Stori ya kusisimua - Taxi

Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (13)

Ilipoishia

“Hamtopata chochote toka kwangu, wala msihangaike,” Abbas alisema kwa ukali huku akiendelea kugugumia kwa maumivu.

“Unaonekana shujaa, eh! Sijawahi kumuona mtu mpumbavu kama wewe, unadhani kwa hiki unachokifanya utaandikwa kwenye vitabu vya kumbukumbu za mashujaa wa nchi hii? Kwa taarifa yako, hata famlia yako hawawezi kukusifia kwa upuuzi huu!” sauti ya Mr. Oduya ilisikika ikiongea kwa hasira kutoka kwenye spika.

“Naona anatuchezea akili zetu, mpe kubwa kama hataki kutapika taarifa muhimu anazozifahamu,” Mr. Oduya alisema kwa hasira.

“Hawezi kuhimili na anaweza kupoteza maisha…” Spoiler alisema huku akiminya midomo yake.

“Nani anajali!” Mr. Oduya alijibu huku sauti yake ikionesha ghadhabu.

Sasa Mr. Oduya alimtaka Mafuru kwenda kusaidia, na bila kuchelewa Mafuru aliingia kwenye kile chumba. Kufumba na kufumbua Abbas alivuliwa nguo zake na kubaki mtupu kama alivyozaliwa kisha alibebwa na kutundikwa kwenye vile vyuma mfano wa vyuma vya kuning’inizia nyama buchani, kichwa chini miguu juu.

Dakika mbili baadaye Spoiler alikuwa ameshika visu viwili maalumu vilivyokuwa kwenye sinia juu ya meza, akavikamata na kuanza kuvinoa kwa kuvisugulisha vyenyewe kwa vyenyewe huku akitembea mbele ya Abbas.

Sasa endelea...


Saa sita na robo mchana, bado kulikuwa na mvua, lakini ilikuwa imepungua na kuwa ya manyunyu mepesi, Sammy alikuwa bado kasimama pembezoni mwa korido za lile jengo lenye maduka ya mavazi na vipodozi katika eneo la Kinondoni Studio.

Baada ya mvua kunyesha kwa takriban saa moja na ushee hatimaye ilianuka na kuliachia jua lenye kupunga la mchana likijitokeza kwenye mawingu na kuifanya miale yake mikali kuleta uhai mpya.

Kukatika kwa mvua kulimfanya Sammy aanze kujivuta taratibu kusogea kwenye kituo cha daladala cha Kinondoni Studio ili apate usafiri wa kumpeleka Tabata Chang’ombe.

Kama yalivyokuwa maeneo mengi ya vituo vya daladala yenye pilika pilika, kituo cha Kinondoni Studio kilitawaliwa na pilika pilika za hapa na pale za kibinadamu. Kulikuwa na wachuuzi wa maji na ice cream, wauzaji wa korosho na bila kusahau wapiga debe waliokuwa wakishindana kuita abiria.

Kwa muda ule wa mchana wa saa sita na ushee hakukuwa na shida yoyote ya usafiri, magari mengi yalikuwa na abiria wachache. Sammy hakusubiri kwa muda mrefu mara akaliona basi moja aina ya Toyota Coaster lililofanya safari zake kati ya Tabata Chang’ombe na Makumbusho, likiwa na abiria waliokaribia kujaza siti huku zikibakia siti chache zilizokuwa wazi.

Sammy alijivuta taratibu na kuingia ndani ya lile basi akiwa na abiria wengine watatu, akaiendea siti ya nyuma kabisa ya dirishani upande wa dereva na kuketi. Kelele za wapiga debe na wachuuzi wa biashara ndogo ndogo ziliendelea kusikika katika eneo lile.

Dakika chache baadaye lile daladala likaanza safari ya kuelekea Tabata Chang’ombe. Muda wote Sammy alikuwa ameketi kwa utulivu akiangalia nje na sura yake ilionesha huzuni kubwa kwa kuwa hakujua hatima yake baada ya kile kilichotokea.

Alionekana kuzidiwa mno na mawazo yaliyomjia kichwani kwake, hasa tukio la kukutana na Mr. Oduya nje ya fensi ya hoteli ya Udzungwa Beach Resort, na lile tukio la kuzuka kwa mtafaruku kati yake na yule muhuni aliyetumwa na Mr. Oduya lilikuwa bado mawazoni mwake na lilimshtua mno kuliko hata tukio la kupewa barua ya kusimamishwa kazi.

Alihisi donge la uchungu likimkaba kooni, alimeza mate kwa nguvu mithili ya mtu aliyejaribu kumeza pande la nyama mbichi lililokuwa limemkwama kooni, kuna wakati alishindwa kuuzuia uchungu na kujikuta akitokwa na machozi.

Alipojishtukia aliyafuta machozi haraka na kugeuza shingo yake kuwatazama abiria wengine waliokuwamo humo garini kabla hajayaondosha macho yake haraka na kuangalia nje akihisi macho ya wale abiria yalimtazama muda wote.

Alichukua leso toka mfukoni na kujifuta vizuri uso wake kisha akairudisha ile leso mfukoni, aliendelea kutafakari kwa kina. Alijiuliza ikiwa angeendelea na mpango wake wa kukata rufaa kutokana na kusimamishwa kazi kwa kitendo alichodhani ni cha uonevu au aachane na suala hilo na kutafuta kazi sehemu nyingine!

Hata hivyo, alipomkumbuka Mr. Oduya na timu yake alihisi mwili wake ukisisimka kwa woga, kwani aliamini wasingeacha kumfuatilia baada ya kugundua kuwa alikuwa amesikia mengi ya siri yaliyohusu mipango yao.

Sasa mawazo mengi mchanganyiko yalizidi kutawala kichwa chake na kumfanya ahisi kuchanganyikiwa, kichwa chake kilianza kuwa kizito na alianza kunyemelewa na usingizi.

Mara alijikuta akiwa katika pori lililokuwa na miti mingi mikubwa na nyasi fupi fupi, hali ya hewa ilikuwa haioneshi kama ilikuwa mchana au usiku. Sammy alikuwa anakimbia huku akitweta, hakujua kwa nini alikuwa anakimbia.

Aliamua kugeuka kutazama nyuma na hapo akamuona askari wa kampuni ya ulinzi ya Spark K7, Fred akimkimbilia na mkononi alikuwa ameshika bunduki. Sammy aliogopa sana na kujaribu kuongeza mwendo lakini pumzi zilianza kumuishia.

“Bosi simama, mimi sina nia mbaya na wewe!” Fred alisema huku akihema kwa nguvu.

Sammy hakusimama, alijitahidi kuongeza mwendo lakini kila alivyokuwa akikimbia, miguu yake ilimjulisha kwamba ilikuwa imeishiwa damu na hivyo ilikaribia ganzi. Hakutaka kukata tamaa, alijikaza na kuiburuza wakati ikizidi kunyong’onyea.

Alipogeuka tena kutazama nyuma alihisi miguu yake ikikubali na kumpa hatua, akaamua kuongeza mwendo lakini alishtukia mguu wake wa kushoto ukitumbukia kwenye shimo dogo lililokuwa mbele yake na kumfanya apepesuke kabla hajaanguka kama mzigo.

Fred alimfikia huku akitweta, akamshika bega la kushoto na kuanza kumtikisa taratibu. “Bosi, vipi!”

Sammy alinyanyua uso wake kumtazama Fred kwa mshangao kwani sauti aliyoisikia haikuwa ya Fred bali ilikuwa kavu ya mwanamume mwingine, ilisikika vyema masikioni kwake kisha ikifuatiwa na milio ya sarafu.

Kama ilivyokuwa ada ya makondakta wengi wanavyochezesha fedha za sarafu mikononi kwa mtindo wa kipekee, mlio wa sarafu ulimgutusha Sammy kutoka katika usingizi ambao hakujua ulimpitia muda gani.

Sammy aliinua uso wake kumtazama yule kondakta aliyekuwa akichezesha sarafu huku akimtikisa bega lake taratibu, na hapo akagundua kuwa ilikuwa ndoto aliyoota baada ya kupitiwa na usingizi. Alitazama nje na kugundua kuwa walikuwa kwenye foleni ya kuvuka taa za kuongozea magari barabarani za Buguruni Shell.

Kondakta aliendelea kuchezesha zile sarafu mbele ya Sammy kumkumbusha alipe nauli, na haraka Sammy aliingiza mkono wake mfukoni na kutoa pochi yake, kisha alitoa noti ya shilingi 10,000 na kumpa yule kondakta.

Wakati yule kondakta akirudisha chenji ya Sammy lile daladala lilikuwa linavuka zile taa za kuongozea magari barabarani za Buguruni na kushika uelekeo wa barabara ya Mnyamani iliyokuwa ikipitia Vingunguti.

Barabara ile ilikuwa na watembea kwa miguu wengi waliopita kando ya barabara nyembamba ya Mnyamani, lakini ikiwa na magari machache muda ule wa mchana, yaliyotoka au kwenda katikati ya mji, na mengi yalikuwa ni daladala. Sammy alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku mwili wake ukitetemeka kwa njaa.

Alifumba macho yake na kujiegemeza kwenye siti huku akipiga miayo ya uchovu na njaa. Hakika siku ile ilikuwa ndefu sana kwake, hakujua hatima yake baada ya kile kilichotokea kazini kwake. Aliitupia jicho saa yake ya mkononi na kushtuka baada ya kuona kuwa ilikuwa imeshatimu saa saba na robo.

Inaendelea...
 
Taxi - (14)

Baada ya dakika kadhaa hatimaye walilivuka daraja la Mto Msimbazi uliokuwa ukiyatenganisha maeneo ya Vingunguti na Tabata, na mara mvua ya manyunyu mepesi ilianza tena kunyesha. Muda wote Sammy alikuwa mwingi wa mawazo na macho yake yaliangalia nje. Alikuja kushtuka baada ya kumsikia kondakta akitangaza kuwa wamefika katika kituo cha daladala cha Barakuda.

Daladala lilisimama na abiria wachache wakaanza kushuka. Sammy aliamua kushukia hapo kisha akajiweka sawa na kuruka mtaro uliokuwa kando ya ile barabara, ilikuwa imekwishatimu saa 8:00 za mchana.

Sammy aliamua kuelekea kwenye pub maarufu ya Barakuda ili kupata chakula na ikibidi apunguze uchovu na mawazo huku akitafakari jinsi ya kumweleza mkewe kilichompata kazini kwake.

* * * * *

Ilikuwa imetimu saa 5:30 usiku, Spoiler aliwaongoza vijana wawili, Uledi Mkama na Dulla Mcomoro, vijana shupavu waliokuwa wafanyakazi wa siri wa Mr. Oduya waliotumwa kutekeleza mipango yake haramu, kuingia katika chumba cha mateso, maarufu kama Hell.

Uledi Mkama mwenye umri wa miaka therathini, alikuwa mfupi na alivaa fulana nyeusi iliyombana na kulionesha vyema umbo lake lililojengeka kwa misuli na suruali ya jeans ya rangi ya bluu. Miguuni alivaa buti ngumu aina ya ‘safari boot’ za rangi ya hudhurungi.

Dulla Mcomoro alikuwa mrefu na mweupe mwenye asili ya nchini Comoro, alikuwa na umbo kakamavu kama wachezaji wa mpira wa kikapu wa Marekani. Alikuwa amevalia shati la bluu la mikono mirefu, suruali nyeusi ya jeans na raba nyeusi. Alikuwa na macho makubwa na mekundu yenye uchovu lakini yaliyokuwa na kila dalili ya kuonya.

Walipoingia katika chumba cha mateso waliukuta mwili wa Abbas ukiwa umelala sakafuni ukionekana umechakazwa vibaya na damu zilikuwa zimeenea chumba kizima. Kwanza waliduwaa, hawakuelewa! Ilikuwa kama wanaota ndoto ya ajabu ajabu inayotisha kuliko vitisho vyote.

Walitanabahi kuwa hawakuwa ndotoni, bali walikuwa wanatazama sinema ya kuogofya kupita kiasi. Pamoja na kuwa wamekwisha shiriki katika matukio mengi ya kihalifu lakini kwa mara ya kwanza walihisi kushikwa na kichefuchefu. Hawakuhitaji kutapika badala yake walijikuta wakitokwa na sauti ya mshangao wa ghafla.

Walikuwa wazoefu wa masuala ya utesaji na hata mauaji na walitegemea kuwa hawangeweza kushtuka sana kwa kukabiliana na maiti, lakini hiyo ilikuwa picha ya kutisha, picha isiyoelezeka wala kutazamika kwa jinsi mwili wa Abbas ulivyoonesha kuwa alikuwa amekufa kinyama.

Walimtupia jicho Spoiler huku wakihisi kuwa hakuwa binadamu wa kawaida isipokuwa mnyama. Vinginevyo, angewezaje kumuua yule mtu namna ile! Spoiler aliachia tabasamu, ni kama vile aliyasoma mawazo yao.

“Msijali… huyu bwana alistahili kabisa kufa,” Spoiler aliwaambia huku akibetua kichwa chake baada ya kuwaona bado wamezubaa kisha aliongeza, “Fanyeni kazi yenu haraka, hatuna muda wa kupoteza.”

Waliuchukua ule mwili wa Abbas, wakautoa pale na kuuingiza katika kiroba kikubwa, eneo lile lilisafishwa vizuri kwa maji yenye dawa maalumu, kisha walipulizia dawa maalumu iliyoondoa harufu ya damu na kuliacha eneo safi.

Walipomaliza waliondoka wakakichukua kile kiroba chenye mwili wa Abbas hadi katika buti la gari, wakaondoka zao na kwenda kukizamisha kile kiroba baharini kwenye kina kirefu cha maji.

Habari ya Abbas Dalali, mwandishi mahiri wa habari za uchunguzi wa gazeti la MamboLeo ikaishia hapo...

* * * * *

Zilikuwa zimebakia dakika chache tu kutimia saa 6:00 usiku, katika ukumbi wa wazi kwenye pub ya Barakuda wateja walikuwa wachache wakiwa wameketi kwenye meza za duara na pana za plastiki zilizokuwa zimezungukwa na viti vinne vinne na zikiwa chini ya miavuli mizuri na mikubwa ya kujikinga na mvua au miale ya jua.

