Simulizi ya Kijasusi: Tutarudi Na Roho Zetu?

SEHEMU YA 41 & 42

kuvutia kila macho ya mwanamume. Kwa hiyo, tafadhali leo pitapita madukani ununue kila vazi ambalo litakustahili. Usijali bei. Kumbuka pesa tunayo."
Nuru alizipokea na kumuuliza, "Na wewe huhitaji nguo mpya?"
"Nahitaji. Hata hivyo, sina haraka. Wanaume huwa hawatazamwitazamwi kama wanawake."
"Najua unahitaji muda wa kuwa peke yako," Nuru alimwambia. "Endelea baba, siwezi kukuzuia."
Mara tu Nuru alipoondokaJoram aliingia kazini. Alifungua begi lake na kutoa nyaraka za Chonde ambazo alitumia kila njia, kuzielewa. Akatoa kitabu ambacho alikipata kwa taabu sana kinachoeleza mbinu mbalimbali za kusoma maandishi ya mafumbo.
Akaketi na kuanza kutumia kitabu hicho kuyasoma tena maandishi ya Chonde. Haikuwa kazi ndogo. Ilihitaji muda mrefu na utulivu mkubwa. Alichofanikiwa ni kupata mwongozo ambao ulieleza namna ya kukifungua kile kisanduku. Akakifungua bila tabu yoyote.
Ndani mlikuwa na vijigololi kumi na viwili. Joram alikiinua kimoja na kukitazama kwa makini. Katikati ya kigololi aliona vidude vilivyokuwa vikichezacheza mfano wa saa za electronic. Alikitazama kigololi kwa makini akijaribu kutafuta umuhimu wake, hakuupata. Chini ya vigololi hivyo Joram alipata ramani ambayo alipoikunjua alikuta kuwa ni ya Jiji la Dar es Salaam. Ramani hiyo ilionyesha majengo maarufu kama Ikulu, vituo vya kijeshi, mabenki, na kadhalika. Vitu vyote hivyo vilikuwa vimewekewa namba za kirumi kuanzia moja na kuendelea. Namba ya jengo la benki kuu iliyoungua ilikuwa imewekewa alama ya x kwa wino mwekundu.
Mara baada ya kuona hayo Joram alipatwa na wasiwasi. Alihisi kuwa, kwa namna moja ama nyingine, Chonde alihusika na moto ulioteketeza Benki Kuu. Hofu yake kubwa ilikuwa zile hisia kuwa alama zilizofuata ambazo zilikuwa hazijawekwa x kwa wino mwekundu zilikuwa katika orodha zikisubiri, jambo ambalo lingeleta maafa na madhara makubwa kwa nchi na wananchi. Zaidi, ingekuwa ushindi mkubwa kwa maadui wa taifa. Hivyo, kwa mara nyingine, alifanya sherehe moyoni kushangilia kifo cha Chonde.
Kisha alifunga sanduku hilo kikamilifu na kuirudia meza ambayo aliinamia na kuanza kujifunza tena mbinu za kuyasoma maandishi hayo kwa makini zaidi.

Alikuwa hajatulia vizuri mlango ulipofunguka ghafla na Nuru kuingia huku macho yake yakiwa mekundu kwa mchanganyiko wa hasira na mshangao. Alisimama akitweta na kumtazama Joram kwa namna ya mtu ambaye hakujua la kusema.
"Usiniambie kuwa kuna mtu aliyekuvamia kwa nia ya kukunajisi mchana wote huu," Joram alimwambia kwa dhamira ya kumfariji.
"Acha mzaha Joram. Sikutegemea kama ungekuwa mtu wa kufanya kitendo kama kile."
Joram aliinua uso wake kumtazama.
"Kufanya nini?"
"Kuiba".
"Kuiba?"
Nuru akamkazia jicho la hasira. "Usijifanye hufahamu. Dunia nzima sasa inafahamu. Kwa kweli, sikutegemea kabisa. Imenishangaza kukuona katika televisheni ukitangazwa kama mtu hatari ambaye ameweza kuiba fedha za kigeni ambazo nchi yake inazitegemea kama dawa." Akasita akamtazama kwa chuki ambayo ilichanganyika na mshangao, "Kwanini ulifanya hivyo, Joram?"
***
"Bado siamini kama amefanya hivyo," mtu mmoja alikuwa akifoka pia, akiwa kaketi katika kundi la watu wenye hasira na mshangao kama yeye. Mabega yao yalikuwa yakimeremeta kwa nyota ambazo zilipamba magwanda yao kudhihirisha madaraka yao.
"Amefanya, lakini siamini kama Joram ni mtu wa kutenda kitendo cha aibu kama hiki. Jambo la kusikitisha zaidi ni jinsi habari hiii ilivyovuja kiasi cha kuyafikia masikio ya adui zetu. Leo nimesikia habari hizo na Afrika Kusini," Kombora aliendelea kulalamika.
"Ujerumani pia imetangaza afande," mtu mmoja aliongeza.
"BBC vilevile," mwingine aliongeza.
"Unaona, basi? Unaona habari mbaya zinavyosafiri upesiupesi? Pamoja na kwamba Joram ametuasi kimsimamo tulikuwa na haki ya kumsetiri kwasababu ya vitendo vyake vya nyuma. Sasa nadhani hatuna tunachoweza kufanya. Maji yamekwishakumwagika, hayazoleki. Lililopo ni kutafuta uwezekano wa kumpata na kurudisha pesa zote, hasa za kigeni."
"Hilo ndio tatizo mzee," msaidizi wake mmoja alijibu. "Taarifa za mwisho zinathibitisha kuwa hayupo kabisa hapa nchini. Kuna dalili kuwa ametorokea nchi jirani kwa ndege ya kukodi."
"Lazima, lazima apatikane," Kombora alisisitiza. "Pesa alizochukua ni nyingi sana na zinahitajika sana. Hana haki ya kuzifuja kwa starehe zake binafsi. Wasiliana na nchi jirani zote. Wasiliana na Interpol. Waarifu kuwa tunamhitaji Joram kwa hali na mali. Maadamu siri imekwishafichuka, hakuna haja ya siri tena."
 
SEHEMU YA 43 & 44


Baada ya majadiliano marefu jalada hilo lilifunikwa na kuletwa jingine ambalo lilikuwa “zito” Zaidi. Lilihusu mkasa au maafa yaliyotukia taifa pamoja na lile tishio la maisha na majumba muhimu. Walipima juhudi zao zote wakilinganisha habari mbalimbali. Haikuwepo dalili yoyote ya kujenga matumaini.
Kisha wakavirudia vifo vya watu wawili katika chumba kimoja cha hoteli hapa Jijini. Dalili zilionyesha kuwa marehemu walikuwa watu wasiofahamiana kabisa. Pekuapekua yao katika chumba hicho haikuwapatia kitu chochote zaidi ya mavazi ambayo yalionyesha kuwa yameshonwa nchi za nje. Nyaraka walizohitaji, ambazo zingeweza kuwasaidia, hawakuzipata. Ilielekea vifo hivi vingeingia katika yale majalada ambayo kesi zake hazikuwahi kutatuliwa. Hivyo, baada ya kuzitazama tena picha za marehemu wote, zilirudishwa katika majalada na kufungiwa.
Kikao kikaendelea.

*****

"Kwanini umefanya hivyo, Joram?" Nuru aliendelea kufoka.
Joram, ambaye alionekana kimawazo yuko maili kadha wa kadha nje ya chumba hicho, alimtazama Nuru kwa muda. Kisha ikawa kama amemkumbuka. Tabasamu dogo likamtoka, likifuatwa na sauti nzito, "Ilikuwa lazima nifanye vile, iko siku utaelewa Nuru."
"Nitaelewa!" Nuru alifoka, "Nitaelewa nini, mwanamume mwenye heshima zake na hadhi yake duniani anapothubutu kuingia benki na kuiba pesa ambazo nchi na watu wake wote wanazitegemea? Siwezi kuelewa kabisa, Joram. Ambacho naweza kuelewa ni wewe kuondoka sasa hivi na kwenda zako ofisi ya Ubalozi wetu ukaombe radhi na kurudisha kila senti. Tafadhali fanya hivyo, Joram."
Hilo lilisababisha kicheko kwa Joram. "Nina haki ya kula pesa za Tanzania kama wengi wao wanavyozila, Nuru. Huoni watu wenye mishahara ya shilingi elfu mbili wanavyojenga majumba ya mamilioni? Unadhani wanazipata wapi bila ya wizi? Tofauti yangu na wao ni kwamba mimi nimeiba kimachomacho, wao wanaiba kisirisiri. Mwizi ni mwizi tu." Akasita kidogo kabla ya kuendelea, "Acha tuzitumie Nuru. Acha tuzifaidi. Hii ni nafasi pekee katika maisha yetu ambayo hatujaisahau. Jisikie starehe..."
"Siamini kama maneno hayo yanatamkwa na Joram Kiango. Kwanini umebadilika kiasi hicho Joram?"
Kabla Nuru hajapata jibu mlango uligongwa na kufunguka taratibu. James aliingia. Uso wake ulionyesha kuwa alikuwa na habari ambayo si nzuri sana. Baada ya kubadilishana salamu za kawaida aliwataka radhi na kumchukua Joram chemba.
"Kaka, samahani. Unajua pamoja na kujiita kwako Charles Morris, ni watu wachache sana ambao waliamini? Sura yako si ngeni kabisa hapa Kenya. Umetokea mara nyingi katika magazeti na televishani. Wewe ni yule mpelelezi mashuhuri Joram Kiango. Sivyo, kaka?"
Joram alipochelewa kumjibu, James aliendelea, "Ziko habari mbaya zilizotokea katika vyombo vya habari. Inasemekana umetoroka kwenu ukiwa umechukua fedha nyingi za kigeni. Kwa jinsi ninavyokufahamu nashindwa kuamini kama ni kweli. Lakini hilo si muhimu sana kwa sasa. Nilichofuata ni kukufahamisha kwamba sasa hivi wapelelezi wa hoteli hii wamekaa kikao wakilijadili suala lako. Waweza kutiwa msukosuko mkubwa. Kwa hiyo, nakushauri utafute mbinu yoyote ambayo itakufanya uokoe maisha yako. Nina ndugu yangu anayeishi Nyeri. Anaweza kukuficha kwa muda."
Joram alicheka na kumshukuru James. "Usijali rafiki yangu. Nitajua la kufanya. Kwa sasa niache nijipumzishe kidogo na kufikiria la kufanya." Baada ya hayo aliutia mkono wake mfukoni na kuutoa ukiwa umeshikilia noti kumi za mia mia ambazo zilidakwa na James kabla hazijamfikia. "Kajipatie bia mbili," alimwambia akigeuka na kurudi chumbani.
"Unaona Joram? Twende zetu ofisi ya Ubalozi," Nuru alimdaka juujuu kwa maneno hayo.
"Kufanya nini?" Joram alizungumza kwa upole kama kawaida yake. "Tutakwenda zetu tunakotaka. Sasa hivi uwe binti mtulivu na ufanye kama nitakavyokuambia, tafadhali. Baada ya dakika chache tutakuwa zetu angani tukielekea katika mji mwingine wenye starehe kuliko huu."
"Haiwezekani, Joram. Lazima ukaombe radhi na kurudisha pesa za watu," Nuru aliendelea kukanusha.
"Alikuwa ameishi na Joram kwa muda mrefu. Lakini alikuwa hajapata kumuona Joram anavyokasirika. Leo hii aliziona hasira zake. Aliiona nuru kali na tena baridi, ikijitokeza katika sauti yake ndogo, nzito, aliposema taratibu, "Haya. Nenda zako ofisi za Ubalozi. Chukua na pesa zetu uwapelekee."

******
 
SEHEMU YA 45 & 46

Dakika mbili tatu baadae mzee mmoja wa kiume, mwenye mvi nyingi na ndevu za kutosha alionekana akitoka katika hoteli hiyo. Alikuwa kafatana na kijana wa kiume mwenye sura nzuri ambaye alikifunika kichwa chake kwa kofia pana na macho kwa miwani ya jua. Mikononi mwao walikuwa na mifuko yao. Wafanyakazi waliowatazama wakiondoka hawakuweza kukumbuka wageni hawa waliingia lini na iwapo walikuwa katika vyumba vipi. Waliwasindikiza kwa macho hadi walipotoka nje na kukodi teksi.
Kati ya wafanyakazi walioshuhudia wakiondoka ni James Kamau. Hata ndoto haikumjia kuwa alikuwa akiwatazama Joram Kiango na Nuru wakiondoka.

SURA YA SITA

SAA chache walikuwa angani tena, katika Ndege ya Shirika la Ndege la Uingereza, wakielekea London kupitia Cairo, Misri.
Sasa habari za "Wizi wa Joram" zikiwa zimetapakaa duniani kote, zikienezwa na kila chombo cha habari, haikuwa kazi ndogo kwao kuipata fursa hii ya kuiacha nchi ya Kenya. Polisi mitaani na katika vituo vyote vya usafiri walikuwa macho wakimtazama kila mtu ambaye alielekea kufanana na Joram. Passport na vitambulisho vyao vilitazamwa kwa makini zaidi, huku maswali mengi yakiulizwa. Hata hivyo, Joram na Nuru walifaulu kupenya vizingiti vyote huku wakicheka kimoyomoyo, kwani askari hao hawakuwatazama kabisa kwa jinsi walivyojibadili kimavazi na kitabia, kinyume kabisa cha matarajio ya askari.
Nuru aliuficha uzuri wake kwa kuiondoa ile hali ya uvulana aliotoka nayo hotelini na kujivika nywele zilionekana nusu zingemezwa na mvi. Mavazi yake pia yalikuwa yale ambayo vijana wasingependa kuyatupia macho zaidi ya mara mbili. Jambo ambalo lilifanya wawe sawa na huyu mzee mkongwe aliyekuwa akitembea kidhaifu, mfuko mgongoni na mkwaju mkononi. Hali zao pia zilikuwa za wakazi halisi wa Nairobi. Hati zao za halali pamoja na picha zao zilifichwa vilivyo katika mifuko ya siri iliyokuwemo katika mfuko waliorithi toka kwa hayati Chonde.
Ndani ya ndege Joram alitulia akinywa bia aliyoletewa kwa utulivu, huku mara chache akimtupia Nuru maongezi mafupi mafupi. Baada ya muda ambao haukuwa mrefu alipitiwa na usingizi. Aliamka ndege ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Cairo. Misukosuko ya abiria wanaoshuka na kuingia ilipopungua walizungumza na Nuru maongezi machache ambayo dhamira yake kubwa ilikuwa kuwafanya watazamike kama watu wa kawaida wasio na dosari yoyote machoni mwa wasafiri wengine.

Safari ilipoanza tena Joram alikiweka kiti chake katika hali ya kulala akimwacha Nuru akipekua kitabu chake kutafuta alipokuwa ameishia. Ikiwa safari ndefu, ya kuvuka bahari kubwa kama hii ya Atlantic, Joram alikusudia kutumia vyema kufidia usingizi ambao hakuupata kiukamilifu alipokuwa Nairobi. Na ndivyo ilivyomtukia. Hakupata nafasi ya kuyafumbua macho yake kuyatazama maji mengi yaliyotapakaa kote. Alipoamshwa na Nuru na kutazama dirishani, alishangaa kuona wakizunguka juu ya Jiji la London wakisubiri kutua.
"Imekuwa safari fupi kuliko nilivyotegemea," alisema.
"Hata! Ilikuwa safari ndefu sana kama ilivyo," lilikuwa jibu la Nuru.
Taratibu, ndege ikashuka na kutua bila msukosuko wowote katika uwanja mashuhuri wa Heathrow. Pilikapilika za abiria kuchukua mizigo na kutaka kutoka mapema zikaanza. Joram na Nuru, wakiwa miongoni mwa abiria walioshuka mwisho, walichukua mizigo yao na kupita katika ofisi za forodha na abiria wengine waliokuwa wakisubiri usafiri.
Dereva mmoja, msichana, wa shirika la usafiri la Avis and Hertz, aliwafuata na kuwashawishi kuingia katika gari lake. Akawapeleka mjini katika Hoteli maarufu duniani ya Wilson Place ambapo walijipatia chumba maridadi. Mapokezi yakiwa ya kistaarabu, huduma za kistaarabu, na wahudumu waliosomea ustaarabu, yote yaliwafanya waone kama wako nyumbani badala ya ugenini, jambo ambalo liliwafanya wasijali chochote juu ya malipo makubwa yanayodaiwa na hoteli hiyo.
Kuna mzungu mmoja, mshairi, au mpenzi tu wa taifa lake ambaye aliwahi kusema: "When a man is tired of London, he is tired of life for there is all that life can afford," kwamba binaadamu anayekinaishwa na Jiji la London basi amekinaishwa na maisha kwa ujumla kwani London inacho kila kitu ambacho maisha ya binaadamu yanahitaji. Joram na Nuru wasingemwona mtu huyo kuwa mwongo sana. Pamoja na kwamba wote hawakuwa wageni sana wa jiji hili, macho yao yaliendelea kuvutwa na vitu mbalimbali siku yao ya pili walipoamua kuzunguka jijini.Walikodi gari lililowatembeza kila mahali kufuata matakwa yao. Kwanza, walipenda kuona mto ule maarufu unaougawa mji wa London, Thames. Waliyatazama maji yake yanayopita kwa utulivu pamoja na madaraja yake murua. Kisha walizunguka katika miji ya Kingstone, Bromley, Croyon na kwingineko, wakiona mambo tofautitofauti katika mitaa mashuhuri kama Oxford, Kingsway, Dean na Sheftebury. Usiku ulipoingia walikwenda katika jumba la Her Majesty kutazama michezo ya kuigiza.
 
SEHEMU YA 47




"Kesho tutakwenda kutembea Epping Forest," Joram alimnong'oneza Nuru walipokuwa wakirudi hotelini kwao.
"Ningependa kuingia Richmond Park," Nuru alimjibu.
"Nilipokuja kozi hapa miaka minne iliyopita nilidhamiria kuingia lakini sijui ilikuwaje nikashindwa, safari hii nisingependa kushindwa tena."
"Huwezi kushindwa. Tuna muda na pesa. Tutafanya kila kitu ambacho roho itatutuma kufanya. Nafasi kama hii hutokea mara chache sana katika miaka ya maisha yote ya binaadamu."
Chumbani kwao walivua uzee na kuurudia ujana wao. Wakatazamana na kucheka kidogo. Kisha walikumbatiana na kuongozana kitandani. Muda mfupi baadaye Nuru alikuwa akikoroma taratibu, huku Joram akinyata kukiacha kitanda. Aliiendea mizigo yao na kuikagua kwa makini. Kila kitu kilikuwemo kama kilivyokuwa kimehifadhiwa. Akatoa kile kisanduku chenye vigololi na kuvitazama kwa makini. Kisha alivirudisha na kuchukua vitabu vyake ambavyo alikuwa akivisoma au kufanya majaribio ya maandishi na mahesabu kwa umakini na utulivu. Mara kwa mara alichana karatasi hii na kujaribu ile, mara akiacha kuandika na kuanza kusoma kwa umakini, kisha akianza tena kuandika.
"Siwezi kukusaidia mpenzi?"
Sauti ilimzindua Joram kutoka katika lindi hilo la shughuli iliyokuwa mbele yake. Aligeuka na kumtazama Nuru ambaye alitulia nyuma yake, uchi kama alivyozaliwa, macho yake yakitazama mahesabu katika karatasi za Joram."Samahani kwa kukuvuruga. Nimekuwa nyuma yako kwa zaidi ya saa nzima sasa. Nadhani hata hujui kuwa kumepambazuka."
Ndipo Joram alipotupa macho nje. Hakuamini. Nuru ya jua lililochomoza kitambo ilikuwa ikipenya dirishani kwa uangalifu. "Samahani Nuru. Usingizi ulinipaa ndipo nikaja mezani kupoteza muda," alisema akianza kufunika karatasi zake.
"Kupoteza muda?" Nuru alimwuliza. "Nimekutazama kwa muda mrefu sana. Hata kuna nyakati ambazo ulikuwa ukisema peke yako. Najua una jambo ambalo linakusumbua, jambo ambalo umeamua kuliweka siri rohoni mwako. Hutaki kunishirikisha. Huniamini hata kidogo! Sijui nifanye nini ili uniamini Joram!"
"Ndiyo. Afanye nini ili amwamini?" Joram alijiuliza. Msichana huyo ambaye ameacha kila kitu hata kazi na nchi yake ili awe pamoja naye! Msichana ambaye kuwa nae kumemsaidia sana katika kujifariji na msiba wa Neema na aibu aliyoipata kwa kushindwa kumuua Proper! Msichana ambaye majuzi tu aliyaokoa maisha yake kwa kumwua mtu ambaye angemwangamiza bila huruma! Zaidi ni msichana mzuri wa sura na tabia, msichana ambaye ni ndoto ya kila mwanaume!
“Sikia Joram, huwezi kukadiria kiasi gani nakuamini na kukutegemea. Sifai kuambiwa lolote. Kwako mimi ni mwanamke tu ninayefaa kwa mapenzi ya kimwili. Siwezi kuwa Neema ambaye alikuwa mwenzi wako kikazi ambaye kimwili hukuwahi kumgusa.”
“Sivyo Nuru.”
“Wala sifahi lolote hata kukusaidia katika hesabu za fizikia unazopiga au kusoma maandishi hayo na kuyalinganisha na hayo ya kijasusi kama unavyofanya. Sifai hata kwenda maktaba kukusaidia kupekua walao kitabu unachokihitaji.”
“Nuru!” Joram alifoka kwa sauti ambayo masikioni mwa mtu asiyemfahamu ingekuwa ya kawaida tu. “Nilidhani wewe ni mtu pekee unayeweza kunielewa. Nilidhani unaifahamu tabia na msimamo wangu. Sina tabia ya kuyachukua matatizo yangu na kuyabwaga mikononi mwa binadamu mwingine. Sijazowea kuchukua fumbo ambalo limenishinda kufumbua na kumwomba mtu mwingine anisaidie. Wala tabia hiyo siwezi kuianza leo. Hivyo, ninapokuambia sina la kukuambia maana yake sina la kukuambia. Nadhani umenielewa.”
"Nadhani nimekuelewa. Hata zile pesa ulizozipokonya City Drive, ambazo tunachezea sasa naamini ni fumbo jingine ambalo hukupenda kulifumbua. Sivyo mpenzi?"
Joram akatabasam, "Yaelekea mimi na wewe tutakuwa na safari ndefu kimaisha."
Wakashikana mikono na kurudi kitandani.

*******
Baada ya kuzitawala na kuzinyonya sana nchi zetu nyingi za Kiafrika, na baada ya 'kutoa' uhuru shingo upande, Uingereza iliendelea kujifanya baba na mama wa makoloni yake ya awali. Falsafa hii ndiyo chanzo cha vijimsaada kadha wa kadha. Eti pia Uingereza ndiyo mtaalamu wa habari zinazohusu nchi zilizokuwa chini ya himaya yake. Na habari ambazo hupata nafasi katika vyombo vya habari mara nyingi huwa ni zile ambazo si nzuri sana kwa masikio ya wasikilizaji, yaani habari za aibu, kushindwa, rushwa udikteta, uzembe na kadhalika. Uteuzi huu wa habari hizo mbovu na
 
SEHEMU YA 48

kuacha zile njema ni ushahidi mwingine ambao huonyesha kuwa Uingereza ingependa kuendelea kuitawala Afrika hadi siku ya mwisho ya dunia.
Habari za wizi wa fedha za kigeni katika Tanzania zilikuwa tamu mno katika magazeti, redio na televisheni zote za Uingereza. Zilipambwa kwa wino na rangi mbalimbali na uongo ainaaina hata zikawa kubwa kuliko zilivyostahili kuwa. Hiyo ilitokana hasa na mwizi wa pesa hizo alivyokuwa mtu maarufu duniani. "Ndivyo walivyo waafrika..." liliandika gazeti moja."Kati yao hakuna mwaminifu..." Gazeti jingine lilipendekeza kuwa Tanzania isipate msaada wowote wa kimataifa bila ya pesa hizo kurudishwa. "Tunaamini kilichofanyika ni njama tu baina ya Joram na viongozi wa serikali yake," Televishen moja ilitangaza.
Habari hizo zilianza kuwa za kawaida machoni na masikioni mwa Joram na Nuru. Hawakuzijali wala kuzishughulikia. Hata hivyo, kuna gazeti hili ambalo liliwashtua zaidi. Mwandishi wake alikuwa amesafiri hadi Dar es Salaam ambako alifanya utafiti wake binafsi, akihonga hapa na kuiba habari pale hata akawa ameunganisha taarifa ambayo ilidai kuwa Joram alikuwa ametorokea Nairobi kwa ndege ya kukodi. Mwandishi huyo alisafiri hadi Nairobi ambako utafiti wake ulimfikisha katika chumba alichokuwa Joram na Nuru kwa majina bandia. "Kwa kila hali sasa hivi Joram yuko London," lilieleza gazeti hilo. "Dunia haiwezi kupumbazwa na hila zake za kujibadili sura na umbile. Kwa hali ilivyo, atakuwa akiishi katika hoteli kubwa kwa jina la bandia.”
"Imekuwa tabia ya kawaida," gazeti hilo liliendelea kueleza. "Kila wanapofanya madhambi yao huko kwao hukimbilia huku. London imejaa watu weusi ambao wanaishi wanavyotaka baada ya kufanya maovu - au mema ambayo yalionekana maovu - huko makwao. Wako wachoyo, wahujumu, wazembe, wanafiki na kadhalika. Wengi wameziacha nchi zao zikiwa masikini zaidi huku roho za watu zikiteketea katika vita na mauaji yasiyo na mwisho. Uingereza tunawakaribisha na kuishi nao kama binadamu wenzetu. Miongoni mwa watu hawa sasa yumo Joram Kiango, mtu aliyejifanya na akaaminika kuwa ana roho ya kipekee yenye upendo na ushujaa kama ngao kwa jamii yake. Kumbe alikuwa fisi katika ngozi ya kondoo. Huyu, Uingereza haiwezi kumstahamili. Lazima apatikane, ahukumiwe na kupokonywa kila senti aliyobaki nayo.”
Nuru alimaliza kuisoma habari hii huku akitetemeka kidogo. Lakini ilimshangaza alipoinua uso na kukutana na ule wa Joram ambao ulikuwa ukichekelea. Hilo lilimshangaza. Akiwa mtu ambaye ameishi na Joram kwa kipindi cha kutosha, alikuwa na hakika kuwa amemfahamu Joram vya kutosha. Asingelaghaika kama watu wengine kung'amua wakati gani anacheka kwa hasira na wakati upi anajifanya kuchukia hali amefurahi. Tabasamu hili, ambalo lilikuwa likiendelea kuchanua katika uso wa Joram, halikuwa tabasamu batili, bali tabasamu halisi, tabasamu ambalo huutembelea uso huu kwa nadra sana. Hivyo, ilimshangaza sana Nuru. Alimtegemea Joram kujisingizia kucheka huku rohoni akibabaika na kukata tamaa. Si kushangilia kama aliyepata tuzo au ushindi mkubwa baada ya shindano gumu.
"Sijakuelewa Joram, sidhani kama hii ni habari njema," alimwambia.
"Wala sidhani kama una haki ya kutegemea habari njema tangu ulipokubali kuandamana na mwizi mkubwa kama huyu," Joram alimjibu taratibu. Alipoona uso wa Nuru bado una maswali na dalili za kutoridhika, aliongeza, "Kinachonichekesha ni huyu Mwingereza anavyojifanya ana uchungu na nchi yetu kuliko sisi wenyewe. Utafiti aliofanya hautokani na moyo wake wa kuwajibika bali ni nguvu alizonazo kiuchumi, uwezo ambao ameuiba toka katika makoloni miaka nenda rudi." Alikohoa kidogo kabla ya kuongeza, “Hawawezi kunitisha kabisa. Nitaishi hapa nikistarehe katika jiji hili kubwa ambalo linapendeza kwa madini yaliyoibwa toka makwetu, yaliyochimbwa kwa jasho la babu zetu. Nitaondoka hapa tu tutakapokuwa tayari kuondoka. Sivyo, dada Nuru?"
"Nilichosema ni jinsi unavyoifurahia habari hii badala ya kuionea aibu. Sikutegemea. Au nakosea. Pengine hili ni fumbo jingine?"
Joram hakumjibu.
***
Jioni hiyo maisha yaliendelea kama kawaida. Joram alijipitisha hapa na pale akifanya hili na lile. Sasa ilikuwa dhahiri kwa Nuru kuwa alikuwa katika shughuli kubwa na ngumu kinyume cha
 
SEHEMU YA 49

alivyoiruhusu sura na sauti yake kuonyesha. Nuru hakujisumbua kumuuliza lolote akichelea kupoteza muda wake kwani ingekuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa ukimtegemea kucheza rumba. Hata hivyo, Nuru alipopata wasaa alimkabili Joram na kumwambia taratibu,"Unadhani mwandishi yule anatania anaposema watafanya juu chini kututafuta? Huoni kama tunaweza kupatikana? Hila hizi za kujibadili si zimekuwa teknolojia ya kawaida siku hizi? Sidhani kama zinaweza kutusaidia."
"Najua, mpenzi. Ninachojivunia ni wingi wa watu na ukubwa wa jiji hili. Itachukua muda hadi wafike hapa na kutukamata. Wakati huo hatutakuwa hapa tena, bali tutakuwa angani tukimalizia kuitembelea nchi ya mwisho ya dunia. Usijali Nuru. Starehe bila hofu yoyote..."
Joram hakuumalizia usemi wake kabla ya kuusikia mlango ukigongwa. Wakatazamana huku wakisikiliza. Mlango uligongwa tena kwa nguvu kuliko mwanzo. Joram hakuwa mgeni na ugongaji wa polisi. Kwa mara ya kwanza akajikuta kuwa alikuwa amekosea sana kuwadharau polisi wa Uingereza kiasi hicho. Akamtupia Nuru jicho ambalo lilibeba ujumbe ambao masikioni mwa Nuru ulieleza waziwazi "Cheza nao." Papo hapo akatoka na kuingia bafuni huku akiufunga mlango nyuma yake.
Mlango ulipogongwa tena Nuru aliinuka na kuufungua. Kama alivyotegemea mlango ulipofunguka aliingia askari mmoja mwenye cheo cha Sajenti akifuatana na mmoja kati ya maofisa wa hoteli hiyo.
"Samahani sana dada," afisa huyo alieleza. "Tumelazimika kukusumbua kidogo. Nadhani utatuwia radhi. Huyu hapa ni Sajini Brown kutoka Scotland Yard, yuko katika ziara ya kuwatembelea wageni wote wa hoteli hii ili kutazama hati zao za usafiri na maswali madogo madogo ambayo nadhani utamjibu. Ni mzunguko wa kawaida tu kwa ajili ya tukio dogo ambalo wangependa kulikamilisha ili wasirudi tena katika hoteli hii."
"Bila samahani,"Nuru alijibu akimgeukia polisi huyo ambaye alikuwa akitoa kitambulisho chake.
"Kwa kawaida hapa kwetu hatusumbui wageni," askari huyo alieleza. Tunatimiza ombi la INTERPOL tu," alisita akimtazama Nuru kwa makini zaidi. Sijui dada unaitwa nani?"
"Mrs Prosy Godwin".
"Kutoka?"
"Naijeria".
"Yuko wapi bwana Godwin?"
"Ametoka, nadhani atarudi baada ya dakika chache."
"Naweza kuona hati zenu za usafiri pamoja na nyaraka nyingine kama zipo?"
"Bila shaka," Nuru alimjibu akiendea mfuko ambao aliufungua na kutoa hati. Akazikabidhi kwa askari huyo ambaye alianza kuzipekuapekua.
Dakika hiyohiyo mlango wa bafu ulifunguka. Askari alipogeuka kutazama alikutana na pigo ambalo lilitua katika shingo yake kikamilifu. Pigo lililokusudiwa kummaliza, lakini halikutimiza wajibu. Lilimfanya apepesuke na kuegemea ukuta. Mkono wake ukapaa kukinga pigo la pili huku mkono wake wa pili ukisafiri kuitafuta bastola. Joram hakuruhusu mkono huo utoke na bastola. Aliachia judo ambayo ilitua ubavuni mwa askari huyo na kumlegeza. Pigo lililofuata lilimlazimisha kuanguka sakafuni. Baada ya kazi hiyo ndipo Joram alipomgeukia afisa wa hoteli ambaye alikuwa kaduwaa, mdomo wazi, kama asiyeamini macho yake.
"Mwinue ndugu yako na umpeleke bafuni," Joram alimwamuru.
"Vipi bwana Godwin? Nadhani hukumwelewa huyu bwana. Alikuwa hana nia mbaya zaidi ya... ya..."
Joram hakuwa na muda wa kuchezea. Alijua afisa huyu alihitaji nini kumtoa mshangao. Pigo moja tu, ambalo halikutegemewa lilimfanya afisa huyo aanguke chini kama gunia. Hima, Joram alianza kuwavutia bafuni mmoja baada ya mwingine. Kisha aliufunga mlango wa bafu kwa funguo na kumfuata Nuru ambaye pia alikuwa ameshangaa.
"Kwa nini umefanya hivyo Joram? Haikuwepo kabisa haja ya kuwashambulia. Askari huyo asingegundua lolote. Sasa watajua kuwa uko hapa na wataanza kututafuta kwa udi na uvumba."
Si kitu. Kwa nini tujikombekombe kwao? London si mji mzuri pekee yake katika dunia hii. Bado tuna haja ya kuiona miji mingine."
***
"…Ni mtu wa hatari duniani. Ameidhihirishia dunia kuwa hana tofauti na yule mwuaji mwingine anayetafutwa duniani kote, Carlos. Sasa kinachotakiwa kufanyika si kumtafuta yeye bali roho yake. Vinginevyo, dunia itakuwa imestarehe ikisubiri kuimarika kwa kiumbe mwingine wa hatari zaidi ya faru mwenye wazimu.”
Hayo yalikuwa mapendekezo ya mwisho katika gazeti lile lililohisi kuwepo kwa Joram Jijini London, na hatimaye kuandika juu ya tukio la kutisha lililowapata askari wa Scotland Yard na Afisa wa hoteli. Watu hao ambao walifunguliwa kutoka katika bafu saa kadha wa kadha baada ya Joram kuondoka zake, walieleza jinsi walivyowakabili watu ambao mtu yeyote asingefahamu kuwa wangeweza kuwa Joram Kiango na Nuru. Askari huyo alieleza hayo akiwa katika chumba cha X-ray, kuangalia uwezekano wa kuungika kwa mbavu zake tatu zilizovunjwa na Joram.
Baada ya kuongea nao kwa marefu na mapana ndipo waandishi wa gazeti hilo wakatoa habari hizo zikiwa zimepambwa kwa picha nyingi za kuchora, picha ambazo ziliwachora Joram na Nuru katika sura na mavazi tofauti; wakijaribu kuonyesha jinsi gani wanavyoweza kujibadili. Chini ya michoro hiyo kulikuwa na maelezo yaliyoandikwa kwa herufi nzito yakisema; "Unashauriwa kujihadhari nao. Ukimwona ua kwanza, uliza maswali baadaye."

ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 50

ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA

Baada ya kuongea nao kwa marefu na mapana ndipo waandishi wa gazeti hilo wakatoa habari hizo zikiwa zimepambwa kwa picha nyingi za kuchora, picha ambazo ziliwachora Joram na Nuru katika sura na mavazi tofauti; wakijaribu kuonyesha jinsi gani wanavyoweza kujibadili. Chini ya michoro hiyo kulikuwa na maelezo yaliyoandikwa kwa herufi nzito yakisema; "Unashauriwa kujihadhari nao. Ukimwona ua kwanza, uliza maswali baadaye."

SASA ENDELEA

Gazeti hilo lilisomwa kote duniani. Maelezo yake yalidakwa na TV na redio zote duniani. Watu wengi, ambao walimchukia Joram walizidi kushangilia, hali wale waliompenda walizidi kushangaa.
"Sijui amepatwa na nini mtoto huyu,"Inspekta Kombora alifoka huku akilitupa gazeti hilo mezani. "Yuko London na anafanya anavyojua. Anazidi kulipaka matope jina lake ambalo tayari amelichafua.”
Ilikuwa dhahiri kwa yeyote amtazamaye Kombora machoni kwamba alikuwa hajapata usingizi wa kutosha kwa muda mrefu. Mambo mengi yalimkabili kichwani kiasi cha kumpokonya hata hamu ya kula. Angewezaje kustarehe wakati siku zilikuwa zikisogea huku halijapatikana lolote la haja katika kukomesha tishio kutoka nchi adui ambalo lilitaka serikali iache msimamo wa kimapinduzi, la sivyo ajali zingeendelea kutokea. Tanzania kuacha kuzisaidia nchi zinazopigania haki na uhuru wake ilikuwa ndoto ya kupendeza. Kamwe isingetokea. Lakini kuendelea kusaidia nchi hizo huku ukisubiri maafa ya hatari sana, kwa nchi yake na rafiki zako hali huna uwezo wa kufanya lolote ilikuwa ndoto ya kusikitisha sana, ndoto ambayo ingeweza kutokea.
Walikuwa wamefanya yote ambayo wangeweza kufanya katika juhudi za kuhakikisha usalama. Yote; mema kwa maovu. Magereza ya Keko na Ukonga yalikuwa yamejaa wageni wengi ambao ama waliingia nchini kinyume cha utaratibu, au hati zao zilitia mashaka. Wote hawa walihojiwa kwa maneno na vitendo. Waliokuwa watakatifu waliachiwa, wenye madhambi ya magendo na uzururaji wakifunguliwa mashitaka. Ni mtu mmoja tu ambaye alielekea kuwa na mengi au machache ambayo yangehusiana na usalama wa nchi.
Huyu alikamatwa katika hoteli ya New Africa baada ya kulala hapo kwa siku moja. Wapelelezi walimshuku baada ya kumsikia akiulizauliza maswali juu ya watu walikufa katika hoteli hiyo; ni wa aina gani na walikufa vipi. Alipokamatwa na kutakiwa kutoa vitambulisho, hati zake zilionyesha kuwa ni mwanachama wa ANC ambaye ametoroka kutoka Namibia. CID waliwasiliana na ofisi hizo. Jina la Kweza halikuwemo katika orodha ya wanachama wa ANC. Ndipo lilipofunguliwa bomba la maswali dhidi yake. Na ni hapo ilipodhihirika kuwa hakuwa mtu wa kawaida jinsi alivyoweza kuyajibu maswali yote kwa ukamilifu kama ambaye alijiandaa kuyajibu.
Begi lake ambalo lilikaguliwa harakaharaka bila ya kuonekana chochote, lilipekuliwa tena. Baada ya jitihada kubwa iligundulika mifuko ya siri ambayo ilificha silaha, vyombo vya mawasiliano na vitu mbalimbali vya kijasusi. Alipoulizwa alikovipata alikanusha kuwa havifahamu, wala hakupata kuviona vitu hivyo. Ni majibu hayo ambayo yalimuudhi Kombora hata akaamua apelekwe katika chumba cha mateso ili, kama hasemi, autapike ukweli. Taarifa zilizomjibu Ispekta Kombora zilisema kuwa alikuwa hajasema lolote.
Ndipo alipolitupa gazeti alilokuwa akisoma habari za Joram, na kumtoa akilini kwa muda. Akaondoka na kuingia katika lifti ambayo ilimteremsha chini ya ardhi kiliko chumba cha mateso. Kombora hufika katika chumba hiki kwa nadra sana. Harufu ya mchanganyiko wa damu, kinyesi, jasho na machozi ni jambo moja ambalo humfanya aape kuwa asingerudi tena kila anapofika humu. Jambo jingine ni sura za watesaji. Sura hizi humtisha zaidi ya mateso yenyewe, zikimfanya aamini kuwa watu hao kama kweli wana roho, basi wana roho za chuma. Nayo macho ya wanaoteswa si jambo ambalo macho ya mtu mstaarabu yatapendezwa kuangalia.
Leo hii alimkuta Kweza, au kilichosalia katika umbo la aliyekuwa Kweza; akiwa amelala sakafuni, sura yake ikiwa haitambuliki kwa kuvimba na kuchubuka. Vidole vyake vyote tayari vilikuwa vimevunjika, jicho moja limetumbuka na meno manne yamepotea. Watesaji walikuwa wamemwinamia wakimdunga sindano ambayo ilikuwa na waya, iliyotokea katika soketi ya umeme.
"Mwachieni kidogo," Kombora aliamuru akikiendea kiti na kuketi. "Mleteni hapa."
 
SEHEMU YA 52
wali ojua kilichotokea. Polisi waliikuta ndege hiyo ikiwa imesimama kando ya nyumba, marubani wakiwa usingizini kwa kunusa dawa fulani bila kutaraji. Watu walioshuhudia tukio hilo, wakiwa hawajui kinachotokea, walidai kuwa waliwaona "vijana wazuri" msichana na mvulana wakishuka kutoka ndege hiyo na mizigo yao na kuingia katika jumba la jirani ambamo hawakuonekana wakitoka tena.
Harakati na machachari yao katika miji mbalimbali ziliondokea kuwa habari ambazo ziliwavutia sana waandishi wa habari. Mara kwa mara televisheni, redio na magazeti zilitoa habari zinazowahusu; Leo kaonekana hapa; hapa kafanya hivi; pale alifanya vile, na kadhalika.
Habari hizo zilipambwa kwa picha zao zinazovutia, kurudiwarudiwa kwa historia ya maisha ya Joram kiango pamoja na kutiwa chumvi nyingi ili kugusa masikio ya watu wote na kumsisimua kila mmoja. Hivyo, jina lilipanuka na athari kuneemeka. Ilikuwa kama dunia imesita kushughulikia masuala yaliyo muhimu na kuandamana na Joram katika ziara yake hii ndefu, jambo ambalo lilimfanya kila mpelelezi kuwa na hamu kubwa ya kubahatika kumtia mikononi Joram ili amfikishe kunakohusika.



Jambo ambalo lilimshangaza Neema katika mkasa huo mzima ni jinsi ambavyo alielekea kufurahishwa na jinsi habari hizo za aibu juu yake zilivyopata nafasi kubwa katika vyombo vya habari. Iliendelea kumfurahisha Joram badala ya kumchukiza. Nuru ambaye alimfahamu Joram asivyopenda sifa alijikuta akijawa na msgangao kwa mabadiliko hayo ya Joram.

Hata hivyo mshangao wake ulianza kupungua pale Joram alipoanza au alipolazimika kumshirikisha katika baadhi ya mambo aliyokuwa akiyafanya. Jambo la kwanza lilikuwa mazoezi ya viungo. walifanya kila starehe, lakini baada ya starehe, wakiwa chumbani kwao, walifanya mazoezi makali ya viungo. Mazoezi ambayo awali yalimtoa Nuru jasho, machozi na damu. Lakini baada ya muda machozi na damu vilikoma na jasho kupungua. Akawa hodari, akiwa bega kwa bega na Joram katika kila jambo. Zoezi la pili lilikuwa la matumizi ya silaha mbalimbali ambazo Joram alikuwa akizinunua kwa siri sana.

Alimwelekeza Nuru namna ya kuzificha mwilini, namna ya kuzitumia na kumfundisha jinsi ya kulenga shabaha kwa ukamilifu. Nuru alikuwa mwepesi wa kuelimika.

Hayo yaliufanya moyo wa Nuru uwe na tumaini kubwa. Sasa aliamini kuwa Joram alikuwa na jambo fulani zito la muhimu ambalo alikuwa akishughulikia. Pengine katika safari hiZo za mji hadi mji alikuwa akimhitaji mtu kwa madhambi fulani. Mtu gani huyo? Na ni madhambi gani aliyoyafanya?

Maswali ambayo yaliimarika hasa kutokana na simu nyingi ambazo Joram alikuwa akipiga kwa rafiki zake sehemu mbalimbali ulimwenguni, ambazo mara kwa mara zilikuwa katika mafumbo ya aina aina. Japo alimsikiliza kwa makini Nuru hakuambua chochote cha haja, zaidi ya kuishia kuhisi tu. Wakati wote huo Joram hakukoma kujifungia.

Halafu ikaja jioni ya leo, ambapo Joram alionekana mtulivu kuliko ilivyokuwa siku zote. Sigara ziliteketea mdomoni mwake moja baada ya nyingine, macho yake yakimtazama Nuru ambaye alikuwa ameketi juu ya meza ya kuvalia akishughulikia nywele zake. Joram alimtazama kwa makini kwa dakika kadhaa, kisha alimsogelea na kumshika bega.

"Nilichoshika hapa ni kipande murua cha kazi ya sanaa ambayo ni mfano halisi wa kazi ya Muumba. Nadhani hana budi kujivunia mafanikio yake", alisema akitabasamu.

Nuru aliinua uso kumtazama.

"Kwa bahati mbaya kazi hii ya sanaa iki katika hatari ya kuharibika endapo itandelea kuandamana na binadamu wenye akili mbaya kama Joram Kiango".

Hilo lilimfanya Nuru atabasamu. Alijua Joram anaelekea wapi. Siku hizi mbili alikuwa akimchunguza kwa makini na kuona mabadiliko katika fikira zake. Alikuwa akiona na kushuhudia kutoweka kwa ile starehe ya kujisingizia katika nafsi ya Joram na badala yake starehe kamili kuchukua nafasi yake. Mfano wa mtu ambaye yuko katika jahazi hafifu katikati ya bahari iliyochafuka anapobahatika kufika pwani salama. Hivyo alijua kuwa Joram ana neno. Akamhimiza kulisema kwa kumwambia, "Unachotaka kufanya Joram ni kunitisha... Lazima uelewe kuwa sitishiki ng'oo. Tumekuwa nawe katika heri na shari. Tutakuwa pamoja jehanamu na peponi. Usijisumbue kuniambia lolote lenye dhamira ya kututenga".
 
SEHEMU YA 53

Joram akacheka. "Una akili nyepesi sana Nuru", akamwambia. "Nilichokuwa nikielekea kukuomba ni kukushauri urudi nyumbani, uniachie kazi iliyoko mbele yangu. Ni kazi chafu, ya hatari, yenye nuksi, ambayo sidhani kama itanifanya nirudi nyumbani na roho yangu".

"Nimekwisha sema usijisumbue kunitenga. Nina hamu na kazi nzito, chafu yenye damu. Sijasahaun nilivyoshirikishwa kuwaangamiza wakuu wa nchi wasio na hatia. Nahitaji kujitakasa. Ni damu pekee itakayonitakasa. damu ya adui wa Afrika.

Joram aliduwaa huku akimtazama msichana huyo. Hakuwa na shaka kuwa msichana huyo ni shujaa. Lakini hakujua kuwa ni shujaa kiasi hicho. Ndiyo, alimtegemea sana katika msafara wake. Lakini hakukusudia kumwingiza katika mkasa ambao ilikuwa dhahiri kuwa pamoja na ugumu wa maandalizi yake ya muda mrefu hadi sasa matekeo yake yalikuwa gizani. Yeye alikuwa tayari kwenda, tayari kufanya kazi inayompeleka; uwezekano wa kurudi haukumsumbua. Kufa kusingemtisha sana mradi atakuwa ameifanya kazi yake. Kifo chake ni jambo moja, kusababisha kifo cha mtoto wa watu, mzuri kama Nuru, ni jambo jingine.

"Sikia Nuru. Labda huelewi... Nakusudia kwenda toka hapa sio nchi ya kawaida. Ni nchi ambayo kuna watu wenye kiu kubwa ya damu ya mtu mweusi na njaa kubwa ya roho zetu. Na ninahitaji kujipeleka moja kwa moja mikononi mwao. Kwa ufupi nategemea kwenda Afrika Kusini...".

"Tutakwenda pamoja".

...Na ninachokwenda kufanya ni hujuma. Wakinigundua watanitafuna mbichi".

"Watatutafuna pamoja".

Joram akaduwaa. "Labda nikufunulie kila kitu kilivyo Nuru", Joram akamwambia. ""Nisubiri", alisema akiliendea begi lake lililokuwa limefurika kwa vitabu aina aina pamoja na encyclopedia ambazo Joram alikuwa akizitumia kwa muda mrefu kujaribu kuyasoma yake maandishi ya kijasusi ambayo aliyapata katika mfuko wa hayati Chonde. Humo alitoa karatasi ndefu, iliyoandikwa kwa mashine, ikiwa tafsiri ya maandishi hayo. Alimkabidhi Nuru na kumwabia asome haraka haraka.

MPANGO KABAMBE WA KUIFANYA AFRIKA ITUPIGIE MAGOTI

Taarifa hii ni siri kubwa miongoni mwa watu wachache sana, wa ngazi za juu katika serikali yetu. Ni taarifa ya mafanikio ya jaribio lililofanyika muda mrefu, kwa gharama kubwa, baina ya wana sayansi wetu na waliotoka katika nchi marafiki duniani; juu ya uwezekano wa kufanya nguvu za nukria zitusaidie katika kuwaweka Waafrika, na ikiwezekana dunia nzima katika kwato zetu.

Itakumbukwa kuwa kifungu kikubwa cha pesa kilitengwa ili kufanyia majaribio haya. Kwa siri kubwa sana mtambo madhubuti ulijengwa na setilaiti kutupwa angani. Mbili kati ya setilaiti hizo zilidondoka katika nbahari ya Hindi kabla ya kuonyesha matokeao. Lakini setilaiti ya tatu imetimiza majibu. Majaribio yamefanywa na kuleta matokeo ya kuridhisha kabisa. Mtu wetu alitumwa Lagos na kutega gololi maalumu ambazo baada ya kufyatuliwa zimeifanya setilaiti hiyo iliyoundwa kwa madini yanayoifanya isionekane kwa macho iweze kuingia katika anga la nchi hiyo na kuachia bomba la moto mkali ambao uliteketeza uwanja na watu kadhaa. Jaribio la pili lilifanywa huko Harare ambako maghala yaliteketea. Jaribio la tatu na la mwisho linakusudiwa kufanywa Tanzania, katika jengo la Benki Kuu inayojengwa. Hatuna shaka kuwa jaribio hilo litafanikiwa.

Baada ya jaribio hilo ndipo tutaanzisha mpango wa kuzifanya nchi zote zinazojiita za mstari wa mbele, kutupigia magoti. Mtu wetu anayekwenda Tanzania ni mtu wa kutegemewa, aliyeishi huko miaka mingi. Atapewa pesa nyingi zitakazomwezesha kwenda mahala popote duniani, na kumnunua mtu yeyote.
 
SEHEMU YA 54

Huyu atakuwa na jukumu la kusubiri amri yetu ili aachie vipigo vingine ambavyo vitaifanya Afrika itokwe na machozi huku dunia ikilalamika...

Nuru aliinua kichwa ghafla kumtazama Joram. Tayari uso wake ulikuwa umelowa jasho la hofu na mshangao. "Joram" Nuru alifoka, "Mungu wangu. Huoni kama hii ni habari ya kutisha kuliko zote? Tunawezaje kustarehe hivi huku nchi yetu ikiwa mashakani?".

"Imenichukua siku nyingi kuigundua. Waliyaficha maandishi hayo kwa hila ambazo zingemtoa jasho mtu yeyote mwenye akili timamu. Hata hivyo ugunduzi huu hautatusaidia chochote. Kama ulivyosoma setilaiti hiyo iko angani na haionekani kwa macho. Inaendeshwa na mtambo ambao uko katika himaya yao, bila shaka ukilindwa kwa hali na mali. Hakuna njia nyingine zaidi ya kuubomoa mtambo huo".

"Je. Tukitoa siri hii kwa dunia?", Nuru alimuuliza Joram.

"Haisaidii. Umoja wa Mataifa utalalamika na kuilaani Afrika Kusini. Pengine watawekewa vikwazo vya kiuchumi. Unadhani hayo yatawafanya watuhurumie?". Mara ngapi wamelaaniwa? Mara ngapi wamewekewa vikwazo? Hapana Nuru. Lazima nifike Afrika Kusini. Dawa ya moto ni moto".

Nuru alitulia kwa muda akiitafakari taarifa hii kwa makini. Mara aliinuka na kumwendea Joram. Akamkumbatia na kumnong'oneza masikioni. "Samahani sana mpenzi. Nilikuelewa vibaya sana ulipoiba pesa benki. Vilevile nilishangaa unavyozitumia pesa hizo vibaya kwenda huku na kule ukuwa hujali matusi ya waandishi wa habari. Sasa nimekuelewa. Nimeelewa kwanini ulifanya vile. Ulikuwa ukijiandaa kwenda Afrika Kusini. Ulichofanya ilikuwa kuilaghai dunia ili uonekane mhalifu na mkimbizi asiyeweza kuishi popote isipokuwa Afrika Kusini. "Sivyo mpenzi?". Joram alipochelewa kujibu Nuru aliongeza, "Mpenzi. Wewe ni shujaa kuliko mashujaa wengine niliopata kuwasikia. Tutakwenda pamoja Afrika Kusini...".

"Tatizo siyo kwenda Nuru. Tatizo ni kurudi. Unaoneje, tutarudi na zoho zetu?".

Wakati Joram na Nuru walipokuwa wakizungumza hayo, Kombora alikuwa Ikulu mbele ya Rais akitokwa na jasho jembamba. Alifika ofisini, akiwa hoi kwa ukosefu wa usingizi wa siku kadhaa. Mara alipopata simu ambayo ilimtaka kwenda Ikulu mara moja, alilitia gari lake moto na kufunga safari hiyo ya dharura hadi Ikulu ambako alielekezwa katika chumba cha faragha. Humo aliwakuta Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Ulinzi na Katibu Mkuu katika Wizara ya Ulinzi. Aliwasalimu kishujaa, ingawa tayari moyo ulikuwa ukimdunda kwa kujua kuwa hakuwa tayari kuyajibu maswali yao.
"Nini hiki? Rais alimwuliza akimsogezea kijibarua ambacho kiliandikwa kwa mkono.
Kombora alikipokea na kukitazama. Hakuwa na haja ya kukisoma kwani ilikuwa moja kati ya zile barua ambazo zilikuwa zikiwafikia wakubwa wa nchi za mstari wa mbele mara kuwatisha ili waache msimamo wao dhidi ya Afrika Kusini.
"Isome," Rais alihimiza.
Kombora akakisoma. Mara alielewa sababu ya kusisitiziwa aisome. Ilisema: "ONYO LA MWISHO." Ikarudia kutaja sehemu muhimu ambazo aliyeandika barua hiyo alikusudia kuzichoma, sehemu ambazo ni pamoja na Ikulu. Baada ya kuikodolea macho, Kombora aliyarudisha katika uso wa Rais. "Nimeisoma mzee."
"Barua hiyo imekutwa katika ofisi yangu," Rais alieleza. "Ni dhahiri kuwa aliyeileta anao uwezo na nafasi ya kufanya lolote katika nchi na ofisi hii. Kwanini mmempa haki hiyo?"
Kombora hakujibu. Hakujua ajibu nini. Yeye na vijana wake wote walikuwa taabani katika mapambano haya. Majasusi wengi ya Afrika Kusini yalishikwa, lakini halikutokea lolote ambalo lingeweza kusaidia kukomesha vitisho vya ainaaina. Mengi yalikuwa majasusi wa kawaida, ambayo ama hawakuwa na lolote la haja au yalitumwa kwa ajili ya masuala yasiyo na uzito mkubwa. Wapelelezi wake ambao walikuwa nje pia walivitesa vichwa vyao bila ya kupata matunda ya kuridhisha. Nusura Kombora apate hasira kwa lawama hizo ambazo hakuona kama zinamstahili. Alitamani ainuke, atangaze kujiuzulu. Lakini hayo hakuyafanya kwa kukumbuka kuwa hasira si dawa. Na licha ya hayo aliona wazi kuwa lawama zilimstahili. Kufanya kazi ni kupata matokeo ya kazi hiyo. Kazi isiyo na matokeo haiwezi kuitwa kazi.
"Sina haja ya kukulaumu," Rais aliendelea. "Nauona ugumu wa jukumu mlilonalo. Nilichokuitia ili kukukumbusha kwa mara nyingine ni kuwa hata kwa bei ya roho zetu hatuwezi kukubali kufuata masharti ya utawala huu dhalimu. Lazima tupambane nao. Na huu ni wakati pekee wa kuonyesha moyo wetu. Uoga hauwezi kutufanya tukubali kuwa mateka wa utawala haramu kama huu. Lazima tushinde," akasita kidogo akimtazama Kombora kwa makini. "Inspekta," aliongeza kwa sauti ya amri kidogo. "Huu ni wakati wako. Kuna wakati wa njaa; wakulima hutakiwa kuiokoa nchi; wakati wa uhaba wa fedha za kigeni wafanyakazi viwandani huombwa kujitoa mhanga; wakati wa vita jeshi hulazimika kulinda nchi. Huu ni
 
SEHEMU YA 55

wakati wako, Inspekta. Nchi inakuhitaji na kukutegemea. Gavana wa Benki amepewa amri ya kukupa kifungu chochote cha pesa unazohitaji, Mkuu wa jeshi ameambiwa akuruhusu kutumia kikosi chochote na Bunge limependekeza uruhusiwe kufanya lolote. Kazi kwako," Rais alimaliza akainuka na kutoka.
Kombora alipumbazuka kidogo juu ya kiti hicho. Jasho jembamba lilikuwa likimtoka. Mara akajilaani kwa kusita kuleta barua ya kujiuzulu kwake. Hakujua angefanya nini zaidi. Aliwatazama viongozi ambao walikuwa wametulia, wakimtazama. Kiongozi mmoja alitamka neno ambalo halikumfikia Kombora. Mwingine alitikisa kichwa. Kombora akainuka na kuwaaga. Alipoifikia gari yake ndipo alipokumbuka kuwa ile barua ya vitisho bado alikuwa nayo mkononi. Akaitia mfukoni na kuamuru gari limrudishe ofisini.
***
Kidole kimoja kamwe hakivunji chawa; Kombora aliwaza akiwa kaketi ofisini mwake akifikiria afanye lipi zaidi kufanikisha vita hivi ambavyo havikuwa na uelekeo maalumu. Akamwagiza opereta wake kumpatia viongozi wa ofisi zote za usalama katika nchi za mstari wa mbele, pamoja na Naijeria. Alipowapata alipanga nao kufanya mkutano wa dharura ambao ulikusudiwa kujadili hali inayozikabili nchi zao. Ilikuwa kama wote walikuwa wakiusubiri kwa hamu wito huu. Wakaafikiana kukutana Jijini Dar es Salaam siku mbili baadae.
Kombora, akiwa mwenyeji, alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huu uliofanywa kwa siri kubwa. Mkutano huu ulijumuisha watu wenye sura mbalimbali, umri tofauti, viwango tofauti vya elimu; wote wakiwa na dhamira moja. Kila mmoja alieleza tishio lililokuwa likiikabiri nchi yake na kila mmoja alieleza hatua ambazo tayari zilikuwa zimechukuliwa. Lakini wote waliafikiana kuwa matunda ya juhudi zao hayakuwa ya kuridhisha. Wote walifahamu kuwa matunda ya maafa yaliyokuwa mbele yao siku za usoni, endapo yasingekomeshwa, yangesababisha maafa na vilio ambavyo historia haikupata kuvishuhudia.
"Jambo linalotisha zaidi ni maoni au hisia za wanasayansi wetu," mjumbe mmoja alieleza. "Wanaamini kuwa moto huu unatokea angani katika chombo ambacho hakionekani kwa macho. Hivyo, jukumu letu ni kukilipua chombo hicho. Tutawezaje wakati hatukioni?"
"Labda tuilazimishe Afrika ya Kusini ikiteremshe."
"Hilo ndilo tatizo. Tutawezaje kuilazimisha? Tumejaribu kutazama uwezekano wa kuishambulia kijeshi kwa pamoja na kuona si rahisi. Wao wamejiimarisha sana kiulinzi angani, majini na nchi kavu. Nasi Waafrika umoja wetu unalegalega kiasi kwamba hatuwezi kuafikiana mara moja. Vilevile, wakati tutakapokuwa tukijiandaa kwenda huko madhara waliyotishia yatakuwa yakiendelea kutukia."
"Lakini haiwezekani tukubali kuwa hatuwezi kufanya kitu," Kombora alieleza kwa sauti. "Lazima tufanye jambo. Jema au baya, lazima tulifanye mapema."
Aliungwa mkono.
Mara simu ikaroma katika meza ya Kombora. Akaitazama saa yake na kuona kuwa zilikuwa zimesalia dakika nane kutimia saa kumi za alfajiri. Akainua simu hiyo na kusikiliza. Ilipigwa na msaidizi wake ambaye alimwomba atoke nje mara moja. Kombora akawataka radhi wageni wake na kutoka.
Dakika chache baadaye alirudi ndani akiwa kaandamana na mgeni mmoja ambaye alikuwa katika hali ya kusikitisha. Mgeni huyo alikuwa mtu mweupe, aliyevaa mavazi yaliyochakaa. Mwili wake ulikuwa umejaa majeraha na mikwaruzo mingi kiasi cha kumfanya aonekane mahututi. Hata hivyo, macho yake yalikuwa na uhai.
"Huyu ni mgeni ambaye amekamatwa huko mpakani mwa Malawi na Tanzania leo," Kombora alieleza. "Amesema ametoroka kutoka Afrika ya Kusini kuja baada ya kuponea chupuchupu. Maelezo yake nadhani yatatufaa katika kikao hiki," alimaliza akimwashiria mtu huyo kujieleza.


"Kwanza ningependa ieleweke kuwa mimi sio mzungu, "mtu huyo alisema. "Mimi ni mtu mweusi, mzaliwa wa Soweto," alisema akifungua vifungo vya shati lake. Kila mmoja alitokwa na macho ya mshangao kwa kuona kuanzia tumboni alikuwa na ngozi nyeusi. "Ngozi hii nyeupe iliyokaa usoni na
 
SEHEMU YA 56

mikononi ni matokeo ya plastic surgery ambayo nilifanya miaka kumi iliyopita ili niweze kuingia miongoni mwa makaburu na kuiba siri zao ili zitusaidie katika vita vyetu vya kujikomboa," alisita kidogo. Kisha akaendelea. "Nimefanya kazi mbalimbali katika jeshi hilo, daima nikiwa macho kupeleleza hiki na kile. Majuzi ndipo nilipogundua jambo la kutisha zaidi. Niligundua kuwa umejengwa mtambo ambao unaendesha Setilaiti ambayo haionekani kwa macho inayotumiwa kuteketeza majumba na sehemu muhimu za kiuchumi katika nchi za kiafrika. Nikaanza upelelezi wa makini kutafuta uwezekano wa kuangamiza tishia hilo. Kwa bahati mbaya, walinishuku katika upelelezi wangu. Sikuwa na la kufanya zaidi ya kuikimbiza roho yangu. Hata hivyo, nimeona mengi, nadhani naweza kutoa mchango madhubuti ambao utatuwezesha kushinda."
Wakuu hao wa upelelezi walimtazama mtu huyo kwa makini kisha wakatazamana. Mmoja alicheka, mwingine akatabasamu.
"Hatimaye...." mmojawao alinong'ona.

SURA YA NANE

KATIKA jumba fulani, mtaa fulani, jijini Johannesburg, makaburu wanne waliketi katika ofisi moja wakisikiliza taarifa za kijasusi kutoka Tanzania. Jasusi moja lilikuwa likiwaarifu kwa kutumia chombo maalumu juu ya msafara wake na mafanikio ya shughuli zake.
"Nimefika salama na kuwakabili nikiwa katika hali ya kusikitisha iliyonifanya niaminike kama mmoja wao. Wameumeza kabisa uongo wangu. Sasa hivi wananiamini sana. Wameniuliza mwaswali mengi na nimewajibu kiume nikiwapa taarifa za uongo. Nadhani wamekusudia kuwatuma wapelelezi wao huko, ingawa hawakupenda kunishirikisha moja kwa moja. Hata hivyo, msijali, nitakuwa macho nikiarifu kila kitendo chao hatua kwa hatua."
Makaburu wakatazamana tena na kutabasamu kwa namna ya kupongezana. Mmoja wao hakuona kama tabasamu linamtosha. Yeye aliangua kicheko. Kisha aliona kicheko hakitoshi. Akainuka na kuliendea kabati lililokuwa nyuma yake ambamo alitoa chupa kubwa ya pombe kali, aina ya JohnWalker na glasi nne. Akazileta mezani na kuziweka mbele ya kila mmoja. Akaifungua na kumimina. "Lazima tusherehekee ushindi." Baadae akaongeza, "Sitoi ruhusa ya kunywa ofisini isipokuwa inapobidi kufurahi. Mwanadamu hana budi... Cheers..."
Kaburu huyu kwa jina aliitwa Von Iron, kwa sura hakutofautiana sana na mtoto mchanga ingawa kiumbo alikaribiana na kiboko aliyeshiba vizuri. Yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa kamati hii maalumu ya BOSS ambayo iliundwa kuzishughulikia kikamilifu nchi za kiafrika 'zinazojitia kichwa ngumu.' Amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hili la kijasusi tangu lilipoundwa miaka mingi iliyopita. Mara kwa mara kazi yake imekuwa nzuri kwa wakubwa zake. Haikupata kutokea mpango aliouandaa ukashindwa kutoa mafanikio, jambo ambalo lilimpa heshima na hadhi machoni mwa weupe na kumfanya jazanda ya mauti katika fikra za weusi. Ni yeye aliyebuni uwezekano wa kuitumia nguvu ya nyuklia kuwaangamiza Waafrika. Hakuwa Mwanasayansi, lakini alipewa jukumu la kushirikiana nao, akiwa na uhuru wa kutumia kiasi chochote cha pesa hadi majaribio yalipofanyika na kutoa matunda ya kupendeza. Kadhalika, ni yeye aliyebuni mpango wa kuwapa ngozi nyeusi baadhi ya wapelelezi wao, kwa kupoteza pesa nyingi katika hospitali zinazofanya Plastic Surgery. Watu hao waliingizwa kwa hila katika vikundi vya wapigania uhuru na kujifanya wenzao huku wakitoa siri zote na hata kuua inapobidi. Mmoja wa watu hao ni huyu ambaye alikuwa akiwafurahisha sana kwa taarifa zake kutoka Tanzania.
Yeye alifanyiwa mabadiliko ya ngozi yake miaka mitano iliyopita, akawa mweusi na kutibua mambo mengi katika chama cha SWAPO na ANC. Majuzi alirudishwa Ulaya ambako alirudishiwa ngozi ya mtu mweupe usoni na mikononi, kisha akatumwa Tanzania ambako waliona ni chimbuko la misukosuko yote dhidi ya utawala wao, na hasa ili wajue nini kinafanyika katika kutapatapa kwa Serikali na wananchi wa Tanzania juu ya mtambo wao wa aina yake ulioko angani baada ya kutoeleweka kilichomtukia mtu wao, Chonde, hata akafa katika hoteli moja. Zaidi, huyu alikuwa amepewa akiba ya kutosha ya zile gololi zinazouongoza mtambo huo kulipua miradi teule ili wakati utakapowadia waachie pigo hili walilokusudia kulifanya, "Pigo la mwisho."
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom