Muafaka -9
RIWAYA: MUAFAKA
MTUNZI: Amri BAWJI
SEHEMU YA TISA
kichwa chake amekiegemeza kifuani pa Edo, nayo aliiangalia kwa makini, kisha akaitua na kuchukua nyingine ya tatu.
Hii Edo alikuwa amemshika Vicky shavuni kwa kiganja chake cha kulia huku akimuangalia machoni.
Nayo pia aliiangalia akaiweka na kuchukua ya nne na ya mwisho.
Hii Edo alikuwa amekaa juu ya kiti, Vicky nae amekaa juu ya mapaja ya Edo, akiwa mikono yake ameizungusha kwenye shingo ya Edo-huku yeye Vicky akitoa tabasamu kubwa.
Alitulia na picha hiyo mikononi mwake kwa muda usiopungua dakika tatu. Wakati huu wote Onespot alitulia kimya akinywa kinywaji chake taratibu huku akimuangalia Lulu usoni. Lulu kabla hajaiweka juu ya meza picha hiyo ya nne, bila kujijuwa alisikia chozi likimchirizika juu ya mashavu yake.
Kuona vile Onespot alitoa kihanjifu toka mfuko wake wa koti na kunyoosha mkono wake kumpa Lulu. Nae alikipokea na kupangusa machozi yake. Onespot alisema,Pole sana Lulu
I am sorry.
Ahsante sana Onespot!
Je, umeonaje picha hizo?!
We acha tu.
Je, unamfikiriaje Edo?
Nampenda sana!
Onespot ambae wakati akiuliza maswali haya yote alikuwa ameegemea kiti, aliposika hivi alikaa wima na kwa ghafla na kutamka,
Enhee, unasema unampenda sana Edo?!
Lakini
sijui niseme nini!!
Onespot alikuwa hakuelewa, lakini sasa akaanza kumuelewa Lulu.
Usiseme kitu Lulu, fikiri kwanza. Si ulisema ulitaka mkutane na Edo?
Ndio, nilipenda nikutane nae
na yeye pia ameniambia leo, kuwa anataka kukutana na mimi.
Onespot alionekana kufikiri kidogo, kisha akasema,
Lakini Lulu, pamoja na yote haya, ukumbuke tuna kazi kubwa inayotusubiri siku tatu tu mbele yetu
ya onesho la mavazi. Tafadhali naomba utakapokutana na Edo
msije mkakasirishana kiasi cha kususia jukumu hili, kwa hapa lilipofikia.
Lulu hakuwa makini kwa chochote, aliwaza kukutana na Edo tu ili apate ufumbuzi wa picha zile, alimuhakikishia Onespot kuwa asiwe na wasiwasi na suala la onesho, litafanikiwa tu, na kuongeza,
Kwa sasa. Onespot nakuomba unisindikize nyumbani, kwani ninahitaji muda mrefu wa kufikiri kabla ya kesho
na ahsante kwa kunionesha picha hizi.
Jioni ile, wakati Lulu ametoka na Onespot, Vicky nae kabla ya kuondoka ofisini mwao, alitafuta kila njia ya kuzungumza na Edo, ambae kwa siku hiyo nzima hakuonekana kuwa ni mwenye furaha kutokana na kauli ya Lulu kwamba anakwenda kukutana na Onespot.
Kwa kuwa Vicky alilijua jambo hilo, basi alianza kumkera Edo kwa kumuuliza maswali madogo madogo. Edo nae aliyajibu kwa mkato pasipo kuendeleza. Ndipo Vicky alipomsumbua zaidi Edo kwa kumuuliza,
Leo una nini Edo?!
Hapana sina neno, kwani unanionaje Vicky?!
Nakuona huna furaha umekasirika, ambavyo sio kawaida yako!
Mbona nipo kama nilivyo siku zote!
Vicky alitoa tabasamu kubwa lililoambatana na mguno, huku akimtazama Edo usoni, kisha akamwambia
Kama ungekuwa kama ulivyo siku zote nisingekuuliza. Ninajua umekasirika, au tusema ndio umegundua baada ya muda mrefu kupita?
Edo kusikia hivi alitulia kidogo, kisha akamkazia macho Vicky nakumuuliza,Nimegundua?! Nimegundua kitu gani?!
Eeh, lakini usinitangaze Edo nisije nikamwaga unga!
Edo kwa shauku na kusisitiza alimuuliza tena Vicky.
Sema Vicky, kitu gani mbona sikuelewi?!
Nilifikiri
labda umekwishajua kuwa Onespot anatembea na Lulu siku hizi.
Kabla hata Edo hajasema kitu, Vicky aliendelea kusema kwa haraka haraka.
Lakini tafadhali usije ukamwambia mtu kuwa mimi ndiye niliyekuambia, sababu Onespot mwenyewe hufanya ni siri kubwa
hata leo hii wanatoka nje pamoja.
Edo alifikiri kidogo kwa kuinamisha kichwa, kisha akanyanyua uso wake kumuangalia Vicky na kusema,
Hilo jambo la kutoka nje pamoja leo ninalielewa, ameniambia Lulu mwenyewe
na hilo la Lulu kutembea na Onespot siliamini, sio kweli.
Una maana huniamini Edo?
Ninakuamini lakini siamini uniambialo.
Sasaa
unaweza kunisubiri kiasi cha dakika chache nikachukue kitu nje nikuoneshe ambacho kimenifanya nikwambie hivyo, licha ya kuwa ni mengi yanayosemwa kuhusu Onespot na Lulu
nisubiri kidogo.
Vicky alitoka haraka haraka baada ya kusema haya, bila kusubiri jibu la Edo. .Alikwenda moja kwa moja mpaka ndani ya ofisi ya Onespot, wakati huu wafanyakazi wengi tayari walikuwa wamekwisha ondoka. Baada ya muda mfupi alikuja chumbani alimokuwemo Edo, akiwa ameshika bahasha kubwa nyeupe mkononi mwake: Alimsogelea Edo na kumwambia,
Njoo uone mwenyewe kwa macho yako, nadhani baada ya hapo utaamini ninayokuambia.
Edo alimsogelea Vicky pale aliposimama. Vicky alitia kiganja ndani ya bahasha hiyo na kutoa picha zenye ukubwa wa inchi sita kwa inchi nne, kama zile alizooneshwa Lulu na Onespot, zilikuwa nne, lakini hizi zilikuwa zimemuonesha Lulu na Onespot. Vicky alisema,
Tazama, tazama! Huku akizikunjua kunjua picha hizo zilizokuwemo viganjani mwake, kama vile karata. Edo alizipokea picha hizo zote kwa kiganja chake cha kulia na kuanza kuziangalia kwa kutumia viganja viwili, kama vile ameshika karata na yeye, picha ya kwanza ilionesha Onespot amemkumbatia Lulu kwa nyuma. Picha ya pili ilionesha Onespot amemshika mabega Lulu kwa kupitisha mkono mgongoni wakiwa wanatoka chumbani. Picha ya tatu ilionesha Lulu na Onespot wamesimama mbele ya mlango wa gari ya Onespot wakiwa yeye Onespot ameweka viganja vyake vyote viwili juu ya mabega ya Lulu na picha ya nne na ya mwisho inaonesha Lulu yupo nje ya nyumba yao akipungiana mkono na Onespot ambae yupo karibu na gari yake. Edo alizitulizia macho picha hizo kisha akamuuliza Vicky,
Samahani Vicky, picha hizi umezipata wapi?!
Ofisini kwa Onespot, juu ya meza.
Je, unaweza kuniachia picha hizi angalau kwa leo tu?
kesho nitazirudisha!
Hata, kwa hili siwezi Edo. Unataka nifukuzwe kazi?! Tena ninakuambia usimwambie mtu tafadhili, hata huyo Lulu mwenyewe
kwa usalama wangu.
Wakati Edo ameshangaa kumsikiliza Vicky, akiwa amezishika picha hizo, Vicky alizipora ghafla na kuziweka sawa kisha akazirudisha ndani ya bahasha aliyokuwa ameishikilia, Edo alimtazama Vicky, bila kusema neno aliondoka.
* * * *
Usiku ule Edo hakupata usingizi sawasawa mawazo yake yote yalitawaliwa na Lulu, aliwaza hivi kweli Lulu anaweza kukubali kuchotwa na ghiliba za Onespot! Kwani alifahamu wazi kuwa Onespot bado anapigana vita vya kumpata Lulu, lakini jinsi gani anapigana vita hiyo, ndio hakulitambua.
Kilichomsikitisha Edo ni kuwa Lulu amekwishanaswa na mtego wa Onespot. Picha zile aliwaza Edo ni za Lulu akiwa na Onespot mpaka nyumbani kwa akina Lulu, hivyo ni dhahiri kuwa upo uhusiano mkubwa, ukiongezea na kukumbatiana. Usiku ulionekana ni mrefu mno kwa Edo, aliomba kuche haraka.
Wakati huo huo, Lulu nae hali ilikuwa hiyo hiyo kama ya Edo,baada ya kuziona picha zile za Edo na Vicky, alipofika nyumbani, alishindwa hata kula chakula. Aliamini kuwa ni kweli Edo ni mvulana wa Vicky na kwamba yeye Lulu anadanganywa tu. Alifahamu kuwa hakuna neno lolote lile ambalo anaweza kuambiwa na Edo akaamini tena, picha zimekwisha maliza kila kitu.