Kulikuwa na wahudumu wa kike warembo waliokuwa wakiwahudumia wateja wale waliokuwa wameketi kwa utulivu kwenye zile meza huku wakijipatia vinywaji, na eneo lote lilipendezeshwa na taa nzuri za rangi mbalimbali zenye mwanga hafifu.

Kulikuwa na runinga mbili pana zilizokuwa zimetundikwa ukutani pale ukumbini na zilikuwa zimejikita katika kurusha matangazo ya mpira wa miguu wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Hata hivyo, sauti ya muziki laini wa kubembeleza unaoweza kuacha kumbukumbu ya muda mrefu kwa mtu yeyote baada ya kuondoka eneo lile ilikuwa ikisikika kutoka katika spika zilizokuwa zimetundikwa maeneo fulani kwenye kona za ukumbi ule na hivyo kuzikonga vizuri nyoyo za wateja waliokuwa pale.

Sammy alikuwa bado yupo pale kwenye pub ya Barakuda na alikuwa ameketi kwenye meza moja ya pembeni kabisa, karibu na kibanda cha kutolea pesa kwa njia ya simu, akiwa peke yake. Alikuwa ameinamisha kichwa chake na kukilaza juu ya mikono yake aliyoikunja na kuiegemeza juu ya meza. Ni wazi alikuwa amelewa chakari.

Kuna muda alionekana kushtuka na kuinua kichwa chake, akafinya macho yake kwa ulevi na kuangaza huku na kule huku akiyumbayumba kiasi. Mkoba wake mdogo wa kiofisi ulikuwa chini katikati ya miguu yake.

Jasho lilikuwa linamtoka kwenye paji la uso na tai shingoni ilikuwa imelegezwa na kuachwa ikining’inia. Juu ya meza yake kulikuwa na chupa kubwa ya pombe ghali aina ya Grant’s Blended Scotch Whisky, bilauri moja na chupa ndogo ya soda aina ya Club Soda.

Hadi muda ule Sammy alikuwa ameshakunywa aina tofauti za pombe, kwanza kabisa aliagiza Savanna akaigida kama maji na kutaka aletewe nyingine, hiyo nayo aliigonga fasta ikaisha. Kisha aliagiza Heineken na kunywa yote lakini bado alikuwa na stress, hivyo akaagiza konyagi ndogo.

Alipomaliza tayari alikuwa ameanza kuchangamka, akaagiza chupa kubwa ya Grant’s na chupa ndogo ya soda aina ya Club Soda, sasa alianza kunywa taratibu.

Sammy aliitazama ile chupa kubwa ya Grant’s, akasonya na kuinyanyua bilauri iliyokuwa na pombe nusu na kuinywa pombe yote kwa mkupuo mmoja huku akisisimkwa mwili, kisha aliikita ile bilauri juu ya meza na kuinyanyua ile chupa ya Grant’s, alitaka kumimina pombe nyingine kwenye bilauri lakini hakuna kilichotoka. Chupa ilikuwa tupu!

Sammy alisonya tena na kumwita mhudumu, msichana mrefu na mweusi mwenye haiba nzuri ya kuvutia aliyekuwa akipita jirani na meza yake. Yule mhudumu alikuwa na nywele nyeusi ndefu na laini alizokuwa amezifunika kwa kofia ya kapelo.

Alikuwa amevaa sare ya baa, fulana nyeupe iliyokuwa imeyaficha vyema matiti yake makubwa na suruali nyeusi ya jeans. Yule mhudumu alikuwa amebeba kitenga kidogo cha kubebea vinywaji kwa ajili ya kupeleka kwa wateja na ndani yake kulikuwa na chupa mbili za bia zilizokuwa tupu.

“Enhe, unasemaje kaka yangu?” yule mhudumu alimuuliza Sammy huku akimwangalia kwa makini.

“Ongeza chupa nyingine kama hii,” Sammy alisema huku akiyumbayumba.

Yule mhudumu alimtazama Sammy kwa kitambo fulani na kutingisha kichwa chake kukataa. “Umeshalewa sana, isitoshe ni saa sita usiku, muda wa kufunga baa,” alisema.

Inaendelea...
 
Taxi - (15)

Yule mhudumu alimtazama Sammy kwa kitambo fulani na kutingisha kichwa chake kukataa. “Umeshalewa sana, isitoshe ni saa sita usiku, muda wa kufunga baa,” alisema.

“Noo… nimesema leta chupa kubwa ya Grant’s Blended Scotch Whisky, mimi siyo mwanafunzi… sina shida na hapa nimejileta mwenyewe,” Sammy alisema huku akimkazia macho yule mhudumu.

Macho yake yalikuwa yamewiva na kuwa mekundu kwa sababu ya ulevi, alitema mate huku akiiangalia ile chupa kubwa ya Grant’s iliyokuwa juu ya meza.

“Kwanza hii chupa ni ndogo, mimi niliagiza chupa kubwa, au unadhani mimi kipofu, siyo?” Sammy alifoka huku akiinua ile chupa kubwa ya Grant’s na kumuonesha yule mhudumu.

Yule mhudumu alimtazama Sammy kwa mshangao mkubwa kana kwamba alikuwa ameona kitu cha kushangaza sana, akatingisha kichwa chake huku akiachia mguno.

This is small bottle, iko wapi chupa yangu kubwa?” Sammy alifoka kwa hasira huku akiinua ile chupa na kuanza kutikisa tikisa huku akiipunga hewani.

“Hii ndiyo chupa kubwa. We kaka nilikuona mstaarabu kumbe ni mkorofi kiasi hiki!” yule mhudumu alisema kwa mshangao huku akionekana kukerwa sana.

Sammy aliinyanyua tena ile chupa ya pombe na kuipunga hewani, safari hii aliinua uso wake kuitazama kwa dharau sana. “No. This is small bwana! Call the manager.”

“Meneja hayupo…” yule mhudumu alisema huku akigeuka kutaka kupiga hatua za kuondoka na hapo hapo Sammy akamkata kauli.

I don’t care! Call the manager now! Wezi wakubwa nyie… niitie Meneja!” Sammy alifoka kilevi huku akiinuka.

Yule mhudumu aligeuza shingo yake, akamtazama Sammy kwa hasira kisha alianza kupiga hatua za kuondoka lakini Sammy aliwahi kuinuka, akamshika mkono na kuung’ang’ania kwa nguvu.

“We mwanamke, unadhani mimi nimelewa, eh? Sijalewa… mimi siyo mjinga,” Sammy alisema huku akiyumba yumba.

Yule mhudumu aliutoa mkono wake kwa nguvu kutoka kwenye mikono yenye nguvu ya Sammy huku akionekana kupandwa na hasira. Sammy aliyumba na kuanguka chini kisha aliachia tusi zito. Yule mhudumu alimwangalia Sammy kwa makini huku akiwa amekunja sura yake akionekana kutafuta ufumbuzi kisha alishusha pumzi na kuondoka haraka eneo lile.

Sammy aliinua uso wake kumtazama yule mhudumu aliyekuwa anaondoka eneo lile na kusonya kilevi. Alijitahidi kuamka taratibu pale chini alipokuwa ameanguka huku akipepesuka na kufanikiwa, kisha akajiweka sawa.

Alisonya na kuanza kuvuta hatua zake taratibu huku akipepesuka akionekana kutaka kuondoka eneo lile, kama aliyekumbuka jambo, aligeuka akaichukua ile chupa ya pombe na kuondoka huku akisahau ule mkoba wake wa kiofisi.

Mara alisimama na kuanza kujipekua pekua kwenye mifuko yake ya suruali akionekana kutafuta kitu, kisha akafikiria kwa kitambo cha sekunde chache na kurusha mikono yake hewani, akajiweka sawa huku akiyumba yumba.

“Msifikiri nitakaa kimya… lazima niende polisi… kwenye vyombo vya habari… nitawaambia watu woote kwamba ninyi ni wezi! Shenzy taipu!” Sammy alifoka kwa sauti kali ya kilevi na kuwafanya watu wachache waliokuwepo eneo lile kugeuka na kumtazama kwa mshangao.

Aliondoka taratibu na kuruka kizingiti cha uzio uliotenganisha lile eneo la baa na maeneo mengine huku akipepesuka, kisha akashika njia ya kuelekea kwenye barabara ya kuelekea Segerea.

Yule mhudumu alirudi eneo lile akiwa ameongozana na meneja wa ile baa, mwanamume mfupi na mnene mwenye tumbo kubwa na uso wa mtoto mdogo, lakini Sammy hakuwepo eneo lile ila mkoba wake wa kiofisi ulikuwepo! Walimtizama huku na huko lakini hakuwepo!

“Yule kule anaondoka!” mteja mmoja miongoni mwa wateja wachache waliokuwepo eneo lile muda huo alisema akiwaonesha kwa kidole kule alikokuwa Sammy. Walimuona Sammy akitembea kwa kuyumba yumba, akipita kwenye eneo lenye mwanga hafifu.

Wakati huo alikuwa anavuka barabara ya kuelekea Segerea huku akiyumba na kukoswa koswa kugongwa na gari dogo aina ya Toyota RAV4 lililokuwa linapita kwa mwendo wa kasi.

“Afadhali kaondoka, asije akatuletea matatizo,” alisema yule meneja wa baa na kuongeza, “Fungua mkoba wake tuone kuna nini ndani kisha utauhifadhi vizuri kule stoo, najua kesho pombe zikimuisha kichwani ataufuata.”

Yule mhudumu aliufungua ule mkoba wakatazama ndani na kuiona kompyuta mpakato (laptop) aina ya MacBook Pro na nyaraka kadhaa za kiofisi, wakaufunga na kuuchukua kisha waliondoka nao kuelekea ndani ya ile baa.

Sammy aliendelea na safari yake, alipita chini ya miti kisha akakatiza katikati ya kiwanja cha mpira chenye mchanga huku akipepesuka, miguu yake ilionekana kuwa mizito kiasi wakati alipokuwa akipiga hatua na alionekana kana kwamba alikuwa anashindwa hata kuinyanyua sawasawa wakati akitembea. Mkononi alikuwa bado ameshika ile chupa tupu ya pombe.

Mvua iliyokuwa imenyesha mchana wa siku ile ilikuwa imesababisha maji kutuama na kusababisha madimbwi ya maji. Sammy aliteleza na kuanguka mara mbili kisha alijinyanyua akaendelea kutembea huku akipepesuka mithili ya mtoto mdogo aliyekuwa anajifundisha kutembea.

Aliingia kwenye dimbwi kubwa la maji yaliyotuama na kuanguka kwa mara ya tatu, akajaribu kukusanya nguvu zake ili ainuke lakini hakuweza. Alianza kutambaa kwa mikono kama mtoto, akijitoa ndani ya lile dimbwi la maji, lakini kila alipojaribu kujiinua alishindwa.

Alilazimisha kuinuka kwa nguvu na kufanikiwa kusimama wima lakini alishindwa kuhimili myumbo wa mwili wake na kuangukia kando kidogo ya lile dimbwi la maji, akalala chali huku nusu ya kiwiliwili chake kuanzia eneo la kiuno kuelekea miguuni likiwa ndani ya lile dimbwi la maji.

Nguo zake zilikuwa zimelowa chepechepe na muda huo alikuwa anahema kwa nguvu akionekana kukosa kabisa nguvu, alitulia kidogo na kusikilizia akiwa bado ameshikilia ile chupa tupu ya pombe.

Muda ule ule simu yake ya mkononi iliyokuwa imedondoka kando kidogo ya lile dimbwi la maji, kwenye eneo kavu kiasi lenye nyasi ilianza kuita.

Ilikuwa ni simu kutoka kwa mkewe Joyce, na Sammy alikuwa amemhifadhi kwenye kumbukumbu ya majina ndani ya simu yake kama “Wife”. Sammy alianza kutawanya mikono yake huku na huko kupapasa akiitafuta ile simu.

Simu iliita hadi ikakatika, Sammy akakusanya tena nguvu zake zote na kufanikiwa kuinuka, alisimama huku akionekana kuanza kupata nguvu kutokana na kuoga yale maji baridi ya mvua yaliyotuama kwenye dimbwi. Hata hivyo alikuwa hatamaniki kwa jinsi alivyolowa chapachapa.

Muda ule ule walionekana vijana wawili wakora walioelekea kule alikokuwa, mmoja alikuwa ameshika panga na mwingine alikuwa na nondo mkononi.

Sammy aliwaona wakati wakimsogelea na kupatwa na hofu, hata hivyo hakuondoka eneo lile bali alisimama huku akipepesuka tayari kwa kukabiliana nao, wale vijana wakora walimfikia na kumzingira, mmoja mbele yake na mwingine nyuma.

Mambo yanazidi kunoga, tukutane hapahapa kwa ajili ya muendelezo wa kisa hiki cha kusisimua...
 
Ndio style yako lakini inaboa wasomaji. These are constructive criticisms, ignore them at your own risk, consider them at your own progress
Nashukuru kwa maoni yako lakini hiyo ndiyo style yangu ya uandishi, na-enjoy kuelezea kile ninachokiona kwenye akili yangu. Kama hupendi sina namna nyingine ya kukulazimisha...
 
Taxi - (16)

Ilipoishia

Nguo zake zilikuwa zimelowa chepechepe na muda huo alikuwa anahema kwa nguvu akionekana kukosa kabisa nguvu, alitulia kidogo na kusikilizia akiwa bado ameshikilia ile chupa tupu ya pombe.

Muda ule ule simu yake ya mkononi iliyokuwa imedondoka kando kidogo ya lile dimbwi la maji, kwenye eneo kavu kiasi lenye nyasi ilianza kuita.

Ilikuwa ni simu kutoka kwa mkewe Joyce, na Sammy alikuwa amemhifadhi kwenye kumbukumbu ya majina ndani ya simu yake kama “Wife”. Sammy alianza kutawanya mikono yake huku na huko kupapasa akiitafuta ile simu.

Simu iliita hadi ikakatika, Sammy akakusanya tena nguvu zake zote na kufanikiwa kuinuka, alisimama huku akionekana kuanza kupata nguvu kutokana na kuoga yale maji baridi ya mvua yaliyotuama kwenye dimbwi. Hata hivyo alikuwa hatamaniki kwa jinsi alivyolowa chapachapa.

Muda ule ule walionekana vijana wawili wakora walioelekea kule alikokuwa, mmoja alikuwa ameshika panga na mwingine alikuwa na nondo mkononi.

Sammy aliwaona wakati wakimsogelea na kupatwa na hofu, hata hivyo hakuondoka eneo lile bali alisimama huku akipepesuka tayari kwa kukabiliana nao, wale vijana wakora walimfikia na kumzingira, mmoja mbele yake na mwingine nyuma.

Sasa endelea...

Yule aliyeshika panga alimtazama Sammy kwa makini kisha alinyanyua lile panga lake kutaka kumpiga na ubapa mgongoni lakini kabla hajapata fursa hiyo Sammy aliwahi kulikwepa kirahisi na kusababisha lile panga likate upepo.

Pigo hilo lilikuwa kama la kumzindua tu kwani wakati huo huo alifyatuliwa miguu kwa namna ambayo hakuitegemea na kujikuta akiviringika chini kwenye maji machafu. Mara tu alipotaka kuinuka alifyatuliwa tena, na hapo kengere ya hatari ikalia kichwani kwake.

Sammy hakutaka kujilegeza, akiwa amekwisha jiandaa alianguka hali huku akiachia teke lililompata mmoja wao tumboni na kumfanya apepesuke. Kisha alianza kuwarushia ngumi na mateke huku akikwepa lile panga na nondo vilivyomkosakosa kichwani.

Lakini kutokana na pombe alizokuwa amekunywa alikuwa anayumba na hatimaye alianguka chini, alipotaka kuinuka mkora mmoja alimuwahi kwa teke kali la kwenye mbavu na kumfanya aachie yowe hafifu la maumivu huku akijikunja pale chini.

Wale wakora walizidi kumshambulia Sammy kwa vipigo ili kumlegeza, yeye alijitetea huku akipangua mateke, ngumi, ubapa wa lile panga na nondo. Wakati akiendelea kupangua alifanikiwa kusimama lakini ghafla alipigwa pigo moja bila kutegemea lililompata barabara usoni na kumpa kisulisuli, akadondoka huku akitoa yowe kali, nguvu zikaanza kumuishia.

Muda ule ule zikasikika sauti za watu waliokuwa wanakimbilia eneo lile ili kutoa msaada. Wale wakora walimsachi haraka haraka na kuchukua pochi yake, wakachukua fedha na kuitupa kando, mmoja alimvua viatu vyake kisha wakakimbia kutoka eneo lile wakimwacha anatokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili wake.

* * * * *

Palishakucha muda mrefu na ilishatimu saa nne za asubuhi. Sammy alikuwa bado chakari akiwa amelala fofofo na asubuhi ile kwake ilikuwa bado liamba. Alikuwa amelala kifudifudi akiwa ana uchovu mkubwa uliotokana na pombe mchanganyiko za usiku uliotangulia, ‘hangover’.

Chumba chake kilikuwa kikubwa chenye maliwato ya ndani kwa ndani (master bedroom) na hakikuwa na vitu vingi sana isipokuwa kitanda kikubwa cha samadari cha futi sita kwa sita, cha mbao ngumu za mkongo, chenye droo mbili kila upande zilizokuwa na taa za rangi ya bluu.

Pia kulikuwa na kabati kubwa la nguo la ukutani na meza nzuri ya vipodozi maarufu kama ‘dressing table’ iliyokuwa na kioo kirefu cha kujitazama mwili mzima.

Sakafuni kulikuwa na zulia pana la bluu lililokuwa na maua ya rangi nyekundu na manjano. Chumba kilikuwa na madirisha mawili mapana yaliyokuwa yamefunikwa kwa mapazia marefu yenye nakshi za michoro ya maua yaliyodariziwa vizuri.

Sammy akiwa bado yupo chakari akiuchapa usingizi, kichwa chake kilikuwa kizito mithili ya mtu aliyekuwa ametwishwa kiroba cha mchanga.

Ghafla, watoto walioanza kupiga kelele nje ya nyumba walimtoa katika usingizi na kumkera, tena walimkera hasa! Sammy aliinua shingo yake, akakigeuzia kichwa chake upande mwingine huku akiziba masikio na kuendelea kulala, hata hivyo zile kelele zilizidi kumkera masikioni. Akasonya kwa hasira.

Alijaribu kuinua kichwa chake lakini aliuhisi ule uzito wa kichwa na alikuwa bado ana mawenge ya usingizi, ukichanganya na uvivu uliomjaa, vilimpa hali ya kutaka kuendelea kuuchapa usingizi, licha ya jua la asubuhi kuhanikiza nuru ya kutosha mle chumbani mwake.

Miale ya jua la saa nne asubuhi ilikuwa imepenya dirishani na kutuama ikienea hadi pale kitandani alipokuwa amelala tangu kulipopambazuka. Joto la miale ile ya jua lilikuwa limeamsha homa hafifu mwilini mwake, homa iliyotokana na pombe mchanganyiko alizokunywa usiku ulioitangulia siku ile.

Sammy alikuwa mnywaji wa kawaida wa bia mbili au tatu tu basi na hakuzoea kunywa pombe kali, hivyo aliutaka utulivu kwa gharama yoyote ile, japo aweze kumalizia n’gwe ile ya usingizi, hakujua uchovu ule ungekwisha saa ngapi. Alichojua yeye ni kulala tu hadi pale mwili wake ungemruhusu kufarakana na kitanda. Watoto walizidi kumkera kwa kelele zao.

Walikuwa watoto wa pale mtaani, eneo la Tabata Chang’ombe, waliokuwa wanacheza asubuhi ile baada ya kushiba chai ya asubuhi. Hawakuwa na kingine cha kufanya isipokuwa kucheza tu, kwani ilikuwa ni siku ya Jumamosi na hapakuwa na shule.

Hao watoto ndio waliomgutua Sammy toka usingizini, kwa kuwa walikuwa wanacheza karibu na dirisha la chumba chake. Japo nyumba yake ilikuwa imezungukwa na ukuta lakini umbali kutoka ule ukuta hadi pale dirishani kwake ulikuwa mdogo sana, isitoshe kulikuwa na uwanja mpana ulioruhusu watoto kucheza.

Kelele za watoto zilimfanya Sammy ajihisi kama mtu aliyekuwa anapigiwa zumari sikioni, alisonya huku akiminya sura yake kana kwamba alikuwa anahisi maumivu makali ya kichwa. Alikuwa amechefukwa kweli kweli!

Aliwavumilia kidogo wale watoto huku akiinua shingo yake na kuzisikiliza sauti zao kwa makini, akazitambua kwani mojawapo ilikuwa sauti ya mtoto wake wa miaka 8 aliyeitwa Pendo, na nyingine ilikuwa ya dada yake mdogo wa miaka 17 aliyeitwa Winifrida.

“Winnie! We Winnie!” Sammy aliita kwa sauti kali ya kukaripia.

“Abee!” Winifrida aliitikia kwa sauti ya juu huku akisogea zaidi pale dirishani.

“Naomba niondosheeni hizo kelele zenu hapo dirishani kwangu. Alaa!” Sammy alitoa amri yake kwa sauti ya kufoka kidogo huku akihisi kizunguzungu na mate kumjaa kinywani, alikunja ndita usoni.

Winifrida aliwaondosha wale watoto kutoka eneo lile, na muda ule ule Sammy alisikia mlango wa chumba chake ukifunguliwa, aligeuza haraka shingo yake kumtazama aliyekuwa akiingia mle chumbani, macho yake yalikutana na macho ya mkewe, Joyce Jengo.

Inaendelea...

Cc the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel
 
Taxi - (17)

Joyce, mwanadada wa Kidigo kutoka eneo la Pongwe nje kidogo ya jiji la Tanga, alikuwa mrefu mweupe na mwenye uzuri wa asili, akiwa na umri wa miaka 32 alikuwa amejaaliwa uzuri wa sura ya kitoto na umbo. Macho yake yalikuwa makubwa na legevu ya kike, pua yake ilikuwa ndefu kama ya kihabeshi na midomo yake ilikuwa laini yenye kingo pana kiasi.

Joyce alikuwa mbunifu wa mavazi aliyekuwa na ndoto za kuwa mbunifu wa kimataifa na mtayarishaji wa kipindi cha runinga kuhusu ubunifu wa mitindo ya mavazi ya Kiafrika. Alikuwa msomi wa Shahada ya Kwanza ya Ubunifu wa Mitindo (B.A. In Fashion Design) aliyoipata katika Chuo cha Mitindo cha Elizabeth Galloway cha Cape Town, nchini Afrika Kusini.

Asubuhi ile Joyce alikuwa amevalia gauni zuri la kitenge lililoshonwa na kudariziwa vizuri, likimfanya apendeze na kuvutia kwa muonekano wake wa Kiafrika zaidi. Joyce alisimama akamtazama Sammy kwa makini, macho yake yalionesha uchungu fulani.

Sammy hakusubiri tena, alijiinua kutoka pale kitandani na kuketi kitako huku akifinya uso wake, halafu taratibu alijitoa pale kitandani na kuchukua taulo kisha alielekea maliwato huku akipepesuka.

Akiwa na hakika kuwa macho ya Joyce yalikuwa nyuma yake yakimsindikiza, Sammy aliingia haraka maliwato na kuurudisha mlango. Alijimwagia maji na kupiga mswaki, dakika chache baadaye alirudi pale chumbani na kuanza kuchagua nguo kutoka kwenye lile kabati la nguo, akaanza kuvaa huku akionekana mwenye mawazo mengi.

Muda wote Joyce alikuwa akimtizama kwa makini huku akijitahidi kuwa mtulivu, uso wake ulionekana kumtilia maanani Sammy kwa kila alichokifanya. Sammy aliendelea kuvaa taratibu na baadaye alijitazama kwenye kioo kirefu cha meza ya vipodozi, akagundua kuwa alikuwa na jeraha kwenye jicho lake la kushoto.

“Hivi ni nini kilikupata jana ukaamua kulewa kiasi kile?” Joyce alimuuliza Sammy kwa sauti tulivu huku akimwangalia kwa makini.

Sammy alimtupia jicho Joyce na kuyahamisha haraka, akapeleka macho yake kuangalia juu darini, alijaribu kuvuta kumbukumbu ya kilichotokea usiku lakini hakuweza kukumbuka chochote.

“Haki-yanani, ya jana sijapata kabisa kuyaona tangu nikufahamu! Yaani unalewa hadi unaletwa kwenye mkokoteni ukiwa chapachapa! Hii ni kali ya mwaka!” Joyce alisema huku akiachia kicheko hafifu na kupiga kofi moja hafifu hewani.

“Halafu ulisahau kabisa kama jana ilikuwa ni siku yako ya kuzaliwa, tumesubiri jioni tukufanyie ‘surprise’ badala yake wewe ndiyo ukageuka kutusapraizi,” Joyce alisema huku akitingisha kichwa kwa huzuni.

Sammy alitamani kucheka lakini akajizuia, alimsogelea Joyce kisha akapeleka mkono wake wa kulia kwenye uso wa Joyce kumpapasa huku akiachia tabasamu, si kwa kulazimisha.

Don’t touch me… ninapokuwa naongea vitu siriazi sipendi kufanywa katuni… au labda naongea upuuzi!” Joyce alisema huku akiusukuma mkono wa Sammy.

Sammy alishusha pumzi, akashika kiuno chake kwa mikono yake yote miwili huku akimtazama Joyce kwa makini. Alitaka kusema neno lakini akasita na kuinamisha kichwa chake, alifikiria kidogo akionekana kutaka kumwambia ukweli kuhusu matatizo ya kazini kwake, lakini hakujua aanzie wapi.

“Haya, endelea tu kuniona mpuuzi, siku moja utaujua umuhimu wangu,” Joyce alilalama na kumfanya Sammy atingishe kichwa chake kwa huzuni huku akibabaika kidogo.

“Siyo hivyo, unajua… nime… nime-e…” Sammy alitaka kusema lakini akasita baada ya kumuona Joyce akianza kupiga hatua taratibu kuondoka huku akirusha mkono wake hewani kama ishara ya kutotaka kumsikiliza.

Joyce alifungua mlango na kutoka akiurudishia mlango nyuma yake. Sammy alipigwa butwaa asijue la kufanya, alibetua mabega yake juu akionesha kutokuwa na namna nyingine ya kufanya…

Nyumba yao ilikuwa kubwa yenye vyumba vitatu vya kulala na ilizungukwa na ukuta uliojengwa kwa matofali. Ilikuwa na sebule pana yenye seti moja ya makochi ya sofa yaliyopangiliwa vizuri upande wa kulia wa sebule hiyo.

Makochi hayo yalikuwa yanatazamana na seti moja ya runinga pana ya ukutani aina ya Sony Bravia iliyounganishwa na decorder ya DStv yenye chaneli nyingi za kimataifa.

Kwenye kona kulikuwa na meza fupi ya mapambo na katikati ya sebule kulikuwa na meza nzuri ya kioo yenye umbo la yai na stuli ndogo nne zilizopangwa kuizunguka meza hiyo.

Ukutani kulikuwa na saa kubwa na picha tatu kubwa, picha moja iliwaonesha Sammy na mkewe Joyce katika pozi la harusi, picha ya pili ilikuwa ya familia nzima na picha ya tatu ilikuwa ya Joyce akitunukiwa shahada ya ubunifu wa mavazi katika Chuo cha Mitindo cha Elizabeth Galloway.

Upande wa kushoto wa sebule kulikuwa na ukumbi mdogo wa chakula wenye meza kubwa ya chakula iliyotengenezwa kwa mti wa mkongo na ilikuwa imezungukwa na viti sita vya mbao ya mkongo vyenye foronya laini, pia kulikuwa na jokofu kubwa aina ya BOSS.

Jirani na ule ukumbi wa chakula kulikuwa na korido pana iliyoelekea vyumbani na kulikuwa na milango mitano, milango miwili ikiwa upande wa kulia na milango mingine mitatu upande wa kushoto.

Mlango wa kwanza kulia ulikuwa wa kuingia jikoni na mlango wa pili ulikuwa wa chumba cha Sammy na mkewe Joyce. Milango iliyokuwa upande wa kushoto wa kwanza ulikuwa mlango wa kuingia kwenye maliwato ya wote, uliofuata uliingia kwenye chumba cha wageni na wa mwisho kabisa ulikuwa wa chumba cha kulala watoto.

Inaendelea...
 
Taxi - (18)

Pale sebuleni Winifrida Kambona, binti wa miaka 17, aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Zanaki, alikuwa anakata keti vipande viwili vidogo na kuviweka kwenye sahani kisha akaviweka juu ya meza mbele ya Pendo.

Winifrida alikuwa na umbile dogo lakini lililovutia mno. Kwa mlingano wa macho tu, alitoa tafsiri ya kuwa na ule uzuri usiomithilika, hasa kutokana na rangi ya ngozi yake nyeupe mithili ya chotara wa kizungu iliyowafanya wanaume wakware, pasipo kujali umri wao, wasahau kama alikuwa yupo chini ya umri wa miaka kumi na nane, na zaidi alikuwa mwanafunzi.

Ki ukweli Winifrida alikuwa miongoni mwa wasichana walioitwa nusu malaika! Nywele zake zilikuwa zimekatwa kwa mtindo wa ‘Lowcut’ na alikuwa na kope ndefu zilizong’ara na kuyafanya macho yake yawe wazi nusu. Pua yake ilikuwa ndefu kiasi, nyoofu ya wastani ikiiacha midomo yake ijidai kwa kuhifadhi meno meupe yaliyojipanga vizuri huku yakiachia kimwanya kidogo.

Hata hivyo, Winifrida alikuwa mapepe na msumbufu sana kwa kaka yake. Alipoweka vile vipande viwili vya keki alimimina sharubati (juice) ya parachichi na kumpa Pendo kisha aliketi kwenye sofa na kutulia akiangalia kipindi cha wanyama kilichokuwa kikirushwa kwenye kituo cha runinga cha Safari Channel.

Pendo aliachia tabasamu na kujiweka vizuri kwenye kochi. Alikuwa mtoto mchangamfu sana na muongeaji ingawa alikuwa na tatizo la seli mundu (sickle cell) lililomfanya mara kwa mara kulazwa hospitali. Hata hivyo alipenda sana kudadisi mambo na mara kwa mara aliuliza maswali yaliyoonekana yenye utata.

“Anti Winnie, mbona wewe hunywi juisi na keki?” Pendo alimwuliza Winifrida huku akianza kula taratibu ile keki na sharubati. Winifrida aliachia tabasamu huku akijiangalia kwa madaha.

“Aku! Mimi sitaki kuwa bonge… najitunza ili niwe mwanamitindo maarufu duniani,” Winifrida alisema na kuinuka, kisha alianza kutembea kwa miondoko ya madaha aina ya ‘Cat walk’ kama watembeavyo wanamitindo na warembo wanapokuwa katika majukwaa ya urembo.

“Eti Wifi, hebu nicheki sifai kuwa mwanamitindo?” Winifrida alimwuliza Joyce wakati akitembea kwa madaha na kupita mbele yake.

Joyce alikuwa kwenye cherehani akishona nguo huku kipimo cha kupimia nguo kikiwa kimening’inia kwenye shingo yake na alikuwa akitazama jarida maarufu la mitindo ya mavazi. Kando yake kulikuwa na sanamu kubwa la mwanamke likiwa limesimamishwa na kuvishwa vazi la kitambaa cha bazee lililoshonwa na kudariziwa vizuri na kichwani lilikuwa limevishwa kilemba kikubwa.

Aliinua uso wake na kumtazama Winifrida kisha akaachia tabasamu pana. Pendo aliachia kicheko kikali lakini Winifrida hakuonekana kujali, aliendelea kutembea kwa maringo huku akimtazama Joyce kwa bashasha.

“Umeona, eh! Kila mtu lazima azimike na pozi zangu,” Winifrida alisema huku akipunga mkono wake mmoja hewani na kumfanya Joyce aangue kicheko hafifu.

“Wewe andaa tu mavazi yako halafu mimi nitakufanya kuwa mbunifu wa nguo maarufu sana, siyo Tanzania tu bali Afrika yote,” Winifrida alisema na kumfanya Joyce agune.

“Mbona mimi tayari ni maarufu,” Joyce alimwambia Winifrida. Pendo aliendelea kucheka na kumfanya Winifrida ageuke kumtazama Pendo.

“Wewe cheka tu, usishangae siku moja ukiniona kwenye runinga napishana jukwaani na kina Naomi Campbell,” Winifrida alisema huku akilivuta neno la mwisho kwa mikogo mingi, Joyce alikuwa bado amemtumbulia macho.

“Wewe ukionekana kwenye runinga mimi ndiyo n’takuwa meneja wako!” Pendo alisema kwa mbwembwe huku akipunga mkono wake hewani na kuwafanya wote waangue kicheko, hata hivyo kicheko chao kilisitishwa ghafla baada ya Sammy kuingia pale sebuleni akitokea chumbani.

Sammy alikuwa amevaa suruali ya kadeti ya rangi nyeusi, shati la rangi ya samawati na buti ngumu za ngozi miguuni. Usoni alivaa miwani mikubwa myeusi ya jua, japokuwa mle ndani hapakuwa na jua lakini miwani ile aliitumia kuficha jeraha lake kwenye jicho lake la kushoto

Sammy alisimama akawatazama wote kwa zamu akianza na Winifrida aliyekuwa amesimama akiwa kashika kiuno kisha macho yake yalihamia kwa Pendo, akashusha pumzi za ndani kwa ndani na kumtupia jicho la wizi Joyce.

Alisogea alipokuwa ameketi Pendo na kumtazama kwa tabasamu. Aliionja kidogo ile sharubati ya Pendo na kuirudisha ile bilauri juu ya meza na wakati huo Pendo alikuwa akimtazama kwa makini kwenye jicho lake, wakabaki wakitazamana. Pendo alitaka kuuliza swali lakini akaonekana kusita na kubinua midomo yake kitoto akionekana kuzuia kicheko.

Kitambo kifupi cha ukimya kikapita na kuifanya ile sebule ionekane kuwa eneo lenye ukimya sana. Watu wote walibaki kimya wakimtazama Sammy kwa makini.

“Shikamoo, baba!” Pendo alivunja ukimya kwa kumsalimia baba yake huku akikenua meno yake.

“Marhaba mwanangu, naona unajipendelea peke yako,” Sammy alisema huku akimpapasa kichwani.

“Hii ilikuwa keki yako ya bethdei lakini jana ulirudi usiku umelewa ukaanza kupiga mikelele,” Pendo alisema huku akimuonesha Sammy kipande cha keki.

Winifrida alionesha kutaka kucheka lakini akawa anajizuia kwa kufunika mdomo wake kwa kiganja cha mkono, hata hivyo, alishindwa kujizuia na kuachia kicheko hafifu cha chini chini. Joyce alimtazama Winifrida kwa makini.

“Shikamoo!” Winifrida alimsalimia Sammy huku akijikausha na kutazama kando.

“Marhaba, Winnie, mbona leo hujaenda shule?” Sammy aliuliza huku akigeuka kumtazama Winifrida na bila hata kusubiri jibu alianza kuondoka.

“Leo Jumamosi, hatuendi shule, ila baadaye n’taenda twisheni,” Winifrida alijibu.

Okay!” Sammy alisema huku akianza kupiga hatua taratibu ili kuondoka.

“Sasa unaenda wapi hata chai hutaki kunywa?” Joyce alimuuliza Sammy alipomuona akipiga hatua zake kutoka nje.

“Mmh, saa hizi chai haipandi, ngoja nikapate mchemsho wa kuku kwa Elli,” Sammy alisema huku akifungua mlango na kutoka. Watu wote walimsindikiza kwa macho hadi alipotoka kabisa. Kisha Pendo alimgeukia mama yake.

Inaendelea...
 
Taxi - (19)

“Kwani baba kafanya nini kwenye jicho, mbona ameficha macho na miwani?” Pendo aliuliza huku akimkazia macho mama yake.

“Si ungemuuliza mwenyewe alikuwepo hapa! Umemsubiri kaondoka ili uniulize mimi!” Joyce alisema huku akitabasamu.

“Nimeogopa!” Pendo alisema na kumfanya Joyce acheke.

“Makubwa! Leo wewe wa kumuogopa baba yako?” Joyce alisema kwa mshangao.

Kisha Winifrida na Pendo walianza kufanyiana mzaha. Kwa kweli ilionekana ni familia yenye furaha sana.

_____

Sammy alifika kwenye kituo cha daladala cha Tabata Chang’ombe na kusimama kwenye meza moja ya muuza magazeti, aliwakuta watu wakiwa wamezunguka wakipitia vichwa vya habari kwenye magazeti ya siku ile.

Kulikuwa na habari tofauti zilizopewa uzito katika magazeti yale, lakini habari iliyomshtua zaidi Sammy ilikuwa ni ile ya tukio la kutoweka kwa mwandishi mahiri wa habari za uchunguzi wa gazeti la MamboLeo, Abbas Dalali.

Habari ile iliandikwa na gazeti la MamboLeo ikimkariri mke wa Abbas, Bi Somoe Dalali akisema Abbas aliondoka nyumbani kwao Tabata Kinyerezi na watu ambao hawakutambulika katika gari jeupe aina ya Toyota Noah. Abbas alikuwa amemwambia mke wake kwamba anakwenda kuonana na mtu muhimu ili kupata taarifa fulani nyeti na tangu wakati huo hakurudi tena nyumbani na wala simu zake hazikupatikana.

Bi Somoe alikuwa na wasiwasi na usalama wa mumewe, hasa baada ya kuona harudi wala namba zake hazipatikani, hivyo alikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi.

Pia gazeti lile liliandika kuhusu tamko la Kamati inayotetea waandishi wa habari, CPJ, ilipotoa wito kwa serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa kuaminika ili ifahamike kilichokuwa kimemtokea mwandishi huyo mahiri wa habari za uchunguzi.

Sammy alinunua lile gazeti la MamboLeo kisha alipanda kwenye daladala la kuelekea Mnazi Mmoja lililofika pale likiwa na abiria wachache.

* * * * *

Mchana wa saa saba kasoro dakika tatu, Joyce alikuwa ameketi sebuleni kwenye sofa akionekana kuwaza mbali sana, alikuwa ameshika jarida la mitindo lakini macho yake muda wote yalikuwa yakiitazama kwa makini saa ya ukutani mpaka mishale ifike saa saba kamili.

Bila ya sababu, moyo wake ulikuwa unamdunda, hatimaye ilitimu saa saba kamili, kisha dakika moja ilipita, ikaja ya pili na baadaye ya tatu… Joyce hakujua alichokuwa anakisubiri muda ule. Je, alikuwa na miadi na mtu? Nani? Hakuwa na jibu.

Moyo wake ulimpasuka mara tu simu yake ilipoanza kuita kwa fujo, aliinyanyua na kuitazama kwa makini, ilikuwa namba ngeni asiyoifahamu, alishusha pumzi akaipokea na kuipeleka sikioni.

Hallo!” Joyce alisema kwa sauti ya kutetemeka mara baada ya kupokea, kiasi kwamba alianza kujishangaa.

“Mrs. Joyce Kolimba…” Ilikuwa sauti tamu ya mwanamke kutoka upande wa pili wa ile simu, Joyce alipoisikia alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kuminya midomo yake, alihisi kuifahamu sana ile sauti lakini hakujua ni ya nani.

“Ndiyo… n-nani mwenzangu?” aliuliza huku akiwa na wasiwasi kidogo.

Madame Norah…” ilisema ile sauti kutoka upande wa pili wa ile simu na kumfanya Joyce ashtuke sana. Aliikodolea macho ile simu kwa mshangao kana kwamba lilikuwa bomu lililotaka kulipuka muda wowote.

Mmh… Madame Norah! Joyce hakuamini kabisa! Kwa nukta chache alihisi kama moyo wake ulisahahu mapigo yake, na mara yalipoanza tena alijikuta akivuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani, kisha akazishusha taratibu.

Haiaminiki! Madame Norah kampigia simu! Kwani ni yeye Joyce aliyekuwa akihangaika usiku na mchana kutafuta mawasiliano ya Madam Norah bila mafanikio! Alikwishakwenda ofisini kwake zaidi ya mara tatu lakini ilikuwa vigumu kumpata kwani wapambe waliomzunguka hawakutaka kumpa nafasi Joyce… Hapana, haiaminiki! Joyce alidhani labda yupo ndotoni!

Madame Norah mwenye umri wa miaka 50, alikuwa mwanamke mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa, alikuwa amejitosheleza kwa vitu vingi. Alimiliki kituo cha redio na cha televisheni, kampuni kubwa ya samani za majumbani na ofisini, mgahawa wa kisasa katikati ya jiji la Dar es Salaam na duka kubwa la vipodozi na nguo za kike.

Alikuwa mrefu na mweupe mwenye umbo kubwa kiasi lililosheheni vema na kunesanesa, likafanya kila jicho la mwanamume lililomuona kumtazama mara mbili mbili. Alikuwa mcheshi na mwenye ushawishi mkubwa asiyependa kuwa chini ya mwanamume, ndiyo maana hakutaka kuolewa.

Ingawa alikuwa na umri mkubwa, lakini ilikuwa vigumu mno kumtofautisha na wasichana wenye umri mdogo kutokana na urembo wake usiochujuka, hakuwa mwanamke wa kumtazama mara moja tu ukamwacha. Watu wengi walijiuliza kuwa endapo aliweza kuonekana mrembo kiasi kile katika umri huo, ilikuwaje enzi za usichana wake?

Joyce, are you there?” sauti ya Madame Norah ilimgutusha Joyce aliyekuwa ameanza kutekwa na mawazo.

“Oh… Madame Norah! Samahani mama’angu, kwa kweli sikutegemea kabisa kupata simu yako…” Joyce alisema huku akibabaika kidogo.

Mambo yanazidi kunoga! Je, Sammy anaelekea wapi? Na huyu Madame Norah ni nani hasa na kwa nini amempigia simu Joyce? Endelea kuufuatilia mkasa huu wa kusisimua...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom