10/06/2013
Taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu Star TV kujiondoa Star Times.
Tarehe 23 Mei 2013 Star TV kupitia mwanasheria wake iliwataka Star-Times kuiondoa kwenye kingamuzi chao ifikapo saa sita usiku wa tarehe 31Mei kutokana na kurusha na kuuza maudhui na vipindi vyake bila idhini na kukiuka sheria za haki miliki (Copyright laws).
Katika barua hiyo Star TV iliwakumbusha Star Times kwamba hawakuwa na mkataba wa kurusha kituo hicho kwa mujibu wa sheria ya Mawasiliano EPOCA pia hawana haki ya kutumia maudhui yake bila idhini chini ya sheria ya haki miliki ya Tanzania na Kimataifa.
Tarehe 31 Mei 2013 Star Times/Star Media walijibu na kudai kwamba hawajakiuka sheria yoyote wakasisitiza wataendelea kuirusha Star TV kutekeleza matakwa ya sheria ya EPOCA na kanuni zake.
Tarehe 6 Juni, 2013 Star TV iliwaandikia tena Star Times ikisisitiza nia yake ya kuchukua hatua zaidi kutokana na wao kuendelea kukaidi ombi hilo na kuainisha mapungufu kadhaa ya kisheria kwa upande wao yanayoifanya Star TV ijiondoe kwenye kingamuzi chao ifikapo saa sita usiku wa tarehe 08 Juni, 20013.
Star TV Ilieleza Star Media (T) Ltd. ambayo inamilikiwa kwa pamoja na Star Times na TBC ina leseni ya miundo mbinu ya kurusha matangazo ya Televisheni kupitia mfumo wa DTT (Multiplex Operator License). Leseni hiyo inawaruhusu kuingia makubaliano (Service Level Agreement-SLA) na vituo mbalimbali kuwarushia matangazo yao lakini Star-Times hawana leseni ya kutoa huduma ya maudhui (Content Service Provider License-CSP).
Star Times ni kampuni ya kimataifa iliyoandikishwa (China) inayotoa huduma ya maudhui katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania. Ili kupata maudhui inalazimika kuingia mikataba na vituo vya televisheni kabla ya kuviingiza kwenye kingamuzi chake na baadaye kuuza maudhui hayo (subscription/Pay TV) kwa walaji katika mataifa hayo.
Star Times inachukua vituo vya TV ikiwemo Star TV bila idhini yao na kuviweka kwenye kingamuzi chake kwa kisingizio kwamba wanaruhusiwa na sheria ya EPOCA na Kanuni zake. Sheria hiyo inasisitiza juu ya kuwepo kwa mkataba wa makubaliano (SLA) kati ya pande mbili husika.
________________________________________________________________________
Sahara Media Group Ltd. ATC House, Ohio Street, PO. Box: 6404, Dar es Salaam, Tanzania. Ph: 22 2136834, Fax: 22 2134534 HQ: Posta Road, PO. Box: 1732, Mwanza, Tanzania. Ph: 28 2503262, Fax: 28 2500713
Kwamba maudhui ya TV za Tanzania yanauzwa kwa walaji katika nchi nyingine kama vile Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Nigeria na nyinginezo bila idhini ya wamiliki wake. TV zinazomiliki maudhui hapa nchini hazina uwezo wa kuidhibiti Star Times isirushe maudhui yao nje ya Tanzania kwa kuwa baadhi ya maudhui wanayoyanunua nje kama vile tamthilia na vipindi vingineyo haviruhusiwi na watunzi au wasambazaji wake yarushwe nje ya Tanzania (Territorial Rights).
Lakini pia uhusiano wa makampuni haya mawili Star Media (T) Ltd na kampuni ya Star Times ambayo ni ya China yenye matawi katika nchi nyingi za Afrika katika uendeshaji wa matangazo ya Dijitali haujabainishwa vizuri ili kujua nani ni nani na nini anachofanya hapa Tanzania katika misingi ya maelewano ya kibiashara.
Ni kutokana na mantiki ya hoja hizo Star Times waliondoa mara moja Star TV kwenye kingamuzi chao tarehe 08 June 13 kama walivyoelekezwa na Star TV.
Star TV haioni sababu ya kulazimishwa na TCRA kurushwa na Star Times pasipo kuondoa hitilafu hizo za kisheria na bila kuangalia sheria nyingine zinazolinda haki za TV huru kama sheria ya haki miliki na sheria ya ushindani katika soko moja. TCRA kwa kutozingatia hili, inajifanya mmiliki wa sharia hata zisizokuwa chini ya mamlaka yao (supra organ!)
Insert: Serikali ya Tanzania ni mwanachama wa WTO na pia WIPO (World Intellectual Property Rights Organization) na hivyo kwa kulazimisha uvunjaji wa sheria za hati miliki ina maana inavunja haki zetu zilizopo kikatiba! Tutakwenda mahakamani kupata haki yetu hii muhimu.
Sheria hii inaweka kinga kwa vipindi vya radio, television, nyimbo na sanaa zote, kwa kutaka kulazimisha Star-times kupora vipindi vya Star- Tv inadhihirisha kilio cha wasanii wa Tanzania wasivyolindwa na serikali yake.
Taarifa iliyotolewa magazetini na Meneja Mawasiliano wa TCRA Innocent Mungy kwamba chaneli tano za kitaifa lazima zirushwe na vingamuzi vyote bure ni za kupotosha kwa kuwa hata hiyo Star Times haizirushi bure imekuwa ikibadilika badilika kama kinyonga. Lakini makampuni ya kigeni kama vile Dstv, na Zuku wao hawarushi matangazo ya TV nyingine bila makubaliano yanayotambulika kisheria.
Hata hivyo Vituo vikubwa vya TV vikiwemo Star TV, ITV, Channel 10 na TBC na vinginevyo visivyo vya kitaifa vinarushwa na makampuni ya BTL na TIN bila malipo yoyote ya mwezi na kwa ubora zaidi kuliko Star Times lakini inashangaza kuona TCRA inawakingia kifua Star Times wanaowalipisha watanzania badala ya kutetea vituo vya ndani visivyotoza chochote.
Star TV inaamini kwamba kazi ya usimamimizi au tuseme urefa wa matangazo ya TV inayofanywa na TCRA haipashwi kupendelea upande wowote na haipashwi kuingilia masuala ya kibiashara kuilinda Star Times kwa kuwa sio jukumu lao. Kwa mfano, Star TV na TV nyinginezo nchini zilizimiwa matangazo yao ya analojia na TCRA ili kuwalazimisha waingie Star Times na pia kuwalazimisha waTanzania wanunue vingamuzi vya Star-Times bila dhana nzima ya ushindani, watake wasitake hawakuwa na njia nyingine ya kuonyesha matangazo yao.
Sasa miundo mbinu ya humu nchini imejengwa na kampuni za kizalendo kwa
2/4
gharama kubwa na kwa ubora zaidi kuliko Star-Times. Sasa ushindani umewaelemea Star-Times, hivyo TCRA inajaribu kuwasaidia tena. Hili halikubaliki na tupo tayari kuwaonyesha watanzania matumizi mabaya ya chombo hiki kwa maslahi ya wageni na watu wachache wasio waaminifu kwa nchi yao.
Pamoja na kazi ngumu ya kujenga miundo mbinu ya DTT ambayo imewakamua wawekezaji wa Kitanzania, Mkurugenzi wa TCRA hajawahi kuwatembelea kuwatia moyo. Star TV inapinga kwa nguvu zote TCRA kufanya usimamizi kwa mtizamo wa kibiashara kwa kujaribu kuwasaidia Star-Times ambao, nia yao ni kupata bure matangazo yanayotayarishwa kwa gharama kubwa na vituo vya Tanzania na kuhodhi urushaji wa maudhui ya TV za humu nchini kupitia DTT kwa faida yao. Kimsingi Star-Times ni TV ya kigeni na kwa mujibu wa sheria mpya ya EPOCA haistahili kupewa leseni ya ndani ya maudhui kushindana kama local TV.
Hata hivyo, kama inadaiwa kwamba Star Media (T) Ltd na Star Times ni kitu kimoja basi kampuni zote mbili zinafanya kazi kinyume cha sheria ya EPOCA na kanuni zake ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 12(h) kinaonyesha jinsi mwenye leseni ya miundo mbinu (Multiplex) anavyotakiwa kutekeleza majukumu yake. Kinasema: Multiplex Operator hataruhusiwa kurusha maudhui yake mwenyewe, vituo vyake vya TV au kifurushi chenye maudhui yake (Bouquet).
Kwa hiyo Star TV haiko tayari kujihusisha na Star-Times au kufanya biashara na chombo chochote ambacho mwenendo wake wa kibiashara haufuati matakwa ya sheria. Pia, Star-TV haikubali kusukumwa kwenye makubaliano ya kibiashara kwa matumizi ya nguvu na tafsiri potofu ya sheria zetu. Hii ni kugombanisha watanzania kwa kutumia sheria zao wenyewe zinazotafsiriwa vibaya kukidhi tama ya watu wachache waovu hapo TCRA.
Imetolewa na Meneja Mipango na Utafiti wa Sahara Media Group Ltd.
Nathan Lwehabura kwa niaba ya uongozi.