* * * *
Wakati Edo na Lulu, kila mmoja yupo kwake juu ya kitanda anawaza hili na lile na kuomba usiku umalizike, hali haikuwa hivyo kwa upande wa Onespot na Vicky, wao waliomba usiku usimalizike. Vicky na Onespot walikutana siku hiyo, usiku mwingi baada ya Onespot kumpeleka Lulu kwao. Waliagana hivyo, kuwa wakutane ili wabadilishane habari.
Mara baada ya Vicky kuachana na Edo, alirudi nyumbani kwao, akala chakula, kisha akajitayarisha kwa kutoka. Baada ya muda kupita, Onespot alifika kwa akina Vicky na kumchukua kuondoka nae.
Walitafuta sehemu nzuri wakaketi na kuongea. Onespot ndie aliyeanza kwa kuuliza,
Vipi Vicky! Hebu nipe habari za picha zile, Edo alipoziona alisema nini?
Hakusema kitu bali alitaka azichukue na kuzirudisha kesho, nami sikumkubalia.
Very good, angezichukua, kwa ninavyomjua Edo angezichunguza na si ajabu angepata ufafanuzi wa jinsi zilivyochukuliwa na mpiga picha.
Onespot alimpongeza Vicky kwa furaha nae Vicky alitaka kujua na Lulu nae alipoziona picha zake akiwa na Edo alisema nini.Aseme nini! Hakuwa na la kusema bali chozi lilimtoka. Sasa ujanja wao wote kwisha. Tumekwisha gonga gogo tusikilize mlio sasa.
Vicky na Onespot waliongea huku wanapata chakula cha jioni, walipanga mipango yao inayofuata na jinsi ya kuitekeleza, Vicky akiwa moyo wake umefurahi mno.
Hakuhisi wala kufahamu kuwa analolitenda kwa Edo na Lulu ni baya. Lengo lake ni kumridhisha Onespot ambae anampenda sana, basi, jingine lolote kwake yeye si muhimu.
* * * *
Siku iliyofuata Edo alifika mapema zaidi ofisini kwao, kuliko ilivyokuwa kawaida yake. Kabla ya kwenda kwenye chumba cha mazoezi ya onesho, alikaa kimya hapo juu ya kiti akiwa amekunja mikono yake juu ya meza iliyokuwepo mbele yake.
Ofisi hiyo wakati huo ilikuwa tupu kwa maana ya kuwa hapakuwa na mtu mwingine zaidi ya yeye Edo.
Wakati akiwa katika hali hiyo ya utulivu na ukimya aliisikia sauti ya soli ngumu za viatu vya kike vikitembea sakafuni ikizidi kusikika kuelekea chumba cha ofisi alichokuwemo, alibaki kama alivyokuwa akisubiri mwenye hatua hizo aidha apite nje ya chumba hicho au aingie chumbani humo mlango ulikuwa wazi, mara uso wa Lulu ukiwa hauna furaha kabisa ulijitokeza na kubisha hodi.
Edo aliitika, na baada ya kusalimiana alimkaribisha Lulu aketi juu ya kiti kingine kilichokuwepo karibu na meza hiyo. Baada ya kukaa, Lulu alimwambia Edo kuwa anashukuru kumkuta yeye Edo yupo peke yake, kwani alipenda iwe hivi. Edo naye akamwambia Lulu naye pia anashukuru, kwani alikuwa anamuwaza yeye na jinsi ya kumpata akiwa peke yake hapo kazini. Baada ya salam fupi na shukrani hizo walizopeana, Edo alitangulia kumuuliza Lulu,
Vipi mkutano wenu wewe na Onespot ulikwendaje?
Mbona unatanguliza kuniuliza habari za Onespot haraka haraka Edo?!
Kwa sababu mara ya mwisho tulipokutana jana uliniambia unakwenda kumuona au kukutana na Onespot.
Lulu aliguna na kutoa tabasamu la chini chini lisiloeleweka, aligeuza uso wake kando, kisha kwa ghafla akamuangalia Edo na kumjibu,
Afadhali ya mimi nilipokwenda kukutana na Onespot angalau nilikutaarifu na kukuambia kweli kuliko wewe ulipokwenda kukutana na Vicky ukaniambia uongo kuwa unakwenda mazikoni, kudanganyana ni kwanini?!!
Edo kidogo aliduwaa kwa kusikia habari hizo na kumjibu Lulu,
Mimi sijawahi kukutana na Vicky nje ya ofisi hii kama nilivyosema, na ni kweli kabisa juzi tulifiwa na jirani yetu na nilikwenda Kongowe kuzika, sasa lipi nililodanganya?!
Lulu kwa sauti ya ukali kidogo alimgeukia Edo na kusema,
Sikiliza Edo, nimesikia mengi, na nimeona vya kutosha kabisa kuthibitisha kuwa wewe girlfriend wako ni Vicky, kwa hiyo usinibabaishe.
Edo alitaka kupandisha jazba lakini akajikaza na akasema kwa sauti ya chini,Lulu unaonekana umekwisha nasa ndani ya mtego wa Onespot na kwa hiyo unatengeneza visababu vya kunisingizia mimi. Mimi na Vicky hatuna uhusiano wa kimapenzi kabisa, isipokuwa nikuulize wewe, ni kitu gani kilichopo kati yako wewe na Onespot?! Lulu nae hasira zilimpanda, hasira za kike. Mwanamke ni rahisi kumuonea wivu mwanamke mwenziwe kuliko ilivyo kwa mwanamme. Ni wanaume wachache wanaopandisha wivu kwa wanaume wenzao haraka. Lulu alisema kwa hasira kumwambia Edo.
Mimi na Onespot hakuna jambo lolote la kimapenzi, isipokuwa wewe na Vicky lipo, nasema tena lipo. Sasa wewe unanitafutia visababu ili uweze kuendeleza uhusiano wako na Vicky. Unafikiri ningekuwa na uhusiano kama huo unaodhani, ningekuambia kuwa ninakwenda kukutana na Onespot?!
Edo alifikiri na kuona kuwa Lulu amekwisha shawishika alikumbuka zile picha, alijisikia anamuambia Lulu,
Inawezekana uliniambia hivyo Lulu ili nikate tamaa juu yako. Lakini ninalokuambia mimi bado ninakupenda sana. Na kukuthibitishia hili, nijibu swali langu, iwapo umekubali kuolewa na mimi, na ukisema ndio, basi na tuondoke sasa hivi tukatafute padre atuoze.
Lulu aliangua kicheko cha dharau na cha kusikitika.
Ni kweli ninayoambiwa sikujua kama Edo kumbe wewe ni ndumilakuwili. Hivi ni kweli unanitaka tuoane?! Siwezi kuolewa na mwanamme nilie na wasiwasi nae. Ni kweli nami pia ninakupenda, lakini pendo langu linazibwa na shaka niliyonayo juu yako!
Edo alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilichomsibu Lulu, lakini kwa vyovyote vile alikuwa na uhakika wa mkono wa Onespot lazima uwepo, kama alivyoona katika picha. Alimwambia Lulu kwa sauti ya masikitiko,Lulu hivi kwa nini unitilie shaka?! Unajua sikuelewi kabisa! Sielewi sababu za shaka yako juu yangu, sina ovu lolote nililolifanya ndani ya uhusiano wetu.
Lulu alimuangalia Edo kwa jicho kali huku akimuwazia Edo vinginevyo, aliwaza ni kweli Edo ni langhai, sumu ya Onespot ilikwisha anza kufanya kazi, alisema kwa sauti ndogo,
Unakifahamu vizuri ulichokifanya na ndio maana ninakutilia shaka.
Edo alikuwa hajui amwambie nini Lulu, wakati anafahamu ni yeye aliyekosewa kwa sababu ya Lulu kumkubali Onespot kwa kiasi alichokiona kwenye picha. Aliamua asiwe na haja ya kuendeleza kubishana. Jambo moja ambalo halikuwekwa wazi kati yao ni lile la kuwa kila mmoja wao aliona picha za mwenzie, hilo waliliachia katika mazungumzo yao lakini hawakulitaja. Mwisho Edo alisema,
Ninaona hapa tutabishana mpaka kesho, kila mmoja kati yetu anajiona yeye si muhalifu kama anavyoonekana na mwenzie. La kuthibitisha pendo langu kwako nimekuambia tufunge ndoa leo hii; Hilo pia umekataa kwa shaka uliyonayo hii itakuwa ni kazi ya Onespot. Ipo siku utakuja jua ukweli uko wapi.
Lulu alidakia na kusema,
Mpaka hivi sasa nimekwishajua ukweli uko wapi kwa kujifariji, nitamkubalia Onespot kwa analolitaka la kuwa mimi girlfriend wake, huenda ikanisaidia kukusahau wewe.
Fanya hivyo tafadhali, huenda ikakusaidia kuujuwa ukweli. Naminitakusaidia kwa njia niijuayo.
ITAENDELEA