SoC03 Tanzania ya viwanda: Mei Mosi na kundi lililosahaulika ndani yake

Stories of Change - 2023 Competition

DON YRN

JF-Expert Member
Jan 14, 2019
474
999
Ni majengo makubwa makubwa, yenye thamani ya mamilioni ya shilingi yakiwa yamewekezwa. Ndani yake kuna mitambo ya aina mbalimbali yenye kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotumika katika maisha ya kila siku kwa kila Mtanzania. Bidhaa zenye kuzalisha faida za thamani ya mamilioni ya shilingi na kuwafanya wamiliki wake wawe mabwenyenye wenye ukwasi wa kutisha hapa mjini. Majengo haya yanaitwa viwanda! Pamoja na hayo yote yaani kuzalisha bidhaa mbalimbali na mabilioni ya pesa, kuna kundi moja limesahaulika kwenye viwanda na linazidi kusahaulika kila uchao, kundi hili ni wafanyakazi wa kutwa yaani Vibarua. Hapa namaanisha Mei mosi (siku ya wafanyakazi) imewasusa na haina mpango nao na imeziba masikio na kuwa na kiburi juu yao.

Kibarua anaamka asubuhi na mapema kuwahi kazini pengine kuliko hata meneja wa kiwanda, kuliko hata mbunge anayepokea mamilioni ya shilingi kwa mwezi na posho ya kila siku ya mkutano. Kijana huyu mwenye familia inayomtegemea ya baba, mama, wadogo zake, mke na watoto unajua analipwa shilingi za Kitanzania ngapi? Kwa taarifa yako huyu kijana analipwa Tshs 4,000/=, Tsh 4,500, Tshs 5,000 Tshs, Tshs 6,000, Tshs 7,000, Tshs 8,000 na angalau baadhi ya viwanda Tshs 10,000. Kijana huyu unamlipaje Tshs 4,000? Hela hiyo atumie nauli wakati wa kuja na kurudi toka kazini, atumie kula na hapo ategemee kwenye matumizi ya kila siku? Kijana huyu wa Kitanzania ametelekezwa na siku ya wafanyakazi(Mei mosi). Hii siku nadhani inahusika na wafanyakazi wa maofisini tu!

Sekta ya viwanda ni sekta inayochangia kwa asilimia kubwa mno katika Uchumi wa Nchi yetu, kwa lugha nyingine sekta ya Viwanda ni mhimili na kipimo cha ukuaji wa uchumi Tanzania. Badala ya kumuinua kijana wa Kitanzania ili aweze kujikwamua kiuchumi hasa huyu kibarua, imekuwa ni kama desturi kumdidimiza au kumrudisha nyuma ili aendelee kuwa mtumwa wa kuwa kibarua miaka na miaka bila mafanikio yoyote huku Serikali ikiendelea kuchukua mamilioni ya kodi yatokanayo na nguvu za huyu kijana wa Kitanzania.

Hii sekta ilipaswa ipewe kipaumbele zaidi na izungumziwe kwa upekee wake. Napata wakati mgumu kumuelezea huyu kijana kwamba analipwa kwa sheria za miaka ipi zenye unyonyaji wa kiwango kikubwa namna hii huku gharama za maisha zikipanda (mimi siyo mtaalamu wa sheria, wadau nifafanulieni hizi sheria)? Huyu kijana wa Kitanzania yeye hataki kununua Range rover au V8? Kila bidhaa inayozalishwa hapa Tanzania, kuna kijana katumia nguvu zake hadi kumfikia mlaji wa mwisho(mwananchi).

Viwanda vya nondo, vyuma, mishumaa, vifaa vya plastiki, vifaa mbalimbali vya ujenzi, n.k., huyo kijana anayepakia hiyo mizigo kwenye hayo malori hizo bidhaa zenu ili mpeleke kwa wateja wenu ndani na nje ya nchi, ni kweli kijana huyu anapaswa kulipwa kiwango kidogo hicho cha pesa? Kijana aliyepo kwenye godauni hilo la simenti anastahili kulipwa hiyo laki moja au laki mbili kwa mwezi? Muda mwingine anafanya kazi bila hata kutumia vifaa maalum vya kulinda afya yake kama gloves, kofia ngumu, barakoa, viatu maalumu vya kazi!

Kilo moja ya unga ni shilingi ngapi? Mchele? Sukari? Ngano nk? Analipwa hivi kwa sababu kazi za viwandani ni rahisi kupatikana bila CV sababu hajasoma na hawezi omba kazi kwenye ofisi ya Waziri Mkuu au hata udaktari? Lakini hata hivyo wapo waliosoma ila kwa kuwa hawana “koneksheni!”. Wengine hufanya kazi hata nje na zaidi ya muda maalum wa kazi ambao inapaswa alipwe kwa malipo ya ziada, halipwi! Huyu huyu kijana hana hata Bima ya afya anategemea hiyo hela kidogo mnayompa ili akajitibu! Ni kweli mei mosi imemtelekeza huyu kijana, imefumba macho haioni jasho lake linavyopotea bure kuijenga nchi yake Tanzania.

Huyu kijana ndiye anayepiga kura na kuwaweka kwenye hizo nafasi enyi watunga sera na huyu kijana ndiye tunamtegemea aje awe mzee wa miaka ijayo, si ndiyo? Vijana wa miaka ijayo watajivunia kuwa naye huyu mzee goigoi aliyezeeka mwili kwa kazi za viwandani zilizomaliza nguvu zake na hana chochote? Atakuwa mzee wa namna gani? Au ndo tutamuweka kwenye mpango wa kuondoa kaya masikini(Tasaf)? Au tutaanza kumlipa zile elfu ishirini za kila mwezi wanazopewa wazee tena kwa mbinde huku akiigawana na mjumbe wake wa mtaa asiyelipwa mshahara? Hii ndiyo Tanzania ya viwanda tunayotaka kuitengeneza? Kwa nini nchi yake haimtendei haki? Ewe mei mosi, kwa nini unamtenda hivi huyu kijana wa Kitanzania? Mbona hatuoni ukimtetea kama wale wengine? Au kwa kuwa wewe upo mifukoni mwa wenye kauli za mwisho? Huyu kijana anastahili heshima yake bhana hata kama hayupo kwenye mfumo maalumu unaotakiwa!

Ewe mei mosi, jaribu kusikia kilio cha huyu kijana wa Kitanzania! Jaribu kuwakumbusha hawa viongozi wetu wamkumbuke huyu kijana mpambanaji! Jaribu kuwakumbusha kuwa huyu kijana anastahili bima ya afya, anahitaji posho baada ya kufanya kazi ya ziada, anastahili nyongeza ya malipo ya kazi kubwa anayoifanya katika nchi yake pendwa Tanzania!

Wako katika ujenzi wa Taifa,

DON YRN.
 
Back
Top Bottom