TAKUKURU yakamilisha upelelezi dhidi ya Sabaya, kesi kutajwa tena leo

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Wakati kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ikitarajiwa kutajwa leo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema upelelezi umeshakamilika.

Mwananchi lilimtafuta Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikesi kujua mwenendo wa upelelezi wa kesi hiyo na akasema umekamilika na leo huenda kukawa na maendeleo ya kuisikiliza kesi.

“Upelelezi umekamilika, unajua shida ni kwamba mwanzoni walikuwa washtakiwa watano lakini wengine walikiri makosa na akabaki Sabaya, sasa huwezi kuendelea na kesi kama ilivyokuwa mwanzo, ni lazima tufanye adjustments (marekebisho),” alisema Frida.

Kesi hiyo inayopelelezwa na TAKUKURU, waendesha mashitaka wake wanashirikiana na wale wa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

“Mimi naamini wiki ijayo (leo) kutakuwa na progress (maendeleo), upelelezi ulikuwa umekamilika wakati ule wale walipokiri makosa, lakini yeye (Sabaya) hakukiri sasa tulitakiwa kufanya marekebisho,” alisema mkuu huyo wa Takukuru Kilimanjaro.

Wakati mkuu huyo wa TAKUKURU akieleza hivyo, sheria inamtaka DPP kutoa kibali kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa kwa kawaida husikilizwa na Mahakama Kuu pekee.

Leo Sabaya atakuwa ametimiza siku 145 akiwa gerezani tangu afikishwe mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni mosi akiwa na washitakiwa wenzake wanne ambao waliachiwa baada ya kukiri makosa waliyoyatenda na kulipa faini.

Baada ya kusomewa mashitaka yao siku hiyo, upande wa mashitaka ukiongozwa na mkurugenzi msaidizi wa ofisi ya DPP, Tumaini Kwewa kesi hiyo ikuwa umekamilika na ukaomba tarehe ya kuwasomea maelezo ya awali.

Hata hivyo, ilipotajwa Juni 7, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Veridiana Mlenza alisema upelelezi haujakamilika hivyo akaomba iahiriswe kwa siku 14.

Kuahirishwa kwa shauri hilo mara kwa mara kumewafanya mawakili wa Sabaya kuhoji kwa nini kila wakati inapotajwa na upande wa mashitaka kuieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika, wakati siku ya kwanza walisema umekamilika.

Oktoba 10, wakili wa utetezi, Hellen Mahuna aliibua hoja hiyo na kuutaka upande wa mashtaka kufuata mwongozo uliotolewa na DPP kukamilisha upelelezi ndani ya siku 90.

Wakili upande wa mashitaka, Suzy Kimaro aliieleza mahakama siku hiyo kuwa mwongozo uliotolewa na DPP umeanza kutumika Oktoba mosi mwaka huu hivyo hawako nje ya muda tangu utolewe.

“Mheshimiwa hakimu, tangu mwongozo huo umeanza kutumika Oktoba mosi ni siku 10 tu zimepita kwa hiyo siku 90 bado hazijaisha, upelelezi wa shauri hili utakamilika ndani ya siku 90 kama mwongozo unavyoelekeza,” alisema Suzy.

Hata hivyo, Wakili Hellen akasema kama kuna jambo upande wa mashitaka wanatakiwa kulifanya kutokana na mwongozo huo walifanye na wasitegemee una siku 10 tu, waangalie shauri lilifikishwa lini mahakamani hapo mara ya kwanza.

Hakimu Mfawidhi Mkazi Salome Mshasha alisema mwongozo uliotolewa na DPP uzingatiwe na kesi itatajwa tena kesho.

Sabaya anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi inayohusisha kuunda genge la uhalifu, kutumia vibaya madaraka yake na kujipatia Sh30 milioni huku akijua wakati anazipokea, zilikuwa ni zao la uhalifu ambalo ni rushwa.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom