TANROADS: Bajeti ya 2021/2022 tulitengewa Tsh. Trilioni 1.5 na si Tsh. Trilioni 2.9. Yote imeisha tumika kwenye miradi ya maendeleo

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,810
11,980
Meneja wa Awamu ya tatu ya ujenzi wa mradi wa mwendokasi Jijini Dar es Salaam, Barakael Mmari amesema hadi kufikia mwishoni wa Machi 2023 matengenezo ya mradi huo yalikuwa yamefikia katika asilimia 5 (5%).
41da28de-8887-43b0-aa49-629ec774447c.jpg

Barakael Mmari

Mradi huo una urefu wa Kilometa 23.3 unatekelezwa katika Barabara za Nyerere, Bibi Titi, Azikiwe, Maktaba na Uhuru kutoka katikati ya Jiji la Dar hadi Gongo la Mboto. Amesema ujenzi ulianza Agosti mosi, 2022 na unatarajiwa kukamilika Machi 2024.

Amezungumza hayo wakati uongozi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ulipotembelea na kuangalia maendeleo ya Awamu ya tatu ya ujenzi wa mradi wa mwendokasi Jijini Dar es Salaam unaoendelea, leo Aprili 11, 2023.

Akizungumza kuhusu mradi na uendeshaji wa miradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila amesema “Sisi bajeti yetu kwa Mwaka 2021/22 ilikuwa Tsh. Trilioni 1.5 ambayo ndiyo ilipitishwa na Bunge na tulikuwa tunaitekeleza haikufika Tsh. Trilioni 2.9 kama inavyodaiwa.
7feb0a4c-ca68-4fc3-9af9-02acc41769df.jpg

Mhandisi Rogatus Mativila

“Fedha hizo zimelipwa katika miradi inayoendelea, kumbuka sisi tunalipwa kutokana na mradi unavyoendelea, hivyo malipo yote yametokana na kazi iliyofanyika na kimsingi hiyo fedha haipo, imeshatumika kulipa miradi.”

Akifafanua kuhusu ziara yao hiyo, Mhandisi Mativila amesema “Tumetembelea mradi huu kwa kuwa ni mwendelezo wa kutembelea miradi mbalimbali inayofanywa katika maeneo tofauti nchini.

“Mara kwa mara huwa tunautembelea mradi huu kuona maendeleo, tulipata changamoto kutokana na ‘traffic management’, hivyo moja ya sababu ya kuja kutembelea ni kuangalia jinsi maendeleo yalivyo kwa kuwa changamoto kama hiyo tuliipata sana katika BRT 2 ambayo inakaribia kukamilika.

“Mkandarasi ni yuleyule, tulizungumza naye kabla ya kuanza kwa mradi ili kuona atakabiliana vipi na hiyo changamoto na kweli ameifanyia kazi, ndio maana unaona shughuli za Dar es Salaam hazisimami.

“Maendeleo ni mazuri kwa kuwa yupo kwenye 5% japokuwa mipango ilikuwa iwe 15%.
Injinia.JPG

“Mara nyingi unapoanza mradi huwa kuna le hali ya kujifunza kutokana kutokana na mazingira lakini tayari ameshaongeza vifaa na watu, hivyo atafidia hiyo nafasi iliyojitokeza kwa kuwa atafanya kazi usiku na mchana.”

Aidha, ameongeza kuwa kuna mradi wa BRT 4 ambao upo njiani, pia kuna BRT 5 ambao unatarajiwa kuendeshwa na fedha kutoka Ufaransa.

Kuhusu miradi ambayo ilitekelezwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Mhandisi Mativila amesema “Miradi yote mikubwa huwa inakuwa katika mchakato, miradi ya 2021/22, tulianza na taratibu za manunuzi.

"Unapoanza hivyo inamaanisha mradi umeanza, manunuzi mara nyingi yanachukua miezi minne, sita au mwaka mmoja inategemea na manunuzi yenyewe, hasa kama itatokea changamoto ambayo inaweza kuwarudisha nyuma.

“Mnapofanya manunuzi hayo, maana yake mradi huo utakuja kutekelezwa katika Mwaka wa Fedha ujao, huwezi kukwepa kwenye miradi, ndio maana miradi ambayo iliwekwa katika Mwaka 2021/22 kwenye bajeti inahamia katika Mwaka unaofuata kwa kuwa unauwekewa bajeti kila mwaka.

"Ile ambayo ilianza kufanyiwa utaratibu wa manunuzi maana yake mradi umeshaanza, hadi kufikia hatua ya kuona vumbi linatimka ardhini inakuwa ni mwaka unaofuata.

“Kwa hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 kuna miradi 16 ambayo gharama yake ni Tsh. Trilioni 1.4 na ina urefu wa Kilometa 603, ambayo tulisaini mkataba na inaendelea kutekelezwa.

“Kawaida huwa hatupewi fedha tukakaa nayo, kiasi kinachotangazwa huwa ni makisio, mwaka ukiisha mnaanza bajeti upya, inapangiwa upya, mradi uleule unakuwa na bajeti yake na inaweza kuwa kubwa zaidi ya ilivyokuwa awali kwa kuwa ndio mradi unaanza kutekelezwa na mambo yanakuwa makubwa.

“Miradi ya Mwaka 2020/21 inatekelezwa 2021/22 na ni miradi mingi, mfano kule Arusha kuna Mradi wa Mianzini, Ngaramtoni kwingine ni Katavi, Songea n.k

“Hivyo, Miradi ya Mwaka 2021/22 mingi tumeshaisaini mkataba na inatekelezwa kwenye Mwaka 2022/23.

“Pia tunafahamu Bajeti ya Nchi kuna muda haijitoshelezi, lakini angalau tufanye miradi kadhaa ya kusaidia jamii, bado kuna miradi mikubwa ya nyuma ambayo inaendelea mfano uliopo Kigongo Busisi, hivyo kuna kubalansi na siyo kwamba fedha inapotea.

“Aidha, itambulike kuwa sisi hatuletewi fedha tukakaa nazo, mkandarasi akishaleta certificate ya madai, tunaipeleka Wizarani, Wizara ya fedha inatoa fedha kulingana na ulichozalisha.

“Inakwambia leta unachodai na vielelezo vyake, kama hujafanya kazi hauwezi kupata.”

Kuhusu BRT 2
Mradi huo ulikuwa ukamilike Machi 2023, mpaka sasa umefikia 85% kutokana na changamoto mbalimbali katika mradi zilizotokea siku za nyuma, tunatarajiwa utakamilika Oktoba 2023 na wenzetu wa DART waanze kupitisha mabasi.
 
Back
Top Bottom