Muafaka -14 A
RIWAYA: MUAFAKA
MTUNZI: Amri Bawji
SEHEMU YA MWISHO: PART ONE
Nadhani nilikwisha kukupa jawabu la swali hilo, ambalo ni kuwa, sitapiga picha yoyote kuanzia sasa, ambayo ninaagizwa na wewe, hii ni pamoja na kuacha kazi katika kampuni yako.
Kwa nini ufanye hivyo Halfani?!
Kwa sababu ndio njia pekee ya kuonesha kuwa sikuwa pamoja nawe katika nia yako ya usaliti nilipopiga zile picha za Edo na Lulu.
Onespot alibaki kushangaa na kuduwaa wakati Halfani anatoka ofisini kwake.
* * * *
Halfani alikuwa bado hajaonana na Lulu tangu arejee kutoka Arusha.
Aliahirisha kuonana nae kwanza kwa kutaka aonane na Onespot na Vicky kwanza, pili ni kuwa alikuwa anajishauri namna ya kumkabili Lulu na jinsi ya kumpa ujumbe utokao kwa Edo. Kwa kuwa hilo, la kwanza amekwisha lifanya, kwa hiyo jioni ya siku hiyo aliamua aende nyumbani kwa akina Lulu.
Alipofika alikaribishwa vizuri na dada yake Lulu, Flora, baada ya kusalimiana na kujitambulisha, aliombwa akae sebuleni asubiri akaitiwe Lulu.
Baada ya dakika chache, Lulu alitokea akiwa anaoneakana mpole na aliyependeza asiye hatia kama malaika. Alitoa tabasamu kubwa alipomuaona Halfani na kusema,Karibu sana Halfani, jisikie upo nyumbani "Ahsante sana Lulu, tayari najihisi nipo nyumbani.
Kabla hatujaulizana habari Halfani, sijui ungependelea kinywaji gani?!
Soda tu inatosha.
Soda gani unapendelea
Sprite tafadhali, nataka nikate kiu.
Wote walicheka halafu Lulu alitoweka kidogo na baada ya muda wa dakika chache alikuja tena akiwa amenyanyua kisinia kilichokuwa na chupa ya soda ya sprite juu yake.
Aliiweka juu ya meza ya kahawa iliyokuwa mbele ya Halfani na kuifungua ile soda. Wakati Halfani anakunywa soda taratibu, walianza mazungumzo yao.
Halfani alimueleza habari zote Lulu. Alimueleza habari za makutano yake na Edo na akatoa ujumbe aliopewa ampe Lulu, kuhusu muafaka wa Edo na wazaai wake. Lulu alimsikiliza Halfani kwa utulivu na makini na alipokwisha maliza, Lulu alimuuliza tena ili afahamu zaidi kuhusu suala hilo.
Kwa hiyo Edo anaoa mchumba aliyewekewa na wazazi wake?!
Ndio hivyo Lulu, nasikitika nimejitahidi kadri ya uwezo wangu. Na ni kweli niliwakuta hao wazee wakijadili suala lake la harusi.
Lulu alikaa kimya kwa muda pasipo kusema wala kumuangalia Halfani, alionekana amepotea katika msitu wa mawazo. Ilibidi Halfani amtoe katika mawazo hayo kwa kumuuliza,
Vipi Lulu, unafikiria nini ?!....Mbona kimya mno?!
Unajua Halfani siamini kama haya yote yaliyotokea kuwa ni kweli! Ninaona kama vile nilikuwa ndani ya usingizi. Edo ni ndoto ambayo nimeipenda na kuithamini. Onespot nae ni njozi iliyokuwa inanitishia, Vicky ni ndoto isiyoeleweka. Sasa hivi najiona nimetoka usingizini, na wewe Halfani ulie hapa mbele ya macho yangu ndie uliye halisi na unajaribu kuitafsiri ndoto na njozi yangu. Ninashukuru sana sana Bw. Halfani, utabaki kuwa kama kaka yangu. Sasa hivi mimi niko macho, nimekwisha toka ndani ya ndoto yangu, la kufanya ni lile jambo ambalo ninahisi sio ndoto. Nalo ni la mimi kurudi kwetu nikaolewe na yule mchumba wangu niliyewekewa na baba yangu, kwani ndio muafaka. Ni kweli ndoa huandikwa mbinguni.
Halfani alimuangalia Lulu kwa macho ya Huruma, lakini Lulu alionekana kuamini alilokuwa akisema.
Mara alimtazama tena Halfani na kumuambia,
Kaka Halfani, nina ombi moja tu kwako tafadhali.
Sema tu Lulu hata kumi na moja, tena bila ya tafadhali.
Ninarudi nyumbani, baba yangu atafurahi mno nitakapomuambia nimekubali niolewe na yule mchumba niliyepangiwa. Na nina hakika harusi itaanza kuandaliwa mara moja. Sasa ninaloliomba kwako, siku ya harusi yangu, uje unipige picha nikiwa nina mume wangu halafu picha hizo umpelekee Edo, wasemaje?!
Kwa hilo halina shaka Lulu, sasa niambie nitajuaje shughuli hiyo itakuwa lini?!
Uwe unawasiliana na dada Flora hapa nyumbani mara kwa mara, muachie namba yako ya simu nawe chukua yake.
Halfani alifurahia sana wazo hilo, na aliongezea kusema
Hilo ni wazo zuri mno ambalo litanitoa mimi katika hisia za uhalifu. Pia kwa kuongezea nitampigia Edo simu, kama harusi yake itakuwa bado basi siku hiyo ikifika niende, ambayo nina hakika itakuwa hivi karibuni, ili nikampige na yeye picha akiwa na mke wake, wakati nikija kwenye harusi yako nikuletee, hii itanifanya nijikomboe na niwe huru tena au unaonaje?
Sawa sawa kabisa kaka Halfani, fanya hivyo ili niweze kuona picha ya ndoto yangu
* * * *
Baada ya harusi yao kubwa na ya kufana Onespot na Vicky walionekana kuwa watulivu na waliochoka, wakiwa bado wamo ndani ya kitanda kikubwa majira ya saa tatu asubuhi ya siku ya jumapili, Vicky alilaza kichwa chake juu ya kifua cha Onespot kilichokuwa wazi.
Sehemu ya tumbo mpaka miguuni ilifunikwa na shuka kubwa ambayo pia shuka hiyo hiyo ilifunikiwa mwili wa Vicky kuanzia miguuni hadi kwenye matiti.
Mkono wa kushoto wa Onespot uliegeshwa juu ya bega la kushoto la Vicky.
Walikuwa katika hali hiyo kwa dakika kadhaa huku macho ya Onespot yaliyokuwa wazi kabisa yakikodolea dari ya chumba hicho walichokuwemo.
Kimya hicho cha muda kilivunjwa na sauti ya Onespot iliyoita,
Vicky?!
Mmh!
You are my wife now, u mke wangu sasa
Ndiyo,na wewe ni mume wangu sasa
Kabisaa
totally yours
Do you really love me Onespot?, unanipenda kweli?!Nataka kuondoa shaka iliyo moyoni mwangu.
Shaka gani Vicky?! Vicky alinyanyua kichwa chake na kumuangalia Onespot.Hisia zako juu ya Lulu!
Oh! Come on Vicky, let us not talk about her, tusizungumzie habari zake, niliyemuoa ndiye niliyempenda kushinda wote. Leo ni siku yetu ya kupanga tuende wapi fungate?!
Vicky alitoa tabasamu kubwa, kisha akambusu Onespot shavuni na kusema,Samahani mpenzi, wewe unafikiri tuende wapi kwa ajili ya fungate yetu?!
Unanirudishia swali Vicky, haya basi, twende London, Paris, New York, Nairobi, Kampala, Harare au Johannesburg, sema wapi? Popote upendapo tutakwenda na hii ni zawadi ya pendo langu kwako.
Vicky alijihisi kufanikiwa mno, aliona sasa kweli Onespot ni wake yeye kabisa, ndipo alipojibu,
Tuna haja gani ya kwenda kwenye fungate yetu ugenini?! Kama uwezo tunao, kwa nini tusiende kwenye mbuga za wanyama Serengeti na Ngorongoro na kurudi kupumzika Arusha?!
Good idea! Ni wazo zuri sana Vicky, tutapata nafasi ya kuona wanyama na kupumzika vile vile. Sasa nitafanya mpango wiki ijayo tuende safari yetu kwenye fungate ili tusipoteze muda, wiki mbili zitatosha.
* * * *
Furaha kubwa walikuwa nayo wazazi wake Lulu baada ya kumuona binti wao amewasili nyumbani kwao.
Ilizidi maradufu pale alipowaeleza kwamba ameamua kurejea nyumbani na yupo tayari kuolewa na huyo mchumba aliyewekewa na wazazi wake hao.
Ah! Mwanangu Lulu! Hebu nikuuulize, je, vipi hukuweza kupata huyo mchumba wa kumchagua mwenyewe?!
Baba yake Lulu alimuuliza mwanawe kwa taratibu. Lulu alitulia kidogo kabla hajajibu swali aliloulizwa na baba yake, kisha akarudisha pumzo polepole na kusema,Baba, kusema kweli mchumba nilimpata, niliyempenda sana, au ninayempenda sana kuliko nilivyofikiria, lakini kumbe ilikuwa ni ndoto baba, ndoto ambayo sitaweza kuisahau maisha yangu yote yaliyobakia. Aliishiliza kusema kwa sauti ndogo na ya chini. Mzee Frank alimuangalia binti yake kwa masikitiko kidogo, kisha akajaribu kumfariji kwa maneno,
Sikiliza Lulu binti yangu, ndoa hupangwa na Mungu, usidhani wote waliooana walitaka kuoana na hao waliooana nao, hata, sio wote. Mimi baba yako binafsi, nilipokuwa bado mvulana na msela, nilipendana na msichana ambae si mama yako. Niliahidi kumuoa, lakini kabla sijafanya hivyo, nilipata safari ambayo ilinichukua muda mrefu, na niliporudi nilikuta yule msichana amekwisha olewa na mtu mwingine aliyejitokeza kwanza kwa wazazi wake. Nilisikitika lakini sikuwa na la kufanya, bali niliwaomba wazazi wangu wanitafutie msichana mwingine wa kumuoa. Ndipo nilipotafutiwa huyu mama yako. Tulioana na mapenzi yetu yalianza ndani ya ndoa. Leo hii hata nikifa halafu nirudishwe tena mwanzo wa maisha yangu na niulizwe ninataka kumuoa nani, nitamchagua mama yako. Nisingetaka kuoa mwanamke mwingine yeyote zaidi ya mama yako. Mume tunayetaka kukuoza mwanangu tunaamini ni mwema, na amezaliwa na watu wema wanaotoka katika familia nzuri, yenye adabu, huruma, upendo na heshima. Nasi tuna hakika utafurahia maisha yako ya ndoa, mwanangu, nina imani utampenda mume wako.
Baada ya mahubiri haya marefu, Mzee Frank alimuangalia mwanawe Lulu usoni na kuongeza kwa kumuuliza,
Je, mwanangu Lulu, upo tayari kuolewa na huyu mchumba tuliyekuchagulia?!
Ndiyo baba, nipo tayari.
Vema, mama mwanangu, sasa leo pumzika ili ujiandae kwa kesho kukutana na wakwe zako na mchumba wako, kwani bado yupo anakusubiri.
* * * *
Haloo!
Haloo, ni nani mwenzangu?!
Mimi ni Halfani Matai ninayezungumza
Ah, haa! Bwana Halfani ni Edo Oloi anaongea vipi habari za huko Dar?!
Za huku nzuri tu Edo, sijui za huku Arusha?!
Safi tu
Mambo yanaendeleaje, harusi yako tayari?
Hapana, bado, kwani vipi huko?
Huku salama tu, Onespot na Vicky wamekwisha funga ndoa, sasa nilikuwa nina taka kujitolea niwe mpiga picha katika harusi yako
kwa gharama zangu mwenyewe
kama itawezekana!
Ahsante sana kwa kujitolea kwako Halfani, lakini nasikitika kukueleza kuwa kumetokea tatizo kidogo ambalo limefanya harusi ichelewe kidogo. Lakini kama itakuwa tayari nitakujulisha, ninapenda uwe mpiga picha katika harusi yangu.
ITAENDELEA BAADAE