Hapa Tanzania watu mbalimbali wamejitokeza kutengeneza sinema nyingi lakini kuna hii iliyoanzia kwenye igizo dogo tu lenye maudhui ya vita dhidi ya rushwa na ufisadi la Richmond, linaloonesha jinsi watawala walivyo tayari kuumiza wananchi wao ili kutibu majeraha yao wenyewe au rafiki zao ni sinema tamu sana. Sinema hii ndefu ilianza kama mzaha vile: wahusika wakuu wakiwa ni wale wanaojua kufisadi Taifa hili. Jinsi sinema ilivyoanza wengi tulidhani itaishia sehemu moja tu ya Richmond, kumbe jamaa ni wajanja sana kwani walipoona kuwa Watanzania tumepiga kelele nyingi kuhusu Richmond, wakatubadilishia 'Angle' na kutuwekea sehemu ya pili ya filamu; Dowans.Mwandishi wa kisa hiki: Richmond/Dowans, ni mwandishi mahiri sana mwenye kuijua vyema kazi yake. Hubadilisha msuko wa hadithi (plot) kila anapoona ipo haja ya kufanya hivyo bila kuharibu maudhui yake, mwanzoni tulipohoji tuliambiwa kuwa mmiliki wa Dowans hajulikani! Wakati huohuo Waziri wa Nishati na Madini akikomalia kuilipa Dowans! Upepo ulipobadilika ghafla baada ya kelele nyingi zilizopigwa na wananchi, mmiliki wa Dowans akajitokeza na kukataa kupigwa Picha. Ila alitaja kuwa alitoa mamlaka kwa Mbunge Rostam Aziz (ingawa Rostam aliwahi kuikana) kuisimamia Kampuni ya Dowans hapa Tanzania!Watazamaji wa sinema wakaishtukia, mwandishi akabadilisha 'angle' na kutangaza kuwa serikali ikinunua mitambo ya Dowans watafuta kesi. Watanzania wakagoma tena safari hii kwa kelele kubwa sana. Sasa ameleta kitu kipya zaidi kinachoitwa Symbion Power!Hapa ndipo sinema hii inaponoga zaidi, kwani alichokifanya mwandishi wa kisa hiki ni kuuhadaaumma wa Watanzania na mgawo wa umeme ili tuingie mkenge wa nguvu, na tuikukubali Symbion Power ambayo ni Mrithi wa Dowans.Hii yote ni kuwafanya Watanzania majuha wasiojua kitu au kusoma alama za nyakati. Hainiingii akilini kuwa Symbion Power na watuhumiwa wa Richmond/Dowans ni vitu viwili tofauti, watakuwa wamebuni mkakati huu wa kuibua kampuni hii ili kufuta madoa ya Richmond/Dowans usoni kwao. Na sasaTanesco inaingia mkataba na kampuni hiyo ili ituuzie umeme.'Angle' ya mwandishi katika kisa hiki imebadilika sana baada ya kuona kwamba jina la Dowans halitakiwi kabisa na Watanzania ametuletea jina jipya, na kama tuliukataa umeme wa Dowans basi tutasahau itakapoanza Symbion Power. Na wote tutapongeza maana tutaiona kama mkombozi kwa kuwa tayari tumeghiribiwa kwanza kwa kuletewa mgawo wa umeme mkali ili ionekane kuna shida. Sinema hii ndefu ya Richmond/Dowans, na sasa Symbion ina mafundisho mazuri sana kwa jamii: mojawapo ni kuwa nchi yetu haipaswi kabisa kuwa na umeme ulio imara kwa kuwa watu watakosa ulaji. Mgawo wa umeme ni lazima uwepo hata kama tulikwishaambiwa kuwa utabaki kuwa historia. Bila mgawo wa umeme zile kampuni zao za kuuza majenereta zitakufa. Hivyo kwao mgao wa umeme ni dili zuri, zuri mno. Dili litakalowahakikishia ulaji milele na kuendelea kujenga heshima ya kuwa na vitambi vya kuvimbiwa ufisadi.Wasiwasi wangu tu ni kuhusu mwisho wa sinema hii ndefu isiyochosha, kwani watawala wakizidisha ulafi, wa kunywa mchuzi wote, wananchi wanaweza kuingilia kati na kuamua kumwaga ugali, kama watawala wakimwaga mboga. Yatakayotokea baada ya hapo ni dhambi kuyaeleza.