3:50:45 AM Yaliyopita Pekua Tovuti
Sitta: Hatujaolewa EAC
ASEMA WATAWAMWAGA KAGAME,
MUSEVENI, KENYATA
na Salehe Mohamed, Dodoma
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, amesema Tanzania itatoa talaka
kwa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambazo
zimeamua kuanzisha Jumuiya ya hiari nje ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sitta alisema kutokana na nchi hizo kuonekana
kuitenga Tanzania na Burundi ambazo ni
wanachama wa jumuiya hiyo, wameshaanza
mazungumzo ya kushirikiana kiuchumi, kisiasa
na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Watu wa Congo (DRC).
Kauli hiyo ya Sitta inatokana na mikutano ya
mara kwa mara inayofanywa na marais Uhuru
Kenyata wa Kenya, Paul Kagame (Rwanda) na
Yoweri Museveni (Uganda) kuzungumzia
masuala mbalimbali ya kushirikiana nje ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Waziri Sitta alibainisha msimamo wa Tanzania
kutengwa na nchi hizo tatu jana bungeni,
alipokuwa akijibu maswali ya wabunge
mbalimbali waliokuwa wakitaka kujua kauli ya
serikali juu ya vikao vinavyofanywa na marais
hao watatu.
Mbunge wa Viti Maalumu Rukia Ahmed (CCM),
aliitaka serikali ipeleke pendekezo bungeni la
kujitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
kabla haijapewa talaka kutoka kwa Rwanda,
Uganda na Kenya ambazo zimekuwa zikifanya
mikutano inayojadili masuala ya jumuiya bila
kuihusisha serikali ya Tanzania.
Akijibu hoja hiyo Sitta, alisema ni mapema kwa
Tanzania kupeleka bungeni hoja ya kujitoa
katika jumuiya hiyo kwa kuwa kinachofanywa
na nchi hizo kimeshafikishwa kwa Mwenyekiti
wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama
ambaye atakitolea ufafanuzi katika kikao
kitakachofanyika wiki mbili zijazo.
Sitta alifafanua kauli ya Waziri mwenzake wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, hivi karibuni ya kwamba
Tanzania inasubiri talaka akisema yenyewe
ndiyo yenye uwezo wa kutoa talaka kwa
jumuiya hiyo kwa kuwa inamiliki asilimia 52 ya
eneo lote huku nchi zilizobakia zikigawana
asilimia 48 iliyobakia.
Hawa wenzetu wanafanya utoto wa
kutuzunguka, sisi tunatumia hekima za mzee
Mwinyi aliyesema mwongo, mwongoze. Kama
wao wana hila zozote juu yetu, siku si nyingi
tutazibaini, kama ni ndoa kwenye jumuiya basi
sisi ndio tutakuwa tumeoa
hivyo tutatoa talaka
wakati wowote, alisema.
Naye Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango
Malecela (CCM), aliitaka serikali isiendelee na
hatua zozote kwenye jumuiya hiyo ambayo
inaonekana kuelekea kuvunjika.
Akijibu swali hilo, Sitta alisema serikali haijakaa
kimya bali imeamua kutoshiriki vikao vyote
ambavyo nchi za Kenya, Rwanda na Uganda
zitakuwa zimeshayazungumzia masuala husika
na kuamua kuwa na msimamo wa pamoja nje
ya jumuiya.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed
(CUF), alihoji serikali inangoja utafiti gani juu
ya kutengwa kwao kiuchumi na nchi hizo tatu
wakati Kenya wameshaingia makubaliano ya
kibiashara na Ethiopia na Sudan.
Katika jibu lake, Sitta alisema Tanzania
imeshafanya mazungumzo na nchi za DRC na
Burundi kushirikiana katika nyanja mbalimbali.
Alisema kuwa DRC ndiyo yenye manufaa
makubwa kiuchumi kwa Tanzania kuliko
Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi kwa sababu
mizigo mingi hutegemea bandari ya Dar es
Salaam.
Burundi nao wanatengwa kama
tunavyofanyiwa sisi, lakini tumeamua
kushirikiana kikamilifu na DRC pamoja na
Burundi ambao tuna imani wana manufaa
makubwa kwetu, alisema.
Hivi karibuni Tanzania iliingia kwenye mgogoro
na Rwanda baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa
ushauri kwa Rais wa Rwanda, Kagame kuketi
chini na waasi wa nchi hiyo ili kuzungumzia
masuala ya amani kwa nchi yao.