Hii mada ya mahakama ya kadhi inaibua hisia za kidini sana, tusipoangalia tunaweza kugawanyika kwa jambo ambalo si la kimaendeleo bali la kiimani zaidi. Hakuna aliyena ushahidi usioacha shaka kwamba huko kwa Mungu kukoje. Suala hili ukijaribu kuliangalia lililetwa na wanasiasa hasa waccm ili kuwarubuni wenzetu wa kiislamu baada ya kushindwa kuwapa huduma bora za kijamii. Matokeo yake watu hawajili zaidi huduma za kijamii bali wanataka mahakama ili washitakiane na wakose muda wa kuulizia maendeleo. Hapa tulipofikia watanzania hatuna namna, kama ni mbegu sasa imeota hatuna jinsi bali kuvuna. Na kwa bahati mbaya wenzetu waislam hawataki chochote zaidi ya mahakama ya kadhi. Basi wapewe kwani hakuna jinsi bali wahakikishe mahakama hiyo ifanye kwa mujibu wa sheria za kiimani na sio tuanza kuona tena mlundikano wa kesi, majaji kuanza kula rushwa kama hizi tulizozoea.
Angalizo kwa ndugu zetu waislamu, hivi ni kweli huduma nyingine muhimu za kijamii kama maji safi, elimu, afya bora zimewatosheleza na hivyo kilichobakia ni mahakama ya kadhi tu!!? Hamuoni kama mnaipa picha mbaya jamii ya kiislamu kwamba huduma za kijamii sio kipaombele chenu bali kuna nakisi ya uadilifu kwenye jamii ya kiislamu kiasi kwamba mambo mengine si muhimu sana bali mahakama ya kadhi ili mshitakiane? Ni kweli mna upungufu mkubwa hivyo wa maadili mpaka muhitaji mahakama yenu mbali na hizi zilizopo? Kwa mazingira haya ya makundi mengine ya wananchi kukwazika na hili hitaji lenu, mna uhakika wa kuiendesha mahakama yenu kwa uadilifu wa kiimani kwa kiwango hicho, ama mnataka kuleta tena mtafuruku mwingine kwenye jamii pindi vishoka wa imani watakapoingia kwenye mahakama yenu?