Tangulia Lukuga, Dkt. Amani Walid Kabourou - Kinara wa Mageuzi ya Vyama Vingi Nchini. - Mwami Kabuyuki, Mwamba wa Kigoma

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,883
Tangulia Lukuga, Dkt. Amani Walid Kabourou - Kinara wa Mageuzi ya Vyama Vingi Nchini.
- Mwami Kabuyuki, Mwamba wa Kigoma

Asubuhi ya jana, nimeamshwa na simu ya Baba yangu Mzee Kabwe. Sio kawaida yake kunipigia simu asubuhi namna hii, nami nilikuwa nimelala nimejichokea kufuatia kazi za siku ya juzi za kumtembelea diwani wa Chama chetu cha ACT Wazalendo, hapa Kasulu. Licha ya uchovu mkubwa, pia nilichelewa kulala kwa sababu ya Mpira, timu ninayoishabikia nchini Uingereza ya Liverpool ilikuwa inacheza na timu ya FC Porto ya Ureno.

Naitazama simu naiogopa!, simu inakatika! Nikampigia simu baba, ambaye kwa majonzi makubwa akanijulisha kwamba mwamba wa Kigoma hatunao tena! Dkt. Aman Walid Kabourou, mbunge wa kwanza wa jimbo la Kigoma Mjini mara baada ya vyama vingi ametutoka, ametangulia mbele ya haki. Inna lillah waina ilaih raajiun.

Kwa umri wake Dkt. Kabourou ni mjomba wangu , na kwenye siasa yeye ni mlezi wangu. Hivyo wajibu wangu wa kwanza kama mtoto awali ya yote ni kumsitiri mzazi wangu. Baada kupata taarifa hizi za majonzi, nilizungumza na Diwani wetu kule Ujiji, ndugu Fuad Seif wa Kata ya Kasimbu, ambaye ni mkwe wa Dkt. Kabourou, kuhusu mipango ya mazishi. Baadaye nilizungumza na ndugu wa marehemu waliopo Dar es Salaam. Wote walinithibitishia kwamba wosia wa marehemu ni mauti yakimkuta, basi azikwe Ujiji, Kigoma.

Hivyo baada ya kuwa sasa tumeshaandaa taratibu za mazishi yake hapo kesho, nami nimepata wasaa wa kuandika machache juu yake, na hii ni ada kwangu, kuandika tanzia ya kila marehemu anayenigusa binafsi au kuligusa Taifa. Dkt Kabourou ana sifa zote mbili, ananigusa binafsi, na anao mchango mzito kwa Taifa letu, zaidi msiba wake ni jambo zito hapa Kigoma Mjini, mahali ambapo mimi ni mwakilishi wa wananchi.

Hii ni kutokana na mchango mkubwa wa Dkt. Kabourou kwenye ujenzi wa siasa za vyama vingi nchini Tanzania. Yeye ndiye Mbunge wa kwanza nchini kuchaguliwa na wananchi baada ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa nchini 1992!

Yeye ndiye aliyepandikiza mbegu nzuri ya Watanzania kukataa kuburuzwa na kusimamia haki zao, ambapo kupitia kwake mwanga wa ukombozi katika siasa za vyama vingi ulienea kote nchini. Jambo hili alilifanya zaidi hapa Kigoma, kwa maana nyingine, Kigoma ndio mkoa wa kwanza kuonesha kwa vitendo utayari wa kupokea vyama vingi nchini, yote ni kwa sababu ya kazi ya ‘Uamsho’ ya Dkt. Kabourou. Ni mbegu hii ya mageuzi aliyoipanda ndiyo iliyofanya wakati flani Mkoa wote wa Kigoma ukawa na idadi kubwa ya wabunge kutoka vyama vya upinzani.

Dkt. Kabourou ana historia ndefu, tangu zama za usomi wao na rafikiye Manju Salum Msambya, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini. Ujio wa Dkt. Kabourou kwenye siasa haukuwa wa hiari, ulitokana na wito wa wazee wa Kigoma, baada ya habari mbaya ambayo Mkoa wa Kigoma uliipata Oktoba, 1993, ya msiba mzito wa marehemu Rajab Omar Mbano Kakolwa, aliyekuwa mbunge wetu wa hapa Kigoma Mjini, aliyefariki dunia ghafla huko Dar es Salaam.

Kifo cha mzee Mbano kilitustua sana wana Kigoma. Kwa kuwa Nchi ilikwishaamua kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi, uchaguzi mdogo ilibidi ushirikishe vyama vingi. Hapo ndipo jina la Dkt. Aman Walid Kabourou likaibuka kwenye siasa za Kigoma na Tanzania kwa ujumla. Akiwa Profesa wa Historia huko Marekani, aliombwa na kuridhia kurudi nyumbani na kuendeleza kazi ya marehemu Mbano, ambaye alikuwa akishirikiana kwa karibu sana na mzee Manju Msambya. Aidha, katika kipindi hicho Mzee Msambya alikutwa na ajali mbaya ya gari, iliyomfanya alazwe hospitalini kwa kipindi mrefu. Hakika zilikuwa ni nyakati za majaribu kwetu.

Dkt. Kabourou aligombea dhidi ya Azim Premji wa CCM, Hussein Beji NCCR na Kashugu Anzaruni wa TADEA, na kampeni zilikuwa moto sana. Yalipotangazwa matokeo pale ukumbi wa Magereza Bangwe, Premji wa CCM alitangazwa mshindi. Dkt. Kabourou alifungua shauri Mahakamani kupinga ushindi wa Premji, na kesi husika ikatumika kuonyesha namna rasilimali na miundombinu ya Serikali, ilivyotumika kumfaidisha mgombea wa CCM.

Kesi hii ina maana kubwa sana kwa mageuzi, majina ya mawakili wa Dkt. Kabourou, ndugu Boaz na mzee Bob Makani yakawa gumzo mjini Kigoma na nchi nzima. Watu walikuwa wanashinda Mahakama ya Kigoma kusikiliza kesi hii, na watoto wengi Kigoma waliozaliwa wakati huo walipewa majina Makani, Boaz na Vema, kumaanisha kura ya ndiyo (V). Dkt. Kabourou mwenyewe mtoto wake mmoja anaitwa Vema. Rafiki na ndugu yangu wa karibu, Boaz Chuma pia alibadili jina lake alilopewa na Mzee Ndaha na sasa kila mtu anamjua kwa jina la Boaz kwa sababu ya kesi ile. Utaona athari za kesi husika kwetu.

Kesi ilikwenda mpaka Mahakama ya rufaa ambapo Azim Premji alivuliwa Ubunge. Katika Kipindi ambapo kesi husika ilikuwa inaendelea, kazi kubwa ya ujenzi wa chama chake, Chadema ilifanyika mkoani Kigoma, kuelekea Uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Kazi hiyo ya Ujenzi wa Chama, uliiwezesha Chadema kupata Madiwani wa kwanza nchini katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 1994, madiwani hawa ndio wa kwanza kwa chama hicho kabla ya Mkoa mwengine wowote nchini. Shaaban Mambo, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara, ambaye baadaye alikuwa Naibu Meya na Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, miongoni mwa madiwani hao wa mwanzo kabisa.

Kazi ya mafanikio hayo ya Kimageuzi yaliyoletwa naye Dkt. Kabourou haikuwa lelemama, ilikuja na machungu makubwa sana. Katika kata ya Mwandiga, Vijana kama kina Nyembo Mustafa wanaweza kuelezea kwa undani simulizi nzuri na za kusisimua kuhusu namna Dkt. Kabourou alivyokuwa anatembea usiku kucha kwenye mifereji ya maji kujificha kukamatwa na polisi wakati wa ujenzi wa Chama na kuwezesha Diwani Sempa kushinda udiwani kata ya Mwandiga.

Kipindi hiki kilishuhudia Vijana wengi wakifungwa jela kwa sababu za kisiasa. Matukio yanayotokea sasa ya wafuasi na viongozi wa vyama vya upinzani kukamatwa na kuswekwa jela si mapya, sisi Kigoma, chini ya Dkt. Kabourou tumeyaishi, inaudhi tu kuwa sasa tunarudishwa tulikotoka.

Vijana wa Mwandiga wakati mwengine walilala juu ya dari za nyumba zao ili kukwepa polisi. Hakika mazingira ya sasa ya siasa za nchi yetu yanawakumbusha watu wa Kigoma miaka 23 iliyopita. Pia Demokrasia tuliyonayo sasa kwa kiwango kikubwa ilichangiwa na kujitoa muhanga kwa Vijana hawa wa Kigoma chini ya Uongozi wa Dkt. Kabourou na wenzake, kina Mzee Menge (marehemu), Mzee Kasisiko, pamoja na wengine wengi.

Mwaka 1995 ulifanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa tena. Uchaguzi huo ulikuwa wa kihistoria, na Dkt. Kabourou akaendelea kuimarisha historia yake na heshima kwa mkoa wa Kigoma, akawa Mbunge wa kwanza wa Kigoma Mjini kutoka Upinzani kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza. Kipindi hicho chama kikuu cha upinzani kilikuwa NCCR - Mageuzi.

Kwenye uchaguzi huo CHADEMA ilipata majimbo matatu tu ya Kigoma Mjini, Rombo kwa Justine Salakana, na Karatu kwa Dkt. Wilbroad Slaa. Hata hivyo Dkt. Kabourou alipoteza nafasi ya Ubunge kufuatia Mahakama kutengua ushindi wake. Uchaguzi wa marudio ulipofanyika mwaka 1999 vurugu kubwa zilitokea na kupelekea Viongozi zaidi ya 40, akiwemo Mzee Jaffary Kasisiko kuwekwa ndani kwa miezi miwili na zaidi.

Hali ya siasa ilikuwa mbaya sana Kigoma mjini, uhasama dhidi ya wakazi ulikuwa mkubwa sana. Kuna simulizi kwamba aliletwa ngamia Kigoma ili kufanya dua kuondoa uhasama uliokuwepo baada ya uchaguzi huo mdogo uliacha ufa mkubwa kwa watu. Katika kipindi hicho jitihada za kufanya siasa na kusambaza Chama Mkoa wa Kigoma ziliendelea, jambo lililomuwezesha Dkt. Kabourou kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.

Mwaka 2000 Dkt. Kabourou aliongoza kampeni zilizofanikiwa kupata Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Kigoma Ujiji ambapo Chadema ilipata madiwani wengi zaidi. Kipindi hiki alifanikiwa pia kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kabla ya kumpisha Dkt. Slaa kwenye nafasi hiyo mwaka 2004, ambapo pia Dkt. Kabourou alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama chake na Dkt. Slaa akawa Katibu Mkuu.

Kwenye jimbo Dkt. Kabourou alifanikiwa kumaliza muda wake wa Uongozi. Hata hivyo, kwenye Chama chake ukaibuka mgogoro mkubwa kati yake na viongozi wenzake, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kugombania madaraka na chuki binafsi. Ilipofika Mwaka 2005 Dkt. Kabourou aligombea Ubunge bila kuungwa mkono na Chama chake ngazi ya Taifa, jambo lililofanya apoteze nafasi ya Ubunge kwa mwanasiasa mpya kabisa, Peter Serukamba.

Ilikuwa mshtuko mkubwa kwetu, kwani pia ndio mwaka mimi niligombea Ubunge kwa mara ya kwanza, jimbo la Kigoma Kaskazini, Dkt. Kabourou ndiye aliyezindua kampeni zangu Katika kijiji cha Bitale na kunipa baraka zote. Nilitarajia kuwa yeye ndiye angeniongoza Bungeni, lakini hakuweza. Nilifanya Mkutano pale Sign Atlas Ujiji mara baada ya uchaguzi wa 2005, baada ya mkutano watu wengi walitokwa na machozi pale nilipowaeleza namna naenda Bungeni nikiwa mkiwa bila kwenda na Mwalimu wetu wa Siasa, Dkt. Walid Amani Kabourou.

Kuanguka kwa Kabourou mwaka 2005 na hulka ya baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kushindwa kutatua migogoro ya ndani ya vyama vyao, kulimfanya aamue kubadili siasa na kuhamia CCM, akiondoka Chadema, chama ambacho alinunua Ofisi za Makao Makuu yake, pale Kinondoni, mtaa wa Ufipa, wakati akiwa Kiongozi. Baada ya kuhamia CCM aligombea Ubunge wa Afrika Mashariki mwaka 2007 na kushinda. Mwaka 2012 akawa pia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, kwa muda wa miaka mitano.

Uamuzi huo wa Dkt. Kabourou wa kuondoka upinzani ulitakiwa kuwa na funzo kwetu sisi wanasiasa wa vyama vya upinzani, kwamba hakuna tofauti ambazo haziwezi kuzungumzwa na kutatuliwa, maana ni uamuzi uanaoathiri imani ya wananchi juu ya uwezo wetu wa kiuongozi. Bahati mbaya sana tunajifunza taratibu na kuendelea kufanya makosa yaleyale. Jambo hili halina afya kwa mustakbali wa siasa za nchi yetu, ni lazima upinzani tujifunze kutazama picha kubwa ili kuepuka kupoteza miamba ya aina ya Dkt. Kabourou.

Dkt. Kabourou alifanya kazi moja kubwa kwa watu wa Kigoma, alitufungua macho kuhusu haki zetu. Alikuwa mtetezi mkubwa wa haki za watu wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla. Alifungwa jela mara kwa mara kwa kusimamia haki za watu wa Kigoma. Alifanya mikutano mingi na Wananchi kuelimisha watu Kuhusu haki zao kipindi ambacho watu wengi walikuwa kwenye giza nene, katika kipindi ambacho wasomi wengi walikuwa wanajiweka karibu na watawala. Dkt. Kabourou alikwenda katika kila kijiji, mkoa mzima wa Kigoma kufanya kazi ya kutoa elimu ya siasa na kuamsha Wananchi.

Wananchi walikuwa wanakusanya pesa kumchangia mafuta ili aweze kufika kwenye vijiji vyao kuwaeleza masuala mbalimbali ya nchi yetu. Alitujengea ujasiri mkubwa. Aliitwa majina mbalimbali kama vile Lukuga, jina la mto mkubwa unaotoa maji Ziwa Tanganyika kupeleka mto Kongo. Pia Lukuga ni upepo mkali ziwani ambapo ukivuma huwa ni hatihati kwa wenye maboti. Alikuwa ni upepo mkali wa kufukuza udhalimu, alikuwa ni Mwalimu wa Haki, Utu, Demokrasia na Usawa.

Dkt. Kabourou amefariki dunia tukiwa kwenye kazi moja kubwa. Mwaka jana (mara baada ya kuwa ameshindwa Uchaguzi wa Uenyekiti wa CCM Mkoa) nilimnasihi mambo mawili. Mosi ilikuwa ni aanze kuandika historia ya maisha yake ili vizazi visome harakati zake za siasa na kuhudumia Wananchi, mchango wake kwenye Demokrasia ya nchi nk, na pili kuanza mradi wa kuandika Historia ya kwetu mirumbani, Ujiji. Dkt. Kabourou alikuwa mwanahistoria kitaaluma na nilitaka atumie muda wake wa ustaafu kuandika Historia ya Mji wa Ujiji ambao ulianza miaka mingi sana, karne ya 17.

Tayari tulikuwa tumepata andiko la shahada ya uzamivu (PhD) lililoandikwa na mwanahistoria mmoja huko Marekani, mwaka 1973, juu ya historia ya mji wetu wa Ujiji ambalo lilipaswa liwe kianzio cha kazi hii ya kuandika historia ya Ujiji. Sina hakika kama Dkt. Kabourou alianza kuandika kuhusu historia yamaisha yake, kifo chake kinaongeza orodha ya wazee wetu wanaondoka bila kuacha mafunzo ya maisha yao kwa kizazi cha sasa cha Taifa letu.

Sisi Viongozi Vijana wa Kigoma hatukuacha kumtumia Dkt. Kabourou, tukichota busara na hekima zake kila pale inapobidi. Katika kazi zake za mwisho mwisho ilikuwa ni kuhudhuria kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa wa Kigoma, ambapo moja ya ajenda ilikuwa ni kutoa majina kwa baadhi ya mitaa ya Manispaa ya Kigoma Ujiji. Katika Kikao kile tulipanga kutoa majina ya mitaa na barabara kwa kwa wabunge wote wa Mkoa wa Kigoma waliopita. Yeye ndiye aliyenipa orodha ya wabunge wote waliopita.

Mjadala ule wa kuipa majina mitaa yetu ulitugawa, ulipokuwa mkali sana, Dkt. Kabourou alisimama na kuniunga mkono kuhusu suala la kumpa heshima anayostahili mwanaharakati wa Haki ulimwenguni Ernesto Che Guevara wa Cuba, ambaye aliishi hapa Kigoma Ujiji wakati akisaidia mapambano ya msituni ya kumng’oa Dikteta Mobutu Seseseko wa Zaire. Dkt. Kabourou akijenga hoja kuwa si tu kuupa mtaa jina la Che Guevara tunalinda historia yake, bali pia tunalinda historia ya Zaire (sasa DRC Congo) mkoa wetu wa Kigoma, na Taifa kwa ujumla.

Jambo lililoungwa mkono na wajumbe wote, ikionyesha uwezo wake wa ushawishi, busara na hekima zake hata sasa ambapo alikuwa mstaafu. Ernesto Che Guevara tumempa jina la barabara ya kwenda Bangwe kutokea stesheni ya reli, mtaa ambao aliishi wakati wa harakati zake. Kuenzi kazi na mchango wa Dkt. Kabourou kwa mkoa wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla, nitawashauri viongozi na wananchi wenzangu kuipa jina la Dkt. Kabourou barabara ya kutoka Uwanja wa Ndege wa Kigoma (Gombe Mahale Airport) ili kila anayeingia Kigoma kwa njia hiyo ajue kuwa tumewahi kuwa na Mwamba, Rukuga Dkt. Amani Walid Kabourou.

Hakika Kabourou amefariki na Kigoma yake moyoni. Kesho, Mola akitujaalia, tutampumzisha kwa heshima zote anazostahili, kama mzazi na kiongozi wetu. Huyu ni shujaa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla. Tumepoteza Jabali la siasa za mageuzi, tumepoteza upepo (Lukuga) wa kufukuza udhalimu, tumepoteza mwalimu wa Haki, Utu na Demokrasia, tumepoteza Mwanahistoria, na binafsi nimepoteza Mlezi.

Allah ampe pumziko la amani.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Kata ya Muhinda
Buhigwe
Kigoma
Machi 8, 2018
 
Mapungufu ni sehemu ya ubinadamu lakini kwangu Mimi niliyeshiriki siasa tangu chama kimoja, mageuzi hadi vyama vingi nakubali Kaburou ni moja kati ya miamba ya siasa nchini.

Kila shilingi ina pande mbili, upande Wa mazuri ya Kaburou una matunda mengi katika siasa za nchi hii. Aliniudhi aliposhindwa kutatua mgogoro na wenzake, na chanzo cha tatizo kinafanana sana na cha kwako Zitto (Kukosa subira ya Wakati), yaani kuuacha wakati useme wenyewe badala ya kuulazimisha. Hata hivyo mbali ya mapungufu hayo hainifanyi kutotambua mchango wake katika kuimarisha demokrasia nchini.

Nenda Kaburou, Nenda Mwamba Wa Kigoma. Ulitusaidia sana sisi tulioonekana wachache (20%) tuliochagua mfumo Wa Vyama vingi katika kura ya White paper kuonekana watu mbele ya jamii dhidi ya 80% iliyochagua kuendelea na mfumo Wa chama kimoja.

LALA SALAMA MWAMBA WA MAGEUZI!
 
Zitto ameandika vyema Tanzia ya Dr. walid Amani Kabourou. Hata hivyo, kuna mambo mawili yanatakiwa kuwekwa sawa.

Moja; Siyo Kigoma pekee iliyoweza kupata madiwani wa upinzania katika uchaguzi wa madiwani wa 1994. Kulikuwa na madiwani Zaidi ya 20 wa NCCR -Mageuzi nchi nzima. Ninakumbuka mmoja wao, Edward Nfundizeki, kutoka halmashauri ya Bukoba niliyekutana naye kwenye kongamano la demokrasia mwaka 1995, hapa Dar es Salaam.

Mbili; Hitoria ya kisiasa ya Dr. Walid Amani Kabourou, haikuanzia Chadema, la hasha.

Mwaka 1992, akiwa safarini kwenda USA, Dr. Kabourou alipitia ofisi ya makao makuu ya NCCR-Mageuzi, mtaa wa Mchikichi Dar es Salaam aliko nunua kadi (sikumbuki namba yake) ya chama hicho baada ya mkutano wake na viongozi wa chama hicho; Mabere Marando, Prince Bagenda, Ndimara Tegambwage na Mashaka Nindi Chimoto (RIP).

Itakumbukwa kuwa kifo cha Mh. Mbano kilitokea katika muda ambapo kulitokea kifo cha Mh. Stephen Kibona (aliekuwa waziri wa fedha wakati huo wa serikali ya Rais Mwinyi). Kwa hiyo kulikuwa na majimbo mawili - Ileje na Kigoma mjini - yaliyofanya uchaguzi mdogo kwa wakati mmoja mwaka 1993. Katika jitihada za kutafuta wagombea (wakati huo Chadema haikuwa na watu zaidi ya old guards), mwenyekiti wa Chadema, Mzee Edwin Mtei, alisafiri hadi USA kumfuata Dr. Walid Amani Kabourou. Mzee Edwin Mtei alimwambia Dr. Kabourou ujumbe wa uongo kuwa vyama vya NCCR-Mageuzi na Chadema vilikuwa vimekubaliana kugawanya majimbo - NCCR-Mageuzi kiweke mgombea jimbo la Ileje wakti Chadema kikiweka mgombea jimbo la Kigoma mjini. Kwamba safari ile alikuwa ametumwa na uongozi wa NCCR-Mageuzi (Mabere Marando) ampelekee ujumbe Dr. Kabourou ahamie Chadema ili aweza kugombea ubunge jimbo la Kigoma mjni; kisha akampatia kadi ya Chadema.Ni bahati mabaya kuwa tangu awali siasa za Tanzania zimeendelea kujengwaa kwenye misingi ya uongo. Na uongo huo uliopelekea safari ya Dr. Walid Amani Kabourou kujiunga na Chadema.

Mabere Marando, baada ya Kamati ya Utendaji ya NCCR-Mageuzi kumuagiza apige simu kwa Dr. Kabourou kumtaarifu kuwa chama kilikuwa kimemteua aje kugombea ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Dr. Kabourou alibaki midomo wazi na kumwambia Marando kuwa tayari alikuwa ameingia makubaliano/amesaini form za Chadema kugombea ubunge kugombea ubunge kupitia chama hicho. Tunaamini mwenyezi Mungu akitupatia uhai tutaweza kuandika hstoria ya kweli na kuiweka hadharani.
 
Historia itamkumbuka Dr Kaborou ...alifanya makubwa sana nyakati hadi maaskari walikuwa bado makada waziwazi!

Siasa zilikuwa ngumu nyakati zile dola ni dola kweli ...upinzani ulikuwa kama uhaini si kwa dola tu hadi wananchi waliona ni kama watu wanaotaka tuwe kama Rwanda!

Mnakumbuka ITV ilikuwa inarusha documentary gani kipindi hicho hadi zikalalamikiwa? Sasa hivi anaogopwa JPM kipindi hicho inaogopwa dola! Kuna hatua tumepiga hasa uelewa wa wananchi!

Chadema na vyama vingine mnastahili kumpa heshima anayostahili huyu mzee.
 
Tangulia Lukuga, Dkt. Amani Walid Kabourou - Kinara wa Mageuzi ya Vyama Vingi Nchini.
- Mwami Kabuyuki, Mwamba wa Kigoma
...
Allah ampe pumziko la amani.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Kata ya Muhinda
Buhigwe
Kigoma
Machi 8, 2018

Mh Zitto naungana na wewe kwamba ni kweli Taifa limepoteza Jabali la siasa za mageuzi. Roho ya marehemu iwekwe pema peponi, AMINA.

Pia, kama ulivyoandika kuhusu uamuzi wa Dkt. Kabourou wa kuondoka upinzani kwamba Kuanguka kwa Kabourou mwaka 2005 na hulka ya baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kushindwa kutatua migogoro ya ndani ya vyama vyao, kulimfanya aamue kubadili siasa na kuhamia CCM, akiondoka Chadema, chama ambacho alinunua Ofisi za Makao Makuu yake, pale Kinondoni, mtaa wa Ufipa, wakati akiwa Kiongozi. inaonesha ni aina gani ya viongozi walioko kwenye vyama vya siasa. Je, wewe unawavumilia viongozi wenzio?

Isitoshe uamuzi marehemu Dr Kabourou kuondoka upinzani na kurudi CCM, haujawa funzo kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani. Kama ulivyoandika hakuna tofauti ambazo haziwezi kuzungumzwa na kutatuliwa, maana ni uamuzi uanaoathiri imani ya wananchi juu ya uwezo wetu wa kiuongozi. Lakini hadi sasa viongozi wa vyama vya upinzani wanalaumu CCM kuwa inaua demokrasia ya vyama vingi wakati wahusika ni wao wenyewe.

Jambo lingine la kujifunza kutoka kwako Mh Zitto ni pale unapohoji kama Viongozi wa vyama vya siasa wanaacha andiko gani la kukumbukwa na siyo tu kuandikwa na watu wengine! pake unaposema kifo chake kinaongeza orodha ya wazee wetu wanaondoka bila kuacha mafunzo ya maisha yao kwa kizazi cha sasa cha Taifa letu. Naamini wewe umefanya hivyo.

Hakika kuna mengi ya wewe Mh Zitto kujifunza, kwa vitendo, kutoka kwa Dr Kabourou, nguri wa siasa za upinzani, hasa lugha ambayo amekuwa akitumia kuwakilisha hoja zake zilizojengwa kisomi.
 
Zitto ni kweli tumepata msiba ila kwa sasa utekaji ndio jambo ambalo linapaswa kupewa uzito.Haya unaweza kuyaleta siku za mbeleni.

Nyinyi wapinzani vyama vyenu vilitakiwa kukutana hata kwa dharura na kutoa tamko la pamoja la kuunga mkono maandamano yale ya amani.

Nyinyi wapinzani m-take initiative ya kutaka kukutana na viongozi wa dini na muwaombe wawe sehemu ya maandamano.

Kwa sasa ni bora mkawa na kesi kwa mambo tangible kama haya na si kuendelea kupata kesi kwa kauli au matamko ambayo hayawezi kubadilisha kitu.
 
Pumzika kwa amani Dr. AMANI nakumbuka ulivyobebwa mwenyekiti kiti na wanakigoma, kwa siasa za mageuzi wewe na komredi MTIKILA ni majabari.
 
Allah ampe pumziko la amani!

Huyo rafikiye Msambya alikuwa mdini sana hasa akiwa DC Ikungi.

Sina uhakika kama sifa zao zinafanana
 
Hivi kuwaongoza watu wa Kigoma ni kazi ngumu kidogo. Mnahama kwelikweli. Kafulila kamaliza vyama vyote. Wewe Zitto una cha kwako sasa. Kuna yule kijana aliyekuwa MBunge wa NCCR-MAGEUZI sasa yuko CCM.
 
Zitto ni kweli tumepata msiba ila kwa sasa utekaji ndio jambo ambalo linapaswa kupewa uzito.Haya unaweza kuyaleta siku za mbeleni.

Nyinyi wapinzani vyama vyenu vilitakiwa kukutana hata kwa dharura na kutoa tamko la pamoja la kuunga mkono maandamano yale ya amani.

Nyinyi wapinzani m-take initiative ya kutaka kukutana na viongozi wa dini na muwaombe wawe sehemu ya maandamano.

Kwa sasa ni bora mkawa na kesi kwa mambo tangible kama haya na si kuendelea kupata kesi kwa kauli au matamko ambayo hayawezi kubadilisha kitu.

Haina maana kuwa hatuwezi kufanya mengine. Lazima tuwe na uwezo wa kufanya jambo zaidi ya moja.

Sisi Kigoma tumefiwa na lazima tuomboleze. Mnaweza kuendelea na mambo ya utekaji wakati sisi tunamsitiri ndugu yetu. Tutawakuta mbele baada ya maziko
 
Poleni sana wana Kigoma, haya maisha tunapita ndiyo maana tunatakiwa tuwe na huruma, utu maana hakuna aliye cha mkuu atakaye dumu kila nafsi itaonja umauti
 
Hakika Chadema wanapaswa kumuenzi mwamba huyu, kumuita msaliti ni kumkosea heshima maana kumbe hata Ofisi wanayotumia leo alinunua yeye.
 
Zitto ni kweli tumepata msiba ila kwa sasa utekaji ndio jambo ambalo linapaswa kupewa uzito.Haya unaweza kuyaleta siku za mbeleni.
Nyie vitoto vya sasa mnajifanya vinajua sana
Yaani wewe msiba wa kaborou si lolote ni kwa sababu sio chadema na hatoki kaskazini,ila mbwa huwa mnawafanyia mazishi ya kitaifa!

Hoja ya kujiteka haina mashiko kama mtu aliewezesha kununua banda la ufipa,mpaka leo lipo vile vile halafu unataka tujadili watu wanaojiteka
 
Zitto pole sana na watanzania wote.

Lakini siku hizi siwasikii vyuoni kutafuta vichwa imara. Kumbuka hata wewe ulipatikania huko
 
Ahsante zitto kwa taazia yenye kukumbusha yaliopita na kutambua yanayokuja
Zitto ni kweli tumepata msiba ila kwa sasa utekaji ndio jambo ambalo linapaswa kupewa uzito.Haya unaweza kuyaleta siku za mbeleni.

Nyinyi wapinzani vyama vyenu vilitakiwa kukutana hata kwa dharura na kutoa tamko la pamoja la kuunga mkono maandamano yale ya amani.

Nyinyi wapinzani m-take initiative ya kutaka kukutana na viongozi wa dini na muwaombe wawe sehemu ya maandamano.

Kwa sasa ni bora mkawa na kesi kwa mambo tangible kama haya na si kuendelea kupata kesi kwa kauli au matamko ambayo hayawezi kubadilisha kitu.

Punguza wahka kidogo taazia ni muhim sana mkuu
 
Back
Top Bottom