Taxi - (12)
Chumba hiki kilikuwa ndani ya jumba kubwa la kifahari la ghorofa moja, mali ya Mr. Oduya, lililojengwa katika eneo la Kinondoni Makaburini. Lilikuwa jumba la vyumba vitano vya kulala vilivyosheheni samani zote muhimu, sebule mbili kubwa chini na juu, ukumbi wa chakula, ofisi na maktaba ya siri, na chumba cha siri cha mateso.
Kwa nje jumba lile lilionekana ni nyumba ya kistaarabu sana iliyokaliwa na mtu mwenye ukwasi, lakini ukweli ni kwamba halikuwa jumba lililokaliwa na mtu na kilichokuwa kikifanyika mle ndani kilidhihirisha kila aina ya unyama.
Akiwa bado kamkwida Abbas, Spoiler alikuwa amekunja sura yake huku akimtazama kwa ghadhabu.
“Sipendi tuumizane, hebu nitazame vizuri… I’m a monster. Kama hutanipa majibu sahihi ya nilichokuuliza naapa utakufa kwa maumivu makali sana!” Spoiler alimwambia Abbas kwa ukali huku akimwachia.
“One last chance, Mr. Reporter… ni kipi chanzo chako cha habari ulizoandika kwenye gazeti lenu?” Spoiler alifoka huku macho yake yakiwaka kama moto kwa ghadhabu.
Abbas alibaki kimya akimtazama Spoiler bila kusema chochote, alikuwa anavuja damu maeneo ya usoni. Walibaki wanaangaliana kwa kitambo huku kila mmoja akiwa na hasira.
Kitendo cha haraka sana kikatokea, Spoiler alimrukia Abbas na kumpiga ngumi tatu mfululizo za tumbo. Abbas aliguna kwa maumivu makali na kupepesuka, alijaribu kujiweka sawa lakini akapigwa tena ngumi zingine za mfululizo. Kisha Spoiler alimkwida tena na kumbamiza kwenye ukuta.
Spoiler alikuwa amepandwa na ghadhabu, alimkodolea macho Abbas na kuchomoa kisu kutoka kwenye ala yake huku akimtazama kwa ghadhabu, kisha akakielekeza kwenye koo lake.
“Subiri… nadhani sasa yupo tayari kuzungumza,” sauti nzito ya Mr. Oduya ilisikika kutoka kwenye spika zilizokuwa zimefungwa mle chumbani.
Mr. Oduya na mwanamume mmoja aliyeitwa Adam Mafuru walikuwa wamesimama nje ya kile chumba lakini waliweza kuona na kusikia kila kitu kilichoendelea mle chumbani kupitia kioo kikubwa kilichokuwa ukutani.
Mafuru alikuwa mrefu na mweusi mwenye umbo kakamavu la kimichezo. Alikuwa na miaka isiyopungua arobaini na alivalia shati jeupe la mistari ya rangi ya bluu la mikono mirefu, suruali ya jeans ya rangi nyeusi na raba nyeusi.
Macho yake yalikuwa makubwa na mekundu na muda wote yalikuwa makini. Alikuwa msomi wa shahada ya pili ya sheria aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mafuru ndiye alikuwa mwanasheria wa kampuni na familia ya Mr. Oduya kwa miaka zaidi ya kumi.
“Abbas, nadhani umeona kinachoweza kukutokea endapo hutaonesha ushirikiano, tambua hatupo hapa kukuumiza. Ni rahisi tu… tuambie ni kipi chanzo chako cha taarifa kisha tutakuacha uende zako!” sauti nzito ya Mr. Oduya ilivuma ndani ya kile chumba kupitia spika.
Abbas aliendelea kukaa kimya pasipo kujibu chochote. Spoiler alimwachia na kuchukua koleo ndogo mbili kisha akakibana kidole kimoja cha Abbas kwa koleo na kuanza kung’oa kucha.
“Aarrgghh! Fu** you… motherfu***r!” Abbas alipiga kelele kubwa iiliyofuatana na matusi mazito kutokana na maumivu makali.
“Kama hutaki tuumizane sema ukweli ili nisiendelee kung’oa na hizi kucha zingine,” Spoiler alisema kwa ukali lakini Abbas aliendelea kuporomosha matusi mazito, akitukana ukoo wote wa Spoiler.
Spoiler alimchapa kofi kali usoni lililomsababisha kuona vimulimuli, hakuishia hapo, aliachia tabasamu la kinyama na kuanza kumshushia kipigo kikali. Ndani ya dakika tano tu chumba chote kilitapakaa damu na Abbas alikuwa hatazamiki.
“Sasa tueleze tunachotakiwa kujua…” Spoiler alisema huku akishusha pumzi ndefu.
Pamoja na yale mateso makali lakini Abbas aliendelea kuwa kimya, alikuwa ameazimia kutosema chochote, hata ikibidi kuuawa. Uso wake haukuwa na chembe ya mashaka wala uoga. Ni kama alikwisha kata shauri la kufa na siri yake moyoni.
Spoiler alimtazama kwa kitambo kisha alichukua kibubu kidogo cha gesi na kukiwasha, akarekebisha moto kwenye kile kibubu na kumfuata Abbas.
“Tunazo njia nyingi za kukulazimisha uongee ukweli usitake tufike huko, sasa sema ukweli vinginevyo nitakuharibu usiweze kutambulika,” Spoiler alimwambia Abbas huku akiupeleka ule moto wa gesi na kuupitisha kwenye kifua chake.
“Unanitishia kuniua? Wewe ni mpumbavu. Kwa taarifa yako siogopi kifo… hutapata chochote toka kwangu, bora mniue tu kuliko kuendelea kupoteza muda wenu,” hatimaye Abbas alifoka na kumtemea mate Spoiler.
“Naona umejitolea kufa peke yako huku wanaokutuma wakiendelea kustarehe huko waliko,” Spoiler alisema na bila kusita aliujaribu ule moto wa gesi hewani kisha aliupeleka kwenye maeneo nyeti ya Abbas, akaupulizia na kuanza kumuunguza. Abbas alitoa sauti kali ya maumivu.
“Sema ukweli ili nimwambie aache hili zoezi, sipendi tuumizane,” sauti ya Mr. Oduya ilisikika kutoka kwenye spika.
“Hamtopata chochote toka kwangu, wala msihangaike,” Abbas alisema kwa ukali huku akiendelea kugugumia kwa maumivu.
“Unaonekana shujaa, eh! Sijawahi kumuona mtu mpumbavu kama wewe, unadhani kwa hiki unachokifanya utaandikwa kwenye vitabu vya kumbukumbu za mashujaa wa nchi hii? Kwa taarifa yako, hata famlia yako hawawezi kukusifia kwa upuuzi huu!” sauti ya Mr. Oduya ilisikika ikiongea kwa hasira kutoka kwenye spika.
“Naona anatuchezea akili zetu, mpe kubwa kama hataki kutapika taarifa muhimu anazozifahamu,” Mr. Oduya alisema kwa hasira.
“Hawezi kuhimili na anaweza kupoteza maisha…” Spoiler alisema huku akiminya midomo yake.
“Nani anajali!” Mr. Oduya alijibu huku sauti yake ikionesha ghadhabu.
Sasa Mr. Oduya alimtaka Mafuru kwenda kusaidia, na bila kuchelewa Mafuru aliingia kwenye kile chumba. Kufumba na kufumbua Abbas alivuliwa nguo zake na kubaki mtupu kama alivyozaliwa kisha alibebwa na kutundikwa kwenye vile vyuma mfano wa vyuma vya kuning’inizia nyama buchani, kichwa chini miguu juu.
Dakika mbili baadaye Spoiler alikuwa ameshika visu viwili maalumu vilivyokuwa kwenye sinia juu ya meza, akavikamata na kuanza kuvinoa kwa kuvisugulisha vyenyewe kwa vyenyewe huku akitembea mbele ya Abbas.
Nini kitaendelea? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kusisimua...