Stori ya kusisimua - Taxi

Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (57)

Huyu Joyce alikuwa na nini hasa kilichomfanya Madame Norah afanye yale asiyokusudia kuyafanya? Hata hivyo, kitu kimoja alichokuwa na uhakika nacho ni kwamba alijisikia furaha sana moyoni kila alipoamua kumsaidia Joyce, basi!

Baada ya kitambo kirefu cha majadiliano kati yao, Madame Norah aliaga na kuondoka akiwaacha Joyce na Nyaso wanakamilisha maandalizi ya mradi ule.

* * * * *

Baada ya kutoka eneo la Karakata, Sammy alimchukua mtu mmoja aliyemkuta Jet Club na kumpeleka katika ofisi za Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) zilizopo barabara ya Mandela, katika eneo la Tazara.

Alimwacha yule abiria pale TSN kisha akageuza gari lake na kutaka kuingia katika barabara ya Mandela akitaka kwenda Ilala Sharif Shamba, mara akamuona mwanamume mmoja raia wa kigeni aliyekuwa anatokea ndani ya majengo ya kituo cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) aliyemjia mbio huku akimpungia mkono.

Alikuwa mwanamume wa makamo, mrefu na kipande cha mtu aliyejazia vyema. Mwili wake ulichorwa michoro mbalimbali na alikuwa amevaa fulana nyeusi ya mikono mifupi, kaptura ya rangi ya khaki yenye mifuko mikubwa pembeni na miguuni alivaa raba. Mgongoni alikuwa amebeba begi kubwa la safari.

Sammy aliamua kumsubiri. Hata hivyo, alikuwa amesimama katikati ya barabara ya mchepuko iliyotokea katika jengo la TSN na hivyo kuzuia magari mengine. Gari moja aina ya Toyota RAV4 jeusi lililokuwa nyuma yake likitaka kuingia katika barabara ya Mandela lilianza kupiga honi, dereva wa gari lile alionekana kutokuwa na uvumilivu.

Sammy aliendelea kusubiri pasipo kumjali yule dereva wa RAV4 aliyeendelea kupiga honi kwa fujo. Hakutaka kumkosa yule abiria Mzungu aliyekuwa akivuka barabara ya Mandela akionekana kuwa na safari muhimu.

Baada ya dakika takriban mbili yule mwanamume alifanikiwa kuvuka ile barabara na kufungua mlango wa nyuma wa gari la Sammy kisha aliliweka begi lake na kuingia, akakaa katika siti ya nyuma.

Airport please… and thanks for waiting,” (Kiwanja cha Ndege tafadhali… na ahsante kwa kusubiri) alisema yule mwanamume wa kizungu huku akijiegemeza kwenye siti.

Sammy aliliondoa gari lake na kungia katika barabara ya Mandela bila kumjibu chochote yule mwanamume wa kizungu kisha akakata kushoto akiifuata barabara ya Nyerere iliyoelekea Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Muda ule wa mchana barabara ya Nyerere haikuwa na msongamano mkubwa wa magari, hivyo Sammy alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi. Walikuwa kimya kabisa.

Kufumba na kufumbua gari lilikuwa likiivuka yadi ya kuhifadhi makontena ya African Inland Container Depot (AFICD) katika eneo maarufu la Mchicha na sasa walikuwa wakilisogelea eneo la Karakana ya Tazara, hapo yule mzungu akakohoa kidogo kusafisha koo lake kisha akaanzisha mazungumzo.

Do you know English?” (Unajua Kiingereza?) yule mzungu alimuuliza Sammy huku akiachia tabasamu pana la kirafiki.

Yes,” Sammy alijibu kwa ufupi bila kumtazama yule mwanamume.

How did you get this car? I real like it, it’s a unique type of taxi that everyone should want to use it,” (Umeipataje hii gari? Nimeipenda sana, ni aina ya teksi yenye upekee ambayo kila mtu angependa kupanda) yule mzungu alimuuliza Sammy huku akimtazama kwa makini.

Sammy aliachia tabasamu huku akimtupia jicho yule abiria wake kupitia kioo cha katikati cha gari kinachotumika kuangalia nyuma.

You know…” (Unajua…) Sammy alianza kujieleza lakini akasita baada ya kumuona Winifrida akiwa hajavaa sare za shule na badala yake alivaa suruali ya kubana ya jeans rangi ya samawati yenye matobo mapajani na kitopu cheupe na mgongoni alikuwa amebeba begi lake la madaftari.

Winifrida alikuwa ameongozana na kijana mmoja wa kiume aliyekadiriwa kuwa na miaka ishirini na ishirini na mbili, akiwa amevaa suruali nyeupe ya jeans na fulana nyeusi, kichwani alivaa kofia nyeusi ya kapelo. Alikuwa mrefu maji ya kunde na mtanashati sana.

Walikuwa wanatembea taratibu huku wameshikana mikono wakiifuata barabara ya vumbi iliyokatisha katikati ya majengo ya kampuni za Spedag Interfreight na Bureau Veritas Tanzania kuelekea eneo la Kiwalani.

Shit!” Sammy aling’aka kwa hasira huku akipiga ngumi juu ya usukani na kukanyaga breki ya ghafla, gari lake likaserereka huku likiyumba barabarani na kusimama kando ya barabara ya Nyerere, usawa wa jengo la kampuni ya Bureau Veritas Tanzania.

Alishuka haraka akimwacha abiria wake na kukimbilia kule walikokuwa Winifrida na yule kijana huku akiwa amekasirika sana. Yule kijana alishtuka na kutazama nyuma, alipomuona akija mbio alikimbia akimwacha Winifrida ambaye hakuwa na ujanja. Sammy alimfikia Winifrida na kumkamata mkono kwa nguvu huku akifoka.

Winifrida aliishiwa nguvu, Sammy alimkokota kumpeleka kwenye gari lake lililokuwa limesimama kando ya ile barabara ya Nyerere. Muda wote yule abiria mzungu aliyekuwa ndani ya lile gari la Sammy alikuwa amepigwa na butwaa.

Kama mtu aliyeshtuka aliiangalia saa yake ya mkononi na kusonya huku akionekana kukata tamaa. Kwa vidole vyake viwili vya shahada na dole gumba vya mkono wa kulia aliminya pua yake kama anayevuta kamasi huku akiwatazama kwa makini Sammy na Winifrida wakivutana. Akaangalia tena saa yake ya mkononi.

What’s wrong with you?” (Una shida gani?) yule mzungu alimuuliza Sammy kwa mshangao huku akishuka kutoka ndani ya lile gari la Sammy, mara akaiona teksi ikija upande ule, akaipungia mkono, “Taxi! Taxi!

Ile teksi ilipunguza mwendo na kusimama mbele ya gari la Sammy, yule mzungu alifungua mlango wa nyuma wa gari la Sammy na kuchukua begi lake, akamtazama Sammy kwa mara ya mwisho huku akitoa kadi yake.

You’ve been a prank but I want to give you a second chance, not for you but for the car. I may need it for one of my representative’s meetings,” (Umenifanyia mzaha lakini nataka nikupe nafasi nyingine, siyo yako bali kwa sababu ya gari lako. Huenda nikalihitaji kwenye moja ya mikutano yangu) yule mzungu alisema huku akimpa Sammy ile kadi yake.

Inaendelea...
 
Taxi - (58)

Sammy aliipokea ile kadi huku akiitazama kwa makini na kubetua kichwa chake. Yule mzungu aliingia kwenye ile teksi aliyoisimamisha, kisha ikaondoka kwa mwendo wa kasi na kuyafanya magurudumu yake yachimbe ardhi.

Winifrida aliingalia kwa makini ile teksi iliyombeba yule mzungu wakati ikiondoka kisha akageuza shingo yake kulitazama gari la Sammy kwa udadisi, akakiona kibao kidogo chenye maandishi ya ‘Taxi’ juu ya gari. Akashangaa sana.

“Kumbe wewe ni dereva wa teksi! Mi’ nilidhani meneja!” Winifrida alisema kwa mshangao huku akimkazia macho Sammy.

“Achana na habari za teksi, niambie kwa nini hujaenda shule na badala yake unazurura na wanaume?” Sammy alimuuliza Winifrida huku akionekana kukasirika sana.

“Nakubali nimekosa, na wewe kwa nini unaendesha teksi badala ya kuwa ofisini?” Winifrida naye alimuuliza Sammy huku akimtazama kwa makini.

Sammy alitaka kusema neno lakini akasita, aligeuza shingo yake kulitazama gari lake, akakiona kile kibao chenye maandishi ya ‘Taxi’ na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akijiegemeza kwenye gari. Sasa siri yake ilikuwa imefichuka! Winifrida alilitambua hilo na kuachia kicheko hafifu.

“Naamini hutapenda wifi ajue kuhusu jambo hili!” Winifrida alisema huku akiendelea kumwangalia Sammy kwa makini.

“Tafadhali usitake kuingiza mambo yasiyohusiana, suala hapa ni kwa nini huendi shule na badala yake unakuja huku ukiwa umevaa nguo za ajabu ajabu?” Sammy alimuuliza Winifrida huku akijaribu kumtisha.

“Sawa nimekosa, lakini na wewe kwa nini umdanganye wifi kuwa umepandishwa cheo kumbe siku hizi unaendesha teksi? Unataka nimwambie ukweli?” Winifrida aliongea kwa msisitizo bila kuteteleka.

“Naomba usithubutu kumweleza chochote wifi yako, haya mambo hayakuhusu! Ninachotaka uniahidi kuwa utaacha huu ujinga na kwenda shule,” Sammy alisema kwa sauti ya kusihi.

“Ukinisamehe sitasema chochote kwa wifi,” Winifrida alisema huku akifungua mlango wa nyuma wa gari la Sammy na kuingia.

Sammy alimtazama kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akaingia ndani ya gari, akaliondoa na kuelekea eneo la Vingunguti, alipofika usawa wa jengo la kampuni ya East African Cables (Tz) Ltd aliliingiza gari kwenye barabara mchepuko na kugeuza kurudi alikotoka.

Gari liliongeza mwendo likiyapita majengo ya East African Cables (Tz) Ltd, Hoteli ya Blue Supphire, Azania, Spedag Interfreight, Bureau Veritas Tanzania, Karakana ya Tazara na African Inland Container Depot, katika eneo maarufu la Mchicha, wakachepuka na kuingia barabara ya Nyerere, kisha safari ikaendelea.

* * * * *

Saa nane mchana, gari dogo la kifahari aina ya Range Rover Sport L494 la rangi ya bluu lilikuwa linaegeshwa kwenye viunga vya maegesho vya jengo la ghorofa saba la Nuru TV, eneo la Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Ndani ya lile gari kulikuwa na watu watatu. Dereva wa gari na mwanamume mmoja mrefu mwenye umbo kubwa kakamavu kutokana na mazoezi makali. Kwenye siti ya nyuma aliketi kijana mtanashati aliyeonekana kujiamini sana. Hakuwa mwingine bali mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Dynamo Plus, aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka thetathini.

Alikuwa mrefu kiasi mwenye mwili mdogo lakini uliojengeka kwa mazoezi, akiwa amevaa suruali nyeupe ya jeans iliyokuwa imechanwa chanwa sehemu ya mapajani hadi uswa wa magoti na fulani nyeusi yenye picha yake kifuani.

Kichwani alikuwa amezisuka nywele zake katika mtindo wa rasta na alivaa kofia nyeupe ya kapelo na miwani mikubwa ya jua usoni.

Kwa kiasi fulani Dynamo Plus alikuwa amejitosheleza, kwani mbali na muziki alikuwa anamiliki miradi kadhaa ikiwemo studio ya kurekodi muziki, na alikuwa mbioni kuanzisha vituo vya redio na televisheni, kwa msaada wa Madame Norah.

Kwa kifupi Madame Norah alimshawishi Dynamo Plus na wakakubaliana kuingia ubia ili waanzishe vituo hivyo vya runinga na redio kwa kuwa Dynamo Plus alijionesha kuwa kijana mbunifu na mwenye kujituma sana, kiasi cha kuwa mfano kwa wasanii wengi.

Dynamo Plus alishuka kutoka kwenye gari lake na kuongozana na mlinzi wake huku wakimwacha dereva ndani ya gari. Aalipiga hatua akitembea kwa mwendo wa kunesa kuelekea ndani ya jengo akifuatisha midundo ya muziki aliousikiliza kupitia spika (headphone) alizovaa masikioni.

Alielekea kwenye lango la kuingia la jengo lile la Nuru TV huku ile suruali yake ikiwa imevaliwa chini kidogo ya kiuno chake. Alipokuwa akikaribia lile lango la kuingilia alimwona mwanadada mmoja mrembo aliyevaa gauni refu la kitenge cha wax lenye mikono mirefu la mtindo wa pencil dress, akitokea ndani ya lile jengo akionekana kuwa na haraka kidogo.

Dynamo Plus alimtupia jicho mara moja tu na kuendelea na safari yake kuelekea ndani lakini alisita baada ya kusikia sauti laini ikimsemesha.

“Kaka Nasri, hata salamu?” yule mwanadada alimwambia Dynamo Plus na kumfanya ageuza shingo yake kumtazama kwa makini na hapo akakutana na macho legevu ya Joyce yaliyong’ara.

Dynamo Plus alimwangalia Joyce kwa wasiwasi kidogo huku akijiuliza ni wapi alikutana na mwanadada yule, kwani hata jina alilomwita ni jina lake halisi lililojulikana na watu wachache wa karibu. Jina lake halisi aliitwa Nasri Abood.

Dynamo Plus alikunja mkono wake wa kulia na kuupeleka kifuani kwake huku akiinama kidogo mbele katika hali ya kuomba radhi kwa kutosalimia.

“Wakati mwingine unaweza kupoteza video vixen hivi hivi... huyu mdada anafaa sana kupamba video yangu mpya,” Dynamo Plus aliwaza na kuachia tabasamu.

Walitazamana, Joyce naye aliachia tabasamu kabambe huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Habari yako dada yangu?” Dynamo Plus alisalimia huku akinyoosha mkono wake kumpa Joyce.

“Salama, sasa mambo si hayo? Kwani ulivyonisalimia umekufa?” Joyce alisema na kumfanya Dynamo Plus acheke kidogo.

“Nimefurahi sana leo nimekutana na wewe, mimi ni shabiki wako. You are my favorite musician,” Joyce alisema huku tabasamu pana likishindwa kwenda likizo usoni kwake.

Dynamo Plus alijisikia fahari sana kusifiwa na Joyce, aliendelea kuung’ang’ania mkono wa Joyce huku akimtazama kwa makini usoni.

“Nafurahi kusikia kwamba hata watu kama ninyi mnazikubali kazi zangu,” Dynamo Plus alisema huku akishusha pumzi.

Mambo yanazidi kunoga. Winifrida ameshaigundua siri ya Sammy, je atamweleza Joyce au atauchuna? Kukutana kwa Joyce na mwanamuziki Dynamo Plus kinaashiria nini? Usikose kufuatilia stori hii ya kusisimua hapa hapa...
 
Leo nisipofukuzwa Nazi sijui....maana ndio nimeifumania, na sitaweza iachia mpaka niimalize!!! Thanks mtunzi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom