- AUMIZA VICHWA KAMATI YA MZEE MWINYI
Geofrey Nyang'oro na Ramadhan Semtawa
SPIKA wa Bunge Samuel Sitta ametoboa siri ya ujasiri wake akisema inatokana na nguvu za Mungu, ambazo zimekuwa zikimwezesha kutekeleza wajibu wake kwa uhakika, bila kuyumbishwa wala kuogopa kitu chochote.
Katika kujenga kizazi kipya cha viongozi bora wa taifa hili, Spika Sitta alisema vijana wajengewe maadili mema ili kuwaepusha na ufisadi.
Kauli hiyo ya Sitta imetolewa kipindi ambacho baadhi ya watu wamekuwa wakilishambulia Bunge kwamba limewasaliti Watanzania, kutokana na uamuzi wa Spika huyo kufunga mjadala wa kashfa ya Richmond Development (LLC) hivi karibuni.
Wakati makombora hayo yakielekezwa kwenye Bunge analoongoza, jana Spika Sitta alizidi kuonyesha kuwa bado yuko ngangari na kisha kutoboa siri ya ujasiri wake ambayo aliapa kuiendeleza.
Spika Sitta alisema: "Siri ya ujasiri nilionao katika uongozi inatokana nami kuwa karibu na Mungu. Hali hiyo ndiyo inayoniwezesha kutekeleza wajibu wangu kwa uhakika bila kuogopa kitu chochote wala kuyumbishwa".
Spika alisema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa albam ya kwaya ya Kanisa Katoliki Mtakatifu ya Michael, Parokia ya Mtakatifu Xavery Chang'ombe Jimbo Kuu la Dar es Salaam jana.
Pamoja na kusema hilo, vyanzo huru vya habari vilivyo karibu naye vimedokeza kwamba, Spika amesema yeye siye anayepaswa kumuomba radhi Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kuhusu kashfa ya Richmond(LLC), badala yake mbunge huyo ndiyo aombe radhi Watanzania.
Akifafanua siri ya nguvu zake hizo katika hafla hiyo, Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), alisema mtu akiwa karibu ya Mungu neno la Mungu humsaidia kuwa mnyenyekevu mbele ya watu anaowaongoza.
"Inashangaza kuona kuna baadhi yetu husema eti nina shughuli nyingi na kuacha nyumba za ibada. Mungu ametuumba wote tukiwa sawa. Neno la Mungu humfanya mtu kuwa kiongozi bora na pia hupunguza kiburi cha kiongozi huyo mbele ya anaowaongoza," aliweka bayana Spika Sitta.
Spika Sitta ambaye tayari ametangaza rasmi azma yake ya kutetea kiti hicho baada ya uchaguzi wa Oktoba, aliwataka viongozi na watu wote kuwa karibu na nyumba za ibada ili waweze kujengewa uwezo na unyenyekevu mbele za watu wanaowaongoza ili wawe viongozi bora kama viongozi wa dini walivyo.
Katika kuonyesha msisitizo, Spika Sitta aliwapigia debe viongozi wa siasa na sekta nyingine akitaka viongozi wa dini wawaalike katika shughuli kama hiyo kwa vile maeneo kama hayo yatawaweka karibu na Mungu.
Akizungumzia nafasi ya vijana katika uongozi wa nchi, Spika Sitta aliwataka kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kutumia muda wao na nguvu zao kwa maslahi ya taifa.
Spika ambaye anaongoza Bunge kwa kauli mbiu ya Kasi na Viwango, alisema yeye anawapenda vijana kwani kwa mara ya kwanza yeye aliingia bungeni akiwa kijana mwenye umri wa miaka 32 na alipofikisha miaka 34 aliteuliwa kuwa naibu waziri.
Alisisitiza ni lazima vijana warithishwe maadili ili kuweza kulijenga taifa likiwa na amani na utulivu huku akisema, husikia mambo ya ovyo yanayofanywa na baadhi ya vijana aliyoyataja kuwa ni wizi, rushwa na yanayofanana na hayo.
Vyanzo vyetu vilivyo karibu na Spika Sitta vimeeleza kwamba, mkuu huyo wa mhimili huo wa kutunga sheria amekuwa akipasua vichwa vya wajumbe wa Kamati ya Mzee Mwinyi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Spika amekuwa na msimamo tangu kwenye mkutano wa Halmshauri kuu (Nec) ya CCM ambao ulimlazimu Rais Jakaya Kikwete kusema kwamba, Spika na Lowassa wote ni marafiki zake hivyo lazima wasuluhishwe.
"Ndani ya NEC ilibidi mwenyekiti wa CCM (Rais Kikwete) aweke bayana kwamba, Spika Sitta na Lowassa ni marafiki zake na tatizo kubwa ni Richmond hivyo lazima lipatiwe ufumbuzi ndiyo maana kamati ya mzee Mwinyi iliongezewa muda".
Lakini, licha ya kamati hiyo kupewa muda wa kutafuta suluhu, Spika amekuwa na msimamo thabiti huku akielezwa kugoma kumwomba radhi Lowassa badala yake kutaka Mbunge huyo wa Monduli ndiyo aombe radhi Watanzania.
"Alichosema Spika ni kwamba, hata kama kutakuwa na shinikizo haitakuwa rahisi kwake kumuomba radhi Lowassa badala yake yeye (Lowassa) ndiyo awaombe radhi Watanzania kwanza," kilidokeza chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, mzee Mwinyi na kamati yake wamekuwa katika wakati mgumu na huenda wakarejesha ripoti katika muda uliopangwa bila kupata suluhu kati ya watu hao.
"Spika Sitta hawezi kuomba radhi na Lowassa pia inaweza kuwa hivyo hivyo, sasa unategemea kuna suluhu hapo? Spika amekwisha sema hana ugomvi na Lowassa bali anasimamia maadili, sasa aombe radhi ya nini?" kilihoji chanzo hicho.
Tangu kuibuka kwa sakata la mkataba wa kifisadi kati ya kampuni ya Richmond na Tanesco, uliosainiwa Juni 23, 2006, kisha kusababisha Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu na Rais Kikwete kuvunja baraza la mawaziri, CCM na Bunge hata serikali vimejikuta vikiingia katika mgawanyiko mkubwa.
Kundi la Lowassa ambalo linaundwa na watu wenye nguvu ya fedha wamekuwa na ushawishi mkubwa ndani ya CCM na hata bungeni, lakini Spika Sitta akiwa na kundi dogo la watu majasiri wanaojiita wapiganaji kumesababisha msuguano ndani ya CCM na bunge ambalo asilimia kubwa ya wabunge ni wa chama hicho.
Mgawanyiko huo ndiyo uliyoifanya NEC kuunda kamati ya mzee Mwinyi ikiwa na wajumbe watatu ambao ni Abdulrahman Kinana na Katibu Pius Msekwa, kutafuta suluhu hiyo.
Hata hivyo, kamati hiyo iliyoanza kazi Agosti mwaka jana ilishindwa kumaliza tatizo hilo baada ya Spika kukataa suluhu na Lowassa.
Licha ya Spika kukubali kuizika hoja ya Richmond bungeni bado msuguano uliendelea ndani ya chama na hivyo mkutano wa NEC uliofanyika hivi karibuni uliamua kuongezea muda kamati ya mzee Mwinyi kwa kuitaka ichunguze kiini cha tatizo.