Taxi - (109)
ILIPOISHIA
Tunu alilitazama lile gari kwa makini huku akijiuliza kuwa watu wale ni akina nani na kwa nini wamfuatilie. Je, ni watu wa Mr. Oduya? Akaanza kushikwa na wasiwasi, hata hivyo aliamua kuachana nao na kuyakaza macho yake kutazama mbele huku akajitahidi kulisahau gari lile kwa muda, aliipa utulivu akili yake ianze kufanya kazi.
Tayari muda wa dakika takribani kumi na tano ulikwisha yeyuka tangu Tunu alipotoka pale hospitali ya Amana, aligundua hivyo baada ya kuitazama saa yake ya mkononi iliyoonesha vizuri kupitia mishale yake ya dhahabu ilivyokuwa ikimetameta.
Baada ya sekunde chache alifikia uamuzi wa kuwapoteza kwa kuwa hakutaka watu wale wafahamu ni wapi alipokuwa akielekea. Akapanga kubadilisha mwelekeo. Aliutazama mshale wa mafuta ukamwonesha kuwa alikuwa na mafuta ya kutosha kuweza kuzunguka jiji la Dar es Salaam mpaka jioni bila kusimama. Akatabasamu na kuongeza mwendo.
* * * * *
Katika hospitali ya Amana, Sammy alikuwa ametulia nje ya chumba alimolazwa Joyce, alikuwa akitafakari kuhusu mazungumzo yake na Tunu huku akijaribu kujiuliza maswali yaliyokosa majibu. Alitamani sana kufahamu kilichotokea kwa Tunu, alikuwa wapi siku zote? Anafanya kazi gani?
Alikuwa na hamu kubwa ya kutaka kufahamu mengi kuhusu Tunu, ni wapi alikuwa katika kipindi hiki chote cha miaka kumi na moja tangu walipoachana! Pamoja na kupotezana miaka yote hiyo lakini bado Tunu aliendelea kuonekana mrembo sana. Alikuwa bado ni Gift yule yule mwenye mvuto wa ajabu.
Wakati akizidi kuwaza mara akawaona watu wawili wakija na walipofika karibu akawatambua mara moja, walikuwa wazazi wake Joyce, Bwana na Bibi Jengo. Akasimama na kuwalaki.
ENDELEA...
Bi. Pamela alipomwona Sammy alishindwa kujizuia, alifungua mdomo wake kutaka kusema lakini maneno hayakutoka, akabaki mdomo wazi akimkodolea macho Sammy huku donge la fadhaa likimkaba kooni. Akaangua kilio kwa uchungu.
“Mama Davie, usilie tafadhali. Joyce anatuhitaji sana hivyo tunatakiwa tuwe na ujasiri,” Jengo alisema huku akimkumbatia mkewe na kumpigapiga mgongoni.
“Baba Davie, hujui tu ninapitia kipindi gani kwa sasa, mwenyewe unajua tangu nilipopata taarifa hizi nimeshindwa hata kula...” Bi. Pamela alisema na kuchukua kitambaa laini, akafuta machozi.
“Mama, Joyce ni jasiri, naamini atashinda vita hii ya kupigania maisha yake, cha msingi tu tumuombee,” Sammy alisema huku akiwatazama wakwe zake kwa makini.
“Najua mwanangu, lakini nina uchungu, kwa nini wamfanyie hivi kwani kawakosea nini jamani!” Bi. Pamela alisema kwa huzuni. Kikatokea kitambo kifupi cha ukimya, Sammy akawataka waketi kwenye benchi lililokuwepo pale.
“Nataka kufahamu tukio hili limetokeaje?” Rafael Jengo alimuuliza Sammy baada ya kuketi.
“Ni kama nilivyokueleza kwenye simu, mimi sikuwepo nyumbani ila kwa maelezo ya mdogo wangu Winifrida, watu wawili walifika na kuwaweka chini ya ulinzi, shida yao kubwa ilikuwa ni mimi. Hadi sasa sijajua nani aliwapa polisi taarifa, ila wale watu walipogundua askari wameizingira nyumba ndipo wakampiga risasi Joyce na kutoroka,” Sammy alisema kwa huzuni.
“Muda huu nilijaribu kupiga tena simu polisi kujua kama kuna hatua yoyote waliyopiga au kuna mtu yeyote aliyekamatwa lakini mpaka sasa hawajafanikiwa na uchunguzi bado unaendelea,” Sammy alisema.
“Lakini, vipi hali ya Joyce?” Rafael Jengo aliuliza kwa wasiwasi.
“Tuendelee tu kumwombea aweze kupata nafuu maana hadi sasa hajazinduka, usiku walimfanyia oparesheni na kufanikiwa kutoa risasi mbili...” Sammy alisema na kusita kidogo. “Daktari ameniambia ukweli kwamba hali aliyo nayo sasa kupona ni hamsini kwa hamsini hivyo tujiandae kwa lolote litakalotokea,” Sammy alisema huku machozi yakimlengalenga machoni.
“Joyce wangu jamani!” Bi. Pamela alisema kwa uchungu mkubwa huku akishika kichwa, alionekana kusononeka sana. Mara kikohozi kidogo kikamtoka na nyuma yake wimbi la machozi lilikuja mbio. Alishindwa kujizuia na akapiga yowe dogo la kilio. Rafael Jengo na Sammy wakawa na kazi ya kumbembeleza.
Kwa muda wa dakika kadhaa hali ya mahali pale ikageuka kuwa ya simanzi kubwa. Kilio cha Bi. Pamela kikawafanya Rafael Jengo na Sammy wajikute wakitokwa na machozi pasipo kupenda.
“Mama Davie, tafadhali piga konde moyo ujizuie kumwaga machozi. Nimekwambia tunahitaji sana kuwa watu jasiri kwani Joyce anatuhitaji,” Rafael Jengo alimwambia mkewe huku akimfuta machozi. Akamshika bega, “
Listen, ninamfahamu Joyce ni mpambanaji.
She’ll fight this!”
“
I know, and I’m trying my best... lakini sina uhakika na hali ya mwanangu hadi nimuone. Oh jamani mimi!” Bi. Pamela alisema huku akiendelea kulia.
“
Please, Mama Davie, eneo hili halihitaji kelele!
Please!” Rafael Jengo alisema kwa ukali kidogo. “Usikate tamaa kirahisi hivi, naamini Mungu atamsaidia, si vyema kumwaga machozi eneo hili. Ningejua hali itakuwa hivi ningekuacha Tanga, na kama hautakuwa na ujasiri nitakurudisha Tanga leo hiihii!” Rafael Jengo alisema huku akishusha pumzi.
“Samahani, Baba Davie, nimekuelewa. Nitajitahidi ingawa inaniwia vigumu,” Bi. Pamela alisema huku akifuta machozi. “Ah, machozi yangu yawe dawa ya mwanangu na Mungu amponye,” alisema kwa sauti ya chini huku akishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani.
“Kwa hiyo, wanasemaje? Tunaweza kumwona mgonjwa?” Rafael Jengo alimuuliza Sammy.
“Mpaka sasa madaktari hawajaanza kuruhusu mtu kumwona, nadhani wanafanya utaratibu wa...” Sammy alikatishwa na simu ya Joyce aliyoishika iliyoanza kuita.
Aliitazama kwa makini na kuliona jina la Madame Norah kwenye kioo cha simu. Akashusha pumzi za ndani kwa ndani. “Samahani, ngoja nipokee kwanza hii simu,” Sammy alisema na kuipokea ile simu, akaipeleka kwenye sikio lake. “Hallo, Madame!”
“Hallo, baba, tayari nimeshafika hapa hospitali, sijui uko kwa wapi?” Madame Norah aliuliza.
“Njoo moja kwa moja huku chumba cha wagonjwa mahututi walio katika uangalizi maalumu.”
“
Okay, nipe dakika moja tu siko mbali na hapo,” Madame Norah alisema na kukata simu.
Sammy alishusha pumzi na kuitazama ile simu kwa makini kisha akairudisha mfukoni. Kabla hajajua aseme nini mara akamwona Madame Norah akipiga hatua zake haraka haraka kuelekea pale walipokuwa.
Madame Norah alionekana nadhifu sana akiwa amevaa suti ya rangi ya zambarau ya kitambaa ghali toka nchini Italia; suruali na koti, na ndani alikuwa amevaa blauzi nzuri ya rangi ya samawati. Usoni alivaa miwani mikubwa ya jua iliyoyafunika macho yake, mkufu wa dhahabu shingoni na miguuni alivaa viatu vya zambarau vyenye visigino virefu.
Akiwa takriban hatu kumi kabla hajawafikia, alisimama ghafla baada ya kuwaona watu wengine wawili wakiwa na Sammy, kilichomshtua zaidi ni yule mwanamume aliyekuwa amevaa suti nadhifu ya rangi ya kijivu na shati jeusi.
“Jengo?” Madame Norah alijiuliza kwa sauti ndogo huku akihisi miguu yake ikiishiwa nguvu. Aliivua miwani yake na kuishika mkononi. “Ni yeye kweli au nimemfananisha? Ni yeye, naamini macho yangu bado yana nguvu ya kutosha na sina shaka na kile ninachokiona,” Madame Norah alizidi kuwaza huku akimtazama Rafael Jengo kwa makini.
Sammy alishangaa kumwona Madame Norah akiwa amesimama akishangaa kama aliyeona kitu kigeni. “Vipi, mama, mbona unashangaa?” Sammy aliuliza kwa mshangao na kuwafanya Rafael Jengo na Bi. Pamela wageuze shingo zao kutazama kule ambako macho ya Sammy yalikuwa yanaangalia.
INAENDELEA...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper MR KUO dan oseko