Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (5)

ILIPOISHIA

Dk. Masanja hakuitikia ile salamu ya Sammy wala hakumtazama usoni, aliendelea kulikodolea macho lile gazeti aliloshika mkononi huku uso wake ukiwa umesawajika na mawazo yake yakiwa mbali sana.

“Boss mbona leo unaonekana hauko sawa, kuna tatizo lolote?” Sammy aliuliza huku akiwa na mshangao mkubwa.

“Sina shida na salamu yako,” Dk. Masanja alisema huku akivuta mtoto wa meza na kuchukua bahasha ndogo ya khaki iliyokuwa na barua ndani yake, akanyoosha mkono wake kumpa Sammy bila hata kumtazama usoni. Uso wake ulikuwa bado umekunja ndita.

Sammy alishtuka sana na kuitazama ile bahasha kwa mshangao mkubwa, alishusha pumzi za ndani kwa ndani na macho yake yakatulia kwenye uso wa Dk. Masanja. Alimkazia macho huku akionesha wasiwasi mkubwa.

SASA ENDELEA...

“Kwani kuna tatizo gani, Boss?” Sammy aliuliza kwa wasiwasi huku akionekana kuchanganyikiwa kidogo.

“Unashtuka nini, kwani hujawahi kupewa barua?” Dk. Masanja alimuuliza Sammy huku akimtazama kwa mara ya kwanza tangu aingie ofisini kwake.

“Nimeshawahi kupewa, tena nyingi tu…” Sammy alisema huku akihisi jasho jepesi likianza kumtoka na ubaridi wa woga wa aina yake ukimtambaa mwilini.

“Sasa! Kinachokushtua ni nini?” Dk. Masanja aliuliza tena huku akiwa amemkazia macho Sammy.

“Hakuna tatizo, ila…” Sammy alitaka kusema lakini Dk. Masanja alimkata kauli.

“Kama hakuna tatizo basi chukua barua yako na usinipotezee muda wangu hapa,” Dk. Masanja alisema kwa sauti iliyovuma kwa ghadhabu huku akimkazia macho Sammy.

Sammy alimtazama yule mzee kwa makini, alitaka kunyoosha mkono wake kuichukua ile barua lakini akasita. Dk. Masanja alimkazia macho huku akimsisitiza kuichukua ile barua.

Sammy aliipokea na kuichana pale pale, akaifungua na kutoa karatasi iliyokuwa ndani yake, na hapo akakutana na na kichwa acha habari kilicoaandikwa: “Yahusu kusimamishwa kazi kwa utovu wa nidhamu na kuihujumu kampuni”

Sammy alipigwa butwaa na kuiachia ile barua ikadondoka sakafuni. Alishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani huku akihisi mapigo ya moyo wake yakibadili mwendo wake na kwenda mbio isivyo kawaida!

I can’t believe this! Unawezaje kunifanyia hivi?” Sammy aliuliza huku akikihisi joto kali sana likimtambaa mwilini! Alionekana kupatwa na mshtuko mkubwa sana kutokana na barua ile.

Dk. Masanja hakujibu bali alibaki kimya akimtazama Sammy kwa hasira. Kikapita kitambo kifupi cha ukimya huku wakitazamana kama majogoo waliotaka kupigana.

“Nimehukumiwa bila makosa! Sijawahi hata kupewa barua ya onyo, iweje leo naandikiwa kuwa mimi mtovu wa nidhamu na naihujumu kampuni! Lazima kuna kitu kinaendelea hapa, si bure,” Sammy alisema kwa uchungu.

“Kama unadhani hujatendewa haki unaweza kukata rufaa kwenye ngazi husika, ila kwa sasa hutakiwi kuwepo hapa na kampuni haitahusika na jambo lolote linalokuhusu,” Dk. Masanja alisisitiza.

Sammy alionekana kunywea sana utadhani kifaranga cha kuku kilichonyeshewa na mvua. Alifungua mdomo wake kutaka kusema lakini maneno hayakutoka, akabaki mdomo wazi huku akimkodolea macho Dk. Masanja. Donge la fadhaa lilikuwa limemkaba kooni.

Dk. Masanja alionekana kumpuuza Sammy na kuyahamishia macho yake kwenye lile gazeti alilokuwa ameshika mkononi, japo ilionekana wazi kuwa akili yake haikuwa pale.

Sammy aliinamisha uso wake chini na kuanza kutafakari, fikra zikamjia kwamba huenda alikuwa ndotoni, hata hivyo, hisia zake zilimtanabaisha kuwa ile haikuwa ndoto bali ni kitu halisi kilikuwa kinatokea.

Hakujua ni utovu upi wa nidhamu aliowahi kumfanyia mkuu wake wa kazi, kiasi cha kusimamishwa kazi. Hakukumbuka ni lini aliwahi kuihujumu kampuni! Kilichomjia akilini ni jinsi alikuwa akijitoa kwa moyo wake wote kuitumika kampuni ile na alivyomuheshimu mkuu wake wa kazi. Hakutaka kabisa kuamini kwamba kitu kama hicho kingeweza kutokea.

I’m totaly confused! Au pengine huyu boss ana hofu ya kupokonywa cheo? Kwani tangu nimepata tuzo ya kimataifa kutoka taasisi ya Institute of Hospitality ya Uingereza naona kama amebadilika sana!” Sammy aliwaza.

Hata hivyo, aliyafuta mawazo hayo haraka kichwani kwake, kwani alikuwa na uhakika kuwa Dk. Masanja hakuwa na shida yoyote ya kung’ang’ania kile cheo, ingawa naye alikuwa kaajiriwa hapo New Udzungwa Beach Resort lakini alikuwa amejitosheleza kwa vitu vingi.

Mara mbili alitaka kuacha kazi ili akasimamie biashara zake lakini kampuni ilimuomba na hata kumuongezea mshahara mara dufu ili asiache kazi.

Si hivyo tu, alikuwa anamiliki migahawa miwili ya kisasa, mmoja ukiwa jijini Dar es Salaam na mwingine jijini Mwanza, alikuwa na ranchi ya ng'ombe wa kisasa wasiopungua therathini, shamba kubwa la matunda na mazao mbalimbali eneo la Ruvu mkoani Pwani, na nyumba kadhaa za kisasa alizozipangisha katika majiji ya Dar es Salaam na Mwanza.

Mkewe pia alikuwa anamiliki maduka makubwa mawili ya vipodozi na nguo za kike, maarufu kama boutique, yalikuwa katika majiji ya Dar es Salaam na Mwanza, na alikuwa mbioni kufungua duka jingine jijini Arusha. Pia mara kwa mara alikuwa akisafiri nje ya nchi kwenda kununua bidhaa.

Sasa Sammy alijiuliza, kama haikuwa hofu ya kunyang’anywa cheo kulikuwa na tatizo gani kubwa? “I need to find out,” aliwaza na kuzidi kutweta.

Pamoja na uwepo wa kiyoyozi mle ofisini kilichotoa ubaridi mkali lakini alianza kutokwa jasho. Mara kikohozi kidogo kikamtoka, na nyuma yake wimbi la machozi lilikuja mbio. Alijaribu kuyazuia machozi yasimtoke bila mafanikio, aliyafuta kwa kutumia viganja vyake vya mikono.

“Boss, unaweza kuniambia kwa nini unanifanyia hivi?” hatimaye Sammy alimudu kuuliza huku akiwa amefadhaika sana.

“Umefanya jambo la kipumbavu sana lililonifedhehesha mno… sasa toka ofisini kwangu kabla sijasahau kuwa sisi ni marafiki!” Dk. Masanja alimwambia Sammy huku akimtazama kwa macho makali yaliyokuwa yakiwaka kwa ghadhabu.

Sammy alijikuta akihamaki sana, alitaka kusema neno lakini akashindwa kutokana na donge la hasira kumkaba kooni, na mara alishangaa kuona ukungu mwepesi ukianza kutanda mbele ya macho yake. Alianza kupumua kwa nguvu huku miguu yake ikianza kuishiwa nguvu…

_____

Hakujua ni muda gani alikuwa ameutumia akiwa kasimama ofisini kwa Dk. Masanja na hakuamini kama ni kweli mambo yale yalikuwa yamemtokea.

Itaendelea...

Cc the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali
Nimefika Mkuu...

Tunaendelea....
 
Taxi - (34)

Ilipoishia

“Ni jambo zuri lakini kumbuka awamu hii siyo ile ya Rais Sakaya Mkiete, hii ni ya Dk. Funguo, na mfumo wote ndani ya CCU umebadilika, sidhani kama hao mabilionea wana ushawishi mkubwa ndani ya chama, labda nje ya chama. Hata hivyo, bado sina wasiwasi na nguvu yako ingawa hupaswi kujipa uhakika sana,” Balozi Mageuzi alisema huku akimwangalia Mr. Oduya kwa makini.

“Kwa nini unasema hivyo, Balozi?” Mr. Oduya aliuliza huku akimkazia macho Balozi Mageuzi.

“Kwa hali ilivyo, hamasa ya kuwania uteuzi imeongezeka sana ndani ya chama. Ila bado imeendelea kuwa siri ni nani na nani watajitosa kuwania uteuzi. Lakini najua mheshimiwa Tumbo na Dk. Hussein Abbas watawania…” Balozi Mageuzi alisema na kuongeza.

Sasa endelea...

“Dk. Hussein Abbas japo anaonekana kama asiye na nia lakini kwa taarifa nilizonazo atawania nafasi ya kuteuliwa na chama, ni mmoja kati ya wanachama wenye nguvu kubwa kwenye chama na kwa siku za hivi karibuni nguvu yake imeongezeka na kutishia vigogo wenzake serikalini ambao nao wana dhamira kama yake…”

I see! Kumbe mambo ni moto moto kiasi hicho!” Mr. Oduya alionesha kushangaa sana.

“Hivi nikuambiavyo tayari mheshimiwa Tumbo ameanza kampeni za chini kwa chini ili kutafuta uungwaji mkono katika zoezi la kura za maoni na katika vikao vya juu vya uteuzi ndani ya chama…”

“Niseme ukweli, sikutegemea kama Dk. Hussein Abbas angeonesha nia ya kutaka kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taarifa nilizo nazo ni kwamba anaandaliwa kuwa Rais wa Zanzibar, ndiyo maana nilifikiria kumshirikisha kwenye mikakati yangu ya urais!” Mr. Oduya alisema kwa mshangao.

“Hakuwa akitaka ila wazee wamemuomba. Na jambo hili limesababisha makundi ndani ya chama, lipo kundi linalomsapoti Dk. Hussein Abbas na lingine linamshabikia Mheshimiwa Tumbo, kwa hiyo kuna mchuano mkali wa chini kwa chini kati ya vigogo hawa wakubwa serikalini. Kumbuka hawa waliwahi kuwa maswahiba wakubwa lakini kwa sasa wamekuwa mahasimu wakubwa. Kwa ufupi hiyo ndiyo hali halisi ilivyo ndani ya Chama,” Balozi Mageuzi alisema na kutingisha kichwa chake kwa huzuni.

“Nimekuelewa Balozi, kama Dk. Hussein Abbas naye anatafuta nafasi ya kuungwa mkono kugombea urais basi tutegemee mnyukano mkubwa kati yake na mheshimiwa Tumbo. Wawili hawa watakigawa chama katika sehemu mbili, sipati picha mtikisiko utakaokuwepo ndani ya chama katika uteuzi, ndiyo maana naamini kuwa mwisho wa siku ni mimi nitakayeibuka mshindi, japo shaka yangu kubwa ni mheshimiwa Tumbo kutumia siasa za majitaka…” Mr. Oduya alisema huku akijiweka sawa kwenye kiti chake.

“Kweli kabisa, kuna kila dalili za mpasuko ndani ya chama, hawa vigogo wameanza kukigawa chama katikati na hilo ndilo hasa limenifanya nitake kukuona. Cha kwanza nijue msimamo na pili nikupe taarifa ambazo naamini bado hujazipata,” Balozi Mageuzi alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Zipi hizo?” Mr. Oduya aliuliza kwa shauku huku akimkazia macho Balozi Mageuzi.

“Sipendi kukuficha rafiki yangu lakini ni ukweli usiopingika kuwa utapata wakati mgumu sana kuteuliwa ndani ya chama kwa sababu ya vigogo hawa wawili kuwa na nguvu kubwa ndani ya chama na wewe nguvu yako kubwa iko nje ya chama. Hivi sasa kuna mkakati maalumu wa kumshawishi Rais ili jina lako likatwe kabla ya kufika Halmashauri Kuu. Juzi usiku kulikuwa na kikao cha siri Chattle Hotel na mwenyekiti wake alikuwa Katibu Mkuu wa Chama, Dk. Bazil Uledi…” Balozi Mageuzi alisema na kunyamaza kidogo, akailamba midomo yake iliyoanza kukauka.

“Ninazo taarifa za uhakika kuwa mheshimiwa Tumbo tayari ana uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama na wajumbe wengi wa kanda yote ya kusini, pwani na kwa sehemu kubwa ya kanda ya magharibi. Kuna mtandao makini na wa siri umeundwa ili kuhakikisha wanashinda, kusema kweli hawalali, wanafanya kazi usiku na mchana…” Balozi Mageuzi aliongezea.

Maneno yale yalimshtua sana Mr. Oduya, alibaki ameduwaa huku akihisi joto kali mwilini na jasho jepesi likianza kumtambaa sehemu mbalimbali za mwili wake, koo lake lilikauka ghafla na nywele zikamsimama kichwani kwa hofu.

“Wanahangaika usiku na mchana kwa kuwa hofu yao kubwa ni wewe, wanaogopa wakikuachia upenyo kidogo utawashinda kwani jina lako linatajwa sana katika orodha ya watu wenye sifa na uwezo wa kuiongoza nchi hii, kutokana na misaada mbalimbali ambayo umekuwa ukiitoa kwa vikundi vya walemavu, akina mama na vijana,” Balozi Mageuzi alisema baada ya kuona Mr. Oduya yupo kimya akimtumbulia macho.

“Kwani mheshimiwa Rais anasemaje kwenye hili? Umebahatika kusikia chochote kuhusu mtu anayemuunga mkono?” hatimaye Mr. Oduya alimudu kuuliza, hata hivyo bado alikuwa na wasiwasi.

“Sijamsikia kusema chochote, lakini natambua urafiki wenu ulivyo mkubwa, yeye ni mmoja wa watu wanaokukubali, na wapinzani wako wanajua hilo, ndiyo maana hawapati usingizi… hivi sasa wanawatumia watu wa Usalama wa Taifa kukusanya kila taarifa ya kashfa inayokuhusu ili wampelekee Rais,” Balozi Mageuzi alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

Kilipita kitambo kirefu cha ukimya, kila mmoja alikuwa kimya akitafakari. Sasa Mr. Oduya hakuhisi tena joto kali mwilini bali alianza kukihisi ubaridi mkali ukimtambaa mwilini mwake.

“Lakini usihofu, najua yupo mtu mmoja muhimu sana, kama utaweza kumshawishi ajiunge na upande wako utakuwa umemaliza vita kabla hata hujafika kwenye uwanja wa mapambano…”

“N-nani?” Mr. Oduya aliuliza kwa pupa huku uso wake ukianza kuonesha matumaini.

“Makamu Mwenyekiti wa Chama, mzee Fabian Magulu… kama umegundua huyu mzee anakubalika sana, ndiye mwenye ushawishi mkubwa siyo tu ndani ya chama bali hadi serikalini na ndiye alikuwa nguzo muhimu ya ushindi na mafanikio yote ya Rais Funguo, wakati akiwania kipindi cha pili cha urais. Unakumbuka alipigwa sana vita ili aishie kipindi kimoja,” Balozi Mageuzi alisema na kumfanya Mr. Oduya avue koti lake na kulitundika kwenye kiti chake, sasa hakuwa akihisi tena baridi.

Inaendelea

Cc the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego
 
Taxi - (35)

“Unajua sina ukaribu sana na mzee Magulu japo tunafahamiana, sijajua nitamuingiaje!” Mr. Oduya aliuliza kwa sauti tulivu.

“Usipate taabu, ndiyo maana nipo hapa kukusaidia, nipe wiki moja tu nitakuelekeza nini cha kufanya ila kama utakuwa tayari kufuata ushauri wangu…”

“Kwa nini nisifuate ushauri wako wakati ni wewe ndiyo umenifumbua macho?” Mr. Oduya alisema huku akionesha uso wenye matumaini mapya, sura yake sasa ilikuwa imejenga tabasamu pana.

* * * * *

Saa kumi na moja na dakika arobaini jioni ilimkuta Madame Norah akiwa ameketi kwenye kochi kubwa la sofa ndani ya ukumbi mkubwa wa kisasa wenye jukwaa zuri la kisasa lililokuwa linatazamana na viti vingi vya kisasa kwa ajili ya burudani au kufanyia mikutano. Kulikuwa na seti moja ya masofa yaliyokuwa yamepangwa kwa namna ya kulizunguka lile jukwaa.

Ukumbi ule ulikuwa katika jumba zuri la kifahari la ghorofa tatu lililokuwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi katika eneo la Mikocheni, likiwa limezungukwa na miti mirefu ya kivuli. Eneo lile lilikuwa la majumba ya kifahari ya makazi ya kisasa ya watu wenye ukwasi, yaliyozungukwa na miti mirefu na kuta zenye usalama wa uhakika.

Jumba lile lilikuwa limezungukwa na ukuta uliofungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi juu yake na lilikuwa na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri.

Madame Norah alikuwa mrefu na mweupe mwenye umbo la kupendeza japo alikuwa na umri mkubwa, alikuwa amevaa blauzi ya bluu ya mikono mirefu, suruali ya Jamsuit ya rangi nyekundu iliyolichora vyema umbo lake refu maridadi lenye kiuno chembamba lakini imara kikiwa kimebeba minofu ya mapaja iliyokaza kutokana na mazoezi.

Miguuni alikuwa amevaa viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio vya rangi ya bluu na harufu nzuri ya manukato ghali aliyokuwa amejipulizia mwilini ilitamalaki mle ukumbini

Japo alijitahidi kuonekana mchangamfu sana lakini macho yake yalionesha huzuni fulani, hakuwa na furaha kabisa. Alikuwa mbali kimawazo japo alionekana kama alikuwa anamwangalia msaidizi wake na mtayarishaji wa kipindi chake maarufu cha Madame Norah Show, Jessica Walari.

Wakati huo Jessica alikuwa anatoa maelekezo kwa wapigapicha za mnato na video wakati wakichukua picha za matukio mbalimbali za wabunifu wa mavazi waliokuwa wakiandaa mavazi na kuivalisha ‘midoli’ mikubwa iliyokuwepo eneo lile.

Pale kwenye masofa alipoketi Madame Norah pia kulikuwa na wageni wachache mashuhuri waliofika kumuunga mkono Madame Norah katika shughuli zake za kusaidia jamii. Kushoto kwa Madame Norah aliketi kijana mmoja mtanashati asiyezidi miaka therathini na tano, aliitwa Florian na alikuwa mpenzi wa Madame Norah.

Florian alikuwa mweupe, mwenye ngozi nyororo na umbo kakamavu la kimichezo, alikuwa amevaa fulani nyekundu na suruali ya jeans ya rangi ya bluu. Kichwani alivaa kofia nyekundu aina ya kapelo na miguuni alivaa raba ndefu na ngumu za rangi nyekundu.

Kama walivyo vijana wengi wenye tabia ya kupenda wanawake waliowazidi umri kwa sababu ya kutaka fedha zao, Florian hakuona aibu kuambatana na Madame Norah kila alipokwenda, na muda ule alikuwa amejiegemeza kwenye sofa katika hali ya mahaba.

Kuna muda alimnong’oneza jambo Madame Norah wakati akiongea na wageni wake, Madame Norah aligeza shingo yake kumtazama Florian na kuachia tabasamu pana la kimahaba, kisha alinyoosha mkono wake na kumgusa shingo yake.

Florian alikuwa ameweka mkono wake wa kulia juu ya paja la Madame Norah kisha aliuchukua mkono wa kushoto wa Madame Norah, moja kwa moja akaupeleka kwenye uso wake, aliupitisha kwenye paji la uso wake na kumfanya Madame Norah kuligusagusa paji lake.

Muda ukafika wapiga picha wakaweka tayari kamera zao kuzielekeza jukwaani kwa Madame Norah, kisha Jessica alitabasamu na kumpa ishara ya dole gumba kuwa wapo tayari kuanza kuchukua picha ya kilichowaleta pale.

Madame Norah alinong’ona jambo kwenye siko la Florian na kumfanya aachie kicheko hafifu cha mahaba. Madame Norah alitabasamu na kumpiga piga Florian mgongoni kwa mahaba, kisha Florian aliinuka taratibu na kuondoka akimwacha Madame Norah na wageni wake pale jukwaani.

Madame Norah alishusha pumzi za ndani kwa ndani, akaketi vizuri kwenye sofa, na baada ya kupewa ishara na Jessica, alianza kwa kujitambulisha na kuwatambulisha wageni wake kisha akaeleza lengo lake.

“Kwanza niweke wazi, maonesho ya mwaka huu yatakuwa tofauti kidogo na miaka mingine, tumeandaa kitu kinachoitwa Live from the Red Carpet kitakachowafanya watu wote wawe sehemu ya onesho. Litakuwa onesho kubwa kuwahi kufanyika Afrika kwani tumewaalika wabunifu na wanamitindo wakubwa duniani na lengo likiwa kutunisha mfuko ili kuwajengea makazi bora wazee wasiojiweza sambamba na kituo na shule ya watoto wenye ulemavu na waishio katika mazingira magumu chenye miundombinu rafiki kwa elimu yao na makazi. Itakuwa shule ya aina yake na ya kimataifa kwani baadaye tutaweza kupokea hata watoto kutoka maeneo mengine ndani na nje ya nchi…” Madame Norah alisema huku akiachia tabasamu.

“Kupitia Madame Norah Foundation tutazidi kutatua matatizo mbalimbali ya watoto na wazee wasiojiweza ambao ni kundi linaloonekana kusahaulika sana. Tumekuwa tukitoa misaada mbalimbali kwenye vituo vya yatima na hospitalini kusaidia watoto wadogo na hata wazee, tumekuwa tukisaidia huduma za afya, chakula na mambo mengine. Katika utafiti tulioufanya mwaka jana tumegundua kuwa kundi moja limesahaulika sana, ni la watoto wenye ulemavu. Kundi hili linazidi kuongezeka na wanakumbana na changamoto nyingi sana…” Madame Norah alinyamaza kidogo na kumeza mate ili kutowesha koo lake lililoanza kukauka.

Inaendelea...
 
Taxi - (36)

“Kwa miaka kumi sasa tangu niingie katika tasnia ya ubunifu na mitindo, mwaka huu tutayatumia maonesho haya kuandaa pia chakula cha hisani na kuwakaribisha watu mbalimbali mashuhuri, taasisi za serikali, mashirika na watu binafsi ambao watachangia fedha. Na hata tusipofikia lengo la kiasi kilichokusudiwa kukusanywa hatutaacha kujenga… kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Simamia ndoto yako usijali wengine wanasema nini’.” Madame Norah alimaliza hotuba yake na kuachia tabasamu.

Baada ya kutambulisha lengo lake waandishi wa habari walimuuliza maswali ambayo aliyajibu kwa ufasaha kisha alianza kuwatembeza waandishi na wageni kuwaonesha sehemu mbalimbali na kazi walizokuwa wanazifanya pamoja na hatua mbalimbali za ubunifu wa mavazi ndani ya lile jumba.

Baada ya kuwatembeza eneo lote Madame Norah aliagana na wageni wake kisha akaelekea kwenye ofisi yake binafsi iliyokuwa juu kabisa, kwenye ghorofa ya tatu ya lile jumba la kifahari.

Aliingia ofisini kwake na kuketi kwenye kiti kirefu cha kuzunguka cha kiofisi cha ngozi halisi kilichokuwa na magurudumu madogo yaliyokiwezesha kusogea.

Ilikuwa ofisi nzuri yenye samani za bei ghali, ikiwa na kiyoyozi aina ya Boss kilichokuwa kikisambaza hewa safi mle ndani, zulia nene la manyoya la rangi nyekundu sakafuni, meza kubwa ya kiofisi ambayo juu yake kulikuwa na kompyuta moja aina ya IMac Retina 5K ya inchi 27, kidau cha wino, mhuri na kichupa kidogo chenye wino mweupe wa kufutia maandishi.

Pembeni kulikuwa na meza nyingine ndogo ya kioo ya pembe nne na juu yake kulikuwa na chupa kubwa ya mvinyo mwekundu aina ya Navette de Marseille na bilauri, chini ya ile meza kulikuwa na magazeti na majarida mbalimbali ya mitindo.

Meza hiyo ilikuwa mbele ya kochi moja kubwa jeusi la sofa na ukutani juu ya ile meza ya kioo kulikuwa na shubaka la vitabu lililokuwa na vitabu na mafaili yenye nyaraka mbalimbali yaliyopangwa kwa ustadi mkubwa.

Upande wa kulia kulikuwa na madirisha mapana ya kioo yaliyokuwa na mapazia mepesi marefu ya rangi ya samawati, na pembeni kabisa kulikuwa na mlango ulioelekea kwenye maliwato maalumu ndani ya ofisi ile.

Pia kulikuwa na kabati kubwa la ukutani lenye mbao zilizosanifiwa kwa ustadi wa hali ya juu na kulikuwa na kioo kirefu cha kujitazama, pembeni yake kulikuwa na jokofu ukubwa aina ya BOSS lililojazwa vinywaji mbalimbali vya kumchangamsha yeyote aliyeingia humo, hata kama angekuwa amechoka sana baada ya kazi ngumu.

Akiwa na huzuni, Madame Norah alivuta droo moja ya meza yake na kutoa picha tatu, aliziangalia kwa kitambo na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akionekana kukata tamaa.

Zilikuwa picha zake za zamani, akiwa bado binti tineja. Picha moja ilimuonesha akiwa na wadogo zake wawili, wote wa kike, wakiwa wamesimama nje ya nyumba yao ndogo ya nyasi kijijini kwao Mkuzi Wilaya ya Muheza. Picha hiyo ilipigwa kama kumbukumbu baada ya kupata matokeo mazuri ya darasa la saba.

Madame Norah alikuwa amevaa gauni refu la zambarau lenye maua ya rangi mchanganyiko na alikuwa na miaka kumi na tano, wadogo zake mmoja alikuwa na miaka kumi na moja na mwingine alikuwa na miaka mitatu.

Picha ya pili aliipigia shuleni wakati huo akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Usagara jijini Tanga, alikuwa na wanafunzi wenzake na picha ya tatu alikuwa na kijana mmoja mtanashati wakiwa katika mkao wa kimahaba.

Aliitazama kwa kitambo kirefu ile picha ya tatu, mara matukio fulani ya zamani yakaanza kumjia akili kwake, alikuwa kama aliyekuwa anaangalia kipande cha filamu ya kuhuzunisha. Ilikuwa ni mchanganyiko wa picha mbalimbali za msichana mrembo wa miaka kumi na nane akiwa analia kwa uchungu katika chumba kidogo chenye mwanga hafifu wa taa.

Msichana huyo alikuwa mwenye huzuni nyingi na alitazama mbele yake kwa huzuni, wakati huo sauti ya mwanamume ilisikika ikimtaka aondoke haraka na haakutakiwa kuonekana tena pale. Kisha sauti ya mtoto mchanga akilia nayo ikasikika…

Madame Norah alizinduka kutoka kwenye yale mawazo, akaangaza macho yake huku na huko na kugeuka kujitazama kwenye kioo kirefu cha kujitazama, alijitazama kwa kitambo akionekana mwenye huzuni kubwa.

Michirizi ya machozi ilionekana kwenye mashavu yake na muda huo alianza kulia kwa uchungu kilio cha kwikwi. Alijiegemeza kwenye kiti chake huku akikumbatia zile picha kifuani kwake, akatoa leso na kupenga kamasi.

Sasa mawazo yalimjaa kichwani, alikumbuka juu ya taabu zote alizokumbana nazo maishani mwake mpaka kufikia pale. Jina lake halisi aliitwa Nuru Mhina.

Alikuwa na shahada zote za mwanamke mrembo, ingawa aliachishwa shule akiwa kidato cha nne, wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na nane, baada ya kugundulika alikuwa na ujauzito wa miezi sita. Alikabidhiwa barua aliyotakiwa kuipeleka kwa mzazi wake nyumbani, lakini asifike baada ya kukumbuka maneno ya mama yake:

“Unakwenda sekondari na umeshakuwa mwali sasa, kasome na uchunge sana kukaribiana na wanaume. Elimu ndiyo urithi wako pekee na siku ikitokea umefanya ujinga ukapata ujauzito basi utafute kabisa pa kwenda, usirudi hapa nyumbani…”

Mama yake alikuwa amemtolea uvivu wakati akijiandaa kwenda kuanza kidato cha kwanza jijini Tanga. Wakati huo alikwishatimu miaka kumi na tano na chuchu za usichana zilikuwa zimechomoza kifuani kwake kama embe dodo changa na kutishia kutoboa kila blauzi aliyovaa. Alikuwa na uzuri wa asili na ulimbwende wake uliwaka kama karabai gizani.

Lakini huko shule maisha yalikuwa magumu sana, alianza kuwa na kesi za shule kila iitwapo leo; hakuwa mtoro wala mjinga bali alikuwa na kesi za kukosa fedha ya michango ya hiki na kile. Hata fedha ya ada ilikuwa inalipwa kwa mbinde sana, kuna wakati alirudishwa nyumbani, wanakijiji wakachangishana ili kusaidia ndipo fedha ikapatikana. Kiujumla maisha yalimpigisha kwata na shule aliiona chungu.

Maisha ya shida yalimfanya ajiulize kwa nini hakuzaliwa kwenye familia zenye ahueni kama wanafunzi wenzake? Mama na wadogo zake walilazimika kula mlo mmoja tu, tena kwa shida ili yeye aweze kusoma.

Inaendelea...
 
Taxi - (37)

Alijitahidi kuivumilia ile dhiki lakini mambo yalianza kufikia ukomo wa uvumilivu. Alipoingia kidato cha nne alikuwa anaelekea kutimiza mwaka wa kumi na nane tangu kuzaliwa, lakini kwa sababu maisha yalimpigisha kwata ungeweza kudhani alikuwa anaikimbilia miaka therathini tangu alione jua. Usichana wake ulishambuliwa na utu uzima uliomjia ukiwa umevikwa koti la umasikini.

Lakini hadi wakati huo hakuwa amemfahamu mwanamume, alikuwa bado bikira! Ni katika kipindi hicho vishawishi vilizidi na yeye alitamani sana apendeze kama wasichana wenzake, hasa rafiki zake Mainda Shelukindo na Johari Mcharo. Nguo zake zilikuwa zimechakaa na hakuwa na viatu vya maana.

Ilifikia kipindi alitamani atafute fedha. Angezipataje sasa? Hakukuwa na njia nyingine ya kuzipata isipokuwa kufanya kama rafiki zake, hasa Mainda aliyekuwa akimsaidia mara kwa mara kalamu na madaftari, na wakati mwingine alimpa hata nguo zake na viatu alivyovichoka. Lakini hakumpa hivi hivi bali alimsema kwanza kwa kutochangamka. Walikuwa wakimshangaa, walidhani labda alitaka kuwa Mtawa!

Taabu ilikuwa kwamba hakuwa ameyazoea mambo ya umalaya. Haikuwa haiba yake kuukabidhi mwili wake kwa mwanamume kabla ya ndoa ili apewe fedha za kutatua matatizo yake. Hata hivyo, vishawishi kutoka kwa Mainda na Johari vilimpa kisebusebu. Roho ilimchonyota na fedha aliitaka.

Tena aliitaka sana tu na ushawishi wa rafiki zake ulivyomvika nguvu, Nuru akayavua mashaka na kuamua kujitosa. Ni wakati huo ndipo alipokutana na kijana wa aina na kariba yake. Kijana huyo aliitwa Rafael Jengo na alikuwa mtanashati kweli kweli.

Rafael ndiye aliyemwondolea ‘utoto’ wake na kumwingiza katika dunia ya watu wazima. Ndiye yeye aliyejitokeza kuwa faraja na furaha yake katika maisha yale ya shule, tangu alipoufahamu ulimwengu huu.

Walianza taratibu, siku za mwanzo zilikuwa za maumivu makubwa, hata hivyo, hakuwa na namna. Kwani ukitaka kula sharti uliwe! Alijikaza kwa kuwa alifahamu anapaswa kuvumilia ili afanikiwe kama rafiki zake, hasa Mainda. Akakomaa kweli kweli na baadaye akazowea.

Sasa alipopewa barua ya kumkabidhi mzazi wake hakuona sababu ya kurudi nyumbani, aliamua kwenda moja kwa moja eneo la Ngamiani alikokuwa akiishi Rafael, mwanamume aliyemkatizia ndoto yake ya kusoma ili aje kuwa mwanasheria.

Alimkuta Rafael akiwa na msichana mwingine nyumbani, walikuwa kitandani watupu kama walivyozaliwa. Nuru alishindwa kuvumilia. Msirimbi wa kipaji cha uso wake uliumuka, milizamu ikatutusika chini ya masikio yake kama iliyopulizwa, na mara kikamtoka kikohozi kikubwa na michirizi ya machozi ikapasuka machoni mwake.

Alilia kwa uchungu mkubwa mbele ya Rafael lakini mwenzake akakana kumfahamu yeye wala ujauzito wake. Kuona hivyo, Nuru hakutaka makuu, aligeuka akaondoka zake huku akilia kwa uchungu. Jambo moja lilimjia kichwani, atafute vidonge anywe ili afe yeye na mtoto wake tumboni.

Sauti nyingine ilimwambia mtoto tumboni hakuwa na kosa na yeye hakutakiwa kukata tama, kwani hakuwa wa kwanza kupata ujauzito akiwa shuleni. Sasa hakuwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kwenda kuomba hifadhi kwa rafiki yake Mary Mgaya aliyekuwa anaishi eneo la Kiriwani, barabara ya Pangani, nje kidogo ya jiji la Tanga.

Nuru alikuwa amefahamiana na Mary aliyewahi kuishi kijijini Mkuzi kwa mama’ake mdogo, wakati huo Nuru akisoma shule ya msingi. Hivyo Nuru alimwomba Mary asimwambie yeyote kama yeye aliishi kwake. Alijifungua mtoto mzuri wa kike, kisha alirudi tena Ngamiani nyumbani kwa Rafael na kumbwagia yule mtoto, yeye huyo akatorokea jijini Dar es Salaam.

Huko jijini Dar es Salaam alitafuta kazi kila sehemu, mwishowe aliajiriwa kazi ya kutunza nyumba na mama mmoja, mke wa meneja rasilimali-watu wa kiwanda cha Bora. Alilipwa mshahara kidogo wa kujikumu kwa mwezi, chakula bure, malazi bure, nguo alizozichoka mama mwajiri bure. Akatae? Ili iweje?

Maisha mapya yakaanza. Kutokana na uzuri wake wa asili haikuchukua hata mwezi akamfadhaisha baba mwenye nyumba na kumtisha mama mwajiri. Matokeo yake alitupiwa virango, akalipwa mshahara wake na nauli juu, kisha akatakiwa kuondoka mara moja na kurudi kwao Tanga.

Hakurudi. Afuate nini? Kwanza maisha ya nyumbani kwao yalikuwa magumu sana, maisha ya kuishi na mzazi mmoja tu wa kike, tena ya jembe na mpini wake! Halafu angemwambia nini mama yake? Aliamua kubaki Dar es Salaam. Kwa nini? Aliyekuwa baba mwenye nyumba alikuwa amenogewa na sasa alipanga kumlipia kodi kwa siri ili waendelee kubanjuka.

Alipewa fedha nyingi kisha akatafuta chumba eneo la Magomeni Makuti. Chumba chake hakikuwa kikubwa, kilikuwa cha kawaida ila hakikutofautiana na stoo, kilibeba kitanda kidogo cha futi tatu na nusu kwa sita pamoja na majukumu yote ya sebule, jiko, stoo na mengineyo.

Nyumba aliyopanga ilikuwa ya vyumba kumi, sita kwenye nyumba kubwa na vingine vinne vya mabanda ya uani. Alikuta wapangaji wengine, wengi wakiwa wasichana kama yeye, hivyo akawa amepata marafiki. Wakati huo ahueni ndogo ya maisha ilishamtembelea, alikuwa amepata wa kumpa vya kumuwezesha hata kupanga chumba kama kile.

Miezi miwili tu tangu ahamie hapo akapata kazi katika kampuni moja ya samani za ofisini na majumbani kama mkaribisha wateja, baada ya kumfurahisha mfadhili wake.

Nuru alianza kubadilika, alinawiri na kuwa mrembo kweli kweli, hata shoga zake walianza kumuonea donge. Chuki ikaanza kumea baina yao. Hakujali, kwani alikuwa na marafiki wengi wa kiume kuliko wa kike. Na ni hao ambao aliwahitaji zaidi. Mtaa ule akauhama na kwenda kuishi Kijitonyama, na hata jina alibadilisha, hakuitwa tena Nuru bali Madame Norah.

Katika kipindi hicho alifanya makosa mara tatu, mara ya kwanza aliruhusu ujauzito bila taarifa wala hiyari, hakumjua aliyempa ujauzito huo wala hakuhitaji mtoto. Suluhu ikawa kuutoa. Haikuchukua muda mrefu mimba nyingine ikanasa. Nayo akaitoa.

Mwaka mmoja baadaye akanasa ya tatu iliyomhenyesha kweli kweli! Hata hivyo, fedha kidogo alikuwa nayo, akampata daktari mmoja asiye na huruma aliyefanya kazi yake barabara, lakini yeye aliponea chupuchupu.

Inaendelea...
 
Taxi - (38)

Baada ya mwaka mmoja na nusu wa kufanya kazi katika kampuni ya samani za ofisini na majumbani aliachishwa kazi na kuanzia hapo hakutaka tena kuajiriwa, badala yake, alizidi kujitafutia riziki kutoka kwa wanaume mbalimbali, hakujali yupi ajaye, yeyote alikuwa sawa tu kwake ili mradi tu amkatie fedha za kutosha.

Siku moja jioni akiwa katika mawindo eneo la Hoteli ya Mawenzi, alikutana na kijana mmoja wa kizungu kutoka Sweden, Karl Johan. Madame Norah akamfurahisha kweli kweli Karl, kiasi cha kukiri kuwa ingawa alishatoka na wasichana wengi lakini kwa Madame Norah alipiga saluti, sasa aliamua kuchonga mzinga.

Karl akampeleka Madame Norah nchini Sweden, lakini mambo hayakwenda kama alivyopanga. Waliachana huku akimpa fedha nyingi za kujikimu pindi akirudi Tanzania. Lakini Madame Norah hakurudi Tanzania. Afuate nini?

Aliamua kubaki huko huko Sweden akihangaika na haikuchukua muda akaangukia katika penzi la mzungu mwingine aliyeitwa Andreas Gunnar. Andreas aliwahi kuwa balozi wa Norway nchini Tanzania na walikutana katika klabu ya usiku ya Tradgarden iliyopo barabara ya Harmmaby Slussvarg, jijini Stockholm.

Hapo ndipo bahati ya Madame Norah ilikuwa ikimsubiri, Andreas alikolea kweli kweli, kwanza akaamua kumpeleka shuleni akiwa na miaka 24 kumalizia masomo yake. Alimaliza na kupata ‘Daraja B+’, kisha alisoma katika Chuo cha Ubunifu cha Beckmans jijini Stockholm.

Kisha Andreas alimnunulia lile jumba la kifahari la ghorofa tatu eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam na jumba jingine la vyumba vinne katika mji wa Göteborg, mji wa pili kwa ukubwa nchini Sweden. Hakuishia hapo, alimsaidia kuanzisha duka kubwa la vipodozi na nguo za kike jijini Dar es Salaam.

Baada ya uhusiano wao uliodumu miaka kadhaa waliachana, Madame Norah akajiongeza na kuanzisha kampuni aliyoiita Nuru Group iliyokuwa mkusanyiko wa kampuni za vipodozi ya Madame Norah Cosmetics & Fashion; pamoja na kampuni ya Nuru Media iliyomiliki vituo vya Nuru FM na Nuru TV.

Miaka michache baadaye alifungua kampuni ya samani za nyumbani na ofisini aliyoiita Madame Norah Furniture Centre na mgahawa wa kisasa wa Nuru Foods Café (NFC) katikati ya jiji la Dar es Salaam…

Pamoja na mafanikio hayo bado hakuishi maisha ya furaha, alikuwa mtu mwenye maisha ya huzuni muda mwingi japo alijitahidi kuonekana mwenye furaha mbele ya watu. Tatizo nini? Kwanza suala la mtoto wake aliyembwaga kwa Rafael kule Ngamiani Tanga lilimsumbua sana.

Kwa umri wake asingeweza kupata mtoto mwingine kwani alikwisha toa mimba takriban nne na daktari wa mwisho alimtoa kizazi chake. Hakuwa akijua kama mtoto aliyembwaga nyumbani kwa Rafael kule Ngamiani alikuwa mzima au hata yeye alikufa kwa moto.

Alikuwa amekwenda Tanga kumtafuta Rafael baada ya kutoka Ulaya lakini taarifa alizozipata kule zilimchanganya sana, ile nyumba aliyoishi Rafael katika makutano ya barabara ya 10 na Mnyanjiani haikuwepo tena na badala yake ilijengwa nyumba nyingine mpya.

Alipouliza aliambiwa iliteketea kwa moto baada ya kutokea hitilafu ya umeme na kuua watu wanne waliokuwa wamelala ndani akiwemo mtoto mdogo. Hakuna aliyekuwa na kumbukumbu ya majina ya waliokufa! Bahati mbaya Madame Norah hakuwahi kumuuliza Rafael alitokea wapi, huenda angelikwenda kwao kupata uhakika…

Mara mlango wa ofisi yake ukagongwa na kumzundua Madame Norah kutoka kwenye lindi la mawazo. Alifungua mikono yake iliyokumbatia picha zake za usichana kifuani na kufuta haraka machozi yaliyomchuruzika kwenye mashavu yake, kisha alitoa leso na kupenga kamasi huku akizificha zile picha kwenye droo na kujiweka sawa.

Muda ule aliisikia vyema sauti ya mtoto ikilia kwa uchungu masikioni mwake na kuacha mwangwi moyoni na kwenye ubongo wake. Mlango ukagongwa kwa mara ya pili.

“Pita!” Madame Norah alisema kwa sauti tulivu huku akijiweka sawa kwenye kiti chake.

Mlango ulifunguliwa na msaidizi wake Jessica alichungulia na kumwona kisha akaingia ndani. Kwanza alisita, akasimama akimwangalia Madame Norah kwa udadisi na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Lakini hakuuliza.

“Unasemaje Jessica?” Madame Norah aliuliza huku akijaribu kuifanya sauti yake isikike ya kawaida.

“Madame, yule dada wa ile demo ya kipindi cha fashion amekuja,” Jessica alisema huku akiwa bado anamtazama Madame Norah kwa udadisi.

“Okay, mpeleke ukumbini anisubiri nakuja.”

Jessica alitoka, akaufunga mlango nyuma yake na kumwacha Madame Norah peke yake akiendelea kutafakari.

Jessica alikwenda moja kwa moja kwenye ukumbi kulikokuwa na wabunifu wa mavazi, alimkuta Joyce akiwa amesimama akiwatazama kwa makini wabunifu wa mavazi wakati wakikamilisha kazi zao za siku ile.

Alimchukua hadi kwenye makochi ya sofa na kumwonesha sehemu ya kuketi ili amsubiri Madame Norah. Wakati akiketi mara akamuona Madame Norah akija kwa mwendo wa madaha, akasimama na kumlaki, wakasalimiana na kuketi kwa mazungumzo.

Muda wote Joyce alikuwa anazungusha macho yake kustaajabu mandhari ya kupendeza ya eneo la ukumbi wa kisasa wa lile jumba la kifahari la Madame Norah.

Madame Norah alimtazama kwa tabasamu, hata hivyo, bado alihisi huzuni ndani ya moyo wake ikishindwa kwenda likizo japo kwa muda. Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na wakati huo huo Joyce aligeuza shingo yake kumtazama. Wakatazamana na kujikuta wakitabasamu.

Kwa mara ya kwanza, Madame Norah alihisi faraja kwa mbali moyoni mwake na huzuni ikipotea taratibu baada ya kuliona tabasamu la Joyce. Muda huo huo Florian alitokea na kumsalimia Joyce kisha aliketi ubavuni kwa Madame Norah, akaupitisha mkono wake nyuma juu ya bega la Madame Norah na kujiegemeza kwenye kochi.

Madame Norah alimtazama Florian kwa tabasamu na kunong’ona jambo kwenye sikio lake, Florian alimtupia jicho Joyce na kuinuka, akaondoka akiwaacha. Madame Norah alimtazama Joyce na kuachia tabasamu. Kisha kilifuata kitambo fulani cha ukimya.

“Unajua kwa nini nimekuita? Nilipoiona demo ya kipindi chako ilinishtua sana… Ilinikumbusha kitu fulani cha miaka mingi iliyopita!” Madame Norah alianza kusema na kuvunja ukimya.

“Baada ya hapo nikaanza kutafuta taarifa zako ili nikufahamu vizuri, niseme tu nimeipenda sana creativity yako na juhudi unazozionesha katika kutimiza ndoto zako. Keep it up, my dear.”

Endelea kufuatilia stori hii ya kusisimua ili kuujua mwisho wake. Ujue kwa nini tunaifuatilia taxi, ni ya nani na ina nini hiyo taxi?...
 
Taxi - (39)

Ilipoishia jana

Madame Norah alimtazama Florian kwa tabasamu na kunong’ona jambo kwenye sikio lake, Florian alimtupia jicho Joyce na kuinuka, akaondoka akiwaacha. Madame Norah alimtazama Joyce na kuachia tabasamu. Kisha kilifuata kitambo fulani cha ukimya.

“Unajua kwa nini nimekuita? Nilipoiona demo ya kipindi chako ilinishtua sana… Ilinikumbusha kitu fulani cha miaka mingi iliyopita!” Madame Norah alianza kusema na kuvunja ukimya.

“Baada ya hapo nikaanza kutafuta taarifa zako ili nikufahamu vizuri, niseme tu nimeipenda sana creativity yako na juhudi unazozionesha katika kutimiza ndoto zako. Keep it up, my dear.”

Sasa endelea...

Thank you, Madame,” Joyce alisema huku akiachia tabasamu, alihisi fahari kubwa kupewa sifa na mtu kama Madame Norah.

Creative thinking kama yako ni muhimu sana katika kutimiza ndoto ya mtu, na tofauti kubwa kati ya mtu aliyefanikiwa na wengine ni moja tu, kuthubutu…” Madame Norah alisema na kunyamaza kidogo, alimtazama Joyce kwa kitambo kirefu kisha akaangalia kando. Huzuni ilianza kujionesha tena usoni kwake.

Joyce hakuelewa kilichokuwa kikiendelea akilini kwa Madame Norah, alibaki kimya akisubiri kusikia zaidi kutoka kwa mtu aliyemhusudu na kutamani kufuata nyayo zake.

“Kuthubutu…” Madame Norah alirudia tena neno lile la mwisho, kisha akaongeza, “Lakini huwezi kupata uthubutu kama bado unategemea kupangiwa kila kitu na mwanamume. Mimi nimefika hapa baada ya kutambua kuwa ili niendelee ninapaswa kuwa bosi wa maisha yangu mwenyewe.”

Joyce alishtuka sana, akainamisha kichwa chake. Aliona kuwa Madame Norah alikuwa anampa mtihani mkubwa sana. Hata hivyo, Madame Norah alikuwa ameyasoma mawazo yake, akaachia tabasamu.

“Samahani kwa kukwambia haya, wewe ni sawa na binti yangu… ni kwamba huko nyuma nimewahi kutendwa na mwanamume niliyempenda kuliko chochote, aliniharibia maisha yangu na baadaye akanifukuza kama mbwa nyumbani kwake, wakati huo nilikuwa binti mdogo tu, na kilichofuata baada ya hapo sipendi hata kukikumbuka…” Madame Norah alisita kidogo na kufuta machozi yaliyoanza kumtoka.

Joyce alihisi kuingiwa huzuni lakini hakuweza kusema lolote, alibaki kimya akimtumbulia macho.

“Kisha nikawa na uhusiano na wanaume kadhaa lakini wao pia walitaka kunitumia tu. Ninashukuru mmoja wao ndiye alinisaidia kufika hapa nilipo, lakini kwa sasa sitaki mume, sitaki kuwa chini ya mwanaume. Huyu kijana niliyenaye sasa ni kwa ajili ya kujifurahisha tu na siyo kwa ajili ya mapenzi. Ninao uwezo kama wanaume, ninatoa amri na wao wanatekeleza, hivyo sina haja ya mwanamume atakayeniweka chini ya amri zake. Ninaamini katika falsafa ya kuwa: utafanikiwa tu endapo wewe ndiye bosi wa maisha yako!” Madame Norah alisistiza na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Ila kwa wewe uliyeolewa sikushauri umwache mumeo kama hakuzuii kutimiza ndoto yako na usianze kujiona uko juu yake… I know you have an amazing husband and a very strong marriage,” (Najua una mume makini na ndoa imara) Madame Norah alisema na kuachia kicheko hafifu.

Joyce aliachia tabasamu na kuangalia kando akiyakwepa macho ya Madame Norah.

“Unachotakiwa ni kumfanya akuamini na kukusaidia kufikia ndoto yako, kama kweli anakupenda,” Madame Norah alisema na mara akaonekana kukumbuka jambo. Alimwita Jessica.

Nisamehe sana, binti yangu, nimesahau hata kukuuliza utatumia kinywaji gani?” Madame Norah alimuuliza Joyce kwa upole baada ya Jessica kufika.

Joyce alimtazama Jessica kwa makini huku akizungusha macho yake kujaribu kufikiria, alivuta pumzi za ndani kwa ndani na kuminya midomo yake. “Mm… nitakunywa chochote,” hatimaye aliongea baada ya kufikiria kidogo.

“Tuna chai, kahawa, soda, juisi za boksi, bia za kopo, mvinyo mweupe na mwekundu… sijui ungependa nini?” Madame Norah aliuliza tena kwa sauti tulivu huku macho yake yakiweka kituo kwenye uso wa Joyce.

“Naomba juisi ya boksi… kama ipo tropical nitafurahi zaidi,” Joyce hakutaka kujivunga, alisema bila wasiwasi wowote.

“Okay, chukua funguo uende ofisi kwangu, chukua tropical juice kwenye jokofu langu, na mimi niletee chupa yangu ya mvinyo wa Navette de Marseille, ipo juu ya meza yangu,” Madame Norah alimwambia Jessica huku akimkabidhi funguo za ofisi yake.

Jessica alipokea kisha aligeuka na kuondoka haraka kutoka eneo lile, akaelekea kwenye ngazi za kuelekea juu. Madame Norah alishusha pumzi huku akimtupia jicho Joyce na kuachia tabasamu.

“Kwa kweli sijui kwa nini ninasukumwa sana kutaka kukusaidia ili uweze kutimiza ndoto yako, nimefikiria hata kukutafutia personal assistant ambaye nitamlipa…”

“Asante sana, mama… sijui nikushukuru vipi!” Joyce alisema huku akiinamisha kichwa chake mbele kwa heshima zote na kuikunjia mikono yake kifuani kuonesha shukrani za kipekee.

“Usijali… usijali, hata hivyo nina ushauri mdogo kwako, kama kweli unataka kufanikiwa basi simamia ndoto yako bila kujali nani atasema nini juu yako, na usikubali kukatishwa tamaa! Hii imekuwa siri kubwa ya mafanikio yangu,” Madame Norah alisema kwa sauti tulivu ya upole.

Muda ule ule Jessica alifika akiwa amebeba chano chenye vinywaji na bilauri, akakiweka juu ya meza ndogo iliyokuwa mbele yao kisha aliwakaribisha. Joyce aliitazama saa yake ya mkononi na kushtuka sana, ilikuwa imeshatimu saa mbili za usiku.

Mara simu yake ikaanza kuita, aliitazama kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Uso wake ulikuwa umesawajika kidogo kwani ilikuwa ni simu kutoka kwa mumewe Sammy na hakujua angemjibu nini.

Madame Norah alimtazama kwa makini, alijua kwa vyovyote vile, kuna jambo lilimsumbua.

“Ni mumeo huyo, bila shaka!” Madame Norah aliongea kwa sauti tulivu huku macho yake yakiweka kituo kwenye uso wa Joyce. Joyce alibetua kichwa chake kukubali na hapo Madame Norah alimuashiria apokee simu.

“Ooh… mjibu kuwa upo njiani ili usije ukamkwaza, ngoja nikuwahishe mara moja na gari yangu,” Madame Norah alimwambia Joyce huku akiinuka.

Joyce alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kubofya kitufe cha kupokelea, akaiweka simu kwenye sikio.

Endelea...
 
Taxi - (40)

“Nipo njiani nakuja!” Joyce alisema na kusikiliza kidogo huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani, “Haya!” alisema na kukata simu kisha aliinuka na kuchukua boksi lake la juisi. Wakatoka kuelekea kwenye gari la kifahari la Madame Norah.

* * * * *

Zilikuwa zimekwisha pita wiki mbili tangu Sammy aliposimamishwa kazi katika hoteli ya kitalii ya Udzungwa Beach Resort, kipindi chote hicho hakuwa amemweleza mkewe, kila siku alidamka alfajiri na kufanya mazoezi kama ilivyokuwa kawaida yake, kisha akajitayarisha na kuondoka kwenda Ilala Sharif Shamba kwa rafiki yake Elli.

Hata hivyo, katika kipindi kile cha wiki mbili alikwisha fika Udzungwa Beach Resort mara tatu kwa ajili ya kufuatilia stahiki zake.

Siku ya kwanza alimkuta Dk. Masanja aliyemtaka arudi kazini mara moja lakini alikataa akibainisha kuwa hakutaka tena kuajiriwa bali alitaka alipwe stahiki zake ili afanye shughuli zake. Dk. Masanja hakuwa na namna nyingine ila kutoa maagizo kwa mhasibu kuandaa hesabu na kumtaka Sammy arejee siku iliyofuata saa nne asubuhi.

Siku iliyofuata Sammy alifika ofisini kwa Dk. Masanja saa nne asubuhi kama walivyokubaliana lakini alisita baada ya kumkuta Mr. Oduya ndani ya ile ofisi akimsubiri. Dk. Masanja alimtoa wasiwasi Sammy kuwa Mr. Oduya hakuja kwa ubaya na kumtaka aketi kwenye moja ya viti vilivyokuwa ofisini.

Sammy aliketi lakini akiwa bado ana mashaka. Muda wote tangu alipoingia mle ofisini Mr. Oduya alikuwa yupo makini akimtumbulia macho kupitia juu ya miwani yake aliyoivaa kwa kuilegeza.

Pamoja na kuwa na wasiwasi lakini bado Sammy aliwasalimia kwa adabu kisha Dk. Masanja alimweleza kuwa ameshawasiliana na mhasibu na kila kitu kilikuwa kinakwenda vizuri, pia alimweleza kuwa Mr. Oduya alifika pale akitaka wazungumze.

“Kabla hatujaendelea mbele, vipi maisha yanakwendaje?” Mr. Oduya alimuuliza Sammy huku akitabasamu, macho yake yalikuwa yameweka kituo usoni kwa Sammy.

“Maisha yanakwenda vizuri sana,” Sammy alijibu kwa kujiamini huku akimtazama Mr. Oduya kwa makini.

“Vizuri… nimesikia kuwa hutaki tena kurudi kazini, kwa nini hutaki kazi?” Mr. Oduya aliuliza tena huku akiendelea kumkazia macho Sammy.

“Kwa sababu sitaki kuendelea kuwatumikia watu wasio na shukurani, ninaowaingizia fedha nyingi ili wanilipe mshahara, sasa ninataka kuwa bosi wa maisha yangu mwenyewe…” Sammy alisema kwa sauti tulivu huku akijitahidi kuizuia hasira iliyoanza kuchipua ndani yake.

“Mr. Kambona, naomba nisikilize kijana wangu, najua wewe bado kijana na una ndoto nyingi, ungependa kuwa na maisha mazuri zaidi, umiliki kampuni yako mwenyewe, watoto wako wasome kwenye shule bora zaidi na pengine nje ya nchi, utembelee magari ya kifahari na mambo mengine kadha wa kadha… nimekuja hapa lengo langu ni kutaka kukusaidia kutimiza ndoto zako…” Mr. Oduya alisema na kunyamaza kidogo, akameza mate kutowesha koo lake.

“Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikipata sifa zako kuwa wewe ni mwanamkakati mzuri sana wa kiufundi na matukio ndiyo maana umeipaisha sana hoteli hii na kupata tuzo nyingi… lazima niwe mkweli, unastahili makubwa zaidi, ndiyo maana niliposikia hutaki tena kazi nikataka uwe mshirika wangu kwenye masuala yangu ya…”

“Hilo haliwezekani, Mr. Oduya. Siwezi kuwa na ushirika na wewe,” Sammy alimkatiza Mr. Oduya huku akitingisha kichwa chake taratibu.

“Kama hilo haliwezekani then you’ll never make it,” Mr. Oduya alimwambia Sammy huku akitabasamu kwa dharau.

Now you’re threatening me, Mr. Oduya,” (Kwa hiyo sasa unanitishia, Mr. Oduya) Sammy alimwuliza Mr. Oduya huku akihisi damu mwilini mwake ikichemka na kwenda kasi kwenye mishipa yake ya damu.

This is not a threat, young man, this is a warning…” (Hiki siyo kitisho, kijana, hili ni onyo) Mr. Oduya alisema kwa sauti tulivu huku akiendelea kutabasamu kwa dharau.

“Kama hutataka kushirikiana nami basi hutaweza kufanikiwa kwenye mambo yako, ninaweza kuyafanya maisha yako kuwa magumu zaidi,” Mr. Oduya aliongeza.

“Tafadhali, mzee, usijaribu tena kunitisha…” Sammy alisema kwa hasira na kusimama, sura yake ilikwisha badilika na sasa alikuwa ameikunja na kutengeneza matuta madogo madogo usoni.

Calm down, Mr. Kambona. Lengo la Mr. Oduya ni zuri sana ni kwa vile hujamwelewa tu,” Dk. Masanja aliingilia kati kumtuliza Sammy.

Sammy hakutaka kuketi, huku akionesha kujiamini aligeuka na kuanza kupiga hatua kutoka nje. Mr. Oduya alibaki akimtumbulia macho, wakati Sammy akijongea mlangoni na kutoka.

Sammy alipotoka alipita kwa katibu muhtasi wa Dk. Masanja, mwanadada Salha Hamisi. Alimuaga kwa upendo pasipo kuonesha kama alikuwa amekerwa kule ndani, kisha akatoka na kuanza kuelekea nje ya jengo lile. Alipokuwa akipita eneo la mapokezi kuelekea kwenye lango kubwa ili atoke nje akamuona Salha akimjia mbio mbio huku akimwita.

“Unasemaje Salha?” Sammy alimuuliza Salha huku akigeuka kumsubiri.

“Bosi Masanja anakuita,” Salha alisema huku akihema kwa nguvu kutokana na kukimbia.

“Bosi wako anataka nini tena kwangu?” Sammy aliuliza huku akikunja sura yake.

“Sijui, wewe nenda kamsikilize, amesisitiza sana uende,” Salha alisema huku akimtazama Sammy kwa makini.

Sammy alifikiri kidogo, akawa kama anajishauri kisha akakata shauri kutorudi tena kwenye ofisi ya Dk. Masanja siku ile.

“Mwambie nitarudi siku nyingine, kwa sasa kuna sehemu natakiwa nifike kabla ya saa sita mchana,” Sammy alimwambia Salha na kuanza kupiga hatua za haraka kuondoka eneo lile huku akimwacha Salha anashangaa.

Inaendelea...
 
Taxi - (41)

Sammy alipotoka pale alielekea moja kwa moja kwenye mgahawa wa Elli’s, Ilala Sharif Shamba. Lakini hakumsimulia Elli wala yeyote kuhusu kilichokuwa kinaendelea kati yake na Mr. Oduya.

Baada ya siku mbili alirudi tena Udzungwa Beach Resort na kwenda ofisini kwa mhasibu wa kampuni kufuatilia suala la kulipwa stahiki zake. Haikuchukua siku nyingi akawa amepewa hundi, sasa akawa anatarajiwa kupata fedha ambazo zingemwezesha kukamilisha ndoto yake…

Siku ya Jumamosi na Sammy alikuwa nyumbani, hakujisikia kwenda popote, alihitaji kutulia na kupanga mambo yake vizuri kuhusu hatua ambayo ingefuata baada ya kukabidhiwa hundi yake siku mbili zilizokuwa zimeitangulia siku ile.

Pia siku ile alihitaji nafasi ya kumweleza mkewe kwa utulivu kuhusu matatizo yaliyojitokeza kazini kwake na mipango yake ya baadaye kisha angempa nafasi aongee ili asikie mawazo yake, huu ulikuwa ushauri alioutoa kwa Elli aliyemweleza kuwa, ‘kuambiana ukweli ni muhimu katika kuijenga familia’.

Siku ile alikuwa ameamka alfajiri kama ilivyokuwa kawaida yake akafanya mazoezi, kisha aliingia maliwatoni na kujiweka sawa, akarudi kitandani kulala. Alihisi uchovu hivyo uamuzi wake ulikuwa ni kulala tu hadi pale ambapo angehisi kuchangamka.

Ilipotimu saa tatu na nusu, akiwa bado yupo kitandani alishtuliwa na mlio wa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya mkononi. Alinyoosha mkono wake kuichukua na kufungua sehemu ya ujumbe mfupi. Ulikuwa unatoka kwa Elli: “Njoo hapa Ilala twende Kinondoni, kuna gari zuri sana limepatikana…”

Sammy aliachia tabasamu pana huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani. Aliinuka na kuingia maliwato, akashevu ndevu zake vizuri kwa mashine maalumu ya kunyolea ndevu huku akikinga mkono wake kwenye bomba la maji na kunawa uso wake huku akijifuta kidevu chake vizuri kwa maji, alipomaliza alijitazama kwenye kioo.

Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kupapasa kindevu chake akionekana kuridhika, akabetua kichwa chake na kutoka chumbani, alielekea sebuleni alipomkuta mkewe ameketi, akamuaga kuwa alikuwa amepata ujumbe mfupi uliomtaka afike kazini mara moja, kwani kulikuwa na kazi ya dharura. Akatoka na kuelekea kituo cha daladala.

* * * * *

Saa nne ya asubuhi ilimkuta Zainab akiwa amejiegemeza ukutani chumbani kwake, alikuwa kitandani karibu kabisa na dirisha akiangalia nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha, alikuwa akitazama mandhari nzuri ya kupendeza ya Paradise Club.

Alikuwa akiangalia kwenye lile eneo la maegesho ya magari akitaraji kumuona Mr. Oduya wakati akiingia. Hakuwa na raha kiasi fulani ingawa alionekana kujilazimisha. Kitu alichokuwa amekishuhudia asubuhi ile kilikuwa kimekataa kabisa kumtoka akilini mwake.

Hii ilikuwa ni baada ya kustafustahi na kuwasha runinga kisha aliweka chaneli ya taifa na kutazama taarifa ya habari, nia yake ilikuwa kujua kilichojiri duniani, hasa kwa kuwa tangu afike nchini alikuwa akishinda ndani na hakuruhusiwa kabisa kutoka nje.

Hakuwa na shida ya kutoka nje kwani kila alichokitaka basi Lilian alikuwepo kumhudumia. Alikuwa kama malkia aliyekuwa akipewa huduma zote za kimalkia ndani ya jumba la kifalme. Akikohoa tu Lilian huyu hapa kumsikiliza!

Taarifa ya habari ya asubuhi ile ilipofikia ukomo wake alitazama kipindi cha mapitio ya magazeti, kisha aliamua kubadilisha chaneli na kuweka ya burudani iliyorushwa na Nuru TV. Hapo ndipo alipokutana na kitu kilichoufanya moyo wake kumpasuka paa!

Akili yake ilianza kupoteza utulivu huku mitupo ya mapigo ya moyo wake ikiongezeka kasi! Alitaka kupuuza kile alichokuwa akikiona akidhani labda alikuwa ndotoni, hata hivyo, milango yake ya fahamu ilikuwa makini zaidi, na aliishirikisha akili yake kikamilifu katika kumletea taarifa za kuaminika.

Akajiambia kuwa wala haikuwa ndoto bali ni kitu halisi. Hali ile ikasababisha jasho jepesi lianze kumtoka mwilini huku mwili wake ukipigwa ganzi.

Oh my God!” Zainab alimaka kwa mshtuko huku akiikodolea ile runinga, hakuamini kabisa alichokiona. Alivuta pumzi ndefu ndani kisha alizishusha taratibu huku akiulegeza mwili wake na kujiegemeza pale kwenye sofa. Hata hivyo, alihisi kulikuwa na mtu aliyekuwa akimwangalia, akageuza shingo yake na kumuona Lilian aliyekuwa anapita kuelekea jikoni na kugundua kuwa alikuwa akimtazama kwa jicho la wizi.

“Vipi dada, kuna shida yoyote?” Lilian alimuuliza Zainab baada ya macho yao kugongana.

“Hapana, nimevutiwa sana na huyo mama anayeongea kwenye hiyo chaneli ya burudani,” Zainab alijibu huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Aah, huyo ni mwanamama anayejituma kweli kweli! Wengi wanamsifia kwani amekuwa mfano bora kwa wanawake wengi… ana mafanikio makubwa sana. Hiyo Nuru TV ni ya kwake, pia anamiliki kituo cha redio cha Nuru FM, mgahawa wa kisasa wa Nuru Foods Café na kampuni kubwa la vipodozi na nguo za Kike la Madame Norah Cosmetics & Fashion na mali zingine kibao,” Lilian alisema na kumfanya Zainab asisimkwe zaidi.

“Kwani ni Mtanzania na anaishi hapa hapa Tanzania?” Zainab aliuliza huku akishindwa kuficha mshtuko wake, alionekana kushangaa sana na muda wote macho yake yalikuwa yameweka kituo kwenye ile runinga.

“Ndiyo, ni Mtanzania ‘piwa’ na anaishi hapa hapa jijini Dar es Salaam, asili yake ni kutoka Mkoa wa Tanga…”

“Anaitwa nani?” Zainab alimtupia Lilian swali jingine huku akionekana kuwa na shauku.

“Anajulikana zaidi kwa jina la Madame Norah…”

“Madame Norah!” Zainab alidakia akiwa haamini alichokisikia.

“Ndiyo, Madame Norah. Ni mwanamke aliyejitosheleza hasa, anamiliki pia majumba ya kifahari eneo la Mikocheni alikoweka makao makuu ya ofisi za Nuru Group na eneo la Makumbusho kwenye vituo vyake vya redio na televisheni. Wanasema kuwa pia ana majumba Ulaya…” Lilian alisema maneno yaliyozidi kumchanganya Zainab na kujikuta akiishiwa nguvu.

Inaendelea...
 
Taxi - (42)

“Anaitwa Madame Norah!” Zainab aliwaza na kumeza funda kubwa la mate kutowesha koo lake lililokauka ghafla, aliyakaza macho yake kutazama kwenye runinga. Alijiuliza: Je, ndiye yeye yule aliyekuwa akimtafuta miaka yote hii au alikuwa amemfananisha? Na kwa nini atumie jina la Nuru kila mahali? Hapana huyo ndiye yeye!

Aliwaza, asingeweza kukosea na wala macho yake yasingeweza kumdanganya. Ila lile jina la Madame Norah ndilo lililomchanganya kidogo, ni tafauti na lile alilokuwa akilifahamu. Hata hivyo, watu hubadili majina yako, huenda hata yeye alilazimika kubadilisha jina!

“Mbona hata mimi nimebadili jina langu, badala ya Zainab Semaya sasa naitwa Suzanne Ross!” Zainab aliwaza na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Nimewahi kusikia habari za Madame Norah mara kadhaa kila nilipofuatilia habari za Tanzania wakati nikiwa Canada, ila sikujua kama mwenye jina hilo ndiye huyu ninayemshuhudia muda huu kwenye runinga!” Zainab alizidi kuwaza, uso wake ulizidi kupambwa na mshangao mkubwa.

Kwa kweli ile habari aliyokuwa ameisikia kutoka kwa Lilian ilikuwa imemsisimua sana, hata hivyo, akili yake ilikuwa bado ikisumbuka katika namna ya kutaka kufahamu mengi yaliyomhusu Madame Norah.

Alimtazama kwa makini Madame Norah pale kwenye runinga, alikuwa mrefu na mweupe mwenye umbo la kupendeza, alikuwa amevaa blauzi ya bluu ya mikono mirefu, suruali ya Jamsuit ya rangi nyekundu iliyolichora vyema umbo lake refu maridadi lenye kiuno chembamba lakini imara kikiwa kimebeba minofu ya mapaja iliyokaza.

Madame Norah alikuwa akiongea na waandishi wa habari kutambulisha shughuli zake. Zainab alichukua rimoti ya runinga iliyokuwa juu ya mkono wa lile sofa alilokalia na kuongeza sauti.

“…mwaka huu tutayatumia maonesho haya kuandaa pia chakula cha hisani na kuwakaribisha watu mbalimbali mashuhuri, taasisi za serikali, mashirika na watu binafsi ambao watachangia fedha. Na hata tusipofikia lengo la kiasi kilichokusudiwa hatutaacha kujenga… kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Simamia ndoto yako usijali wengine wanasema nini’.”

Zainab alishusha pumzi huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Madame Norah wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari huku tabasamu bashasha likiwa halimtoki usoni kwake. Zainab alikuwa na uhakika kuwa huyo ndiye na wala hakuwa amemfananisha.

Sasa alifikiria kuahirisha safari yake ya kurudi nchini Canada ili kuweka kwanza mambo sawa, aliamua kumsubiri Mr. Oduya ambaye alikuwa amemtuma mtu kwenda ofisi za shirika la ndege la Uholanzi la KLM kufanya mpango wa safari.

Ndipo Zainab alipoinuka na kuelekea chumbani kwake, akaketi kitandani. Akili yake ilizidi kusumbuka: huyu Madame Norah alikuwa wapi miaka yote hiyo na aliwezaje kufikia mafanikio makubwa kiasi kile, kama alivyosikia kutoka kwa Lilian?

Sasa kichwa chake kilianza kulemewa na mawazo, alikuwa akijiuliza maswali yaliyokosa majibu, kwani mwenye majibu alikuwa ni Madame Norah mwenyewe. Muda huo Zainab alikuwa ameketi jirani na dirisha akiyatazama magari yote yaliyoingia na kutoka katika eneo lile la Paradise Club akitaraji kumwona Mr. Oduya ili amsaidie kumpata Madame Norah.

“Enhee! Afadhali amefika,” Zainab alijiambia huku akiliangalia gari la Mr. Oduya aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe lilipokuwa likiegeshwa eneo maalumu la maegesho la Paradise Club, kisha akamwona Mr. Oduya akishuka na kushika mkoba wake wa kiofisi, akaanza kutembea kwa haraka kuelekea kule ndani huku akimwacha dereva wake ndani ya gari akisubiri.

Zainab alijiandaa kumkabili, baada ya dakika chache mlango wa chumbani kwake uligongwa, akakimbilia kuufungua.

“Waoo! Pole sana mpenzi wangu, pole na kazi,” Zainab alimwambia Mr. Oduya huku akimpokea ule mkoba na kuupeleka moja kwa moja mezani.

“Asante sana, mpenzi, mbona unashinda chumbani muda wote?” Mr. Oduya aliuliza huku akishusha pumzi. Alikaa kitandani.

“Nimeingia muda si mrefu,” Zainab alisema, na kama kawaida yake, alimvua koti Mr. Oduya na kufungua tai yake na kumfungua shati lake vifungo kisha akamvua viatu na soksi.

“Nimefanikiwa kila kitu nilichokuwa nakifuatilia…” Mr. Oduya alisema baada ya Zainab kumaliza kazi yake na kuketi kando yake huku akimtazama kwa makini.

Zainab alishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akaitupia jicho saa yake ya mkononi. Saa nne na dakika arobaini. Alimtazama Mr. Oduya kwa kitambo kirefu, uso wake haukuonesha tashwishwi yoyote.

“Vipi mpenzi, kuna tatizo lolote, naona kama hufurahii hiki kinachokueleza!” Mr. Oduya alimuuliza Zainab baada ya kuuona uso wake ukiwa hauna tashwishwi na yeye yupo kimya bila kuchangamka kama ilivyokuwa kawaida yake pindi walipokuwa pamoja.

“Nimeamua kuahirisha safari yangu…” Zainab alisema kwa sauti ya chini iliyobeba huzuni.

What?” Mr. Oduya alimaka kwa mshangao mkubwa huku akimtazama Zainab kwa makini.

“Siwezi kuondoka tena hadi nionane na mtu mmoja muhimu sana,” Zainab alisema huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Mr. Oduya. Alionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema.

“Ni mtu gani muhimu kuliko mimi? Mbona sielewi umepatwa na nini, mpenzi wangu?” Mr. Oduya aliuliza, uso wake ulikuwa bado una mshangao.

“Nimemuona dada yangu mkubwa, unakumbuka niliwahi kukueleza kuhusu familia yangu na jinsi dada yetu mkubwa alivyotoroka baada ya kupata ujauzito wakati nikiwa nina miaka sita…”

“Ndiyo nakumbuka.”

“Leo nimemuona… I need to see her,” Zainab alisisitiza.

“Umemuona wapi? Naona sasa unatafuta matatizo na ikigundulika kuwa upo nchini huoni kama itatuletea sote matatizo!” Mr. Oduya aliongea huku uso wake ukionesha mashaka.

“Wala hakutakuwa na tatizo lolote. Nimemuona kwenye televisheni, ninachokuomba mume wangu, fanya vyovyote uwezavyo unikutanishe naye, hata kwa kumleta hapa, nahitaji sana kuongea naye.”

“Sasa nitampata wapi, na anaitwa nani?”

“Madame Norah…”

What?” Mr. Oduya alishtuka sana, akamkazia macho Zainab kwa mshangao. “Is Madame Norah your elder sister?” (Madame Norah ni dada yako mkubwa?)

Yes, she’s my sister, blood sister,” (Ndiyo, ni dada’angu wa damu) Zainab alisema huku akilengwa na machozi.

Endelea kufuatilia stori hii ya kusisimua ili kuujua mwisho wake. Ujue kwa nini tunaifuatilia taxi, ni ya nani na ina nini hiyo taxi?...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom