Taxi - (20)
Ilipoishia...
Madame Norah mwenye umri wa miaka 50, alikuwa mwanamke mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa, alikuwa amejitosheleza kwa vitu vingi. Alimiliki kituo cha redio na cha televisheni, kampuni kubwa ya samani za majumbani na ofisini, mgahawa wa kisasa katikati ya jiji la Dar es Salaam na duka kubwa la vipodozi na nguo za kike.
Alikuwa mrefu na mweupe mwenye umbo kubwa kiasi lililosheheni vema na kunesanesa, likafanya kila jicho la mwanamume lililomuona kumtazama mara mbili mbili. Alikuwa mcheshi na mwenye ushawishi mkubwa asiyependa kuwa chini ya mwanamume, ndiyo maana hakutaka kuolewa.
Ingawa alikuwa na umri mkubwa, lakini ilikuwa vigumu mno kumtofautisha na wasichana wenye umri mdogo kutokana na urembo wake usiochujuka, hakuwa mwanamke wa kumtazama mara moja tu ukamwacha. Watu wengi walijiuliza kuwa endapo aliweza kuonekana mrembo kiasi kile katika umri huo, ilikuwaje enzi za usichana wake?
“
Joyce, are you there?” sauti ya Madame Norah ilimgutusha Joyce aliyekuwa ameanza kutekwa na mawazo.
“Oh… Madame Norah! Samahani mama’angu, kwa kweli sikutegemea kabisa kupata simu yako…” Joyce alisema huku akibabaika kidogo.
Sasa endelea...
“Ooh… usijali,” Madame Norah alijibu, na papo hapo akauliza, “Kesho Jumapili utakuwa na ratiba gani?”
“Kesho muda gani?” Joyce aliuliza kwa shauku kubwa.
“Jioni.”
“Nitakuwepo tu nyumbani, sina pa kwenda.”
“Naomba uje ofisini kwangu Mikocheni tuongee, japo maongezi yangu yanaweza yasiwe matamu kama ya mumeo! Au wasemaje?” Madame Norah alisema kwa madaha na kuachia kicheko hafifu.
“Sawa tu nitafika muda huo, sijui saa ngapi?” Joyce aliuliza huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
“Saa kumi na mbili…” Madame Norah alisema na kuongeza, “
See you at that time.”
“
Okay, Madame!” Joyce alisema huku akipitisha ulimi wake kwenye mdomo wake ulioanza kukauka, na hapo simu ikakatwa. Joyce hakuamini, alibaki akiitazama simu yake huku uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu bashasha. Alionekana kuwa na furaha isiyo kifani.
Kisha alijiegemeza kwenye sofa huku akiendelea kutabasamu, na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Muda huo kipindi cha “
Madame Norah Show” kilichokuwa kinaendeshwa na Madam Norah mwenyewe kilikuwa kinarushwa kwenye runinga, Joyce alichukua
rimoti ya runinga akaongeza sauti.
Muda wote tabasamu lake lilikataa kwenda likizo, alimwangalia Madame Norah kwenye runinga kwa makini sana na kuonekana kuvutiwa naye. Pendo alikuwa ameketi kwenye sofa jirani na mama yake akifuatilia kwa makini kila kilichokuwa kinaendelea pale sebuleni. Hakusema neno bali alikuwa anamwangalia mama yake kwa makini.
Winifrida aliingia pale sebuleni akitokea jikoni na kuketi juu ya mkono wa sofa huku akimwangalia Joyce kwa makini, kisha akaguna.
“Wifi, mbona umefurahi sana, inaonekana unampenda sana Madam Norah!” alisema Winifrida.
“Madame Norah ni mfano mzuri wa mwanamke mjasiriamali… natamani sana kufikia mafanikio kama yake,” alisema Joyce huku akishusha pumzi ndefu.
“Mama, kwani na wewe unataka kuwa kama Madam Norah?” Pendo alimwuliza mama yake huku akimkazia macho kwa makini.
“Ndiyo mwanangu, natamani sana na ninaamini Mungu atanisaidia.”
“Kwa hiyo na wewe utamwacha baba yangu?” Pendo alimwuliza tena Joyce na kumfanya amtazame kwa mshangao.
“Kwa nini nimwache baba yako? Kwani haya maneno huwa unayapata wapi we mtoto!” Joyce alimwuliza pendo huku akiendelea kumtazama kwa mshangao.
“Si wanasema Madam Norah hataki wanaume!” Pendo alisema kwa kujiamini na kuwafanya wote wamkodolee macho kwa mshangao. Winifrida aliziba mdomo wake kwa kiganja cha mkono.
“We mtoto wewe… ni nani kakwambia maneno haya?” Joyce aliuliza huku mshangao ukiwa bado haujamtoka usoni kwake. Winifrida aliachia kicheko hafifu na kumfanya Pendo naye acheke.
“Watu wanasema, hata anti Winnie alikuwa anasema…” Pendo alisema huku akinyoosha kidole chake kumuonesha Winifrida.
“Aka! Lini mimi nimekwambia? Utakuja kusutwa we mtoto!” Winifrida alimkata kauli Pendo na kumruka huku akiinuka na kubetua mabega yake juu. Joyce aliguna tu na wala hakujua la kufanya wala kusema.
* * * * *
Sammy alikuwa ameketi kwenye kiti kifupi chenye foronya laini ndani ya mgahawa mkubwa wa kisasa wenye kuta safi za vioo, uliokuwa ukimilikiwa na rafiki yake, Elli Kiango, na juu ya meza ya mbao ya mti wa
mpodo kulikuwa na chupa kubwa ya maji baridi ya
Kilimanjaro na bilauri ndefu.
Nje ya ule mgahawa kulikuwa na bango kubwa jeupe juu yake lililokuwa na maandishi makubwa ya rangi nyekundu yakisomeka ‘
ELLI’S’. Pia kulikuwa na eneo la maegesho ya magari na kulikuwa na takriban sabini yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho ya magari na mengi yalikuwa ya watu wenye vipato vya juu.
Elli’s ulikuwa mgahawa wa kisasa kabisa wenye kila aina ya vionjo vya daraja la kimataifa, ukifananishwa na migahawa mikubwa duniani kama McDonald;
Royal Dragon;
West Lake ulioko Mji wa Changsha, China;
Varsity Downtown wa Atlanta, Georgia;
Lundy’s wa Brooklyn, Newyork;
Cosmo wa Croydon, Uingereza n.k.
Kutokana na umaarufu wa mgahawa huo, Elli’s ulikuwa na uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 2,000 kwa siku na uliajiri wafanyakazi zaidi ya 200 waliotoa huduma mbalimbali katika mgahawa huo.
Mgahawa huo ulikuwa na mandhari yenye ubora iliyowafanya wageni wengi kuingia kwa wingi na kujionea mandhari yake na vivutio vilivyopo kwenye mgahawa huo.
Pia ukubwa wa majengo yake yaliyotengenezwa kwa ustadi wa hali juu yakiambatana na nakshi zilizochorwa na kutengenezwa kwa ustadi zikiashiria mila na tamaduni za makabila yaliyopo Tanzania ndiyo sababu zilizowafanya watu wengi pamoja na wageni mbalimbali kutembelea mgahawa wa Elli’s.
Ulikuwa na ukumbi maalumu mkubwa wa vyakula mbalimbali (
dining hall) vya watu wa mataifa tofauti uliokuwa na utulivu wa kutosha, ukiwa na meza ndefu za kisasa zilizozungukwa na viti vizuri vya sofa vyenye foronya laini. Ukumbi huo ulikuwa na uwezo wa kubeba takriban watu 500, ambapo wateja walikaa kwa vipindi fulani (
shifting zone).
Pia kulikuwa na ukumbi mwingine mkubwa wa kisasa uliotumika kwa ajili ya burudani au mikutano mbalimbali, ukumbi ule ulikuwa na jukwaa zuri la kisasa lililokuwa likitazamana na viti vingi vya kisasa na ulikuwa na uwezo wa kuingiza watu wasiopungua 1,000 kwa wakati mmoja bila bugudha yoyote.
Huduma ya mtandao wa intaneti ya
WiFi (
Wireless Fidelity) haikukosekana ndani ya ukumbi ule, hasa kwa mtu mwenye kifaa kilichoweza kunasa taarifa za kimtandao wa intaneti, kama simu za kisasa za mkononi, kompyuta na kadhalika.
Muda ule wa mchana kulikuwa na sauti ya muziki laini wa taratibu iliyosikika kutoka katika spika zilizokuwa sehemu fulani ndani ya ule mgahawa na kuzikonga vizuri nyoyo za watu waliofika kwa ajili ya chakula, vinywaji au huduma zingine muhimu.
Inaendelea...
Cc
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego