Simulizi ya Kijasusi: Tutarudi Na Roho Zetu?

SEHEMU YA 20

"Kifo chako," Chonde alimjibu kijeuri. "Siwapendi vijana watundu kama wewe. Kufa, huna budi.”
"Kosa langu."
"Unapenda kufa?"
Joram alifikiri kwa makini angefanya nini kuiahirisha hukumu hiyo ya kifo. Muda. Alihitaji muda ili ikiwezekana itokee njia moja au nyingine ya kuyaokoa maisha yake. Akaanza maongezi kwa sauti ambayo aliifanya dhaifu kuliko ilivyokuwa, akimwuliza Chonde hili na lile. Chonde alikuwa mgumu wa kutoa habari kama jabali. Kati ya maneno ya kashfa na matusi kwa Joram, nchi na bara zima hakutamka neno lolote ambalo lilimfanya Joram amjue yeye ni nani na anafanya nini katika ulimwengu wa ujasusi. Alichoambulia ni zile hisia tu kwamba Chonde hakuwa raia wa kawaida.
"Umeahirisha sana kifo chako," Chonde alisema baadaye kama aliyekuwa akizisoma fikra za Joram. “Sasa iliyobaki ni kazi ndogo ya kukutoa uhai. Nitakuua kwa mkono wangu wa kushoto. Maiti yako itaokotwa kesho ikiwa imevunjikavunjika kama mtu aliyeanguka toka ghorofani. Kwa jinsi ulivyobadilika kitabia watu hawatashangaa kusikia kuwa umejirusha dirishani.”
Baada ya maneno hayo, aliinuka na kumwendea tena Joram kwa utulivu kama awali, lakini macho yake yalitangaza kitu kimoja tu, kifo.
Joram alijiandaa, akijua kuwa vita vilivyokuwa mbele yake vilikuwa vikubwa kuliko vyote alivyowahi kupambana navyo, vita vya kuitetea roho yake. Akaikusanya akili yake yote na kumsubiri Chonde kishujaa.
Mara mlango ukagongwa.
Chonde aligutuka kwa mshangao na kuutazama mlango huo. Joram hakuipoteza nafasi hiyo. Aliruka na kuufanya mguu wake utue katika shingo ya Chonde. Lilikuwa pigo ambalo Chonde hakulitegemea. Likamtia mweleka. Lakini pigo la pili alilitegemea, akalikwepa na kuachia judo ambayo Joram aliikinga. Papo hapo mlango ukagongwa tena na kufunguka ukiruhusu sura ya msichana mzuri kuingia.
Alikuwa yule msichana wa mapokezi wa hoteli ya Embassy. Alitokwa na macho ya mshangao kuona miili yenye jasho, michubuko na damu, ya wanaume hao, ikiwa tayari kuvamiana. Wote walimtazama msichana huyo, Chonde akimlaani, Joram akimshukuru. Akiwa kama hajui lipi la kufanya msichana huyo aliduwaa mlangoni, Mdomo wazi.
 
SEHEMU YA 21

"Karibu ndani. Tulikuwa tukifanya mazoezi ya viungo na huyo rafiki yangu," Chonde alimhimiza akivaa tabasamu ambalo lilificha kabisa mauaji yaliyokuwa katika uso huo dakika iliyopita. "Karibu ndani. Nawe ndugu yangu nenda zako sasa. Tutakutana siku nyingine".
Joram aliyarekebisha mavazi yake na kutoka chumbani humo taratibu. Hakuwa amesahau kumwachia msichana huyo tabasamu jingine la shukrani.

********

"Nadhani hakuna njia nyingine zaidi ya kumlazimisha," Kombora alikuwa akifoka katika kikao cha dharura kilichofanyika usiku huo. "Hawezi kuachwa aendelee kustarehe katika mabaa huku taifa na bara zima likiwa mashakani. Mchango wake unahitajika."
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wote wa ngazi za juu katika idara zote za usalama nchini. Kiliitishwa ghafla baada ya kuokotwa barua moja ya vitisho katika ofisi ya Waziri Mkuu, barua ambayo iliandikwa kwa ufupi sana ikidai kuwa ajali za kimiujiza zingeendelea kuipata nchi ya Tanzania na zote zilizo mstari wa mbele, endapo serikali isingechukua hatua za haraka kukomesha msimamo wake wa kupinga utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Barua hiyo iliongeza kwamba safari hii moto ungeiteketeza hospitali ya Muhimbili, hoteli ya Kilimanjaro, Jengo la Kitega Uchumi na baadae Ikulu.
Aliyeiokota barua hiyo na kuisoma aliwaonyesha wakubwa wake ambao waliikabidhi kwa Waziri Mkuu. Baada ya kuisoma yeye pia, alikwenda Ikulu ambako alimpa Rais.
"Upuuzi ulioje huu. Hatutaacha kuwatetea ndugu zetu wanaoteswa bila makosa kwa ajili ya vitisho hivi. Havikuanza leo. Wala haviwezi kwisha leo. Tutapigana hadi mtu wetu wa mwisho katika kuilinda hadhi ya mtu mweusi katika bara letu hili." Pengine Rais alijibu hivyo akifoka kwa hasira. "Barua hiyo wakabidhi watu wa usalama. Nadhani hawatakubali kuendelea kuchezewa kiasi hiki. Waambie kwamba hatutaki upuuzi wowote ulioandikwa katika waraka huu haramu utokee." Huenda Rais aliongeza hayo.
Hakuna aliyeshiriki katika maongezi yao ya faragha, isipokuwa hisia hizo zinakuja kwa jinsi Waziri Mkuu alivyomwita Inspekta Kombora katika ofisi yake na kumkabidhi barua hiyo. Baada ya Kombora kuisoma kwa makini
 
SEHEMU YA 22

Waziri Mkuu alimwambia, "Ni barua ya khatari sana. Na imeandikwa na watu khatari, watu wenye kichaa. Kufuatana na hali ilivyo hatuwezi kukubali kuwa watumwa au mateka wa Makaburu kwa kuhofia ukatili wa vitisho vyao. Lazima tupambane nao ana kwa ana kama tunavyopambana nao katika uwanja wa mapambano. Tuliwashinda Msumbiji, Angola na Zimbabwe. Kwa nini tusiwashinde Namibia na Afrika Kusini? Tutawashinda. Wao wanajua hivyo, ndiyo sababu inayowafanya wakimbie toka katika uwanja wa mapambano na kuja huku kupigana kiuoga."
"Kama tulivyoshuku kitambo, mikasa hii haikuwa ya kawaida. Kulikuwa na mkono wa mtu, mkono wa mtu huyu ambaye ameandika barua hii na kuthubutu kuipenyeza katika ofisi yangu. Ingawa haijafahamika mbinu gani wanatumia kuweza kuanzisha mioto hii, nadhani hutashindwa kufanya juu chini ili uugundue na kuukomesha kabisa upuuzi huu."
Akijua uzito wa jukumu hilo ndipo Kombora aliporudi ofisini na kuitisha kikao hiki kilichokuwa kikiendelea. Walijadiliana kwa mapana na marefu kulikuwa na nini hasa hata majumba yalipuke moto ilihali uchunguzi kamili ulionyesha kuwa haikuwepo kasoro yoyote ya umeme. Hawakupata jibu. Walijaribu kuzijumuisha taarifa zote za upelelezi juu ya nani anaweza kuwa alihusika katika kusababisha mioto hiyo lakini bado hazikuwepo dalili zozote zilizoleta matumaini. Wakapanga mipango mipya. Wakawaandaa wapelelezi na vyombo kadha wa kadha katika majumba yaliyotajwa. Wakawekwa watu katika mahoteli, viwanja vya ndege na vituo vyote vya usafiri kuchunguza nani anaingia, nani ametoka na ameleta nini. Zaidi ya yote hayo, ndipo lilipotolewa tena pendekezo la kumshirikisha kila mtu mwenye uwezo wa kuchangia katika upelelezi. Hapo ndipo jina la ‘Joram’ lilipowatoka midomoni. Ikawashangaza wajumbe kusikia kuwa hata baada ya kuombwa na Kombora alikataa katakata kushiriki katika kazi hiyo. Joram waliyemfahamu alikuwa hangoji kuombwa au kutumwa bali alijituma. Vipi Joram huyu?
Ndipo mzee Kombora alipoibuka na uamuzi wa kumshurutisha. "Lazima tumlazimishe. Kama ameacha upelelezi kwa ajili ya mwanamke, basi atarudia upelelezi kwa ajili ya mwanamke. Yote hayo niachieni mimi," Inspekta
 
SEHEMU YA 23

Kombora aliwaambia.
Baada ya kikao hicho, alimchukua msaidizi wake mmoja na kumpeleka chemba. "Sikia," akamweleza, "Nakutaka uwe msiri wangu, wewe peke yako. Unaweza kutunza siri?"
"Bila shaka. Isipokuwa ya wizi na mauaji tu."
"Hii si ya mauaji wala wizi. Nataka unisaidie kumteka mtu nyara."
"Kuteka mtu nyara? Hiyo mbona haiko mbali sana na wizi? Na kama sikosei ni hatari zaidi ya wizi."
"Ndiyo. Lakini mtu tunayemtaka atafurahi sana. Bado ni msichana mzuri sana," Kombora alivuta pumzi kwa nguvu kisha akaongeza, "Nataka tumteke yule msichana wa Joram. Hiyo ndiyo njia pekee ya kumlazimisha."
Baada ya kujadiliana kwa muda walielewana. Wakaandika barua ambayo ilikusudiwa iwe imetoka kwa mteka nyara akidai kuwa amemteka msichana huyo na angemwua endapo Joram angethubutu kujihusisha na upelelezi unaoendelea nchini dhidi ya maafa ya kutatanisha. Licha ya barua hiyo, pia waliandaa damu ambayo ilipatikana kwa msaada wa daktari mmoja wa hospitali yao Ocean Road ili waidondoshe chumbani humo kuonyesha kuwa kulikuwa na mapambano ambayo yalisababisha damu kumwagika.
"Tunacheza mchezo mchafu sana, mchezo wa aibu. Lakini hatuna budi," Kombora alisema baada ya matayarisho yote ya kwenda katika chumba cha Joram.
Uchunguzi uliwapa fununu kuwa Joram alikuwa akiishi katika hoteli hiyo ya Embassy. Habari za mwisho usiku huo zilieleza kuwa Joram alipoachana na Kombora usiku huo alikuwa peke yake akinywa bia wakati msichana wake alipoondoka kwenda chumbani, na kwamba baada ya muda mrefu Joram alionekana akitoka nje na hadi sasa alikuwa hajarudi. Kombora alitegemea kuwa muda huo ulitosha kumfikia msichana huyo, kumshawishi na akikataa, kumlazimisha kisha kuondoka naye kwa siri kabla Joram hajarudi.
Walifanya hivyo.

Waliifika hoteli na kukiendea chumba chake kwa siri kubwa. Mlango waliukuta ukiwa wazi. Wakaufungua na kuingia huku wakiufunga nyuma yao. Macho yao yalivutwa na dalili za vurugu katika chumba hicho. Vitu vilikuwa vimetupwa ovyoovyo, matandiko yakiwa yamepinduliwa na masanduku
 
SEHEMU YA 24

kufunguliwa. Juu ya meza kulikuwa na karatasi yenye damudamu. Upande wa pili wa karatasi hiyo kulikuwa na maandishi ambayo yalikuwa barua ya wazi kwa Joram Kiango, barua ambayo haikutofautiana sana na ile ambayo Kombora aliiandaa:
Ndugu Joram,
Tunayo furaha kukufahamisha kuwa tumemchukua msichana wako na tutakuwa nae hadi hapo tutakapomaliza shughuli zetu. Hii ni kwa ajili ya kukuonya usithubuti kujihusisha na mambo yoyote yanayoitokea nchi hii. Endapo utakuwa mtoto mtiifu kama ulivyo siku hizi, hatadhurika, nawe utakuwa salama. Vinginevyo, utakipokea kichwa chake kwa njia ya posta na kisha kitafuata kifo chako.
Amri
Kombora aliisoma tena barua hiyo, kisha akamgeukia msaidizi wake na kumnong'oneza, "Tumechelewa sana. Wenzetu wametuwahi." akampa barua hiyo ili aisome.
"Sasa tutafanya nini?" askari huyo aliuliza baada ya kuisoma.
"Rudisha kila kitu kama kilivyokuwa. Fanya hima tuondoke hapa haraka," alimhimiza akianza kusogea mlangoni.
"Nilidhani tungemsubiri Joram!"
"Hakuna haja. Akirudi atajua la kufanya." Wakatoka na kuifuata njia ya kawaida. Wakiwa katika mavazi ya kiraia, watu wachache sana waliwatupia macho zaidi ya mara moja. "Jambo moja la kupendeza ni kwamba," Kombora alikuwa akisema. "Wamemchokoza Joram. Hawamfahamu vizuri. Wataujutia uamuzi wao"
***
Joram alifika chumbani kwake dakika kadhaa baadaye. Akiwa mchovu, jicho moja likiwa limevimba kwa pambano lake na chonde, alipitiliza hadi bafuni ili ayaepuke maswali ya Nuru. Huko ndani alioga vizuri, akaisafisha damu yote na kushevu kikamilifu. Kisha akarudi chumbani ambako macho yake yalivutwa na vurugu iliyokuwa imetokea.
Alitazama vitanda vyote na kutoiona dalili ya Nuru. Akaenda mezani ambako hakushangaa kukuta ujumbe ule ukiwa juu ya karatasi yenye damudamu. Akausoma kwa makini, akiuchunguza mwandiko huo ambao ulikorogwa katika hali ya kupoteza uhalisi wake. Akatikisa kichwa na kutokwa na tabasamu jembamba.
Usiku huo alilala huku kalisahau tabasamu hilo katika uso wake.
 
SEHEMU YA 25


SURA YA NNE

ASUBUHI hiyo, baada ya kuoga na kufungua kinywa, Joram alichukua simu na kupiga namba mbili tatu akitaka kuzungumza na rafiki zake wa zamani. Alipowapata aliwapa maekelezo fulanifulani kwa lugha ambayo wangeielewa wao tu. Baada ya hapo akajitokeza mitaani na kuanza matembezi. Akiwa kavaa vizuri suti yake ya kijivu aina ya three peace, kofia ikiwa imezifunika nywele zake ili kuficha mchubuko uliokuwa upande wa kushoto na miwani myeusi ikilificha jicho lake ambalo lilikuwa halijatii dawa kikamilifu, alionekana kama alivyotaka, mwungwana asiye na tatizo lolote mwilini wala akilini.
Msafara wake wa kwanza uliishia Barabara ya Sokoine katika tawi la Benki ya Taifa ya Biashara City Drive. Aliingia ndani na kuomba kuonana na meneja. Akaelekezwa hadi katika chumba ambamo alikaribishwa vizuri na afisa huyo ambaye uso wake ulimdhihirishia Joram kuwa hakuwa akiwajibika ili kuitikiwa wito bali kuwajibika kulikuwemo katika damu yake tangu alipozaliwa.
"Nikusaidie nini ndugu yangu?"
"Naitwa Joram Kiango. Ninayo akaunti hapa."
"Nakufahamu sana, ingawa ni mara yangu ya kwanza kukuona ukija huku kwetu. Mara nyingi unaishia huko huko kwenye pesa." Baada ya kutabasamu kidogo kwa mzaha huo aliongeza harakaharaka. "Umefuata mkopo?"
"Hapana mzee," Joram alimjibu. "Nikikopa nitashindwa kulipa. Ninachohitaji ni kutazama uwezekano wa kuweka mali yangu fulani ya thamani katika akaunti mnayoita Self-Custody. Ningependa mnifahamishe utaratibu ulivyo."
Meneja alitikisa kichwa huku akisema, "Hilo tu? Kwanini wamekusumbua hadi huku? Utaratibu wake si mrefu sana. Ziko fomu maalumu ambazo utajaza. Baada ya hapo utakabidhiwa ufunguo mmoja, ufunguo wa pili tutakuwa nao. Utakwenda huko chini na kuhifadhi mali yako hadi siku ambayo utapenda kuikagua au kuichukua. Malipo yake ...."
Joram alimsikiliza kwa makini, akitupa swali moja moja. Kisha alimwomba meneja akatazame hali ilivyo huko chini kabla hajajaza fomu zozote. Meneja akainuka na kushuka nae hadi shimoni. Walipita vyumba vya kuhifadhi nyaraka, baadhi vinahifadhiwa pesa na kimoja alielezwa kuwa kiliazimwa na Benki Kuu baada ya jengo lao kuharibika kwa moto. Baada ya kupewa picha kamili ya ulinzi na usalama wa hifadhi hiyo Joram aliaga na kuahidi kuwa angerudi baadaye kukamilisha kazi hiyo.
Toka hapo Joram alipita hapa na pale akifanya hili na lile, sigara baada ya sigara zikiteketea mdomoni, mwendo wake ukiwa wa utulivu kama mtu asiye na tatizo lolote ulimwenguni. Ungemwona kamwe usingefikiria kama mtu ambaye usiku wa jana mpenzi wake alitekwa nyara, bila shaka baada ya kuteswa sana.
Ni hali yake hiyo ya utulivu ambayo ilimshangaza Inspekta Kombora alipokutana nae katika mtaa wa Samora. Kombora alisimamisha gari lake na kumfuata Joram kando ya duka alipokuwa kasimama. "Joram," alisema baada ya kumsalimu. "Nasikia yule msichana wako ametekwa nyara".
"Hata mimi nasikia hivyo," lilikuwa jibu la Joram.
"Mbona hufanyi lolote."
 
SEHEMU YA 26

"Nifanye nini? Barua imenionya nisithubutu kufanya lolote. Vinginevyo, msichana wa watu atauawa. Unapenda afe, Inspekta?"
Kombora alitikisa kichwa kwa mshangao. "Joram niliyemfahamu mimi alikuwa hapokei amri kwa watu kama hao, hasa katika suala hili ambalo ni la uhai na kifo cha mtu na taifa zima. Mimi nilidhani wamekuchokoza. Nikategemea kuwa wangejutia uamuzi wao. Nilikosea?"
"Umekosea sana Inspekta. Joram unayezungumza naye si yule wa awali. Usishangae, Inspekta. Usiupoteze bure mshangao wako. Bado kuna mengi utayasikia juu ya Joram huyu ambayo yatakushangaza zaidi," Joram alisema huku akitupa kipande kimoja cha sigara na kuwasha nyingine. Alipomuona Kombora kama mtu ambaye hajui la kufanya au asiyeyaamini masikio yake, akaamua kuondoka polepole. Kombora alimsindikiza kwa macho yake yaliyojaa mshangao na huzuni.
Baada ya pitapita hii ya hapa na pale, Joram alirejea chumbani kwake ambako alijipumzisha kwa muda.Wafanyakazi na baadhi ya wapangaji wenzake, ambao walikuwa wamemzoea Nuru, walimsumbua Joram kwa kutomuona.
"Anaumwa?"
"Hapana. Kapata safari ya ghafla."
"Bila kuaga?"
"Ilikuwa ghafla."
Aliujenga vyema uongo wake huo hadi ukafanana na ukweli. Jioni hiyo, baada ya kula, kuoga na kupiga simu nyingine alijitokeza mitaani na kuanza matembezi yake. Safari hii matembezi hayo yaliishia Ilala, nyumbani kwake. Alielekea chooni ambako alifunua mahala fulani pa siri ukutani na kutoa kijisanduku alichokuwa kakificha hapo. Alishangaa kukuta kikiwa kitupu bila ya bastola na risasi zake ambazo alikuwa ameziweka huko. Hifadhi hii ilikuwa siri yake binafsi. Mtu pekee ambaye aliifahamu siri hiyo ni Neema Idd ambaye sasa ni Marehemu. Mtu mwingine ambaye angeweza kufahamu ni Nuru. Uko usiku mmoja, kati ya zile chache ambazo waliwahi kulala katika nyumba hii, alimtoroka Nuru akidhani yuko usingizini, akaja hapa na kuisafisha bastola hii. Pengine Nuru aliwahi kumchungulia. Lakini Nuru huyo sasa yuko mikononi mwa wateka nyara. Nani mwingine aliyeijua siri hii? alijiuliza kwa hasira, hasira ambazo zilimfanya atupe kasha hilo na kutoka nje baada ya kuifunga milango yote kwa ukamilifu. Msafara huu uliishia katika hoteli ya Embassy. Akaagiza vinywaji na kuanza kunywa. Baada ya bia mbili akaenda kaunta kuzungumza na yule msichana wa mapokezi.
"Shem, za kutwa."
"Nzuri sana, shemeji," msichana huyo alizungumza kwa furaha huku akimtazama Joram kwa mshangao. "Pole sana shemeji," aliongeza.
"Kwa?"
"Ule mchezo wa jana. Unajua mimi mpaka sasa siamini kama mlikuwa mnacheza tu. Nilidhani mlikuwa mnapigana. Yule bwana kashikilia kuwa ni mchezo tu".
"Ulikuwa mchezo. Mazoezi ya viungo. Wazungu huita practice."
"Mpaka mtoane damu?"

Je nini kilifuata??
Usikose kufuatilia sehemu zijazo

ITAENDELEA


BURE SERIES
 
SEHEMU YA 27 & 28


ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA

Nzuri sana, shemeji," msichana huyo alizungumza kwa furaha huku akimtazama Joram kwa mshangao. "Pole sana shemeji," aliongeza.
"Kwa?"
"Ule mchezo wa jana. Unajua mimi mpaka sasa siamini kama mlikuwa mnacheza tu. Nilidhani mlikuwa mnapigana. Yule bwana kashikilia kuwa ni mchezo tu".
"Ulikuwa mchezo. Mazoezi ya viungo. Wazungu huita practice."
"Mpaka mtoane damu?"

SASA ENDELEA

Hakujua Joram alivyoisherehekea habari hiyo. Alitupa maneno mengine mawili matatu, kisha akairudia meza yake. Akaendelea kunywa na kuvuta. Japo alionekana katika hali ya utulivu, lakini macho yake yalikuwa makini, yakimtazama kila anayeingia na kutoka. Aliwaona wengi. Na kati yao alikuwemo yule ambaye alihitaji kumwona.
Alikuwa rafiki au adui yake, Chonde. Aliingia na kuifuata meza ambayo haikuwa na mtu, akaketi. Mara tu Joram alipomwona akainuka na kwenda kupiga simu ambayo alizungumza maneno machache sana. Kisha alikirudia kiti chake na kumwita mhudumu ambaye aliombwa kuleta bia nne. Mhudumu huyo alipozifikisha chupa hizo Joram alimwelekeza azipeleke kwa Chonde. Kisha alitulia akimtazama Chonde alivyokuwa akibishana na mtumishi huyo kwa zawadi hiyo ambayo hakujua ilikotoka hadi alipoelekezwa na kumwona Joram. Akazipokea na kuanza kunywa.
Lakini baada ya dakika kumi meza ya Joram ilifurika kwa chupa kumi zilizoletwa na mtumishi yuleyule kwa niaba ya Chonde. Walitazamana kwa muda. Baada ya muda Chonde alihamia meza ya Joram.
"Za tangu jana?"
"Siyo mbaya."
Wakaendelea kunywa kwa muda. Kila mmoja akimsoma mwenzake. Kisha Chonde alitokwa na kicheko chembamba. Joram aliungana naye kwa tabasamu dogo.
"Pole sana."
"Kwa?"
"Yale ya jana."
"Lilikuwa zoezi tu. Usijali."
Kikafuata kimya kingine, kimya ambacho Joram alikivunja kwa kuanzisha maongezi ambayo Chonde alizungumza kwa uangalifu akiepuka lolote ambalo Joram alihitaji kufahamu juu yake. Pamoja na Joram kuzungumza kwa ujanja na hila za kila aina, bado Chonde alimfanya ajione mtoto sana katika dunia ya upelelezi na mzembe katika elimu ya saikolojia. Ni hapo alipozidi kuamini kuwa Chonde hakuwa mtu wa kawaida. Na kama alikuwa jasusi bado hakuwa jasusi la kawaida. Alikuwa zaidi. Jambo hilo liliongeza hasira za Joram dhidi ya mtu huyo. Amshinde vipi katika mapambano ya mwili na amshinde tena katika mapambano ya kiakili? Hata hivyo Joram hakujali sana, akijua kuwa dakika hii ambayo anaipoteza na Chonde, mahala fulani, yuko mtu ambaye anaifanya kazi ile ambayo yeye alishindwa kuifanya jana, kazi ya kufungua kile kijaluba cha Chonde na kuona kimehifadhi nini hata kilindwe kwa kiwango kama kile. Hivyo, akaamua kumruhusu Chonde aendelee kumlaghai na kumdhihaki.
"Mwanamapinduzi aliyekata tamaa," Chonde alisema. "Aibu ilioje kukata tamaa hali nchi yako iko mashakani? Si ungejaribu kutoa mchango wako?"
Joram hakumjibu.
Kisha kama aliyekumbuka jambo Chonde alisema ghafla, "Nasikia msichana wako ametekwa nyara!"
“Umesikia wapi?"
"Kwani ulidhani siri?"
Hilo lilimshitua Joram. Alishangaa kuona mtu huyo alivyo mwepesi wa kupata habari. Baada ya kuisoma barua ile Joram hakuipeleka polisi wala kuchukua hatua zozote zaidi ya kutabasamu tu. Lililomfanya asifanye lolote hasa ni kule kuwa kwake na uhakika kuwa barua ile aliielewa zaidi ya mwandishi wake alivyotaka aielewe. Bila shaka mtu huyo alikuwa amezidokoa habari hizo kwa polisi. Jambo hilo lilimfanya azidi kumfanya Joram kuamini kuwa hakuwa mtu mwenye mkono mrefu tu bali alikuwa na masikio mapana.
Yeyote aliyeketi kando akiwatazama watu hawa wawili wakiongea angeamini kuwa ni kikao cha marafiki wa siku nyingi. Asingeamini kuwa yalikuwa kama maongezi baina ya Chatu na Mbwa, au baina ya Malaika Gabriel na Ibilisi.
Yule msichana wa mapokezi alikuwa mmoja kati ya watu walioamini hivyo. Alikuwa amewatazama kwa muda mrefu na kushuhudia wanavyocheka na kutabasamu, akayasahau mashaka yote aliyokuwa nayo juu ya urafiki wao na kuamini kuwa pambano la jana lilikuwa zoezi la viungo. Hivyo, alizama katika shughuli zake na kuwatupia jicho mara moja moja.
Chonde alikuwa akifunua mdomo kuongea kitu wakati saa yake ilipotoa mlio ambao haukuwa wa kawaida. Ulikuwa mlio wa sauti nyembamba sana, ulimfikia Joram kwa mbali sana. Chonde aliitazama saa hiyo kwa utulivu, kisha alimtazama Joram kwa makini zaidi. Dakika mbili baadae
 
SEHEMU YA 29 & 30

aliendelea kunywa kwa utulivu. Dakika ya tatu aliinuka na kuaga kuwa anaelekea msalani. Joram alisubiri dakika tano, kisha akamfuata. Hakumkuta. Akafahamu kuwa mlio katika saa ya chonde ulikuwa ishara ambayo ilimkumbusha kitu fulani, jambo lililomfanya Joram kuhofia mtu wake ambaye wakati huu alikuwa katika chumba cha Chonde. Hivyo, akakiendea kibanda cha simu na kuzungusha namba za simu za chumba hicho. Haikupokelewa. Toka kwenye simu, Joram alitoka nje ya hoteli na kukodi gari ambalo lilimpeleka New Afrika. Akajipenyeza kwa hila hadi ghorofani, mbele ya chumba hicho. Akatega sikio na kusikiliza kwa makini. Chumba kilikuwa kimya kabisa. Ukimya huo ulimtisha sana. Aliyaamini sana masikio yake. Na kwa vyovyote alitegemea kuwa na mtu chumbani humo. Akasikiliza kwa makini zaidi. Bado hakusikia chochote. Akaufungua mlango taratibu na kuchungulia.
Macho yake yalivutiwa na mtu aliyelala chali juu ya sakafu utumbo wake ukiwa nje, macho yake yakidhihirisha kuwa roho ya mtu huyu pia ilikuwa nje. Kabla Joram hajajua kuwa ilimpasa kuingia chumbani humo au la, sauti nzito aliyoifahamu sana ilimhimiza ikisema, "Usiogope. Karibu ndani."
Msemaji alikuwa kajificha nyuma ya mlango, bastola kubwa ikiwa mkononi mwake ikimtazama Joram kwa uchu.
"Ingia na ufunge mlango. Nadhani hutapenda kufia hapo mlangoni kama paka. Njoo ndani ufe kistaarabu kidogo."
Joram akaingia. Hakujishughulisha kumtazama Chonde aliyesimama nyuma ya mlango na bastola yake. Badala yake alimtazama marehemu na kushuhudia alivyouawa kinyama. Tumbo lake lilikuwa limebomoka kwa kitu ambacho hakikuwa risasi wala kisu. Bila shaka ulikuwa mlipuko wa bomu. Kifo hicho kilimsikitisha sana Joram. Huzuni ikamshika. Kwa huzuni hiyo alimgeukia Chonde na kufoka kwa hasira akisema, "Shetani mkubwa. Kwa nini umemwua mtu huyu asiye na hatia?"
"Ni wewe uliyemwua," Chonde alimjibu Joram.
"Mimi! Nimemwua vipi?"
"Usijifanye hufahamu. Bila shaka ni wewe uliyemtuma kuifanya kazi ile ambayo mwenyewe ilikushinda. Kazi ya kujua katika kisanduku hicho mna nini. Nami nikifahamu kuwa pamoja na kukuadhibu, kama nilivyokuadhibu usiku wa jana usingekata tamaa ndipo niliamua kutega bomu dogo kando ya kisanduku hicho. Wakati huohuo mtu yeyote anayekigusa saa yangu inaniashiria. Hivyo tulivyokuwa tukinywa hapo hotelini nilishangaa kuona dalili za mtu.
“Nikafahamu kuwa mtu asiye na hatia anakufa. Nimemkuta kisha kata roho.” Akageuka kumtazama marehemu kwa muda. Kisha aliyarejesha macho katika uso wa Joram na kusema, "Ni wewe uliyestahili kuwa chali, utumbo nje, badala ya mtu huyu, Joram.”
Joram asingeweza kukanusha. Kifo cha kijana huyo kilimsikitisha sana. Alikuwa mmoja kati ya vijana wake smart ambao huwatumia kwa hili na lile, kijana ambaye alikuwa amemsaidia sana katika harakati zake zilizopita. Hakupata kushidwa hata mara moja isipokuwa leo ambapo ameyapoteza maisha yake. Joram akajilaumu kumtuma katika kadhia hiyo. Hamu yake ilikuwa ni kumshinda na kuutawanya ubongo wake sakafuni...
Kama aliyekuwa akiyasoma mawazo yake, vilevile Chonde aliongeza kwa sauti nzito, "Hata mimi sikufahamu kama wewe ni mtu hatari sana Joram. Unastahili kufa mara moja."
Maisha yakiwa ukingoni, Joram alijua kuwa alihitaji kuikusanya akili yake yote ili ajiokoe. Hakujua afanye nini. Walikuwa na bastola moja tu, na ilikuwa katika mikono ya Chonde. Kuipata bastola hilo ilikuwa ndoto ya mchana. Chonde alikuwa macho kama kipepeo. Na bado Joram asingemudu kuitumia mikono yake. Hata hivyo, alitegemea kitu kimoja tu kimsaidie kutafuta muda wa kuokoa maisha yake. Muda. Muda waweza kufanya maajabu. Hata asipookoka, si inapendeza endapo ataufaidi uhai wa dakika chache zaidi.
"Najua ninakufa," alisema. "Nadhani unafahamu vizuri kuwa nakufa kwa ajili ya tamaa ya kutaka kujua siri uliyoificha katika kijisanduki hicho. Nifanyie basi wema wa mwisho. Nifungulie kisanduku hicho nife nikijua mna nini."
Chonde alicheka, "Tatizo lako Joram ni kule kufikiria kuwa unacheza na mtoto mdogo. Unachojaribu kufanya ni kuvuta muda. Wakati huohuo unathubutu kuendelea na upelelezi wako ili endapo lolote litatokea - kitu ambacho siamini - utoroke na kutoa siri hiyo nje. Kwa taarifa yako siri iliyoko katika kisanduku hicho ni nzito kuliko bara zima la Afrika. Kwa maneno mengine, ni siri
 
SEHEMU YA 31 & 32

ambayo dunia nzima inapigania kujua. Kwa bahati mbaya watu tunaoifahamu siri hiyo ni wachache sana. Na tumeshona midomo. Hata maiti siwezi kuisimulia siri hiyo. Nadhani hilo linakutosha. Sasa jiandae kufa. Ungependelea risasi ya kichwa au kifua?"
Joram alimtazama usoni na kuliona tabasamu la kifedhuli katika macho yake, tabasamu ambalo halikuwa na mzaha. Akajaribu kuicheza tena karata yake ya mwisho. "Jana ulinishinda kwa judo. Vipi ukiniua kwa mikono? Nadhani ni aibu na dalili za uoga kutumia risasi pasipo na umuhimu."

Chonde alicheka tena. "Ningependa kukuua kwa mikono mitupu. Hata hivyo, sina muda wa kutosha. Umebakiwa na nusu dakika ya kuishi. Utapenda kufa ukiwa umefumba macho au nikuue ukinitazama?"
Sasa mzaha ulikuwa mbali na sauti ya Chonde. Mauaji yalikuwa wazi katika macho yake. Joram akajua kuwa maisha yake yamefika ukingoni. Akiwa ameshuhudia vifo vingi vya risasi alitabasamu kimoyomoyo na kuamini kuwa hatimaye zamu yake imefika. Hata hivyo, bado aliyapenda maisha. Bado aliipenda dunia. Na alikuwa akiiacha moja kwa moja. Hivyo, badala ya kuyafumba macho yake aliyafumbua kwa nguvu na kuyakaza usoni. Hiyo pia aliifanya kuwa karata yake ya mwisho kwani kuua si mchezo, hasa kumwua kiumbe asiye na uwezo wa kujitetea.
Ilimsaidia. Nusu ya dakika ilipita Chonde kaielekeza bastola katika kifua cha Joram, kidole chake kikigusa kiwambo cha kufyatulia risasi, lakini alisita kuifyatua. Mara mlipuko wa bastola ukasikika. Joram alijirusha kando na kutua chini ambapo aliruka tena hadi upande wa pili wa kitanda. Risasi mbili tatu zaidi zikasikika, kama zinazopigwa bila shabaha yoyote. Kisha kimya kikafuata. Kimya hicho kilitoweka kwa mkoromo wa mtu aliyekuwa akikata roho. Ndipo Joram alipojiinua na kuchungulia. Ikamshangaza kumuoa Chonde kalala chini, kifudifudi, damu zikimvuja katika tundu kubwa la risasi katika uso wake. Joram alichupa na kuirukia bastola iliyokuwa mikononi mwa Chonde. Akajicheka kwa kuona akipokonya bastola kutoka katika mikono ya marehemu aliyekata roho kitambo. Akaikimbilia suit case ya chonde pamoja na kile kisanduku. Akavichukua na kuanza kutoka.
Mara mlango ulifunguka ukifuatwa na bastola ambayo ilichungulia kwa uangalifu. Bastola ikaingia ikifuatiwa na binadamu ambaye aliufunika uso wake kwa kofia kubwa na miwani. Alikuwa kavaa suruali na koti la kiume katika hali ambayo ingemfanya mtu yeyote amfikirie kuwa pande la mwanamume. Lakini Joram alimfahamu mara moja. Akaitelemsha bastola yake ambayo aliishika na kumkimbilia huku akisema kwa furaha, "Nuru nawezaje kukushukuru Nuru?"
Walikumbatiana na kubusiana kwa furaha.
Kisha walitengana mara moja na kutazamana. "Umewezaje kunifahamu mara moja kwa urahisi kiasi hiki? Tangu nimetoweka watu wanashindwa kunifahamu".
"Nadhani nakufahamu zaidi ya wanawake wote. Zaidi ya hayo nani mwingine ambaye anaweza kuhatarisha maisha yake kuipenyeza risasi katika tundu la ufunguo ili kumwua mtu ambaye alikuwa tayari kuniangamiza? Kwa kweli sijui namna ya kukushukuru Nuru!"
Wakakumbatiana tena.
"Nuru! Niliwahi kukwambia kuwa u mzuri? Niliwahi kukuambia kuwa hawakukosea waliposema kuwa wewe ni binadamu aliyekuja duniani kwa makosa badala ya kuwa malaika kama ulivyokusudiwa? Nadhani walikosea Nuru. Wewe ni malaika. Tazama ulivyo mzuri! Tazama ulivyotokea na kuipokonya roho yangu kutoka katika kinywa cha mauti. Nuru, nawezaje kukushukuru Nuru?"
Hayo yalipita katika kichwa cha Joram wakiwa wamekumbatiana. Joram alitamani kuyatamka kwa sauti, lakini hakufanya hivyo. Badala yake alisema, "Nakupenda."
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Nuru kumsikia Joram akilitamka neno hilo. Mara kwa mara alimtesa kwa kutojua kama kweli alimpenda au la. Ingawa walifanya mapenzi, mara nyingi, lakini bado Joram hakuwahi kulitamka neno hilo kwa sauti ambayo ililipa uzito kama huo. Kadhalika, macho yake hayakufichua mapenzi yake kwa hali yoyote. Hivyo, kwake ilikuwa zaidi ya habari njema. Hata hivyo, bado alikuwa na la kusema. "Sikuamini Joram," alimnong'oneza. "Pamoja na kutoweka kwangu nikiwa nimetekwa nyara hukujishughulisha kunitafuta. Walao kutoa taarifa polisi."
Joram akaangua kicheko. "Usinichekeshe Nuru. Waweza kuwa ulifanikiwa kuwalaghai watu wote pamoja na polisi, lakini mimi hukunidanganya. Nilijua kuwa ilikuwa hila uliyoiandaa tu ili unishawishi kuingia katika vita. Mwandiko wa barua ile pamoja na kuuvurugavuruga, kwa mtu
 
SEHEMU YA 33 & 34

aliyesomea miandiko kama mimi, nilifahamu kuwa ni wako. Vilevile ile damu iliyodondoka pale haikuwa na uzito wowote. Nilijua umejikata kidole makusudi. Na ile vurugu iliyofanyika chumbani haikuwa na umuhimu. Kwa vyovyote, majasusi khatari kama hawa wasingefanya mchezo usio na umuhimu kama ule. Hivyo, nilikuwa nikikusubiri nikitegemea utokee na tuendelee na starehe zetu."
"Starehe?" Nuru aliuliza kwa mshangao. Alishangaa kuona Joram alivyoigundua hila yake kwa urahisi. Ilimshangaza zaidi alipodai starehe wakati wamesimama kando ya maiti mbili ambazo zilikuwa hata hazijapoa kwa ajili yao. "Starehe Joram? Nilidhani tumeingia kazini."
Joram akatabasamu. "Sikia Nuru, siyo tabia nzuri kuzungumza kando ya maiti za binadamu. Pamoja na kwamba bastola zilizotumika zilikuwa na viwambo vya kupoteza sauti bado mtu yeyote anaweza kutokea na kutukuta katika hali hii. Nasi hatuna muda wa kuyajibu maswali ya polisi. Twende zetu mara moja," alimaliza akiichukua mizigo yake na kuanza kutoka. "Nifuate. Twende kwa utulivu kama tutokao chumbani kwetu."
"Kumbuka tu wanaume wawili," Nuru alisema akitabasamu.
Waliteremka na kuiacha hoteli bila ya tatizo lolote. Watu wawili watatu waliokutana nao waliwatazama kikawaida.
Baada ya kuingia mitaani Nuru aliifichua bastola na kumpatia Joram akisema. "Chukua bastola yako. Samahani kwa kuichukua bila idhini yako. Nadhani uliihitaji sana. Ningeweza kukupotezea maisha."
Tabasamu likamtoka Joram. "Hata hivyo umeniokoa. Kama ningeingia nayo pengine Chonde angeniua kwanza na kunisimanga baadaye," Joram alijibu. "Nimepata nyingine. Hii umeipataje?"
"Nilienda kwako kuichukua".
"Na umewezaje kunusa kuwa niko katika chumba kile nikisubiri kufa hata ukaja kuniokoa?"
"Ni rafiki yako aliyekuokoa. Hayati Edward ambaye, kwa bahati mbaya, mshenzi yule amemwua. Unajua nilipotoka hotelini kwa kisingizio cha kutekwa nyara, nilienda kujificha kwake? Tulijadiliana nae namna ya kurudisha moyo wako katika msimamo unaotakiwa. Mara ukampigia simu na kumpa maelekezo ya kwenda kufungua kisanduku hicho. Aliponieleza maelezo yako na jinsi ulivyoponea chupuchupu mara ya kwanza ndipo nilijua kuwa umerudi kazini. Nilitaka nije kwako mara moja. Lakini yeye aliniomba nisifanye pupa. Akaniomba nifuatane nae katika hoteli na kujificha kando nikimlinda. Nilifanya hivyo. Mara nikaona mtu mwenye dalili za kikafiri akiingia chumbani humo, bastola mkononi; ingawa ilifichwa sana. Kabla sijafahamu la kufanya nilikuona wewe pia ukinyatia na kuingia. Ndipo nilipojivuta mlangoni na kuchungulia katika tundu la ufunguo. Nikamwona Chonde akiwa tayari kukuua. Sikuwa na la kufanya zaidi ya kumlenga na... na ..."
Mara Nuru aliangua kilio. Akamgeukia Joram na kumkumbatia kwa nguvu akisema, "Nimeua mtu... Nimeua mtu, Joram..."
"Watu huuawa," Joram alimnong’oneza. "Hebu jitahidi kuwa msichana shujaa kama ulivyo, Nuru. Usingemwua angeniua. Watu watakusikia. Twende zetu chumbani."
"Lakini nimeua, Joram... nimeua..."
******

Ulikuwa usiku mfupi sana kwa Joram. Alikuwa na mengi ya kufanya ambayo hakuweza kuyatekeleza. Ilimchukua muda mrefu kumshawishi Nuru kwa vinywaji na mahaba ili asahau hofu yake ya kuua mtu. Baada ya usiku wa manane ndipo Nuru alipoacha kuweweseka na kupitiwa na usingizi mzito. Lakini alimkumbatia Joram kwa nguvu. Ilimlazimu Joram kutumia hila fulani na kujitoa mikononi mwake na kumfanya akumbatie mto.
Akinyata kwa utulivu, Joram alikiendea kisanduku cha marehemu Chonde na kutazama uwezekano wa kukifungua. Isingekuwa kazi rahisi. Ilihitaji utaalamu wa hali ya juu au risasi ya bastola. Joram hakuwa tayari kuitumia risasi kwa hofu ya kumwamsha Nuru. Na utaalamu siyo jambo ambalo lingepatikana kwa dakika moja. Hivyo, alikiweka kando kisanduku hicho na kuuchukua mfuko wa Chonde ambao haukumchukua muda kuufunua mifuko yake ya siri ambamo alitoa nyaraka mbalimbali na kuzisoma kwa makini. Yale maandishi wa kijasusi ni jambo jingine ambalo lilihitaji muda na utulivu mkubwa ili kueleweka. Hivyo, hakupoteza muda kujaribu kuyasoma. Badala yake alichukua hati ya kusafiria ya Chonde, kile kijisanduku na nyaraka zote alizoona muhimu. Vitu vingine alivifungafunga katika mfuko na kuvificha mahala ambapo aliamini kuwa visingepatikana kwa urahisi.


Baada ya hapo alichukua begi lake na kutoa vitu vyote vilivyokuwemo. Alichukua kinyago fulani cha hoteli na kukifunga katika mfuko wa nailoni na kuutumbukiza katika begi lake. Akalinyanyua kupima uzito wake. Kisha akaliweka mezani, na kuacha balbu ambayo ilikuwa ikitoa nuru
 
SEHEMU YA 35 & 36

nyekundu iendelee kuwaka. Akalitupa taulo lililokuwa kiunoni mwake na kujilaza kitandani kwa utulivu akiutoa mto aliokuwa ameukumbatia Nuru na kuichukua nafasi hiyo. Akainua mikono ya Nuru na kuifanya ituwe kiunoni mwake. Akayafumba macho yake na kujifanya kulala. Lakini asingeweza kulala alikuwa akiyasubiri mapambano kwa hamu.
Joram hakujua kuwa alikuwa amepitiwa na usingizi mzito. Alipoamka alikutana na macho mazuri ya Nuru yakimtazama kwa utulivu. "Za asubuhi, mpenzi," Nuru alimsalimu Joram.
"Nadhani siyo mbaya."
Nuru alitulia kidogo kabla ya kuongeza, "Nilikuwa nikisubiri uamke ili tuzungumze mpenzi. Nadhani haya yatakuwa maongezi yetu ya mwisho".
"Kwa vipi?"
"Unajua jana nimeua mtu? Wakati wowote polisi watafika hapa na kunitia pingu. Endapo nitanusurika kitanzi siwezi kunusurika kifungo cha maisha." Akasita tena na kuongeza, "Leo nimeota mpenzi. Nimeota nikining'inia juu ya kitanzi. Wewe na watu wengine mkiwa kando mkinicheka. Nilijaribu kukuita unisaidie lakini sauti haikuweza kutoka."
Joram akacheka. "Nani aliyekwambia kuwa utafungwa? Polisi wangemfahamu mtu aliyemwua bila shaka ungepata medali ya dhahabu badala ya kukuvika pingu. Licha ya hayo, hawawezi kabisa kufahamu nani alimwua. Unajua, uliingia hotelini mle ukiwa mwanamume? Ni mimi tu niliyeweza kukufahamu," Joram akacheka tena. "Lakini yote hayo ya nini? Leo tunaenda zetu Nairobi."
"Kufanya nini?"
"Kutumia."
Nuru akashikwa na mshangao. "Nilidhani umeingia kazini Joram."
Joram alitabasamu kabla ya kumjibu akisema. "Kuna mpelelezi mwenzangu maarufu anayeitwa Willy Gamba, aliwahi kusema kazi na dawa. Mpelelezi ni binadamu vilevile. Lazima astarehe na kuburudika. Yawezekana tutaenda Nairobi tukiwa kazini. Sasa, sikia Nuru. Nitafunga mizigo yetu yote na kukutaka ukanisubiri Uwanja wa ndege. Hapana usiende Terminal II nenda kanisubiri Terminal I uwanja wa zamani. Nataka twende kwa ndege ya kukodi."
"Ndege ya kukodi!" Nuru hakustahamili kuficha mshangao wake. "Kwa kweli, suala zima linanitatanisha. Kwanza, nadhani hatuna pesa za kutosha kutuweka hotelini kwa siku tatu zaidi."
"Nani aliyesema kuwa hatuna pesa?"
Saa mbili baadaye Joram alikuwa mtaa wa Sokoine akielekea benki ya City Drive. Mkononi alikuwa na mfuko wake mkubwa ambao ulionekana mzito. Alipoingia benki alimfuata meneja aliyeongea nae jana ambaye alimpokea katika hali ya kujuana. Baada ya salamu za kawaida Joram alipewa fomu alizotakiwa kujaza. Akajaza kwa makini na kuzirejesha kwa meneja ambaye alizipitia. Kisha alitakiwa kuonyesha mali yake aliyohitaji kuhifadhi kwa utaratibu wa Self-Custody. Akafungua begi lake na kutoa kinyago.
"Ni hicho tu?" meneja aliuliza. "Nilidhani una kidani cha almasi," akamjibu kwa sauti ya mzaha.
Moyoni meneja huyu aliamini kabisa kuwa ndani ya kinyago hicho mlikuwa na kipande cha almasi au Tanzanite. Kwani hakuona sababu nyingine ambayo ingemfanya Joram ajiingize katika gharama kubwa kwa ajili ya kinyago cha Mmakonde mmoja.
"Hiki kina thamani kama roho yangu," Joram alimjibu meneja.
"Ni kumbukumbu ambayo iliachwa na babu mzaa babu ambayo inalinda ukoo wetu. Niliwahi kudhani kwamba ni utamaduni wa kipuuzi nikakidharau, lakini yalinipata makubwa. Nusura nipoteze roho. Tangu nimekithamini na kuwa nacho, mambo yameniendea kama ninavyotaka."
Meneja huyo alielekea kumwamini. Wakainuka na kuelekea shimoni. Waliwapita wafanyakazi wanaotunza akaunti za watu, ambao hawakujishughulisha kuwatazama zaidi ya ule mtazamo wa kawaida. Wakateremka ngazi na kuingia vyumba vya chini. Ni hapo Joram alipomgusa meneja huyo bega na kumwambia, "Sikia bwana meneja. Sihitaji kuhifadhi kinyago hiki wala kitu kingine. Nahitaji pesa. Za kigeni."
Sauti yake ikiwa ileile, makini, iliyotulia, ikamfanya meneja huyo kudhani kuwa huo ulikuwa utani mwingine wa Joram. Hivyo, aligeuka akitabasamu. Lakini tabasamu lake liliyeyuka ghafla na nafasi yake kumezwa na hofu iliyochanganyika na mshangao mara alipokutana na bastola kubwa ikimchungulia kifuani.
"My God," aliropoka kwa hofu.
"Usiogope," Joram alimnongoneza. "Endapo hutakuwa mbishi hutaumia. Kwanza pesa hizo sio zako. Nifunguliea nichukue kidogo na kuondoka zangu."
"Sina ufunguo," meneja alijibu. "Zaidi ya hayo, vitasa hivi hufunguliwa na watu wawili kwa pamoja. Sioni unavyoweza kuzichukua." Akavuta pumzi kwa nguvu kabla ya kuongeza, "Licha ya hayo ndugu Joram, nashindwa kuamini kama kweli unadiriki kukifanya kitendo hicho. Unajua
 
SEHEMU YA 37 & 38

wewe ni mtu mwenye hadhi kubwa hapa nchini na duniani kote. Kwa nini uichafue hadhi hiyo? Kama unataka pesa hata ungeiomba serikali ungepewa. Hakuna asiyejua mchango wako katika kuilinda nchi hii."
"Yaelekea huufahamu ubahili wa serikali hii wewe," Joram alimcheka. "Sasa tusipoteze muda. Mimi ninazo funguo ambazo zinafungua kila kufuli. Sidhani kama kufuli zenu zitashindikana. Nitakupa funguo hizo ujaribu mmoja baada ya mwingine. Nitakuwa nyuma yako nikikutazama. Ukifanya ujinga utapoteza maisha yako."
Juhudi hizo hazikufua dafu. Ndipo alipoamua kufumua kitasa kwa risasi. Bastola ilikuwa na kiwambo cha kupoteza sauti, na, kwa hivyo, ulitokea mlio wa kawaida tu.
Dakika iliyofuata walikuwa ndani ya chumba cha fedha za kigeni, Joram akiwa kamsimamia meneja ambaye aliamriwa kutoa kinyago na kupakia mabunda ya noti za Dollars, Pounds na nyinginezo. Mfuko uliposhiba, Joram alimwamru meneja huyo kuondoka. Aliuchukua mfuko na kumtaka atangulie.
"Tutatokea mlango wa uani na kwenda nje kupitia geti. Bastola itakuwa mfukoni lakini tayari kuvunja mgongo endapo utafanya ujanja au ujinga wowote. Tembea kama kawaida bila kugeuka nyuma."
Walitoka na kuelekea uwani badala ya ofisini. Wafanyakazi wawili watatu waliwatazama kwa mshangao lakini tabasamu la Joram liliufanya mshangao wao utoweke. Tabasamu hilohilo liliwafanya askari wa geti wasishuku lolote kumwona meneja wao katangulia akitokea mlango ambao huutumika kwa nadra sana.
Barabarani Joram alimtaka meneja huyo kuendelea na safari akiifuata barabara ya Samora bila kugeuka nyuma. Meneja huyo alitembea kwa dakika kadhaa. Aliipita Benki ya Nyumba na kuifikia barabara ya Samora. Hapo alisimama kungoja amri nyingine. Hakusikia. Akatulia kwa muda akiogopa kugeuka nyuma. Alipoona macho ya wapita njia yakianza kumtazama kwa maswali ndipo alipojitahidi kugeuka nyuma. Akajikuta akiwa peke yake. Hakujua Joram yuko wapi. Kwanza aliduwaa kwa muda. Kisha alirudiwa na fahamu, akainuka na kuondoka mbio kurudi ofisini. "Tumeibiwa," alimwambia mfanyakazi wa kwanza aliyekutana nae. Akaingia ofisini kwake na kuvuta king'ora cha ishara. Dakika chache baadaye polisi waliwasili na kuanza kuuliza maswali yao.
Wakati huo Joram alikwisha badili mavazi yake na kuvaa yale ya kizee pamoja na ndevu za bandia zilizojumuishwa na miwani kumfanya aonekane mtu mwingine kabisa. Kadhalika alikwisha badili teksi mbili ambazo zilimteremsha sehemu mbalimbali. Hii ya tatu alimwambia dereva, "Airport, tafadhali. Fanya mwendo wa kuruka."
Dereva hakumwangusha.
Wakati polisi walipoanza kuweka vizuizi vya njiani, yeye alikuwa akimaliza kumlipa bwana fedha nauli ya ndege.

SURA YA TANO*

JIJI la Nairobi lilimraki Joram Kiango na Nuru kwa hewa yake yenye ubaridi ambao ulikuwa kinyume kabisa cha joto waliloliacha Dar es Salaam. Waliuacha Uwanja wa Kimataifa wa Kenyatta kwa teksi ambayo iliwafikisha Hilton Hotel.
"Mr. and Mrs. Charles Moris," Joram alijitambulisha katika kitabu cha wageni.
Mhudumu wa mapokezi aliwatazama kwa muda akivutiwa na sura na maumbile yao. Kisha aliwapatia chumba kimoja Self-Contained, kama walivyotaka. Akawakabidhi kijana mmoja ambaye aliwaongoza hadi katika chumba chao ghorofa ya nane. Baada ya kuwafikisha aliwapa ratiba ya chakula, vinywaji na maelekezo mengine ambayo masikioni mwa wasikilizaji wake yalikuwa kama wimbo baada ya kuyasikia mara kwa mara. Walimkubalia yote na kumtupia maswali huku mara kwa mara wakimuonyesha meno kulijibu tabasamu lake ambalo halikuwa na mpaka. Kisha Joram alimfukuza kwa kumpa noti ya shilingi mia moja ambayo ilidakwa kwa heshima zote na kupotelea mfukoni.
"Wakati wowote, ukihitaji chochote usisite kuniita, mzee. Naitwa James," alieleza akitoka.
"Bila shaka, James".

Mara tu walipobaki peke yao, Nuru alimtupia Joram jicho lililojaa maswali. Alipoona Joram hatamki lolote aliamua kuzungumza. "Nadhani una mengi ya kunieleza Joram. Kila nilipojaribu kukuuliza kisa cha safari yetu tulipokuwa angani hukupenda kunijibu."
"Sidhani kama kweli. Ulikuwa hupendi kuzungumza mbele ya yule rubani."
"Kwa nini? Kwani kuna siri yoyote?"
"Bila shaka. Ulipokuwa uwanja wa ndege Dar es Salaam ulikuwa umejivika mavazi ya kizee tofauti na ulivyokuwa asubuhi. Ulipofika hapa jambo la kwanza ulilofanya ilikuwa kujibadili mavazi na kuwa kama ulivyo. Tulipofika hapa umelipa kwa fedha za kigeni bila shaka yoyote. Umezipata wapi? Na..."
 
SEHEMU YA 39 & 40


"Alaa! Hivi sijakwambia? Kati ya pesa nyingi tulizopata katika mfuko wa marehemu Chonde nyingi zilikuwa za kigeni," Joram alidakia. "Nadhani nilikuonyesha Nuru."
"Ulinionyesha. Na kwa nini umeamua kupanga kwa jina la bandia?" Nuru aliendelea kusaili. "Na hapo watakapoomba kuiona hati ya usafiri utawaonyesha nini?"
"Hilo lisikusumbue. Uongo sikuanza jana. Lakini sababu kubwa iliyonishawishi kuandika jina la bandia ni hofu ya kusumbuliwa na waandishi wa habari. Unawajua walivyo, Nuru. Mara nyingi hawana kitu cha kuandika. Hivyo, wanapopata kijambo watakikuza ili kijae ukurasa. Umaarufu wangu nchini Tanzania ni jambo ambalo waandishi wa Nairobi wanaweza kuliondolea uvivu kwa haki kabisa." Akasita na kucheka kidogo. Halafu akaendelea, "Hapana Nuru. "Tumekuja kustarehe. Tunahitaji kustarehe. Nairobi ni mwanzo tu wa starehe zetu. Toka hapa, tutakwenda zetu London, Paris, Hong Kong, New York na kokote ambako roho itatuita. Lazima tufurahi.Binadamu huishi mara moja tu. Hana budi kuitumia nafasi hiyo ili akifa awe amefaidi maisha."
Joram aliongea kwa sauti imara, ingawa Nuru alihisi na kuamini kuwa hakuwa mkweli. Hata hivyo, kwa kadri alivyomfahamu alihisi kuwa Joram alikuwa na jambo, jambo ambalo lilikuwa halijakamilika kichwani mwake na hakuona haja la kuliongelea. La sivyo, ingewezekanaje Joram ashambuliwe na mtu, Nuru amuokoe kwa kumwua mtu huyo, waache maiti chumbani na kukodi ndege hadi huku, wapange kwenda zao bila sababu yoyote maalumu? Hiyo si itakuwa hadithi? Bila shaka kuna jambo.
Nuru alilingoja jambo hilo kwa hamu. Baada ya kuwa na Joram kwa muda mrefu, baada ya kukinaishwa na starehe, na baada ya risasi aliyoifyatua kuondoa roho ya mtu, roho ya Nuru ilikuwa juujuu ikitegemea jambo, jambo jipya. Jambo ambalo litampa haki na wadhifa halisi wa kuwa na Joram Kiango kama alivyokuwa hayati Neema Idd. Alikuwa ameamua kuichukua nafasi ya Neema, katika mwili na akili ya Joram si kuichukua kwa kunywa pombe na kucheza muziki. Ni kuichukua kikazi. Na ni kazi hiyo ambayo aliisubiri kwa hamu.
Nuru alipomtazama tena Joram alimwona kazama katika mawazo mengi. Akamwacha na kuingia bafuni ambako alioga kwa utulivu. Alipotoka bafuni hakumuona Joram. Badala yake alipata kipande cha karatasi Joram akimtaka radhi kuwa amelazimika kwenda maktaba mara moja.
Upweke ulimfanya aamue kwenda chumba cha maongezi ambako alijipatia bia mbili huku akiitazama televisheni. Aliangalia vipindi kadhaa vya burudani na taarifa za habari. Hakukuwa na mapya zaidi ya yale ambayo yameondokea kuwa ya kawaida masikioni na machoni mwa binadamu. Macho yalipokinai televisheni, aligeukia chupa ambayo ilikuwa mbele yake.
Mara akatanabahi ameketi na mtu ambaye alikuwa akizungumza. "Nasema, samahani naweza kuketi nawe?"
"Bila samahani?"
Mtu huyo aliketi na kuanza kumwaga vinywaji na maongezi. Maongezi yake yaligeuka kumtaka Nuru. Alisema mengi, akidai kwa viapo kuwa hakupata kumuona msichana aliyeumbika kama Nuru, kwamba alikuwa tayari kufa ili ampate. Mara mikono yake ikakosa utii. Ikaanza kutambaa juu ya mapaja ya Nuru. Ni hilo lililomwondoa hapo na kumrudisha chumbani kwao.
***
Joram alikuwa hajarudi. Saa kadhaa tayari zilikuwa zimepita. Alipotahamaki, usiku ulikuwa umeingia. Alikula peke yake chumbani humo akiogopa kwenda chumba cha maakuli ambako kulikuwa na wanaume ambao hawakuzoea kukubali kuwa mwanamke angeweza kuwa pale peke yake. Uchovu ulimfanya ajilaze kitandani. Hakujua usingizi ulivyomchukua. Alipoamka alijikuta yuko mikononi mwa Joram.
"Samahani mpenzi," Joram alimnong’oneza.
Hakujishughulisha kumjibu kwa maneno. Badala yake alilijibu busu la Joram kwa vitendo. Kisha usingizi ulimchukua tena. Alipoamka aliupeleka mkono kumkumbatia Joram. Akajikuta akigusa godoro tupu. Joram hakuwa kitandani. Alipofumbua macho alimwona kainama mezani akisoma kwa makini. Akanyoosha mkono na kuichukua saa yake ndogo ya mkono kuitazama. Ilikuwa saa kumi na nusu za alfajiri. Hakuona sababu ya kumsumbua Joram. Akajifunika na kujaribu kulala. Usingizi haukuafikiana nae. Baada ya kuoga na kufungua kinywa asubuhi hiyo Joram alimwomba Nuru kuwa angerudi tena maktaba. "Leo nitamaliza shughuli zangu. Baada ya hapo tutakuwa pamoja katika kila la heri na shari," alimweleza. Kisha akampatia kitita cha noti akimwambia."Unajua tutakuwa na msafara mrefu? Nataka uende huko ukiwa katika hali halisi ya
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom