Stories of Change - 2023 Competition

Mohamed mpera26

New Member
Jun 4, 2023
1
2
Ilikuwa majira ya kiangazi saa Saba mchana, mbingu ilionekana na uhaba mkubwa wa mawingu hali iliyopelekea jua kuwa Kali sana kuliko ilivyozoeleka. Joto lilikuwa Kali sana kiasi ya kwamba Machinga walio kuwa kando mwa barabara wakijitafutia riziki zao waliloa kwa jasho lililokuwa likiwatiririka. Lakini kwa hali ya maisha ya jiji la Dar es salaam, watu waliendelea na shuguli zao bila ya kujali namna jua lilivyokuwa likiwachoma na kuwa unguza kwani watu kwenye jiji husema "tumekuja kutafuta pesa mjini na sio mchezo mchezo".

Nyakati hizo za mchana, watu wakiendelea na purukushani za hapa na pale, alionekana mwanadada mmoja aliyejulikana kwa jina la Tabu, alikuwa mwanamke mwenye umri upatao miaka ishirini na Saba, alionekana amevalia mavazi ya heshima kwani alikuwa amevaa Viatu vyeusi vilivyo nadhifu, Suruali ya kitambaa, Shati jeupe na Koti jeusi la suti kwa juu alikuwa amejifunga Ushungi safi mweupe na mkononi alikuwa ameshika bahasha.

Tabu alionekana na mawazo sana huku akitembea kandokando mwa barabara, uso wake mzuri na wa kuvutia ulipoa kama vile mtu aliyepata taarifa za msiba. Nyakati hizo za mchana, Mwanamke huyu alikuwa akitoka kwenye ofisi za Serikali zilizojulikana kwa jina la NAYATA, Taasisi hii ilijihusisha na usimamizi pamoja na uendeshaji wa miradi mbalimbali ya Serikali katika wilaya ya Kigamboni.

Wiki kadhaa nyuma, Serikali kupitia Taasisi ya NAYATA ilitangaza nafasi za ajira kwenye vitengo mbalimbali vya Taasisi hiyo na Tabu aliweza kutuma ombi la nafasi moja wapo kwenye Taasisi hiyo. Wiki moja iliyopita Tabu na wenzake kadhaa walibahatika kuitwa kwenye mahojiano na Taasisi hiyo, na siku hiyo asubuhi ndio waliambiwa wafike ofisini hapo kwaajili ya matokeo ya mahojiano yao na Taasisi hiyo, lakini kitu kilichomkosesha furaha Tabu ilikuwa baada ya kuwasili ofisini hapo asubuhi na wakati wa kupewa majibu kufika. Kwa mshangao mkubwa, watu wote waliotajwa na Meneja muajiri wa NAYATA aliyefahamika kwa jina la Mtendaji Kitambi kuwa wamechaguliwa kama wafanya kazi wapya wa Taasisi hawakuwepo siku za mahojiano.

"Duuh! Sio poa!" Alisema kijana aliyefahamika kwa jina la Pasua Kichwa na alikuwa miongoni waliokosa nafasi kama Tabu baada ya Mtendaji Kitambi kukamilisha orodha ya waajiriwa kisha akaendelea "Hiyo haiwezekani, mbona hao watu hatuwajui?" Aliuliza , hivyo Tabu na wengine waliokosa nafasi wakaanza kulalamika lakini jitihada zao hazikuzaa matunda kwani walinzi wa NAYATA waliwatoa nje ya ofisi hizo zilizopo Kigamboni. Hivyo ndivyo ilivyotokea mpaka Tabu kuonekana akirudi nyumbani kwao Mtoni Mtongani bila furaha.

Bada ya tukio hilo siku zilisonga, Tabu aliendelea na shughuli zake za kila siku dukani kwa baba yake aliyejulikana kwa jina la mashaka, baba yake huyo alikuwa akijishughulisha na shughuli nyingi za kibiashara jijini hapo na duka lililokuwa likisimamiwa na Tabu lilikuwa duka la vifaa vya ujenzi lilipatikana Kwa Azizi ally, Mama wa Tabu aliyefahamika kwa jina la Matumaini alishafariki kwa ajari ya gari miaka mitatu iliyopita.

Siku moja yapata saa moja unusu usiku, Tabu alikuwa ameshafunga duka tayari kurudi nyumbani kama ilivyo kawaida yake fedha ya nauli aliihifadhi kama akiba kwani hujisemea mwenyewe "Akiba haiozi" na yeye alitembea kwa miguu toka kwa Azizi Ally mpaka Mtoni Mtongani kwani sio mbali sana.

Lakini akiwa njiani alikutana na aliyekuwa rafiki yake aliyeitwa Sijali, wawili hao waliweza kuhitimu pamoja Elimu ya chuo kikuu. Sijali alionekana amevalia nguo fupi sana zilizoonesha baadhi ya sehemu ya mwili wake, baada ya kusalimiana Tabu aliuliza "unaenda wapi, Shosti?","naelekea pale mara moja ,nipo na haraka kwa hiyo tutaonana siku nyingine" alijibu Sijali na baada ya hapo ilikuja bodaboda na kumchukua Sijali na kuondoka nae

Siku iliyofuata, Tabu alijaribu kuulizia kwa jirani kuhusu Sijali na kupata taarifa kuwa Sijali ameanza tabiya ya kujiuza na huwa anatoka kwa Siri sana usiku. "Dooh! Hata ikiwa ngumu kiasi gani,siwezi kujitoa thamani namna hiyo" alisema kimoyoni Tabu.

Siku moja, Tabu akiwa ameketi huku akiwa anaangalia kurasa mbalimbali za Serikali mtandaoni kwa kutumia simu janja yake aliweza kuona tangazo ,tangazo hilo lilisema hivi "TAASISI YA KUTOKOMEZA RUSHWA (TKR) inakupa nafasi Wewe Mwananchi ikiwa umekumbana na janga la Rushwa na umeikosa haki yako, unaweza kuja ofisini kwetu iliyopo Magomeni Mapipa na Sisi tutawasikiliza bila kujali chochote na kutunza Siri ya malalamiko yako na mtapewa haki zenu endapo itagundulika mlizikosa kwa sababu ya Rushwa"

Hapo ndipo Tabu alimkumbuka Mtendaji Kitambi wa NAYATA, bila kuchelewa Tabu alianza kutafuta mawasiliano na mtu yeyote aliyekuwepo kwenye sakata la kukosa Ajira kwenye Taasisi ya NAYATA. Alibahatika kuwasiliana na Pasua Kichwa, hatimaye waliweza kuwakusanya wenzao na wakaweza kwenda kutoa malalamiko yao kwenye Taasisi ya Kutokomeza Rushwa(TKR). Hivyo Taasisi hii ya kupambana dhidi ya Rushwa ilianza upelelezi na uchunguzi juu ya uendeshaji na uajiri wa NAYATA na kubaini kuwa Rushwa ilitumika kuwapa ajira baadhi ya wafanya kazi wa Taasisi ya NATATA.

Baada ya uchunguzi na upelelezi kukamilika ,Mtendaji Kitambi na Wale wafanyakazi waliotoa Rushwa ili wapate kazi walisimamishwa kazi mara moja.

Hivyo uongozi mpya wa haki ukawekwa kwenye Taasisi ya NAYATA kitendo kilichopelekea Tabu, Pasua Kichwa na wengine waliokosa nafasi kwenye Taasisi hiyo kupata kazi na Maisha yao kubadirika kwa ujumla.
 
Back
Top Bottom