Muafaka -12
RIWAYA: MUAFAKA
MTUNZI: AMRI BAWJI
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
Well come, well come beauty queen, karibu sana Malkia wa urembo Lulu Frank.
Thank you, thank you King of fools, ahsante sana mfalme wa majuha Onespot Pato, nimeshakaribia.
Lulu aliketi juu ya kiti mbele ya meza ya Onespot kwa kishindo. Onespot alihisi vita. Lakini kama kawaida yake hakujali, alitulia na kumuuliza Lulu,
Vipi Lulu umekuja kunipongeza au kunitukana?!
Nikupongeze kwa lipi mpumbavu kama wewe, kwa hakika nimekuja kukutukana.
Kwa kuwa nimekuacha solemba eheh! Haha hahaaah! Mimi ndio Onespot Pato, siachwi bali naacha. Hakuna msichana anayethubutu kusema Hapana kwangu mimi. Yuko wapi Edo wako sasa?! Ninamuhurumia.
Kwa mshangao wa Onespot, Lulu aliangua kicheko kikubwa kushinda cha kwake yeye Onespot, alicheka kwa nukta kadhaa, kisha akatulia na kumtazama bosi wake huyo usoni. Akatamka,
Kama yuko wa kuhurumiwa, basi ni Vicky. Ah! Masikini Vicky, msichana mrembo kama yule kutaka kuolewa na janaume pumbavu kama wewe Onespot! Wewe!! Unamuhurumia Edo kwa lipi? Edo hahitaji huruma zako. Edo anacho kila kitu ambacho wewe unacho, kila kitu ambacho wewe huna jumlisha na pendo langu.
Lulu alitulia kidogo, kisha kwa kujiamini na kuringa aliendelea kusema,
Eti, nimekuacha solemba, Lulu alisema maneno haya kwa kumuigiza sauti ya Onespot, na mara akarudia sauti yake na kuendelea,
Unajua maana ya kuacha mtu solemba wee! Si ndio maana ninakwambia wewe juha. Licha ya wewe kuwa hujawahi kuwemo moyoni mwangu, pia sijawahi kufanya mapenzi na wewe, hujawahi hata kubusu kiganja changu wala sijawahi chako. Sasa solemba hiyo uliyoniacha ni ipi?! Hivyo kunipeleka hoteli na kuninunulia chakula?! Hivyo kunitembeza kuuona mji?! Jambo ambalo hata watoto wa mitaani wanalifanya kila siku kwa watalii! Hebu fikiria Onespot umjinga kiasi gani?! Kama yupo mwanamme aliyewahi kuniacha solemba kwa maana hasa ya kuniacha solemba. Basi ni Edo, I love him, I love him so much, and I will always do. Wewe..wewe
kitu gani kwangu. Linalonisikitisha ni kukosa nafasi ya kumueleza Edo upumbavu wako, na kuwa amekushinda. Hukuweza kulipata pendo langu. Kila nililolifanya pamoja na wewe, namaanisha huko kutoka nje ni kwa sababu ya kumuudhi Edo kwa kuwa ninampenda, na sio kwa sababu ya kukufurahisha wewe, ambaye si chochote kwangu. Hata baada ya Edo kuacha kazi, nilitoka na wewe kwa kujaribu kumsahau Edo, jambo ambalo nimeshindwa.
Onespot kwa mara ya kwanza katika maisha yake alitulia tuli kumsikiliza Lulu na kutafakari na kuona upo ukweli katika anayoyasema msichana huyo. Lulu alinyanyuka taratibu na kusimama kutaka kutoka nje ya ofisi hiyo, lakini kabla hajatoka, alimuangalia Onespot kwa dharau na huruma na kumwambia.
Kwa ushauri wa bure Onespot, mwanamme alie barabara na mjanja, siku zote hashindani na wanawake, huwa anashindana na wanaume wenzake. Kwa hiyo vita yako dhidi yangu umedhihirisha upumbavu wako. Na vita yako dhidi ya Edo, amekushinda, hata niolewe na mume mwingine, Edo atakuwa anayo sehemu ndani ya moyo wangu. Mwisho kabisa, Vicky anakupenda sana, nawe jaribu kumuenzi na kumpatiliza, una bahati kupata msichana kama Vicky
lakini kwa upande wako
sijui.
mfanye awe ana bahati nae, kwa heri. Lulu alitoka ofisi ya Onespot na kuingia ofisi ya Katibu Muhtasi... Vicky, ambae alikuwepo mezani pake. Lulu kabla hajamsalimu, alimtulizia macho na kumuangalia, alimtulizia macho na kumuangalia kiasi cha dakika tatu bila mmoja kusema chochote kwa mwenzake. Mwisho Vicky alishindwa kumtazama Lulu usoni, aliinamisha uso wake kwa huzuni na kuangalia chini. Ndipo Lulu alipotamka kwa kusema,
Pole sana vicky.
Pole ya nini unipayo Lulu?! Lulu alitabasamu kidogo na kumtulizia macho Vicky.
Pole kwa yote uliyofanya.
Yapi?!
Hayo ya kuvunja uhusiano wangu mimi na Edo!
Vicky aliinamisha uso wake chini kidogo, na kufikiri la kumjibu Lulu. Nae Lulu aliendelea kusema,
Licha ya hayo, nakupa pole Vicky kwa mwanamme kama Onespot kuwa mumeo mtara-jiwa!
Kwani ana nini? Alijibu Vicky haraka haraka kwa sauti ya mshangao.
Anazo kasoro nyingi ambazo itakubidi ufanye kazi ya ziada ili uzipunguze
Nitajie kasoro moja tu uijuayo wewe Lulu
kama siyo wivu wako?! Vicky alimuuliza Lulu kwa sauti ya chini.
Lulu aliangua kicheko kusikia hivyo, kisha akatulia kucheka na kusema kwa kuuliza na mshangao,
Wivu?!... Wivu?!... Nimuonee nani wivu? Kwa lipi? Kwa kuwa u mchumba wa Onespot?! Usijidanganye Vicky, hata wewe unajua sina haja ya Onespot, hata siku moja. Onespot mwana-ume mwenye kasoro chungu nzima mojawapo ikiwa ni msaliti, au hujui hili?! We si ndiye uliyemsaidia katika kulisaliti pendo langu mimi na Edo?! Vicky alishangaa kidogo kutokana na shutuma hizo na kuone-sha kutahayari, lakini alijikaza na kujibu.
Kila nilichofanya, nilikifanya kwa ajili ya pendo langu kwa Onespot, kama kulikuwa na madhara katika hayo niliyotenda, basi mimi sikuyaona, love is blind mapenzi ni upofu. Vicky alisema haya bila kumuangalia Lulu usoni kisha akaendelea,
Na wewe Lulu ungekuwa unampenda Edo kweli kweli usingeona kasoro zake ungeendelea kuwa naye labda pendo lake juu yako ni la wasiwasi na ndio maana ukamtilia shaka. Lulu kidogo alihamaki kwa usemi huu wa Vicky, alitamani ampige kofi, lakini alijizuia na kumwambia Vicky,
Pendo langu juu ya Edo, halina shaka, lakini si pendo pofu. Upofu wa pendo siku zote unakuja kwa watu dhaifu, na bahati nzuri mimi si mtu dhaifu kama wewe. Mimi siye mtu wa kuambiwa ukitaka nikupende fanya hivi au vile palipo na wasiwasi au shaka, hata kwa mtu nimpendae, nitatia shaka tu.
Vicky hakuoneakana kuwa mwenye hisia zozote juu ya sura yake nzuri, alimwambia mrembo mwenzie Lulu.
Sikuwa na shaka na ahadi ya Onespot ya kuwa nae pamoja, na nashukuru ameitimiza, leo hii mimi ni mchumba wake, na siku za karibuni nitakuwa ni mke wa ndoa.
Lulu alidakia na kumjibu Vicky kwa sauti ya mkazo
..
Lakini kwa gharama ya nani? Ndio, utakuwa mke wa ndoa wa Onespot, lakini huoni kuwa ndoa yako itakuwa inakosa amani kila utakapokumbuka kuwa umeolewa kwa sababu ya kuwatenganisha watu wawili wanaopendana?!
Ndio maana ninakuambia pole sana Vicky, ni dakika chache zilizopita tu, nilikuwa ninamuambia mchumba wako kwamba, ana bahati sana kupata msichana kama wewe kuwa mke wake, sababu nilitambua upofu wa pendo lako juu yake. Vile vile nilimuomba ajirekebishe, na akupende ipasavyo. Nitajitahidi katika sala zangu, nimuombe Mungu amfanye Onespot awe mume bora kwako, si kwa sababu yoyote ile, bali ni kwa ajili yako wewe Vicky
kama mwanamke mwenzangu,
nisingependa Onespot amuumize mwanamke mwingine yeyote yule zaidi ya alivyokwisha kuniumiza mimi, kwa heri
Vicky.
Lulu alivuta hatua kutaka kuondoka , alisikia jina lake likiitwa na Vicky, aliitika
Beeh!
Samahani Lulu, nisamehe kwa yote yaliyotokea.
Wa kumuomba samahani ni Edo, sio mimi, kwani nimekwisha kusamehe!
Kwa sasa hivi unafikiri ninaweza kukusaidia nini Lulu?!
Ulikuwa wapi nilipokuwa ninahitaji msaada wako Vicky?! Umekwisha chelewa,
.maji yamekwisha mwagika. Kwa wakati huu Lulu alijikaza chozi lisije likamdondoka, na Vicky nae alioneakana mwenye sura ya kujuta na huzuni, waliachana.
* * * *
Lulu alimkuta Halfani Matai mpiga picha, anamsubiri. Nae Halfani kumuona Lulu tu, alimuuliza,
Vipi Lulu uko tayari tuondoke kuelekea kwa Edo?
Ndio, nipo tayari, twende zetu
Umeonana nae Onespot?!
Wote, pamoja na Vicky pia nimeonana nae
Wamesemaje?
Mengi ya kusema nilikuwa nayo mimi, wao waseme nini!
Lulu na Halfani walitoka nje ya ofisi yao na kuingia ndani ya gari ndogo iliyokuwa imeegeshwa hapo nje.
Ilikuwa ni gari aina ya Toyota Carina ya Halfani, Halfani alikaa nyuma ya usukani na kuanza kuendesha. Baada ya kupita mitaa kadha ya Sinza, mwishowe walisimama mbele ya nyumba aliyokuwa akiishi Edo.
Kwa shauku kubwa wote wawili waliteremka kutoka gari hiyo, waliuendea mlango mkubwa wa mbele wa nyumba aliyokuwa akiishi Edo, baada ya kuvuka geti na kuanza kugonga kubisha hodi, mara alitokea mama mmoja wa makamo. Alijitokeza nusu ya kiwiliwili chake sehemu ya juu. Walisalimiana nae vizuri, kisha Halfani alimuuliza mama huyo.
Samahani shangazi, tumekuja kumuona Edo, sijui yumo au ametoka?
Mama yule aliwaangalia vizuri kabla hajawajibu, kisha nae akauliza,
Kwani nyie wanangu mnatoka wapi? Na
samahani, ni nani zake Edo?! Halfani alikuwa ndiye msemaji mkubwa siku hiyo, alijibu,
Sisi shangazi tunatokea ofisi aliyokuwa anafanya kazi Edo, sisi ni wafanyakazi wenzake, mimi ni Halfani na huyu mwenzangu ni Lulu.
Lulu?!
Yule mama alirudia jina la Lulu na kulitamka kwa mshangao.
Ndio mama, huyu ni Lulu, kwani vipi, mbona umeshangaa?
Hapana mwanangu sikushangaa, lakini ukweli ni kuwa Edo amekwishahama hapa. Amesema ameacha kazi na anarudi kwao Arusha. Pia ameacha barua hapa, amesema iwapo msichana aitwae Lulu Frank kutoka ofisi aliyokuwa akifanya kazi iwapo atakuja kumuulizia, basi apewe barua hiyo,au apelekewe ofisini. Sasa je, wewe mama ndiye Lulu Frank?..Unafanya kazi pamoja na Edo?
Lulu alijibu haraka haraka, hakungoja kujibiwa na Halfani.
Ndio, ndie mimi Lulu Frank mama!
Basi ngoja nikakuletee hiyo barua, tulikuwa tunataka kuileta ofisini.
Mama yule aliingia ndani , akiwaacha Lulu na Halfani wamesimama hapo barazani nje. Baada ya muda mfupi tu yule mama alitoka tena, huku ameshikilia barua kiganjani mwake, alisema,
Samahani wanangu sikuwakaribisha hata ndani, karibuni mpite ndani.
Kwa shauku aliyokuwa nayo Lulu ya kutaka kujua hiyo barua toka kwa Edo imeandikwa nini,aliomba radhi kwa mama huyo na kujidai ana haraka sana. Yule mama alimkabidhi hiyo barua yake.Halfani na Lulu walirudi ndani ya gari na kungoa kuelekea ofisini kwao. Walipofika,kabla ya kuingia,Lulu aliamua aisome kwanza ile barua, ilikuwa na maneno haya.
"Mpenzi wa moyo wangu,Lulu Frank.Ninaandika barua hii fupi, nikiwa sina matumaini ya kuonana tena na wewe. Nina matumaini kuwa utakapopata barua hii, utakuwa tayari umekwisha mfahamu Onespot ni mtu wa aina gani, nakutakia maisha mema kama mtaamua kuishi pamoja. Jambo lingine ninapenda kukuambia wakati unasoma barua hii, nadhani nitakuwa tayari nimekwisha oa yule mchumba niliyewekewa na baba yangu, au nitakuwa kwenye matayarisho ya kufanya hivyo. Pamoja na kuwa bado ninakupenda, nimeona ni bora kuafikiana na wazee wangu kwa wanalolitaka. Ndoa ya mapenzi kwa mimi na wewe nikupendaye imeshindikana, heri nifikie muafaka na wazazi wangu katika ndoa ya kupangiwa.Akupendaye daima,Edward Oloi (Edo)"
Lulu aliangua kilio bila ya kujizuia mbele ya Halfani. Mpiga picha huyo alijaribu kumbembeleza kwa maneno ya kumfarji na kumpa matumaini. Mwishowe Halfani alimwambia Lulu.
Tafadhali Lulu nyamaza, kilio chako na unisikilize
Lulu alisinasina huku akifuta machozi kwenye macho yake mazuri yalikuwa yamegeuka rangi kidogo kwa sababu ya kilio alimuangalia Halfani.
Sikia Lulu, mimi binafsi ninajihisi kuwa nina hatia zaidi kuliko mwingine yeyote katika suala hili. Ninaona ndiye mimi niliyevunja uhusiano wako wewe na Edo. Kwani isingekuwa hivyo kama ningekataa kupiga zile picha.
Lulu kwa sauti ya chini na ya huzuni naye alijaribu kumwambia Halfani
Hapana Halfani, huna haja ya kujihisi kuwa una hatia, hii yote ni kazi ya Onespot. Hata kama wewe ungekataa kupiga zile picha, kwa kuwa yeye amekwisha dhamiria ubaya, angemtafuta mpiga picha mwingine
ni bahati mbaya tu kuwa wewe ndiye uliyeingia mtegoni kama nilivyoingia mimi. Edo alikwisha hisi jambohili pamoja na kuwa hakuelewa linaendeshwaje, ni mimi tu niliyekuwa mpumbavu.
Lulu aliuziba uso wake kwa viganja vyake vyote viwili na kuuinamisha chini baada ya kusema hayo,
Mimi ninakwenda ofisini kuuliza anwani za Edo za huko Arusha, ambazo nina hakika zitakuwepo ndani ya faili lake. Kisha nifanye safari nimfuate huko kwao. Sitapumzika mpaka nimekutana na Edo. Wacha nikurudishe nyumbani Lulu,ili mimi nianze safari, au utapenda kubaki ofisini? Halfani alisema habari hizi kumfahamisha Lulu, akiwa na amedhamiria kabisa. Lulu hakutaka kurudi nyumbani kwao kwa wakati ule, alimuomba Halfani amuache hapo hapo ofisini.
* * * *
Kuna gari zaidi ya mbili za kifahari zimeegesha nje ya nyumba nzuri aliyokuwa anaiendea Halfani, ni siku mbili baada ya yeye kuagana na Lulu. Nyumba hiyo ilikuwa kando ya mji wa Arusha, ilikuwa ni nyumba ya baba yake Edo, Mzee Oloi. Wakati huo ilikuwa ni majira ya saa kumi alasiri. Halfani alipoikaribia zaidi nyumba hiyo, alitupia macho huku na huku kwa matumaini ya kuona mtu kabla hata hajagonga mlango. Kweli , alimuona kijana mmoja aliyekuwa amevaa kaptula na fulana iliyokuwa haina mikono, nguo zilikuwa zimechafuka kwa udongo. Mvulana huyo mkononi mwake alikuwa amenyanyua reki na jembe, alionekana wazi kuwa alikuwa ndani ya shughuli za bustani inayoizunguka nyumba hiyo. Kijana huyo alimsogelea Halfani, na baada ya kusalimiana alimuuliza amsaidie nini. Nae Halfani alimjibu kwa kumuuliza,Samahani kijana, hapa ndipo nyumbani kwa akina Edward
..Edward Oloi?!
Eeeh, ndio hapa.
Sijui Edward mwenyewe yumo?!
Ndio, yuko ndani.
Ahsante kijana, naomba ukaniitie
huyo Edward.
Nimuambie anaitwa na nani?
Muambie Bw. Halfani Matai kutoka Dar es salaam.
Kijana aliondoka na kuelekea ndani ya nyumba hiyo, lakini sio kwa kupitia mlango wa mbele, bali alizunguka nyuma ya nyumba. Baada ya dakika chache, kijana yule alirudi akiwa ameongozana na Edo. Halfani alipomuona Edo, alitoa tabasamu kubwa la shukrani. Edo alikuja moja kwa moja mpaka alipokuwa amesimama Halfani, alikunjua mikono yake na kumkumbatia huku nae akitabasamu na kusema
Siamini macho yangu, karibu sana Bw. Halfani, karibu ndugu yangu, hapa ndio kwetu bwana.
Alimpokea begi ndogo aliyokuwa ameishika Halfani, akampa kijana na kumuashiria aipeleke ndani, kisha Edo alimchukua yule mgeni na kumuingiza ndani ya nyumba kwa kupita njia ileile aliyotokea Edo, nyuma ya nyumba. Edo aliendelea kusema,
Duh! Its realy a surprise visit, lakini kwema?! Karibu sana nimefurahi
.samahani sana rafiki yangu, ninakupitisha kuingia nyumbani kupitia mlango wa nyuma sababu huko mbele, sebuleni, kuna wazee wana kikao chao muhimu.
Edo aliyasema haya yote wakati wanaingia ndani ya nyumba. Baada ya mgeni yule kukarimiwa kwa taadhima zote, ilipofika jioni ilibidi akae pamoja na Edo wazungumze. Edo alianza
Enhe! Lete habari Halfani, kulikoni?! Halfani alionesha kuhuzunika kidogo, alisema kwa sauti ya chini bila kumuangalia Edo usoni.
Bwana Edo, nimekuja kwako rasmi kwa madhumini mawili, la kwanza ni kuhusu mimi mwenyewe na la pili ni kuhusu Lulu.
Alitulia kidogo kumpa nafasi Edo amuelewe anayomueleza, kisha akasema
Itaendelea