Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,983
- 10,804
Simulizi : TUTARUDI NA ROHO ZETU?
Mwandishi : BEN R. MTOBWA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
SEHEMU YA 1
KAMA maji ya bahari ya hindi yangekuwa na hisia, basi yangejisiskia fahari sana kwa kupata fursa nyingine ya kuiburudisha miili ya viumbe hawa wawili ambao walikuwa wakiogelea kandokando ya ufuko huku wakicheza na kucheka. Walifanya picha ya kuvutia sana, hasa sura zao nzuri zilipoibuka na kutoka majini na kumezwa na tabasamu lililosababishwa na mzaha waliokuwa wakifanyiana chini ya maji.
Baada ya kuogelea kwa muda walirejea nchi kavu ambako walijibwaga juu ya mchanga ulioruhusu joto likaushe maji miilini mwao.
Ufuko pia ungekuwa na kila sababu ya kusherehekea johari ya kulaliwa na viumbe kama hawa kwani walioana kimaumbile kama pacha, ingawa hawakuwa mtu na dada yake. Walikuwa kama jozi ya kiatu cha kiume kwa cha kike. Mwanamume hakuwa mwingine zaidi ya yule kijana mwenye umbo refu, kakamavu, lililokaa kiriadhariadha na sura nzuri, yenye dalili zote za hekima, ushujaa na ucheshi. Kwa jina anaitwa Joram Kiango.
Naye msichana alibahatika kupewa umbo lenye kila kitu ambacho msichana anahitaji kuwa nacho, wakati huohuo akiwa na kile ambacho mvulana legelege asingekuwa nacho. Ni yule ambaye akutazamapo ungependa aendelee kukutazama, achekapo unafarajika, atembeapo unaburudika, yule ambaye kuna madai kwamba alikuja duniani kwa makosa baada ya kuumbwa ili awe malaika. Kama madai hayo si kweli, basi yako mbali sana na uongo. Hata jina lake halikutofautiana sana na sura yake. Wanamwita Nuru.
Baada ya kuhakikisha kuwa miili yao ilikuwa imekauka, wakajifuta vizuri; kisha wakayachukua mataulo yao na kwenda kwenye gari lao. Macho ya watu wengi, Waswahili kwa watalii ambao walikuwa katika ufuko huo, hayakukoma kuwafuata. Kutazamwatazamwa, hasa wanapokuwa pamoja, halikuwa jambo geni tena kwao.
Mara kwa mara macho ya kiume yalimwandama Nuru, hali ya kike yakimfuata Joram, kila mahala walipopita. Walijifunza kuyazoea hata wakaanza kusahau kuwa wanatazamwa. Hivyo, walipolifikia gari waliingia na kulitia moto wakilielekeza mjini kwa mwendo usio wa haraka.
Hawakuwa na sababu yoyote ya kufanya haraka. Ratiba yao ya starehe ilikuwa