Mzee Kitila Mkumbo, heshima yako Mkuu.
Napenda kutofautiana na wewe kidogo. Binafsi nadhani kinachoiweka nchi yetu katika ukingo wa shimo la giza, sio CCM, bali ni watu wanaojiita CCM. Hivyo, yatupasa kuwa makini, ama sivyo tutaishia kwenye bottomless pit of oblivion. Ukiiondoa CCM, alafu watu wanaojiita CCM wakabaki madarakani, matatizo yetu yatabaki palepale. Hii mantiki katika hesabu inaitwa commutative law of addition and multiplication. Switching the order of any two numbers being added or multiplied together, does not change the result.
Nathubutu kusema kuwa vyama vya upinzani vya Tanzania vina mkosi. Miaka 50 iliyopita, Ghana ililikuwa nchi ya kwanza katika Afrika kupata uhuru. Hakika Kwame Nkurumah alifurahia sana siku hiyo. Alikaliliwa akisema kuwa, "kwa mara ya kwanza, sisi waafrika tumepata nafasi ya kujiamulia mambo yetu wenyewe". Hakuna shaka kwamba uhuru wa Ghana ulihamasisha wananchi wengi wa bara la Afrika. Kumbuka, wakati ule, wananchi wengi hawakuwa na elimu ya uraia, na pia walikuwa hawajasoma. Lakini wakoloni walikiona cha mtema kuni.
Bila shaka, maneno ya Nkurumah yaliingia doa, kwani toka wakati wa ukoloni, mpaka leo hii, wananchi wa Afrika hawajawahi kupata nafasi ya kujiamulia mambo yao wenyewe. Maamuzi ya mambo ya Afrika yamekuwa yakifanywa na makundi ya watu wachache. Kwa baadhi ya viongozi, na tena mara chache, baadhi ya maamuzi, wakati mwingine yamekuwa kwa manufaa ya wananchi, wakati mwingine kwa manufaa ya wachache (mfano;Tanzania). Na kwa viongozi wa mapinduzi ya Afrika waliowengi, maamuzi yote yalikuwa yakifanywa na makundi ya watu wachache kwa manufaa ya wachache (mfano;Zaire).
Vita baridi kati ya Marekani na Urusi, ilichangia kuchafua hewa katika bara la Afrika. Lakini ukweli ni kuwa viongozi wengi wa mapinduzi katika Afrika waliwaacha wananchi kwenye mataa. Wananchi walishiriki kikamilifu katika kudai uhuru wa nchi zao. Bila wananchi kujitoa muhanga, hakuna hata nchi moja ya Afrika ambayo ingepata uhuru. Baada ya walijitambua kuwa viongozi katika hizo harakati kushika kushika hatamu, wakawageuka wananchi kwa kuwanyima uwezo wa kujiamulia mambo yao wenyewe. Viongozi wengi wa mapinduzi, wamechukuwa roho za wananchi wengi waliotaka kudai hiyo haki yao ya msingi (mfano; Uganda -Obote, Malawi-Kamuzu).
Kutokana na msukumo wa ndani na nje ya nchi, Afrika ikashuhudia upepo mwingine mnamo miaka ya tisini. Huu upepo ni wa viongozi wetu wa mageuzi (mfano; Mapalala, Fundikira, Kasanga Tumbo-Tanzania, Chiluba-Zambia, Abdoulaye Wade-Senegal, Bakili Muluzi-Malawi). Wachambuzi wa mambo ya siasa walidiriki kuita haya mageuzi kuwa ni "wind of change". Nadhani walitumaini kuwa historia ingejirudia. Ghana ilivyowahamasisha wananchi wa Afrika kudai uhuru, basi hata chama kimojawapo cha upinzani kikichukuwa madaraka, wananchi wa nchi nyingine wangeiga mfano.
Ndio maana nasema kuwa, labda vyama vya upinzani vya Tanzania vina mkosi. Kwasababu vyama vya upinzani vya nchi nyingine vilivyotangulia kupata madaraka, vimevurunda. Vimefanya kosa lilelile kama walilofanya viongozi wetu wa mapinduzi (akina Nkurumah). Kama ilivyokuwa wakati wa kudai uhuru, wananchi wa hizi nchi walishiriki kikamilifu kuviangusha vyama vilivyoziletea hizo nchi uhuru. (Mfano;Ghana, Senegal, Kenya, Malawi, Zambia). Again, bila wananchi wa hizi nchi kujitoa muhanga, hawa viongozi wa vyama vya upinzani (mageuzi), wasingefika kokote. Lakini waliposhika hatamu, wamewapiga teke wananchi. Wamewanyima nafasi ya kujiamulia mambo yao wenyewe.
Viongozi wa mageuzi wa Tanzania walitamba sana Chiluba aliposhika madaraka. Waliwambia CCM kuwa mwenzio akinyolewa, wewe tia maji. Muda ulivyokwenda, majigambo ya Viongozi wa mageuzi kufifia. Mwishowe, Zambia ikaondolewa kwenye orodha ya nchi za kuigwa. Malawi je? (Akha!) Senegal je? (hao ndio wameluka mkojo na kuanguka kwenye kinyesi). Ghana je? (wanafanana na wanaCCM). Tulitaka kuunganisha vyama tuwe kama Kenya. Lakini siku zinavyozidi kuyoyoma, naona wazo hili linapigwa kaputi.
Satili za kuvurunda katika Afrika zinafanana. Mfano, nchini Kenya, hakukuwa na kitu kinaitwa KANU. Kulikuwepo na watu waliojiita KANU. Katika ule mkumbo wa kuing'oa KANU madarakani, hata wale waliojiita KANU walikuwemo. Matokeo yake, KANU ikang'olewa, lakini wale waliojiita KANu bado wako madarakani. Ndio haohao wanaowafanyia unyama wananchi wa Kenya. Mzee Kitila Mkumbo, wanaotembea kifua mbele sio wananchi wote wa Kenya, bali ni wale walioko madarakani. Ndio maana inakuwa ngumu kwa vyama vya upinzani Tanzania kutoa takwimu za Kenya, Zambia, Senegal ambazo zinaonyesha mabadiliko ya maana ya kile walichokuwa wanapigania kabla ya kuingia madarakani.
Hivyo, vyama vya upinzani Tanzania vimekuwa kama watoto wakiwa. Huu mkosi kwa vyama vyetu vya Tanzania, ni mbaya kwa vyama vyenyewe, unaineemesha CCM, lakini yawezekana ni ishara njema kwa wananchi wa Tanzania. Ni ishara njema kwa maana kuwa, vyama vya upinzani vya nchi yetu vinapata changamoto ya kuangalia hivi vyama vyote vimevurunda wapi? Bima pekee ya kuondoa huu mkosi ni kuruhusu mawazo mapya yapenye, fikra zirutubishwe na fikra nyingine, badala ya kuziacha zikavia na kuzaa watoto taahira kutokana na kujamiiana kwa muda mrefu baina ya fikra zilezile.
Hizi tabia mfu za vyama vya siasa (vyote), kujifanya kuwa wanajua matatizo ya wananchi kuzidi wananchi wenyewe wanavyoyajua zizikwe. Hakuna mbadala wa maoni ya wananchi na utashi wao. Viongozi wote wa vyama vya siasa wanawajibika kuwasikiliza wananchi wanasema nini na kuyatilia maanani hayo yasemwayo na wananchi. Haya mambo ya kungoja siku za uchaguzi na kwenda kuwahutubia wananchi yafe. Tukifanya hivyo, basi tukubali matokeo yake.
Tusiwaite wananchi wajinga eti kwa sababu wameshindwa kutuelewa tulichowaambia na kutuchagua. Tusiwaone wajinga ati kwasababu wanaona CCM wanafanya ulafi na wizi wa mchana, lakini wanashindwa kuwaondoa. Labda kila mtu ana maana tofauti ya ujinga. Kama wananchi wa kizazi hiki ni wajinga, je wale waliomng'oa mkoloni walikuwa na welevu upi? walisoma shule gani wale? Lakini wananchi wa leo wakiwa welevu wakaiondoa CCM wamuweke nani? Na kwa bima ipi?
Tujifunze kukubali matokeo ya matendo yetu. Tusiseme tumeibiwa kura. Unaweza kuwaongopea watu wote kadili unavyotaka. Lakini ukianza kumuongopea "the man in the mirror", unatafuta kiama chako. Conscience is like an open sore, only the truth can heal it. Kama unaweza kuibiwa kura milioni nane na ushee, basi hufai kuongoza nchi. Aliyekuibia hafai, lakini hata wewe hufai. Manake ukipewa nchi itaibiwa kwa ujumla wake.
Mwisho ningependa kuwagawa wananchi wetu katika mafungu ili kujua tatizo liko wapi. Kwasababu ukisema wananchi ni wajinga, ina maana kila mtu Tanzania ni mjinga? Siamini hivyo. Kundi la kwanza ni la Wakulima (90% ya watanzania wote) ni wapenzi wa nchi yao. Lakini mapenzi kwa nchi yao yamechanganyikana na unyonge. Ujinga sio unyonge. Kundi la pili ni la Wabunge (vyama vyote) pamoja na vyama vyao vya siasa. Hili kundi sio wote, lakini wengi wao wanaendekeza mambo ya kipuuzi. Kundi la tatu ni la viongozi (wote). Hawa wanaendekeza mambo ya kipumbavu. Kundi la nne ni la wasomi, na wale ambao bado wanasoma, hata "born town". Hawa ni wajuvi, na wanaendekeza mambo ya ushabiki.
Tukishajigawia vitengo na kujua nafasi zetu katika jamii. Itakuwa rahisi sana kutabiri nini kitatokea mwaka 2010. Note: makundi niliyoyaweka juu simaanishi watu wote wako hivyo. Naongelea kwa ujumla wake.