Tanzania limekuwa taifa la wacheza kamari (Tanbet)

tpaul

JF-Expert Member
Feb 3, 2008
21,856
18,271
Naingia kwenye mada moja kwa moja pasipo kuwachosha. Inasikitisha kuona kwamba nguvukazi ya taifa inapotea bure kwa kujikita kwenye uchezaji wa kamari. Kwa utafiti mdogo nilioufanya, kamari imekita mizizi kila mahali. Mara nyingi watu wanapobishana kuhusu jambo fulani utawasikia wakiwekeana dau (kamari). Hiki ni kiashiria kuwa kamari imeingia damuni mwa kila mtanzania.

Redio zote nchini Tanzania, ikiwemo TBC, wanachezesha kamari, na nyingine huchezesha kwa saa 24 na kutoa matokeo kila baada ya nusu saa. Tunajenga taifa la wacheza kamari kwa lazima kisa tu serikali inapata mapato. Kibaya zaidi na serikali inaweka mkazo kwenye kamari kuliko kutafuta mbinu mbadala za kujenga ajira kwa vijana ili kuokoa taifa linalotopea kwenye uraibu wa kamari.

1687447095711.png

Kijana aliyelemewa na uraibu wa kamari (Chanzo: JamiiForums Facebook page)

Niliwahi kutembelea kijiji kimoja ambako wizi wa mazao, mifugo na mali umeshamiri kwa kiasi kikubwa. Nilipofanya utafiti nikagundua chanzo cha wizi ni vijana ambao huiba mali za wananchi ili wapate fedha za kuchezea kamari. Tunajenga taifa la namna gani? Wallah miaka michache ijayo hata serikali nayo itaanza kucheza kamari kwa kutumia kodi za wananchi!

Katika hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24, jedwali namba tano linaonyesha mgawanyo wa bajeti kisekta. Sehemu inayoonyesha "Maendeleo ya Uchumi", utaona kuwa Vijana, Kazi na Maendeleo ya Kukuza Ujuzi, fedha ambazo zimetengwa ni Sh20.3 bilioni. Zikiwa zimepungua kutoka Sh31.2 bilioni, mwaka wa fedha unaoishia, yaani 2022-2023.

Taarifa hiyo itakushitua mno ukisoma ripoti ya uchumi wa michezo ya kubahatisha Tanzania. Mwaka wa fedha 2018-2019, mapato ya michezo ya kubahatisha yalikuwa Sh96 bilioni, yakiwa yamepanda kutoka Sh78 bilioni mwaka uliotangulia. Hiyo ni ripoti ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Mtandao wa utafiti na takwimu za kibiashara kwenye tasnia mbalimbali duniani, Statista Market Forecast, inaeleza kuwa mapato ya michezo ya kubahatisha Tanzania mwaka 2023 yanatarajiwa kufikia dola 75.09 milioni (Sh180 bilioni).

Kwa mujibu wa Statista, thamani ya soko la michezo ya kubahatisha Tanzania itakuwa dola 110.1 milioni (Sh260.4 bilioni), ifikapo mwaka 2027. Hali ikiwa hivyo, Serikali inapunguza fedha kwenye eneo la upishi wa vijana kuwa wataalamu.

Ukisoma Sheria ya Michezo ya Kubahatisha Sura ya 41 utaona kuwa mkazo mkubwa kwa sasa ni serikali kukusanya mapato kwenye michezo ya kubahatisha. Na pia serikali inakwenda kupunguza maumivu kwa wachezesha kamari kwa kuwapa punguzo la kodi kwenye mapato ghafi kutoka asilimia 25 hadi asilimia 18. Hapa maana yake waendeshaji wa kamari wataona ahueni zaidi. Hivyo, tutarajie makampuni yanayochezesha kamari kuongezeka hapa nchini.

Ukiachana na bajeti kuu ya Serikali, Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Fedha 2023-2024 inaonesha kuwa hadi Aprili 2023 Bodi ya Michezo ya Kubahatisha ilishatoa leseni 8,778 za michezo ya kamari. Hii ni sawa na asilimia 114 ya malengo. Mwaka ujao wa fedha leseni mpya 11,880 zitatolewa.

Ufafanuzi huo unamaanisha kuwa mkazo wa kukuza sekta ya kamari ni mkubwa na wakati huohuo uwekezaji kwa vijana ni mdogo. Maneno ni mengi kuanzia nyumba za ibada hadi kwa wapinzani kwamba vijana wasiwe waraibu wa kamari badala yake wafanye kazi za vipato.

Kamari au michezo ya kubahatisha, kama ilivyo jina lake, inapaswa kuchukuliwa kama michezo ya kujaribu bahati na kujifurahisha. Hivi sasa vijana wengi, tena siku hizi hadi wazee, wamegeuza michezo ya kubahatisha kuwa vyanzo vya mapato.

1687446563570.png

Vijana wakicheza kamari katika kituo cha kuchezea kamari (Chanzo: Mtandao)

Serikali kwa kutambua hilo inapaswa kuwekeza vizuri kwenye eneo la vijana kwa kuwajengea ujuzi na uwezo waweze kujiajiri au kuajiriwa. Wimbi la vijana kuona michezo ya kubahatisha ni fursa za kimaisha, hadi kuwa mateja wa kamari, ni matokeo ya kukosa machaguo (options) ya kimaisha.

Mzunguko wa kifedha kwenye michezo ya kubahatisha, unashawishi vijana kuuona utajiri wa ghafla bin vuu kwa kucheza kamari. Bajeti inayoombwa kwa ajili ya Wizara ya Madini kwa mwaka ujao wa fedha ni Sh89 bilioni. Maana yake inazidiwa mbali na mapato ya michezo ya kubahatisha.

Rejea matarajio ya mapato ya michezo ya kamari kuwa Sh260 bilioni ifikapo mwaka 2027 halafu pitia fungu la Biashara na Viwanda kuwa Sh324.2 bilioni. Je, huoni dalili za michezo ya kubahatisha kuelekea kushindana na sekta nyeti ya Viwanda na Biashara?

USHAURI
Baada ya uchambuzi kuhusu sekta ya kamari na kuonyesha jinsi inavyochochewa na serikali, naishauri serikali iache mara moja kuharibu watoto (na wazee) wa watu kwa kuwajengea uraibu wa kamari. Badala yake serikali itafute fursa za ajira kwa vijana ili waache kucheza kamari wafanye kazi halali zenye staha zitakazowaingizia kipato halali.

Nafahamu watoto wa watunga sera hawahusiki kwenye uraibu wa kamari. Watoto wa wanasiasa wanakula maisha mazuri huko waliko. Ni watoto wa walalahoi tu ndio wamejikita kwenye kamari. Ipo haja ya kuwaonea huruma wapiga kura hawa kwa kuwa ndio wanaowaingiza madarakani. Nafahamu wanawaacha wapiga kura wapigike ili iwe rahisi kuwatumia kisiasa kupitia umaskii na kupigika kwao lakini yapaswa watambue kwamba Mungu anawaona. Hata kama hawawaogopi wanadamu, basi wamuogope Mungu.

Nawasilisha
 

Attachments

  • 1687446791530.png
    1687446791530.png
    27.3 KB · Views: 25
kwakweli hili tama mimi nilkuwa naliwaza mnoo. yaani tbc redios mdq wote wanahimiza kamali badala ya kuhimiza watu wafanye kazi. inakera mnoo mnoo. viongozi ebu mwambie huyo mkurugenzi wa tbc kama hawezi kazi aondoke mara moja mjinga mmoja tu. tunajenga taifa gani hili?
 
Watu wanataka pesa bro,kama huko kwenye KAMARI ndiko kunahela wameamua kuzifata huko.

Pesa yake,Muda wake na akipoteza amepoteza chake sasa wewe unaumia na nini?

Wewe hutaki kucheza nenda kalime mazao ili uje uwauzie wacheza kamali kwa bei kubwa,hayo ndiyo maisha!.,Usitake kila mtu afanye ambacho wewe unataka wakati kila mtu kaumbwa na uhuru wa nafsi na dhamiri!.Ukiona Vijana wanapoteza muda kwenye kubeti wewe pita kimya kimya nenda kafanye kazi kwa juhudi ili ujipatie maendeleo yako naya kizazi chako!.

Kubeti hakujaanza leo mkuu,kulikuwepo tangu enzi hizo,hivyo waache walioamua kubeti wabeti na wewe kama hubeti hayo ni maisha yako!.

Kila mtu afanye kile anachodhani kwake kitampa maisha na faraja ilimradi tu usimkwaze mwingine na kuvunja sheria.

Kubeti siyo biashara haramu kiasi kwamba uipigie kelele,zipo biashara haramu ambazo zinawaingizia watanzania mabilioni ya pesa lakini sijaona unapigia kelele,siku betting ikiwa biashara haramu ndiyo inapaswa upaze sauti,lakini kama ni halali kwa sheria zetu waache watu wajinafasi.

Kila mtu atavuna alichopanda,kama wao wamepanda mbegu ya betting basi watavuna betting,na wewe kama umepanda kutobetting basi utavuna kuto betting!.

Kila mtu afanye kinachomhakikishia unafuu wa maisha,hivyo usidhani wanao beti ni wajinga kwasababu ukidhani hivyo na wao pia wanakuona wewe usiye beti ni mjinga wa kwanza duaniani!.
 
Back
Top Bottom