Tanzania: Nini tatizo letu kama Taifa? Tunajikwamuaje?

Ndugu zangu nyote mnaotoa maoni katika Jukwaa la Siasa, mimi nina ombi kwenu. TULIOKOE TAIFA LETU. Tunaandika na kutoa maoni, lakini kusema kweli Taifa letu linaelekea pabaya.

Bajeti imenichanganya! Bilioni 19 kutengwa kwa chai na bilioni 35 kwa safari ni jambo la kusahgaza sana wakati tunaambiwa kwamba kuna mtikisiko wa uchumi.

Fedha zilizotengwa kuzilipa kampuni zilizonunua mazao, nazo ni tatizo. Kampuni hizi ni ngapi na zinadai kiasi gani? Je, zikiundwa Kagoda, ili fedha ipatikane kiulaini kuiingia kwenye kampeni za CCM mwaka ujao? Maana CCM imejijgengea utamaduni wa kushinda kwa kutumia fedha.

Ni lazima kitu kifanyike. Tuache maneno na kuanza kufanya kazi ya kuwaelimisha watu. Tuna kazi ya kuwlatoa usingizini. Watanzania wachache wanaweza kusoma habari ndani ya mtandao. Watanzania wachache wanaweza kusoma magazeti, watanzania wachache wana redio na runinga. Hivyo ni lazima tubuni mbinu za kuwaelimisha watu wetu ili tuliokoe taifa letu. Vinginevyo tunaangamia na kuliangamiza taifa letu la Tanzania.:(:(:(
Lingamie mara ngapi.. wewe umeshtuka leo!
 
Hata ingekuwa million 1 kwa ajili ya chai na vitumbua watu bado tungelalamika maana hakuna haja ya kunywa chai mara mbili yaani asubuhi nyumbani kwako na pia offisini...

Maji ya bomba yangewatosha kama mamlaka ya maji yangehakikisha kwamba maji yake ni safi na salama kwa kunywa...

Lakini kwa kuwa ukinywa maji ya bomba bongo yasiyo-chemshwa una hatari ya kupatwa na Typhoid, ya nini basi ku-risk kunya maji haya wakati wakijua kwamba si salama...

Nionavyo mimi bajeti hiyo ya chai na vitafunwa ingewekwa ili miundombinu ya maji katika wizara na idara za serikali irekebishwe ili iweze kutoa huduma ya maji na sio kwa mawaziri pekee bali pia wa watumishi wote wa idara na wizara zotew za serikali...
 
Ni kweli bajeti yetu imetenga bilioni 19 kwa chai na bilioni 35 safari za viongozi. Lakini Waziri amefafanua kwamba si chai bali samani kwenye nyumbaza viongozi. Maana yake ni kwamba kila mwaka ni lazima viongozi wetu wanunuliwe samani! Ni lazima kulikoa taifa letu.

Wizi unalindwa kwa kisingizio cha SIRI za Jeshi. Wapi na wai Jeshi la Wananchi,kuwa na siri? Hata hivyo Bunge, hatukusikia Mizinga na vifaa vingine vya kijeshi. Kilichoulizwa ni wizi!

Ukimya wangu, hauna maana wa kutoyajua mambo, ila ni kielelezo kwamba si watanzania wengi wanaweza kumudu kuingia kwenye mtandao kila wakati. Wengine hata hawana uwezo kununua gazeti na kusikiliza redio. Hivyo ninaingia hapa mara chache, lakini nikiingia ni kigongo cha nguvu.

Mutekanga, ni Mutekanga - jina hili maana yake ni yule asiyeogopa! Si jina kutunga wala kujificha, hili ni jina langu. Mimi siogopi! Tanzania itajengwa na watu wasioogopa. Lakini wale wanoaficha majina yao, na kuanza kutupatia habari moto moto, hawawez kutusaidia. Acheni kuficha majina yetu, jitokeze tupambane! Ni lazima kulioko taifa letu leo na si kesho!
 
Kwa ufupi ni nadhani tatizo letu sasa hivi ni kukosa UTAWALA WA SHERIA. Matatizo yote tunayokumbana nayo yanatokana na kusokosekana kwa utawala wa sheria. Imarisha utawala wa sheria, utakuwa umepiga vita almost everything, rushwa, ufisadi, nk. Bila kuimarisha utawala wa sheria hatuwezi kupiga hatua ya maendeleo!
 
Pamoja na yote yaliyosemwa, suala jingine ni kwamba tanzania hatuna msukumo sahihi wa uongozi. Mara nyingi kinachosukuma watanzania kuwania nyadhifa mbali mbali kunufika na rasilimali za taifa na kuzigawa kwa ndugu, mahawara na marafiki .kimombo hii tunasema ni negative leadership incentive. Issuing handouts to colleagues and seems to be the prime motive that pushes people to vie for leadership. Secondaly, our institutions dont work in a coordinated manner, infact two men can run the country by issuing directive right from their beds. Sio kwamba ukiondoa mahakama na bunge things will come to standstill, it will be business as usual because most of our institutions are redundant. What matters is the party chairman wa sisiem na wapambe wake.
 
Kwanza, Mi nadhani transition yetu ya kutoka Ujamaa kwenda Uchumi huria tuliiendea kwa pupa bila tahadhari zinazostahili. Tuliuvamia ubepari kama vile kipofu kaona mwezi. Pupa hiyo ndiyo imezaa matatizo chungu mzima: ubinafsi wa kujilundikia mali, ubinafsishaji holela wa njia kuu za uchumi, uongozi corrupt na kila aina ya ufisadi. Huku "kumekucha" ndiko kumeleta matatizo mengi zaidi kwani kila aliyepata nafasi alitaka na kuitumia vyema ili aondokane na umaskini binafsi uliosababishwa na speed governor ya siasa za ujamaa

Pili, Watu pia hawakuwa wameandaliwa kuingia kwenye mfumo huu mpya. Kumbe wengi wakabaki na wamebaki mpaka leo wakishangaa tu hawajui wafanye nini. Ni watazamaji tu kama watazamaji wa filamu ukumbini wakiangalia jamaa wanavyojishughulisha.

Tatu, Historia ya mazingira yetu ya utulivu yamefanya watu wabweteke na kusinzia. Tungekuwa kwenye mazingira harsh watu wangeamka na kuwa aggressive katika maisha ili kuweza ku-survive. Wangepambana vilivyo na kuwa wabunifu ili kuweza kulinda maisha yao. Na hapa msukumo wa maendeleo ungekuja. Kwa hiyo hapa kuna suala la fikra.

Nne, hatukuwekeza vya kutosha katika elimu kwani elimu ni msingi wa maendeleo na dira ya maisha. Wananchi walio na elimu ni rahisi kujua nini cha kufanya ili kundokana na umaskini.
 
TUACHE MAFISADI WAFUKARISHE TAIFA?

Source wanaBIDII

Na Ananilea Nkya

Umaskini wa kupindukia wa kipato (ufukara) unaowasumbua wananchi wengi vijijini na mijini hapa nchini,wanawake na wanaume, huenda usipatiwe ufumbuzi wa kudumu kwa kutumia ushindani wa sera za vyama wa vyama vya siasa na ubora wa uongozi kama tatizo la ufisadi ambalo linalitikisa taifa letu hivi sasa, halitang'olewa na mizizi yake.

Ufisadi na rushwa ni adui namba moja wa haki ya wananchi katika kudai uwajibikaji wa viongozi kwa sababu vitendo hivyo viovu vinaharibu kabisa dhana nzima ya uadilifu katika uongozi na hivyo kuhatarisha maendeleo ya uchumi, amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Kwa vile ufisadi ni tatizo linalohusiana moja kwa moja na uongozi wa nchi, na kwa vile uongozi wa nchi yetu unatokana na siasa za vyama, dawa ya kukomesha ufisadi itapatikana endapo tu wanasiasa wataweka pembeni maslahi yao binafsi na ya vyama vyao na kujali zaidi maslahi ya taifa. Waswahili husema ni rahisi kuziba ufa kuliko kujenga ukuta. Au ni heri nusu shari kuliko shari kamili.

Ni viongozi, makada na wanachama wangapi wa vyama vya siasa ambao wanafahamu kuwa katika zama hizi za utandawazi vyama vyao vinaweza kutekwa kirahisi na mafisadi na hivyo chama kujikuta kinakuwa mawakala wa mafisadi wenye lengo la kuiba na kuhamisha utajiri wa nchi yetu kwenda kutajirisha nchi nyingine?

Je wapo viongozi wa vyama vya siasa hapa nchini ambao wakichungulia ndani ya mioyo yao wanabaini kabisa kwamba wanao upendo usiotiliwa shaka kwa nchi yetu na watu wake? Ni wangapi watakuwa tayari kujitoa mhanga hata kama kwa kufanya hivyo watakuwa wamepoteza maslahi yao binafsi na/au ya vyama vyao ili kuliokoa taifa lisiendelee kuharibika kutokana na athari mbaya za ufisadi?

Ni viongozi wangapi wa kisiasa ambao wako tayari kujitoa mhanga kuona kuwa demokrasia ya vyama vingi vya siasa inaimarika na kustawi vizuri nchini ili vyama hivyo viweze kuwa chimbuko la kuibua fikra mpya, sera mpya na mipango mipya ambayo itachochea kasi ya maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa wananchi wengi mijini na vijijini ambao leo hii wanaishi maisha ya ufukara wakati nchi yetu ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika na duniani zenye utajiri mkubwa wa mali asili?

Kila kiongozi, kada na mwanachama wa vyama vya siasa (DP, TLP, CCM, UDP, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na vingine vyote) nchini akitafakari maswali haya bila unafiki, kisha akayafanyia kazi bila woga majibu yanayotoka kwenye moyo wake, muda si mrefu ufisadi unaweza kuwa jambo la historia a hivyo janga linaloinyemelea nchi kutokana na ufisadi kuzimwa.

Ufisadi kimsingi ni wasilisho au ainisho la wananchi hapa nchini kwetu kuhusu vitendo vya rushwa, wizi, ukwapuaji au udanganyifu mkubwa wa kupindukia wa fedha na mali za umma unaofanywa na kikundi kidogo cha watu (mtandao) kinachohusisha baadhi ya viongozi wa serikali na baadhi ya wafanya biashara wakubwa.

Kimsingi ufisadi hufanywa kwa ajili ya wahusika kujinufaisha binafsi kiuchumi na kuwawezesha kubaki madarakani kwa gharama yoyote ile hata kama kwa kufanya hivyo kutaathiri kwa kiwango kikubwa uwezo, heshima, kiwango na thamani ya uongozi katika mfumo wa demokrasia inayopaswa kuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa wananchi na taifa lao.

Neno ufisadi lilianza kutumika rasmi hapa nchini baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mwembeyanga, Temeke jijini Dar es Salaam mwaka 2007 ambapo viongozi kadhaa waandamizi serikalini wa awamu hii na awamu awamu iliyopita walitajwa hadharani (list of shame) kwamba wamehusika na vitendo vya ufisadi vilivyochangia kulifukarisha taifa letu ikiwa ni pamoja na wizi wa shilingi bilioni 133 kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika benki kuu (BOT).

Hadi sasa wananchi wanaendelea kuwatilia shaka viongozi waliotajwa katika tuhuma hizo kuhusu uadilifu wao kama viongozi kwa sababu hakuna hata mmoja alishakwenda mahakamani kukanusha tuhuma hizo.

Hatari ya viongozi waliotuhumiwa kwa ufisadi kutowajibika kutokana na tuhuma hizo ni nini? Taifa limeanza kushuhudia kasi ya ajabu ya kushamiri kwa vitendo viovu nchini jambo linaloashiria kuwa makundi mengine ya watu nje na ndani ya serikali yanafanya mambo maovu kadha wa kadha bila woga pengine kutokana na kuidharau serikali kwa vile baadhi ya viongozi walioko madarakani wametuhumiwa hadharani kwa kuhusika na ufisadi lakini hawajawajibika au kuwajibishwa na mamlaka.

Maovu ambayo yameshamiri kwa kasi kubwa hapa nchini katika miaka ya hivi karibuni ni pamoja na wimbi la matumizi mabaya/wizi wa fedha za serikali, ajali nyingi za kizembe, biashara ya viungo vya binadamu, udanganyifu na wizi wa mitihani, matukio mengi ya mauaji ya kikatili, watu taaluma kukimbilia siasa, wanasiasa kuchochoe migogoro ya kidini na kuingizwa nchini bidhaa feki ikiwa ni pamoja na chakula na madawa ya bianamu.

Kadhalika kumezuka mitandao mingi ya watu kujipatia fedha haramu, wanyonge kuporwa mali zao hasa ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji, rasilimali za nchi kuporwa kiholela kama madini, samaki, magogo napembe za ndovu na wanyonge kukosa haki mbele ya vyombo vya sheria.

Mengine ni rushwa za kutisha kutawala katika chaguzi, migomo ya wafanyakazi, ongezeko la vifo vya wananchi maskini vinavyoweza kuzuilika, wanataaluma kudhalililishwa, viongozi kuzomewa na wananchi, viongozi kuwa wababe na kutoona aibu juu ya makosa wanayofanya na mambo mengine ya aina hiyo yanayolitia aibu taifa.

Ufisadi unapokuwa ni sehemu kubwa ya utamaduni kwa taifa ni jambo la hatari kubwa sana. Hii ni kwa sababu rushwa, wizi na udanganyifu wa kutisha havitaishia kufanywa na watu wenye mamlaka serikalini peke yake, bali vitendo hivyo husambaa na kujengeka kama tabia ya wanajamii kwa sababu mienendo, vitendo na tabia za watawala huigwa kirahisi na watawaliwa.

Je ni nini chanzo cha kushamiri kwa ufisadi nchini? Tanzania ni moja ya nchi za Kiafrika ambazo baada ya kupata uhuru wake ziliweka utaratibu wa kupata viongozi wake wa kuongoza taifa kwa kutumia mfumo wa chama kimoja cha siasa. Wakati huo chama kilikuwa kinaweka misingi thabiti ya uongozi ili kuhakikisha kuwa anayependekezwa na chama kugombea uongozi ni mtu mwadilifu anayeweka maslahi ya taifa mbele.

Lakini kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1990, kutokana na mabadiliko duniani, nchi hizi zililazimika kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kwenda sambamba na mfumo wa uchumu wa utandawazi ambao chanzo chake ni kuanza kuanguka kwa mfumo wa ubepari duniani. Mfumo wa ubebari ni mfumo wa unyonyaji ambao hutajirisha watu wachache na kuwaacha wengi wakiwa fukara.

Katika siasa za vyama vingi, kunakuwepo na ushindani mkubwa katika suala zima la kupata madaraka ya kuongoza nchi. Ushindani siyo tu unakuwa baina ya vyama, bali pia ndani ya vyama kunakuwa na ushindani unaohusisha makundi/mitandao yanayotafuta kwa udi na uvumba kushika madaraka ya nchi.

Katika ushindani wa kupata madaraka na au fursa ya kuchuma utajiri, hata ndani ya chama inawezekana watu (raia au wageni au wote wawili kwa kushirikiana) wenye malengo hayo wakatumia fedha safi na chafu kufikia malengo yao.

Kimsingi ufisadi huwa unaikumba nchi endapo chama tawala kwa wakati husika, hasa kama viongozi, makada na wanachama wake wanajali zaidi maslahi yao binafsi na ya chama chao kuliko maslahi ya taifa lao.

Lakini zaidi ufisadi kirahisi huikumba nchi kama nchi hiyo haijaweka itikadi/misingi rasmi na imara ya taifa ambayo kila chama kinapoingia madarakani kitalazimika kuifuata kwa maslahi ya nchi. Hivyo baadhi ya watu wenye fedha nyingi na malengo binafsi ya kiuchumi na /au kisiasa, hujenga mahusiano makubwa na vyama vikubwa hasa chama tawala na uhusiano huo hushamiri kutokana na hitaji la chama kupata ufadhili kwa ajili ya kushinda uchaguzi.

Kutokana na kutaka kung'ang'ania madaraka ya uongozi wa nchi kwa ajili ya maslahi binafsi zaidi, chama hicho tawala kinaweza kuamua kufanya kila linalowezekana, liwe jema au baya, ili mradi kishinde uchaguzi.

Kinaweza kufanya hivyo kwa kutoa propaganda za kuhadaa umma kwa kutumia hoja mfilisi kwamba vyama shindani (upinzani) hasa vyenye nguvu kwa wakati husika kwamba havina sera, au vina udini, ukabila, urangi, ujinsia utabaka na mambo mengine ya aina hiyo ili mradi lengo kuhalalisha ushindi lifanikiwe.

Wakiona wana ushindani mkubwa utakaohatarisha ushindi wao na wenyewe hawana fedha za kutosha kwa ajili ya mikakati ya ushindi, wanaweza kufanya mbinu za kupata fedha zaidi kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi walioko madarakani wakati husika kufanya mambo machafu.

Wanaweza kupata fedha wanazohitaji kwa ajili ya kupata ushindi kwa kuiba/kukwapua kutoka taasisi za serikali kama kwenye mabenki au miradi mikubwa ya umma yenye fedha nyingi.

Vile vile wanaweza hata wakatafuta watu ambao watapewa zabuni feki za serikali ambazo watalipwa fedha nyingi kwa makubaliano kwamba watamega fungu kubwa la fedha zitakazochotwa kifisadi kukisaidia chama kushinda uchaguzi.

Isitoshe inapokuwa ni utamaduni chama tawala kushinda uchaguzi kwa gharama yoyote ile, fedha za kutengeneza ushindi zinaweza zikawekwa kimkakati katika bajeti ya serikali kwa kuingiza shughuli/miradi hewa na/au zikapatikana kutokana na mikataba mibovu na dhalili ya uwekezaji. Kwa mfano mwekezaji anaweza kumilikishwa mali yenye thamani ya fedha nyingi lakini anapewa mkataba ambao serikali itapata manufaa kidogo tu mradi mwekezaji huyo akisaidie chama kushinda chaguzi.

Fedha za kutafuta ushindi zinaweza kutafutwa kwa njia njingine chafu pia ikiwa ni pamoja na kuunda mitandao ya ujambazi ambayo inaweza kuendesha wizi wa kutisha katika shughuli za wananchi kwa mfano wizi kwenye maduka makubwa ya bidhaa, maduka yanayoendesha biashara ya fedha, vituo vya mafuta, migahawa na baa, kuvamia maofisi siku za kulipa mishahara na kwingineko kokote zinakoweza kupatikana fedha.

Chama cha siasa kikishafikishwa hapo, kimsingi kinakuwa ni chama cha mafisadi au wakala wa mafisadi kwa kujua au kutokujua. Hivyo dola (serikali, bunge na mahakama) yake kwa vyovyote itakuwa imetekwa na mafisadi. Kwa hiyo dola hiyo penda isipende itakuwa inatekeleza matakwa ya mafisadi waliowezesha chama kupata ushindi.

Hii ndiyo sababu chama husika kikishapata ushindi, waliosaidia ushindi kupatikana wanakuwa wanalindwa kikamilifu ili malengo yao yatimie. Katika hali hii wanaoingia madarakani wanakosa wanakosa nguvu na ujasiri wa kufanya lolote hata kama wale waliosaidia watakuwa wanatenda mambo ya kutia taifa dosari kubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kibaya zaidi kama fedha za kuwezesha kushinda uchaguzi zitakuwa zimepatikana kifisadi, na ikatokea siri ya ufisadi huo ikavuja, basi kazi kubwa waliopata madaraka kutokana na uchaguzi huo inakuwa ni kubuni mikakati mbali mbali na kwa gharama yoyote kuhakikisha ufisadi huo unafunikwa

Hali ya chama tawala husika kuogopa kushindwa uchaguzi au kuumbuka kwa ufisadi inaweza kusababisha chaguzi zitakazofuata kugubikwa na ufisadi mkubwa zaidi tena wa kutisha na ambao pengine haitakuwa rahisi kufichuliwa kutokana na ukweli kwamba uzoefu wa kufanya ufisadi kwa ajili ya kushinda uchaguzi utakuwa unajengeka na kuimarika kutoka uchaguzi mmoja hadi mwingine.

Ikiwa lengo kuu la chama cha siasa ni kushinda uchaguzi, shughuli kubwa siku zote itakuwa ni kutafuta mbinu za kupata ushindi hata kama ni kwa ufisadi au kufanya chochote kile kichafu au kisafi, labda makundi makumba yenye uchungu na hatma ya nchi yawe jasiri na kukimama imara bila kugawanyika kuhakikisha waliohusika/chama husika kinawajibishwa kabla sumu hiyo haijasambaa na kuigwa na vyama vingine vikubwa ambavyo vinaweza kushinda chaguzi zinazofuata.

Ni kwa sababu ya ukweli huu ndiyo maana hata kama baadhi ya wale waliosaidiwa kuingia madarakani watakuwa na nia njema ya kutaka kuwatosa waliowasaidia, hawatathubutu kufanya hivyo kutokana na hofu kwamba mipango ya kushinda chaguzi zinaofuata itavurugika na hivyo kukiweka chama katika hatari ya kushindwa.

Ili kuhakikisha kushindwa hakutokei, uhakika wa fedha za kuwezesha chama kishinde ukishakuwepo, kitakachofanyika ni kutumia fedha hizo kupata ushindi hasa kwa kucheza na saikolojia na mahitaji ya msingi(chakula, vinywaji, mavazi na hata kiroho) ya wapiga kura hasa wasiojua kinachoendelea na madhara yake kwa ustawi wa demokrasia, amani na maendeleo yao binafsi na ya taifa lao.

Hii inawezekana kwa kuweka mkakati mahususi ikiwa ni pamoja na kuhonga wananchi fedha, mavazi, chakula au vitu vingine vidogo vidogo kukidhi mahitaji ya fukara, kununua shahada za wapiga kura ili wasiweze kupiga kura, kuwatisha wananchi kwa kutumia vyombo vya dola, kuunda vikundi vya kihalifu kuwashambulia, kuwafilisi na kuwatisha watu watakaoonekana kuunga mkono vyama vingine.

Kama mambo ni magumu zaidi wanaweza kununua baadhi ya maafisa wa tume ya uchaguzi ili majina ya wapiga kura yavurugwe wapiga kura hasa kwenye maeneo yenye upinzani mkubwa wasiweze kupiga kura kabisa au kwa wakati uliopangwa.

Vile vile sheria za nchi hasa zinazohusu uchaguzi kwa wakati husika hata kama ni nzuri kiasi gani, wanaweza kucheza nazo kwa ajili ya kuwezesha ushindi.

Kwa mfano, sheria inaweza kuwa inatoa fursa kwamba mgombea Urais au mgombea Mwenza wa Urais akifariki dunia kabla ya uchaguzi, uchaguzi huo utahairishwa ili chama hicho kiweze kutafuta mgombea mwingine.

Sheria hii inawezekana kuonekana ni nzuri, lakini hebu fikiria, wagombea Urais wanaweza kuwa ni wengi baadhi kutoka vyama vikubwa na wengine kutoka vyama vidogo sana ambavyo kwa wakati husika havina uwezo kisiasa kushinda hata udiwani lakini vimesimamisha mgombea wa Urais iwe ni kwa vyama husika vyenyewe kutaka kutumia demokrasia iliyopo au ni kwa kushinikizwa na mafisadi kwa malengo mahususi la kuwezesha chama kilicholengwa kusaidiwa kupata ushindi kiweze kushinda.

Sheria hiyo nzuri inaweza kutumiwa na watu wenye malengo mabaya ya kuweka madarakani watu ambao watalinda maslahi yao zaidi kwa sababu wenye malengo mabaya wanaweza kuhonga mwanasiasa ambaye wanajua yuko taabani kiafya agombee kwa lengo la kutumia fursa hiyo kutekeleza mikakati ya ushindi.

Kwa vile ukwapuaji wa mali za umma kwa malengo ya kiuchumi na kupata madaraka ni kitu ambacho ni kichafu kwa jamii yoyote, na kwa vile wanaoumizwa na ufisadi ni wananchi fukara mijini na vijijini, wanawake na wanaume, vijana na wazee, siri ya ufisadi ikivuja wahusika wanachofanya ni kuhakikisha kuwa kila sauti ambayo inaweza kuinuka na kudai uwajibikaji dhidi ya uovu huo inazimwa.

Inaweza kufanyika kwa kupenyeza mamluki kwenye vyama shindani vya siasa ili kutengeneza migogoro au kusababisha mazingira ambayo baadhi ya vyama hivyo navyo vinajitumbukiza katika mambo yatakayovipunfguzia sifa mbele ya umma au mambo ambayo yatawanyang'anya ujasiri wa kudai uwajibikaji wa waliotumia ufisadi kushinda uchaguzi.

Mbinu nyingine ya kuzima uwajibikaji dhidi ya ufisadi ni kwa wanataaluma kwa wanahabari kutishwa ili waogope kufanya kazi yao kikamilifu ili kushinikiza uwajibikaji wa watawala wa wakati husika kuhusiana na ufisadi. Pia wakati mwingine baadhi yao hasa wahariri na wanahabari makini na pengine hata wamiliki wao wanaweza kununuliwa kwa kujua au kutokujua njama hizo mradi tu wasiweze kutumia fursa na taaluma zao kukomesha ufisadi.

Wengine wanaoweza kununuliwa na mafisadi au mawakala wake ili kuzima uwajibikaji kwenye ufisadi ni viongozi wa vyama vya wanataaluma kwa mfano wanasheria/mawakili, vyama vya wahadhiri vyuo vikuu, vyama vya wanafunzi, vyama vya wafanyakazi, taasisi za dini, mitandao ya mashirika yasiyo ya kiserikali na wasanii mashuhuri na wanamuziki.

Mambo mbali mbali yanaweza kufanyika kisiasa kuhakikisha kuwa makundi hayo yanapata ganzi/kigugumizi au kuona kuwa hakuna ufisadi au ufisadi ni sehemu ya maisha na hivyo hakuna umuhimu wa wao kushiriki kudai uwajibikaji dhidi ya vyama vya siasa vinavyokumbatia ufisadi ili watu binafsi na vyama hivyo vinufaike kisiasa.

Kwa mfano wanasiasa wenye malengo binafsi wanaweza kutengeneza jambo ambalo litazusha mjadala unaoleta mgawanyiko na pengine chuki katika ya makundi ya jamii husika kutokana na imani za dini, mila na desturi, kijinsia, urangi na/au ukabila.

Lengo ni wenye uchu wa madaraka kubaki madarakani na wenye maslahi ya kiuchumi waweze kuendelea kuchuma. Lakini kamwe hawatathubutu kuzusha jambo litakalozua mjadala katika tatizo la mzingi ambalo ni siasa kutumika kutengeneza matajiri wa kupindukia na huku wananchi wengi wakiwa ni maskini wa kutisha.

Vile vile wabunge jasiri kutoka chama tawala husika ambao watathubutu kutaka vinara wa ufisadi katika chama chao au serikalini wawajibishwe, wanaweza kufanyiwa vitimbi na vitisho pamoja na kusukiwa mikakati ya kuhakikisha kuwa wanashindwa katika chaguzi zinazofuata.

Kadhalika watu waadilifu hasa wazee, vigogo, viongozi wastaafu na makada kwenye chama kilichosaidiwa kuingia madarakani kwa fedha za ufisadi nao pia wanaweza kufanyiwa vitimbi mbali mbali ili washindwe kufurutika kuwajibisha uwajibikaji kwenye chama chao.

Wanaweza kufanyiwa mambo yatakayowajengea hofu kuhusu hatma yao wenyewe na/au hatma za familia zao hasa kisiasa na kiuchumi. Kwa mfano wanaweza kutengenezewa tuhuma za kupika ili na wenyewe waonekane mbele ya jamii kuwa ni watuhumiwa wa ufisadi.

Lakini zaidi wazee, viongozi na makada wadilifu katika chama wanaweza kushindwa kutoa sauti zao dhidi ya ufisadi hasa endapo mfumo utakuwa umewawezesha kunufaika kiuchumi kutokana na chama chao kuwa madarakani.

Baadhi wanaweza kuwa wana kampuni ambazo ni mawakala wa kukusanya ushuru ambapo sehemu kubwa ya fedha zinazokusanywa zitanufaisha wakala na serikali inaambulia fedha kidogo sana. Katika hali hii hawataweza kuwa na sauti ya kukemea ufisadi katika chama wala serikali kwa sababu na wenyewe wanaweza kuonekana mbele ya jamii kuwa ni watu wanaoinyonya serikali na hivyo kufukarisha wananchi.

Zaidi ya hayo, kwa sababu ufisadi una tabia ya kuwajengea wahusika jeuri ya kifisadi kutokana na nguvu ya madaraka na nguvu ya fedha, hata kama zipo sauti nyingi zinazodai uwajibikaji, wahusika wanaweza kuzipuuza sauti hizo na kuamua kuziba masikio kwa sababu liwe liwalo wanakuwa na uhakika wa chama chao kushinda chaguzi zijazo. Hivyo kwao kuogopa wananchi au kuwatumikia kikamilifu si jambo la lazima wala lenye umuhimu.

Ikifikia hapo wa demokrasia ya vyama vingi inakuwa haina maana yoyote katika kuharakisha maendeleo ya nchi sababu wanaoshika madaraka wanapata madaraka hayo kutokana na jinsi walivyo karibu na waliowezesha chama husika kushinda uchaguzi na siyo uwezo wao katika kubuni mbinu za kuisaidia taifa kusonga mbele.

Kibaya zaidi, vyama vingine vya siasa vikishabaini kuwa chama tawala ni king'ang'anizi wa madaraka na tena kinafanya ufisadi kupata ushindi, navyo ikifika mahali vikaishiwa uzalendo vinaweza kulazimika kuiga mbinu hizo chafu au pengine chafu zaidi na zenye maumivu makubwa zaidi kwa taifa na hivyo demokrasia kuzima kabisa sauti za wananchi maskini zisisikike na kufanyiwa kazi na watawala ili waondokane na ufukara.

Kitakachofuata katika hali hiyo ya kila chama chenye nguvu kutafuta ushindi kwa mbinu za kifisadi ni nchi kutumbukia katika machafuko. Machafuko kutokea katika nchi kutokana na chama tawala kutafuta ushindi kwa namna yoyote ile kumeshajidhihirisha katika nchi kadhaa za Afrika ikiwepo nchi jirani ya Kenya na pia Zimbabwe.

Je kwa hali ilivyo sasa nchini kwetu kuhusu ufisadi, kweli tutaweza kusalimisha taifa letu lisiingie katika mgogoro wa kugombea madaraka? Kama tutakubali kurudi nyuma au kuyumbishwa ili tupuuze au kuogopa kusimama kidete kushinikiza uwajibikaji katika ufisadi, je kuna yeyote miongoni mwetu ambaye hataguswa kwa namna moja au nyingine amani ikichafuka nchini kwetu?

Kwa hiyo, kama sote hatutaki ufisadi uhatarishe demokrasia ya vyama vingi, amani, mshikamano na maendeleo ya taifa letu, ni vema makundi yote muhimu katika jamii yajitoe mhanga kushinikiza uwajibikaji dhidi ya tuhuma za ufisadi zinazoikabili nchi hivi sasa ili hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha kuwa wanaotaka kupeleka taifa kubaya hawaogopwi na wanawajibishwa..

Lakini zaidi ni vema wale wote wanaotumia ufisadi kung'ng'ania madaraka wakubali kuwa sehemu ya mabadiliko ya kidemokrasia yanayotokana na mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Vinginevyo wasipobadilika na ikatokea sauti za wananchi zikashinda ufisadi, wanaweza kujikuta mabadiliko yenyewe yakiwalazimisha nao wabadilike na ikifikia hapo wanaweza wakawa katika hatari ya kufedheheka.

Tukiamua Watanzania, tutashinda adui ufisadi kwa manufaa ya taifa zima.
MUNGU IBARIKI TANZANIA.





Ananilea Nkya
Executive Director
Tanzania Media Women's Association (TAMWA)
P. O. Box 8981, Sinza-Mori
Dar es Salaam, TANZANIA
Tel: +255-22 2772681 Fax +255 22 2772681 E-mail:*******@yahoo.com
Cellphone:+255-***-***-***
 
Katika gazeti la Tanzania daima toleo la leo uk wa 6, kuna taarifa kwamba Waziri mkuu wa Japani(Bwana Aso) amevunja bunge la Nchi. Sababu kubwa iliyopelekea bunge hilo kuvunjwa ni kushindwa kutimiza malengo na ahadi zilizotolewa wakati wa kuomba kura. Waziri huyo anaendelea kusema, anaomba radhi kwa kufanya hivyo, lakini kwa bahati mbaya wabunge wameshindwa kutimiza malengo waliojiwekea. "Ingawa tumepata ushirikiana mzuri kutoka kwa chama na wadau wetu wengine kwenye chaguzi zetu, lakini tumeshindwa kufikia malengo yetu ya msingi tuliyojiwekea," alisema waziri huyo, kupitia hotuba yake aliyoitoa katika televisheni....
Ndugu zangu wanajf, hebu tujadili sisi kama watanzania, wana jamii, wanasiasa, wapenda mabadiliko chanya, Great Thinkers, tunasemaje kuhusiana na hili? Na je tatizo letu nini hasa tunashindwa kuwajibika katika nafasi zetu pale ambapo tumetenda kinyume na malengo tuliyojiwekea? Karibuni!
 
Katika gazeti la Tanzania daima toleo la leo uk wa 6, kuna taarifa kwamba Waziri mkuu wa Japani(Bwana Aso) amevunja bunge la Nchi. Sababu kubwa iliyopelekea bunge hilo kuvunjwa ni kushindwa kutimiza malengo na ahadi zilizotolewa wakati wa kuomba kura. Waziri huyo anaendelea kusema, anaomba radhi kwa kufanya hivyo, lakini kwa bahati mbaya wabunge wameshindwa kutimiza malengo waliojiwekea. "Ingawa tumepata ushirikiana mzuri kutoka kwa chama na wadau wetu wengine kwenye chaguzi zetu, lakini tumeshindwa kufikia malengo yetu ya msingi tuliyojiwekea," alisema waziri huyo, kupitia hotuba yake aliyoitoa katika televisheni....
Ndugu zangu wanajf, hebu tujadili sisi kama watanzania, wana jamii, wanasiasa, wapenda mabadiliko chanya, Great Thinkers, tunasemaje kuhusiana na hili? Na je tatizo letu nini hasa tunashindwa kuwajibika katika nafasi zetu pale ambapo tumetenda kinyume na malengo tuliyojiwekea? Karibuni!

Bwana Kyachakiche,

Unajua tabia haina dawa,ni kama rangi ya ngozi !

Sisi Hatuna uchungu na nchi kabisa!

Nitaenda mbali zaidi kwa kusema ile consciousness labda haikuwekwa

"kimaumbile" katika miili yetu.

No more!
 
Tatizo letu tunapractise kitu kinachoitwa "everyman for himself policy" yaani faidika wewe na familia yako. Nobody gives a damn about what happens to the nation
 
Tutakapofikia kuwa na tume huru, ambayo haitoingiliwa na yeyote, hapo tunaweza kusonga mbele. Tatizo ni kuwa CCM wanatufanyia mambo yote mabaya kwa kujua wakirudi tena kuomba kura watashinda, iwe kwa kutumia uelewa mdogo ama umasikini wa wapiga kura, ama kwa kutumia tume ya uchaguzi na sheria zake kushinda. Tuna safari ndefu katika kuikomboa nchi yetu, waliowekwa kulinda katiba ndio wanaitumia vibaya madaraka yao kukaa madarakani milele japo hawatakiwi.
 
Bwana Kyachakiche,

Unajua tabia haina dawa,ni kama rangi ya ngozi !

Sisi Hatuna uchungu na nchi kabisa!

Nitaenda mbali zaidi kwa kusema ile consciousness labda haikuwekwa

"kimaumbile" katika miili yetu.

No more!
Mkuu umetoa maneno mazito sana hapo juu. Lakini pia naona kama onaonyesha ishara ya kukata tamaa. Na hakuna kitu kibaya kama kukata tamaa. Sasa ni nini kifanyike kuchochea uchungu wa nchi yetu? Je tumrudie muumba wetu tukimwomba atuwekee mang'amuzi wa kweli kwenye maumbile yetu kama unavyosema? Uwajibikaji uko wapi?
 
Tatizo letu tunapractise kitu kinachoitwa "everyman for himself policy" yaani faidika wewe na familia yako. Nobody gives a damn about what happens to the nation
Tuko pamoja mkuu, ingawa hivyo, wengi wetu tunaelewa kama ambavyo umesema, sasa kwanini hawabadiliki? Ni kwanini hatujifunzi kutokana na makosa?
 
Tutakapofikia kuwa na tume huru, ambayo haitoingiliwa na yeyote, hapo tunaweza kusonga mbele. Tatizo ni kuwa CCM wanatufanyia mambo yote mabaya kwa kujua wakirudi tena kuomba kura watashinda, iwe kwa kutumia uelewa mdogo ama umasikini wa wapiga kura, ama kwa kutumia tume ya uchaguzi na sheria zake kushinda. Tuna safari ndefu katika kuikomboa nchi yetu, waliowekwa kulinda katiba ndio wanaitumia vibaya madaraka yao kukaa madarakani milele japo hawatakiwi.
Mfumwa,
Kweli umenena vyema. Lakini Tume au CCM vinaongozwa na binadamu tena Watanzania wenzetu, hizi roho za kutowajibika wanapotenda ndivyo sivyo wamezitoa wapi? Na sisi wengine kwa nini tunawapa kura huku tukijua wazi hawakutenda kama vile walivyotuahidi? Ni nini hasa kinatupumbaza hata tushindwe kuwaadabisha mara warudipo kuomba kura? Je, si uoga wa kinafiki?
 
Kama wewe ni mtanzania kijana, mwenye akili timamu na mwenye mwono wa Tanzania bora ijayo basi kwa sasa lazima uwe na wasiwasi sana. Mimi naamini ni mmojawapo wa watanzania ambao nina wasiwasi sana na wakati ujao. Ninaamini Tanzania ya leo ina tatizo kubwa la watu wazima ambao Tanzania ijayo wengi hawatakuwepo basi wameamua wasiijali nchi ya baadaye. Wameamua kukifunza kizazi cha leo cha vijana kuwa kila kitu ni siasa na utaalamu wowote ule kutoka katika taasisi za kielimu si lolote wala chochote katika kutenda kazi.

Siasa imefanywa ndio egemeo kuu la utendaji katika maamuzi yote ya kiserikali. Naamini kuwa nchi yoyote ile inaongozwa kwa kuegemea sera na ilani ya chama cha kisiasa ambacho kina hatamu za kuongoza nchi hiyo. Lakini ni wazi kuwa sera hizo za chama na ilani ya uchaguzi ni vyema iendane na kanuni za kiutawala ambazo kimsingi zinazingatia hatua mbalimbali za kiuweledi katika utekelezaji.

Kwa nchi yetu ya Tanzania siasa imefanywa ndio ngao kuu ya maamuzi na hata utendaji wa viongozi na hata wananchi katika ngazi mbalimbali za kiutawala kuanzia Kata hadi Taifa. Tumefikia mahali ambapo haipendezi kabisa ambapo viongozi wetu wakuu wa nchi wameamua kufanya kuwa nchi yetu ni ya Chama kimoja. Wananchi wengi kwa kuzingatia uelewa mdogo wa mambo ya haki za kidemokrasia na Mada nzima ya Demokrasia basi wananchi wengi wamebaki wakidhani nchi yetu ni ile ile ya kabla ya mwaka 1992.

Kuna mambo kibao ambayo yanatia kichefuchefu katika nchi hii inavyotawaliwa. Nikiwa kama kijana bado tangu nimeanza kukua sijaona kizazi kipya cha viongozi. Sioni tofauti ya mitizamo ya akina Kingunge, Nyerere, Kawawa, Mwinyi, Mkapa na hata Kikwete ingawa hawa wote wametawala katika enzi tofauti. Ni jambo la kusikitisha sana hadi leo bado Tanzania tangu awamu ya kwanza haijapata kiongozi mwenye mitizamo mipya ambayo itasaidia kuleta mabadiliko ya kifikra kwa wananchi na viongozi. Bado wataalam, wasomi wetu hapa nchini wanaweka mbele zaidi maslahi ya Chama tawala katika maamuzi yao. Ni wazi inajionesha kuwa watanzania wengi wanaamini vyeo walivyonavyo ni zawadi ya kukitumikia chama badala ya kutumikia kwa kufuata utashi wao wa kimaadili.

Wanasiasa wote badala ya kuhangaikia maendeleo ya wananchi wao wamebaki kutunishia misuli watendaji wa serikali kutenda kwa kuzingatia maslahi ya chama bila kuzingatia matokeo ya matendo yao kijamii na kiuchumi.
Ukiitizama Tanzania unashangaa wanasiasa wetu: wabunge na madiwani ambao ndio chachu kuu ya maendeleo yetu wamebakia kupoteza muda wao mwingi kuchafuliana majina miongoni mwao huku wafuasi wao wakiwaona kama mashujaa pale wanapowashinda wenzao. Utafikiri wananchi waliwatuma kwenda kuchafua majina ya wapinzani wao; lakini la kushangaza wanapofanikiwa kuwachafua wenzao basi wanakuwa ni mashujaa kwa wananchi wao. Nchi imekwisha ninapoyaona haya.

Urithi ambao vijana wa Taifa la leo wanaachiwa na wazee wao kwa bahati mbaya kama haturekebishi mwenendo wa kitaifa, tutaendelea kushuhudia ukichaa wa kisiasa wa kila hali unaofanywa na wengi wa wanasiasa wetu kwa sasa hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi. Nikiitizama nchi yetu tuna viongozi kedekede waliofilisika kimtizamo. Hebu tutizame jinsi ambavyo kiasi kikubwa cha rasilimali za kitaifa kinavyotumika hovyo kwa maslahi ya kisiasa badala ya mambo ya kimsingi kama vile usalama, vita dhidi ya umasikini na maendeleo hasa ikizingatiwa nusu ya watanzania wanaishi chini ya mstari wa umasikini (poverty line).

VITA DHIDI YA WATUHUMIWA WA RUSHWA

Kama kuna kitu kinachogharimu maendeleo ya nchi zote za watu weusi ulimwenguni ni rushwa na ufisadi. Ukiitizama Tanzania ya leo inatia kichefuchefu. Bunge letu ambalo limemaliza kikao chake cha bajeti hivi karibuni ni chombo ambacho kinategemewa sana katika vita hii achilia mbali taasisi kama Takukuru.

Nimetizama na kufuatilia jinsi wabunge wengi wanaotoka katika chama tawala walivyoonesha hisia zao juu ya kashfa za akina Mkapa inashangaza sana kuona watu wazima, wasomi na waelewa jinsi walivyojitahidi kumtetea huyu mzee wetu licha ya mazuri aliyowahi kuifanyia nchi yetu asikumbane na vyombo vya sheria dhidi ya tuhuma alizofanya akiwa Ikulu.

Ukiitizama ripoti ya kashfa ya Richmond iliyowasilishwa bungeni na jinsi ilivyopokelewa na wabunge wetu kimya kimya kwa stahili ya funika kombe mwanaharamu apite basi unapata tafsiri rasmi ya nini maana ya mwanasiasa: “ Ni mtu yeyote aliyeamua kwa utashi na makusudi kujiunga na kikundi cha watu wenye nia ya kutetea mambo yote mazuri na hata mabaya ilimradi anafaidika nayo bila kujali maslahi ya wananchi anaowawakilisha”. Kwa maana nyingine ninaamini nchi yetu imetekwa na kikundi cha watu ambao wanaitafuna hii nchi watakavyo kwani wanajua vyombo ama taasisi zote nyeti za nchi ziko mikononi mwao. Si ajabu nikisema kwa sasa Tanzania inakaribia ama inaweza kufananishwa na mifumo ya “kimafia”. Kuna kila dalili za umafia miongoni mwa wanasiasa wetu.

Kwanini nasema hivi? Mosi, ni wazi kuna watu walishiriki katika wizi mkubwa kama wa Kagoda, EPA, Deep Green, Meremeta na wizi mwingine ambao tutaujua hapo mwakani wakati wa kampeni lakini watu hao hawakamatwi, hawahojiwi wala kutetemeshwa na kelele za wanaharakati na wabunge wachache wenye kujua nini maana stahili ya kuwa mwanasiasa. Hawaguswi kwa sababu, katika taasisi ambazo zina wajibu wa kuwakamata wamehakikisha wameweka watu wao kuziongoza taasisi hizo.

Na si hilo tu, bali pia kwa vile tayari wameshazoesha mfumo Fulani wa utawala kwa kuwapa watu vyeo na kuwaaminisha wenye vyeo kuwa hiyo ni zawadi ya chama basi wanajua mtaalam yeyote atatenda si kwa matakwa ya kiuweledi kwa kuzingatia mahitaji ya taaluma bali maslahi ya kisiasa ya chama. Hii ndiyo hatari kuu ambapo sasa nchi inaongozwa na utashi wa kisiasa na kuweka pembeni utaalam.

Ukitaka kujua bunge letu si taasisi makini hebu jikumbushe hivi majuzi wakati wa hoja ya Mfuko wa Jimbo” (CDF). Wabunge wote wanang’ang’ania mfuko wa jimbo; kwangu si vibaya ila siamini kama ni kweli miongoni mwao wana utashi wa dhati kupeleka fedha hizo katika majimbo yao kama si kufaidi mfuko huo. Ninatatizwa kidogo hapa:

Kwa mfano, kama kupeleka mfuko wa Jimbo ni muhimu kwa maendeleo ya watu kwanini wasing’ang’anie kiasi cha fedha ambacho kingepelekwa kupitia mfuko huo basi kipelekwe kama nyongeza ya bajeti ya wilaya na majimbo wanakotoka na maadam wanahusika katika vikao vya Halmashauri zao basi hapo ndipo ushawishi wao uonekane badala ya kung’ang’ania fedha utadhani hawana imani na mifumo ya kiserikali ambayo wao ndio wasimamizi wakuu katika majimbo na halmashauri zao. Na kama wanashindwa kushawishi na kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya Halmashauri ikizingatiwa wao ndio watunga sheria, je ni vipi tuwaamini kuwa wabunge wataweza kusimamia CDF kwa ufanisi wa dhati? Hivi wajibu wa mbunge ni kugawa mafedha kwa wananchi? Je kuna haja ya Mbunge kuwa ndiye kinara wa kukabidhiwa fedha? Ina maana wabunge wameshindwa kuwa na ushawishi wa dhati kuwashawishi wataalam katika Halmashauri zao hadi waone kuna haja ya kupewa fedha wao wenyewe ndio tupate tija?

Sipendi mfuko huu uwaendee wabunge kwani naamini ni wachache sana watakaozitumia fedha hizi bila kuweka utashi binafsi. Napendekeza wananchi wafungue kesi mahakamani tupate ufafanuzi kama kidemokrasia ni sahihi kwa Mfuko wa CDF. Lakini pia niulize kwanini hili jambo likaja leo wakati wa uchaguzi? Ni wazi ni kielelezo kingine kuwa siasa ndio jambo la msingi tunalowaza kuliko kingine chochote kile katika akili zetu wabunge. Nchi imekwisha na sijui ni urithi gani akina baba na mama wa leo bungeni mnawaachia vijana wa Taifa hili.

VIONGOZI WA KIDINI

Tuwaache wabunge kidogo twende kwa viongozi wa dini: hawa nao wamekuwa ni watu wa kuheshimiwa sana katika jamii. Tangu ninakuwa hadi umri wangu wa utu uzima, hawa wamekuwa ni watu nilioamini ni watu wasioyumbishwa (very objectives) na wasioegemea misimamo ya kisiasa (non partisan). Viongozi wa dini walikuwa ndio tegemezi wa busara kwa wananchi na hata viongozi pale mambo yanapokwenda kombo nchini. Leo hii hali si hivyo tena; sina maana kuwa viongozi wa dini wa kale walikuwa hawafanyi makosa, ila ni mara chache sana ungeona viongozi wa dini wakitoa matamko ama wakijihusisha na siasa kama ilivyo sasa. Mfano, “Mteule Fulani wa uongozi kuitwa ni chaguo la Mungu” inakinzana na weledi wa kiongozi wa kidini.

Viongozi wa dini walikuwa wakichukua uangalifu wa kina katika kutoa matamshi ama kufanya maamuzi yeyote ya kijamii. Walikuwa tayari kukemea maovu ya kijamii yanapojitokeza; lakini leo hii sivyo kabisa, viongozi wa dini wamekuwa ndio maswahiba wakuu wa viongozi wetu. Mwanasiasa anapata kashfa, kiongozi wa dini anahusika katika kuongoza mkutano mkubwa wa hadhara kumpa pole ama kumpongeza; hii ni kama vile kiongozi wa dini anajaribu kuonesha kukerwa na hatua zilizomfika swahiba wake.

Leo hii viongozi wa dini wamegeuka na wanagombea ubunge na nafasi kadhaa za kisiasa. Mitizamo yao baadhi imejaa mwelekeo wa kisiasa wa chama Fulani cha siasa na mara nyingine kwa kupitia mitizamo ambayo haijafanyiwa utafiti wa kina. Hebu angalia Tanzania ya leo viongozi wa dini wanachezesha mchezo wa Upatau “DECI” wengine wameamua kuwa wabunge kabisa ama wanashiriki siasa. Ni mkanganyiko wa kipekee ambao unaimaliza nchi yetu taratibu.

Hebu tujiulize kwa mfano, hivi kiongozi wa dini ambaye ni mwanasiasa wa chama fulani atawezaje kuwaongoza waumini wake kisahihi (objectively)? Askofu anayeongoza kumpokea kiongozi wa kisiasa kurejea jimboni mwake baada ya kuathiriwa na vita ya ufisadi; je kiongozi huyu anaweza kweli kuwaongoza waumini wake katika kupambana na ufisadi na uoza wa kila aina uliojaa nchini Tanzania?

Pili, kiongozi wa dini ambaye ni muumini na kada wa chama cha siasa Fulani atawezaje kuwa mweledi kimtizamo hasa katika kuwaongoza waumini katika mambo ya kisiasa bila kutekwa na hisia za kiuchama? Hii yote ni political utilitarianism na ndio hapa wazungu wanaita kuwa mambo ya kiimani yanageuzwa kuwa siasa na weledi wote wa kimtizamo (objectivism) yametupiwa mbwa. “thrown to the dogs”.

Mimi ninayeandika makala hii pamoja na wewe utakayesoma wote tumeathirika na gonjwa kuu kitaifa: “tumetawaliwa na siasa”. Ndio maana wachache wa marafiki zetu walio katika nyadhifa wanapata urahisi katika kuliibia taifa letu kupitia “miradi mbalimbali ya maendeleo”. Kwa mfano, hatuna tabia ya kuhoji wala kuuliza: “Kwanini miradi mingi ya maendeleo, hata huu wa Mfuko wa Jimbo, inaanzishwa mara nyingi kipindi cha karibu na uchaguzi? Tunasubiri tu kipindi cha kampeni ndipo tuwe na miradi kibao ikitekelezwa utadhani ndio utaratibu.

Na ndio maana wakati wa kampeni tunadiriki kuhudhuria mikutano ya kampeni ya watuhumiwa wa ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi bila woga. Kutokana na umbumbu wa wengi wetu, hatuchoki kusikiliza hotuba za mafisadi zikitufunza juu ya uwazi, ukweli, demokrasia, utawala bora. Haishangazi tunawaona mafisadi kama ndio mfano bora katika masuala ya uongozi.

Watanzania kwa ujumla wengi tunapenda kufanya mambo kwa mizengwe. Hatujali kanuni na ukijali kanuni wengi wetu tunachukia sana. Hii kukumbatia mizengwe ya kisiasa katika kila jambo la maendeleo ndio chanzo cha kuirudisha nchi yetu nyuma kila kukicha. Tunahitaji kufikiri zaidi ya ukichaa tunaouishi leo hii na tuamue kukataa kuburuzwa na mafisadi wa kisiasa na kidini.

Huu ni wakati wa kutaka viongozi wawazi, na kuachana na siasa za kipumbavu zinazobeza weledi na kung’ang’ania maslahi ya chama badala ya maslahi ya umma. Tukiweza hili basi tutafanikisha demokrasia ya kweli na mafanikio ya kiuchumi kwenye jamii imara. Pasipo hili, basi umasikini utaendelea hadi kiama chetu kwa demokrasia gagari tukidhani ndio maendeleo.
 
Jamii inapoamua kubadilika na kukua kimaadili , naamini kila kitu kitakuwa sawa kuanzia viongozi wao , watoto wao , wafanyakazi na wengine wengi waliozunguka katika jamii hizo , lakini jamii isipoamua kubadilika na kukua kimaadili basi viongozi wao , watoto wao na wafanyakazi wataumi vibaya kama sasa hivi jamii ya kitanzania inapoelekea
……………………………………………………………………………………………………………………………
wakati Fulani niliwahi kuwa kariakoo katika shuguli zangu tu , ghafla nikaona watu wengi wanamtoa kijana mmoja dukani wakaanza kumpiga mpaka walipomfikisha kati kati ya barabara , askari wa jiji walivyoona wakaenda kuamulia kumtoa Yule kijana asiendelee kupigwa tena , mara wengine wakaanza kuwazingira wale askari wajiji wamtoa Yule kijana waendelee kumpiga zaidi wale askari wakajitahidi kumwingiza kwenye daladala moja dereva akaendesha kasi akaondoka .
hiyo ilikuwa ni kariakoo uhuru ni sehemu ya watu wengi ile mtu anapigwa kwa zaidi ya dakika 10 hakuna askari kanzu au wenye uniform aliyefika eneo hilo wakati kituo cha polisi kiko msimbazi tu kama Yule kijana asingeokolewa angeuwawa na vijana wale wanaoitwa raia wenye hasira .
katika vyombo kadhaa vya habari tunasikia na kusoma habari nyingi siku za karibuni kwa watu kuamua kuchukuwa sheria mkononi kupiga na wakati mwingine kuuwa raia wenzao hata kama ni wezi wamewaibia kwanini wasifikichwe katika vyombo vya sheria na vidhibiti ili waweze kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria ?
kuna baadhi ya raia wanadiriki kusema kwamba wakipelekwa katika vituo vya polisi basi baada ya muda kadhaa utawaona mitaani wanadunda wanaamini polisi hakuna sheria bora waamue wenyewe kuwamaliza , sasa huyo mtuhumiwa ataendeleaje kukaa kituoni kama mlivyompeleka hakukuwa hata na ushahidi chembe au vidhibitisho vingine kuhusu uhalifu huo ?
baadhi ya watu utasikia wameibiwa simu , wamempeleka mtu kituoni kisha hapeleki simu yake iwe kama ushahidi anaondoka nayo inaenda kuibiwa au kupotea tena , wengine hizo simu wanakuwa wamezipata kwa njia ambazo sio halali ni za wizi pia huu ni ukweli kwa asilimia kubwa lakini yeye ndio wakwanza kurusha jiwe kwa mwenzake .
kwa kuwa hii tabia ya raia kujichukulia hatua imeota mizizi katika jamii sasa hivi vyombo vya usalama kwa muda mrefu sana vimeona hali hii ikiendelea vikazembea na kuacha tu sasa hivi raia hao hao wanaweza kuingia mpaka katika vituo vya polisi kumtoa mtuhukiwa na kumwadhibu au kuwaadhibu polisi wenyewe kama ilivyotokea katika mikoa ya mbeya na kagera katika siku za karibuni .
raia wengi wanaofanya uhalifu huu ni wale wasiojua chochote kuhusu mtuhumiwa huyo zaidi ya kusikia tu Fulani wanaitana mwizi au kaniibia na kuamua kutekeleza adhabu hizi .
sasa ni wakati kwa jeshi la polisi na vyombo vya usalama kuhakikisha vinadhibiti hali hii na kiongozi yeyote wa mtaa ambaye itadhibitika raia amefia mtaani kwake au kupigwa kiongozi huyo awe na dhamana kuhusu tukio hilo kama ameuwawa raia huyo kiongozi huyo ashitakiwe yeye pamoja na wenzake waliopewa dhamana ya kulinda maslahi ya eneo husika .
jeshi la polisi nalo inabidi lijipange vizuri na kupokea taarifa kuhusu watu hawa wanaoendeleza wimbi hili la mauaji dhidi ya raia wenzao au ufanyaji wowote wa fujo watakaokamatwa kwa makosa hayo wasipewa dhamana wanatakiwa kupewa vifungo virefu na adhabu kali .
jamii nayo kuanzia baba , mtoto na jirani wajue wajibu wao wa kulinda amani katika maeneo yao hata maeneo ya jirani au sehemu za makazi na shuleni , watoto wafundishwe adabu na kuheshimu haki za wengine haswa zinazohusu maisha na amani kama wengine wanavyoishi vizuri katika nchi zingine .
 
Niko tofauti kidogo. Tatizo sio jamii ni Jeshi la Polisi Mkulu nitakupa sababu, asilimia kubwa ya kesi nyingi zinazopelekwa Polisi hazifanyiwi kazi kwa madai kwamba polisi hawana vitendea kazi, Kesi za kusingiziwa, Rushwa, Unyanyasaji, pamoja na kuwa na mitandao ya ujambazi. Leo hii jiulize kwanini Polisi wanatengwa na jamii? Polisi sio rafiki yako. Chukulia kwa mfano waalimu, wamachinga na watu wa tabaka la chini wakilalamika kudai haki zao ni polisi hao hao kupitia FFU ndio wanawahukumu kwa kuwapiga kwa marungu mpaka wengine wanajifungua bila kupenda. Wewe unayesema Polisi analinda amani ni mwongo. Polisi analinda mfumo wa chama tawala pamoja na wale walio madarakani.

Polisi hawana lolote na kamwe siwezi kukubaliana na hoja egemezi kwani Polisi ndio wameifanya jamii iwe na kiburi kwa kujichukulia sheria mikononi. Kama Polisi wakijisafisha basi na jamii nayo itakuwa tayari kuwaunga mkono.

Kama kutakuwa na Utawala wa Sheria basi na jamii nayo itawaunga mkono Polisi, Kama Polisi wakiunga mkono vita dhidi ya ufisadi basi jamii nayo itawaunga mkono, kama Polisi itatambua haki na wajibu wa raia kwa vitendo basi jamii itawaunga mkono, Kama Polisi atapiga vita rushwa basi jamii itawaunga mkono, Kama polisi wataacha kuwatetea tabaka tawala na dhalimu pamoja na madhambi yao basi hakuna shaka jamii itawaunga mkono.

Lakini kwa sasa waache wafe kwani nao wanaua raia wasiokuwa na hatia na wanawatetea mafisadi pamoja na kuwabeba na ving'ora huku wananchi wakifa maskini. Watajifunza na kupata akili wawaone wenzao wa Phillipines walivyowaunga wananchi mkono mpaka Estrada akaachia madaraka.
 
Back
Top Bottom