Taxi - (59)
ILIPOISHIA JANA
Walitazamana, Joyce naye aliachia tabasamu kabambe huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
“Habari yako dada yangu?” Dynamo Plus alisalimia huku akinyoosha mkono wake kumpa Joyce.
“Salama, sasa mambo si hayo? Kwani ulivyonisalimia umekufa?” Joyce alisema na kumfanya Dynamo Plus acheke kidogo.
“Nimefurahi sana leo nimekutana na wewe, mimi ni shabiki wako.
You are my favorite musician,” Joyce alisema huku tabasamu pana likishindwa kwenda likizo usoni kwake.
Dynamo Plus alijisikia fahari sana kusifiwa na Joyce, aliendelea kuung’ang’ania mkono wa Joyce huku akimtazama kwa makini usoni.
“Nafurahi kusikia kwamba hata watu kama ninyi mnazikubali kazi zangu,” Dynamo Plus alisema huku akishusha pumzi.
SASA ENDELEA...
“Kwani mimi nina tofauti gani na watu wengine?” Joyce aliuliza huku akimkazia macho Dynamo Plus.
“Wewe ni mtu mkubwa, watu kama ninyi muda mwingi mko bize, sina hakika hata kama mnapata muda wa kusikiliza nyimbo zetu,” Dynamo Plus alisema huku akipitisha ulimi kuilamba midomo yake mikubwa.
“Nina ukubwa gani mimi!” Joyce alisema na kuangua kicheko hafifu, akaendelea, “Tuyaache hayo, Aisha yuko wapi siku hizi? Nimemmisi sana,” Joyce aliuliza huku macho yake yakiwa yameweka kituo usoni kwa Dynamo Plus.
“Aisha dada’angu! Kwani mnafahamiana?” Dynamo Plus aliuliza kwa mshangao baada ya kufikiria kidogo.
“Ni
best wangu sana, nilisoma naye kidato kimoja Sekondari ya Wasichana ya Tabora.”
“Anaishi Sweden siku hizi. Nimefurahi sana kukufahamu dada…” Dynamo Plus alisema na kuonekana kusita kidogo na kuachia kicheko hafifu huku akishika kichwa chake kuonesha kuwa amelisahau jina la Joyce.
“Joyce… Mrs. Joyce Kambona,” Joyce alisema huku akiachia tabasamu.
“
Oh yes, dada Joyce…
you are a fashion designer, right?” Dynamo Plus alisema huku akimtazama Joyce kwa makini. Joyce aliachia tabasamu pana zaidi la bashasha.
“
Yeah! How do you know?” Joyce aliuliza huku akihisi furaha moyoni kwa kuwa Dynamo Plus alionesha kumfahamu.
“Nadhani tumewahi kukutana, pia nimekuwa nikisikia habari zako. Hasa Madame Norah amekuwa anakuongelea sana.
She real admires you!” Dynamo Plus alisema na kumfanya Joyce azidi kujisikia fahari baada ya kugundua kuwa kumbe watu walikuwa wanaongelea habari zake.
* * * * *
Saa kumi alasiri, kwenye viunga vya maegesho ya magari vya mgahawa wa kisasa wa Elli’s, mtangazaji na mtayarishaji wa kipindi maarufu cha ‘Mbunifu Wetu’ katika kituo cha runinga cha Mzizima, Maximilian Njamba alikuwa amesimama kwa mbali akionesha kidole chake lilipokuwa limeegeshwa gari aina ya Cadillac DeVille lenye muundo wa kizamani likiwa na kibao cha “Taxi” juu yake.
Maximilian Njamba alikuwa mwanamume wa makamo mwenye umri wa kati ya miaka arobaini na tano na hamsini, si mrefu wala mfupi kwa kimo, pia hakuwa mwembamba wala mnene na alikuwa na sura ya ucheshi muda wote.
Alasiri ile Maximilian alikuwa amevaa kofia nyeusi ya pama, shati la mikono mirefu la pundamilia, suruali pana ya kijivu na viatu vyeusi ya ngozi miguuni.
Alikuwa amefika katika mgahawa wa kisasa wa Elli’s baada ya kuambiwa na rafiki yake kuhusu uwepo wa gari aina ya Cadillac DeVille lililosajiliwa kuwa teksi, alipoliona alijikuta akiupenda sana ubunifu uliotumika kulifanya lile gari kuwa la kibiashara.
Muda ule alikuwa ameshika kipaza sauti chenye nembo ya
Mzizima TV akiwa mbele ya mpiga picha wake. Alikuwa akielezea jinsi alivyovutiwa sana na ubunifu uliotumika kwenye lile gari aina ya Cadillac DeVille.
Hii ilikuwa baada ya kumtafuta mmiliki wa gari lile, Sammy Kambona na kutaka kufanya naye mahojiano lakini Sammy alikataa katakata na kumuonya Maximilian asijaribu kulipiga picha gari lake bila idhini yake.
Kwa kuwa Maximilian aliiona ile teksi kama njia nzuri ya kuhamasisha ubunifu aliamua kuitumia ile fursa adimu ili kuwavutia watazamaji wa kipindi chake waweze kuhamasika kufikiria ‘nje ya boksi’ kwa kufanya vitu ambavyo watu wengine wangedhani haviwezekani.
Lakini tatizo lilikuwa ni Sammy, alikuwa amekataa kuhojiwa wala kupigwa picha, hivyo Maximilian aliamua kuvizia, pindi Sammy alipoingia ndani ya ule mgahawa wa Elli’s, akasimama kwa mbali lakini akihakikisha lile gari linaonekana kwenye kamera na kumtaka mpiga picha wake kulivuta gari karibu ili liweze kuonekana vyema.
Baada ya mpiga picha kuweka sawa mitambo yake na kumpa ishara kuwa alikuwa tayari, Maximilian alianza kazi iliyompeleka pale huku akiwa makini.
“Huu ni ubunifu wa hali ya juu sana, ila tunasikitika mmiliki wake amekataa kufanya mahojiano nasi, tungefahamu alifikiria nini kulifanya gari hili aina ya Cadillac DeVille lililotengenezwa zaidi ya miaka hamsini iliyopita kuwa teksi! Kwa kweli hii ni teksi inayovutia hasa, na kila mtu angependa kuwa abiria wake…” alisema yule mtangazaji wa kipindi maarufu cha ‘Mbunifu Wetu’ kilichorushwa na Mzizima TV.
“Na cha ajabu zaidi, licha ya kuwa ni gari la kizamani lakini ni kama mpya, haina matatizo yoyote na inaweza kukufikisha kokote uendako pasipo hofu ya kuharibika njiani… sasa ngoja nisikie maoni ya wakazi wa jijini Dar es Salaam kuhusu gari hili,” alisema Maximilian na kuelekea mtaani akijaribu kupata maoni ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Aliwauliza hasa wakazi walioishi jirani na eleo la mgahawa wa Elli’s kama wameshawahi kuliona gari aina ya Cadillac DeVille la muundo wa kizamani lililokuwa likitumika kama teksi na nini maoni yao kuhusu gari lile.
Wapo wakazi waliosema kuwa hawajawahi kuliona na wale walioliona walionekana kusifia sana akili ya kibunifu iliotumika kulifanya lile gari aina ya Cadillac DeVille la muundo wa kipekee kuwa teksi, wakidai kuwa lilikuwa ile hali ya upekee ingeweza kuwavutia watu wengi kutaka kuwa abiria wake na hivyo kulifanya gari liwe bidhaa adimu.
Wapo waliodai kuwa japo walikuwa wameliona ndani ya siku chache tu lakini tayari lilikwisha fahamika sana utadhani lilikuwa lina zaidi ya mwaka mmoja, wote walikiri kuwa wangependa kuwa abiria siku moja kutokana na upekee wake.
* * * * *
Saa moja jioni Sammy alikuwa anatoka ndani ya mgahawa wa kisasa wa Elli’s uliopo Ilala Sharif Shamba na kutembea haraka akikatiza kwenye viunga vya maegesho ya magari vya mgahawa ule, akalifikia gari lake aina ya Cadillac DeVille na kufungua buti la gari.
Inaendelea...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki