Taxi - (47)
Ilipoishia jana
Winifrida alijibwaga juu ya kitanda kilichokuwa kimetandikwa vizuri kwa shuka la rangi ya waridi lililofumwa maua katikati akionekana kuchoka, kisha akajilaza chali, miguu kaining’iniza sakafuni na kushusha pumzi. Sasa alionekana kujiwa na mawazo, aligaragara juu ya kitanda kile, kisha aliuchukua mmoja wa mito miwili iliyovikwa foronya rangi moja na ya lile shuka na kuukumbatia halafu akajilaza kifudifudi.
Hapo tena fikra zilianza kutembea kichwani mwake na kuanza kujiuliza vipi angeweza kuendelea kuvikabili vishawishi kutoka kwa wanaume wakware waliokuwa wakimwita kila alikopita? Na vipi angeweza kuyakabili mapenzi ya kijana Jackson yaliyoanza kumwingia moyoni na kuitawala akili yake ilhali yu bado mwanafunzi?
Alifikiria kwa kitambo kidogo huku fikra zikizidi kuranda na kupigana vikumbo ndani ya kichwa chake, mara aligutuka na kunyanyuka kutoka pale kitandani. Sasa mawazo yote aliyokuwa nayo yalipeperuka kwa muda na kuanza kuvua zile nguo alizovaa.
Alipogeuka alikikabili kile kioo kirefu cha kujitazama kilichopachikwa kwenye meza ya vipodozi, na kama kioo kile kilikuwa kikimtua, aliinuka na kukisogelea. Alianza kujianglia kwenye kioo namna alivyoumbika. Alijitazama na kujitazama tena, halafu akageuka na kujitazama huku na huku na alipohisi hajajifaidi bado, alikwenda kufunga mlango.
Alisimama mbele ya kioo akaendelea kuvua nguo zake na kubakiwa na chupi tu. Alijishika kiunoni kwa mikono yake na kujitazama tena huku na huku. Alijigeuza nyuma na kujiangalia matiti yake na kuyatomasatomasa huku akiyachezea.
sasa endelea...
Alijigeuza tena mbele na nyuma na mara kwa ghafla, kama mtu aliyeshtuliwa, aliondoka mbele ya kioo na kufungua kabati la nguo, alitoa sketi fupi ya pundamilia na blauzi nyepesi nyeusi, akavaa haraka na kutoka.
* * * * *
Kwenye ukumbi wa kisasa wa chakula katika mgahawa wa Elli’s, Sammy na Elli walikuwa wameketi kwenye kona moja ukumbini wakinywa sharubati na kuongea. Sammy alikuwa na wasiwasi kuhusu namna ambavyo angemkabili mkewe kumweleza suala la kununua gari, kwa kuwa hakuwa amemshirikisha tangu mwanzo.
“Ukweli hata mimi najiuliza, utamwelezaje mkeo, kwamba hili gari umelipataje?” Elli alimuuliza Sammy huku akimtazama kwa makini.
“Hata sijui, maana ataniuliza kwa nini hatukushauriana kwanza kabla sijalinunua!” Sammy alisema huku akishusha pumzi.
“Kwa hiyo bado utaendelea kumficha kuhusu matatizo ya kazini kwako?” Elli alimuuliza Sammy huku akimkazia macho.
Sammy aliachia tabasamu, akashusha pumzi za ndani kwa ndani na kuzungusha macho yake mle ukumbini, aliwaangalia kwa muda wateja wachache waliokuwemo mle ndani muda huo, kisha akatoa leso mfukoni na kufuta paji la uso wake.
“Sidhani kama bado nahitaji kumficha ukweli, nimefikia uamuzi wa kumweleza kila kitu leo, natumai atanielewa,” Sammy alisema na kumeza mate kutowesha koo lake.
“Ni bora ufanya hivyo, maana hizi ni changamoto tu katika maisha na kila mtu humtokea, isitoshe mkeo ni mwelewa sana,” Elli alisema huku akibetua kichwa chake akionesha kukubaliana na Sammy.
“Kumficha mkeo ni kuruhusu matatizo zaidi yaibuke ndani ya ndoa yenu, hasa pale atakapokuja kujua kuwa ulimficha. Si hivyo tu, anaweza kunichukia hata mimi kwa kudhani nilikupotosha. Kwa hiyo jaribu kuweka mambo wazi ili mjadili na msonge mbele,” Elli alisisitiza na kumfanya Sammy ashushe pumzi.
“Sasa vipi kuhusu suala la vibali? Nataka gari lianze biashara mara moja.”
“Suala la vibali niachie mimi, hilo limo ndani ya uwezo wangu. Ninaye mtu kwenye mamlaka husika, ni ndani ya siku tatu tu kila kitu kitakuwa kimekamilika,” Elli alisema akimhakikishia Sammy. Na hapo tabasamu pana likachanua kwenye uso wa Sammy.
* * * * *
Saa kumi na mbili kamili Madame Norah aliwasili katika viunga vya Paradise Club akiwa ndani ya gari lake aina ya
Mercedes Benz E-Class la rangi nyeusi. Aliingia baada ya kuvuka vizuizi vitatu vyenye ulinzi wa uhakika.
Alikuwa amevaa suti nadhifu ya kike ya rangi ya kijivu iliyokuwa imemkaa vyema na kumpendeza, begani alitundika mkoba mzuri wa nguo ya pundamilia uliomgharimu fedha nyingi na viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio.
Mkono wa kushoto alikuwa amevaa bangili nyingi za pembe na mkono wake wa kulia alivaa saa ghali ya kike aina ya
Cartier La Dona iliyotengenezwa kwa dhahabu nyeupe ya karati 18, ikiwa na gerentii ya miaka hamsini.
Aliambatana na wanaume wawili wenye miraba minne, walinzi wake waliokuwa wamevaa suti maridadi nyeusi, miwani mikubwa myeusi iliyofunika macho yao na miguuni walikuwa wamevaa buti ngumu nyeusi za ngozi imara ya mamba.
Madame Norah na walinzi wake waliwasili na kupokewa na Mafuru aliyekuwa akiwasubiri muda wote katika viunga vya maegesho ya Paradise Club, kisha aliwaongoza kuelekea ghorofani kwa Mr. Oduya.
Kama kawaida, wale walinzi hawakuwaruhusu wapite hivi hivi bila kukaguliwa, japo walikuwa na taarifa zao, waliwakagua na kuhakikisha hawakuwa na silaha au kitu chochote hatarishi walichobeba, kisha waliwaruhusu wapite.
Mafuru aliwaongoza kuingia katika sebule kubwa walikomkuta Mr. Oduya akiongea na simu lakini mara tu alipowaona alisitisha mara moja maongezi na mtu aliyekuwa akiongea naye kwenye simu na kusimama kwa heshima kumlaki Madame Norah, huku uso wake ukipambwa na tabasamu la bashasha.
“Madame, karibu sana Paradise Club,” Mr. Oduya alisema huku akimpa mkono Madame Norah.
“Ahsante sana mheshimiwa Rais mtarajiwa,” Madame Norah alisema kwa utani na kuwafanya wote waangue kicheko.
“Mdomo wako uwe wa heri, na iwe kama usemavyo,” Mr. Oduya alisema huku akiendelea kucheka kwa furaha kisha aliwaelekeza wageni wake sehemu ya kuketi.
“Madame ni furaha yangu kukutana nawe siku ya leo na kabla ya yote
ninapenda kwanza kusema ahsante sana kwa kukubali mwaliko wangu wa kutaka kuonana nawe jioni hii,” Mr. Oduya aliongeza baada ya wote kuketi kitako.
“Kiukweli mwaliko wako umenishtua sana,” Madame Norah alisema huku akimtazama Mr. Oduya kwa makini.
“Najua, hata hivyo mimi ni nduguyo kabisa, tena ndugu wa damu…”
“Undugu huo
veepe, mbona sikuelewi! Wewe Jaluo na mimi Mbondei wapi na wapi!” Madame Norah alisema huku akiendelea kumtazama Mr. Oduya kwa makini zaidi.
“Ni ndugu kwa kuwa wote ni Watanzania, hata hivyo kabla ya yote sijui mtatumia vinywaji gani?” Mr. Oduya aliuliza huku akiwatazama kwa zamu.
“Nadhani ungeeleza kwanza ulichoniitia, suala la vinywaji siyo lililonileta hapa,” Madame Norah alisema huku akionekana kuwa makini zaidi, hakuwa na muda wa kupoteza.
“
Okay, sitaki nichukue muda mrefu sana wa kuongea nawe… kwa kifupi nimefuatilia baadhi ya shughuli unazozifanya na nimejikuta nikiguswa sana. Hongera sana kwa kujitoa kusaidia jamii, ni wengi tunajaribu kufanya kama unavyofanya lakini wengi hatufanyi kwa kujitolea kama unavyofanya. Nimeguswa zaidi na hiki ulichoamua kukianzisha sasa…” Mr. Oduya alisema na kunyamaza kidogo. Madame Norah alibaki kimya akimsikiliza lakini akiwa makini kuliko simba jike.
Inaendelea...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali