Imamu azungumzia mgogoro wa UVCCM Arusha
Na John Ngunge
29th May 2011
B-pepe
Chapa
Maoni
Imamu wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa Mkoa wa Arusha, ametoa tamko kuhusu mgogoro unaofukuta ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), mkoani hapa na amewaasa vijana wa Kiislamu wanaojihusisha katika mgogoro huo kujitoa.
Aidha, amewaasa Watanzania kwa ujumla kutokubali kutumiwa na chama cho chote ili kuleta vurugu nchini.
Imamu huyo, Muhammad Said Hambal, alisema hayo kufuatia mgogoro uliopo ndani ya UVCCM ambao umedhihirisha kuwepo kwa makundi mawili yanayotumiwa na baadhi ya mafisadi.
Alisema kuna baadhi ya watu aliowaita kuwa ni mafisadi wanawatumia vijana kuleta vurugu kwa malengo wanayoyajua wao na akaonya kuwa hali hiyo ikielendelea inaweza kuleta machafuko makubwa katika jamii.
Ndani ya CCM kuna vijana wanaonyesha mpasuko wa wazi
nawaasa vijana wote wa Kiislamu kuacha, wajitoe katika vurugu hizo mkoani hapa, alisema.
Imamu Hambal alisema vijana hao wanafahamika na akaahidi kwenda kuwaona kila mmoja binafsi kuwaasa wajiondoe katika mgogoro huo.
Alisema hivi karibuni kumekuwa na madai yanayotolewa na baadhi ya vijana ndani ya umoja huo wakitishia kuchoma moto jengo la makao makuu ya CCM mkoa.
Ofisi ya CCM ni mali umma, sasa ikichomwa moto wataleta madhara
sisi hatutaki madhara, na ndio maana tunakemea vurugu zozote, alisema.
Alisema wamepata madhara makubwa katika maandamano yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yaliyofanyika mapema Januari mwaka huu ambapo watu watatu waliuawa na polisi kwa risasi.
Tumepata madhara makubwa katika maandamano yale ya Chadema, hilo ni funzo na tusingependa mambo haya yatokee tena, wengi walioathitika ni Waislamu, alisema na kuongeza, waathirika wa mabomu walikuwa wa hapa mjini kati ambao pia mali zao ziliharibiwa na nyingine kuibwa.
Akizungumzia hatua ambazo watazichukua iwapo watakaidi, Imamu Hambal, alisema wataenda kuwaona wazazi wao na kama itashindikana wataacha.
Hata hivyo, alionyesha matumaini kuwa vijana hao hawatakaidi tamko lake pale aliposema, kila muumini anatakiwa kuwatii viongozi wake na kama hawatatii sisi tutawaacha.
Alisema CCM ni chama kikubwa na kama kuna kasoro basi wakae chini na kuzitafutia ufumbuzi badala ya kukaa kimya na kuwapa faida mafisadi kuwatumia vijana kwa lengo la kuleta vurugu.