (RISE), Mradi wa uendelezaji wa Miji 45 (TACTIC) na Mradi wa Agri connect,” amesema

Jukumu kubwa la TARURA ni kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za Wilaya. Tafiti zinaonesha kuwa maeneo ya kilimo vijijini yakiwa yanafikika kwa mwaka mzima, inaongeza ukuaji wa kilimo na kupunguza umaskini na hasa ukizingatia takribani asilimia 65.1 ya watanzania wanaishi vijijini na Sekta ya kilimo kwa Tanzania inachangia pato la taifa kwa takribani asilimia 26.

IMG-20230824-WA0165(2).jpg
IMG-20230824-WA0167(1).jpg
IMG-20230824-WA0167(2).jpg
IMG-20230824-WA0164(2).jpg
 
Back
Top Bottom