Sehemu ya 36.
Kwa kumwangalia mara moja tu usingeweza kuwa na shaka kwamba Angelina alikuwa anaumwa, alipungua sana na kila alipokuwa akipita mbele ya watu waliokuwa wakimfahamu walimshangaa, alipungua na kuhuzunisha mno.
Chuoni hakuwa na furaha, alisema baada ya kufanikiwa na kwenda kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam basi angeweza kutumia muda wake mwingi na mpenzi wake lakini mambo yakabadilika, sasa huko chuo kukawa kama jehanamu.
Hapakuwa na mtu aliyejua kama yeye na Edmund walikuwa na mahusiano ya kimapenzi, wengi walihisi inawezekana walikuwa marafiki tu kwa kuwa walikuwa wakifahamiana tangu shuleni, moyo wake ulichoma, kila alipokuwa akimuona Edmund, alisikia kabisa maumivu moyoni mwake.
Hakuamini kama ingetokea siku moja maumivu hayo yangetoka, kwake alijua kabisa yangeishi milele yote. Ilikuwa ni lazima afanye tiba ya moyo huo na kitu kikubwa ambacho alikifikiria ni kuondoka Tanzania na kuelekea Ujerumani kwa ajili ya kusoma moja ya chuo cha huko kutimiza ndoto zake.
Haraka sana akawasiliana na Gideon na kumwambia kuhusu mpango huo, kwa sababu tayari alikwishaambiwa na Amon, hakuwa na tatizo, akamkubalia msichana huyo na hivyo kuelekea Ujerumani.
Akiwa njiani, shauku yake kubwa ilikuwa ni kuonana na Amon tena na kumuomba msamaha, alijuta kwa kilichotokea hivyo alitamani sana kurudiana naye na kamwe kwenye maisha yake asingeweza kumuacha tena.
Hakujua kama Amon angekuwa tayari ama la lakini kwa jinsi alivyozungumza naye na kuonekana kuwa kawaida, aliamini angemsamehe na hatimaye kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa mara nyingine tena.
Baada ya siku kadhaa akawa nchini Ujerumani, alifika leo tu na kesho akasikia taarifa kuhusu kupotea kwa Amon. Moyo wake uliumia sana na hakujua hasa kilichotokea, alifika nchini humo kwa ajili ya kusoma, ila jingine lilikuwa ni kuonana na Amon na kumwambia kuhusu kurudiana naye, mbaya zaidi mwanaume huyo alipotea.
Wakati Gideon akiondoka kuelekea nyumbani kwa Amon alitaka kwenda naye ila Gideon akakataa, alifanya hivyo kwa sababu hakutaka kwanza ajue kuhusu Jenniffer, angeweza kuharibu kitu huko na kuonekana vibaya.
Akabaki nyumbani lakini akaanza kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Alimuomba Mungu Amon apatikane, alihisi kabisa mwanaume huyo alizaliwa na kuletwa duniani kwa ajili yake na alikuwa na uhakika angemsamehe zaidi kwa kukubali kuwa naye tena kwa mara nyingine.
Alitamani kumshirikisha kaka yake kuhusu kile kilichokuwa moyoni mwake lakini aliogopa kufanya hivyo, aliyakumbuka maneno aliyomwambia wakati akiwa amemuacha Amon, aliyakumbuka vilivyo kitu kilichomfanya kujisikia vibaya zaidi.
“Nimwambie? Hapana! Nitaanzaje? Nilimuacha Amon kwa maneno machafu sana,” alisema Angelina.
Maneno aliyotumia kumwacha Amon yalijirudia kichwani mwake na kumfanya kujisikia vibaya mno. Kuna wakati alijiona kuwa mjinga sana, hakujua ni kwa sababu gani alidanganyika na kuwa na Edmund na wakati kulikuwa na mwanaume aliyekuwa akimpenda sana.
Akajilaumu lakini kuna kipindi alitakiwa kukubaliana na kile kilichotokea, ndiyo alifaya makosa, alikuwa mjinga lakini wakati mwingine alijiona kusimamia alichokuwa akikiamini, ndicho kitu alichokisema Amon alipokuwa akizungumza naye, hivyo hakutakiwa kujutia.
Alikaa kwa siku kama mbili hivi, kila alipomwangalia kaka yake alionekana kabisa kuwa na majonzi tele, alimkumbuka rafiki yake, Amon, hakuwepo tena, alitekwa na watu wasiojulikana na hakujua mahali alipokuwa.
Baada ya siku hizo mbili, jioni moja ndipo Gideon akapigiwa simu na Jeniffer na kuambiwa Amon alipatikana akiwa mzima wa afya kabisa. Gideon akashtuka, hakuamini alichokisikia, haraka sana akamuuliza Jeniffer alipokuwa, akamjibu nyumbani.
Akamwambia Angelina, msichana huyo hakutaka kubaki, yaani kwa kipindi hicho ilikuwa ni lazima kwenda huko, kumuona Amon, alimkumbuka mno, na kile kilichotokea, hakika kilimfanya kutamani kumuona tena.
Ndani ya gari hamukuwa na mtu aliyeongea lolote lile, walikaa kimya mpaka baada ya dakika kadhaa, wakafika alipokuwa akiishi Amon na kuelekea ndani, walipofika humo, wakamkuta Amon akiwa na Jeniffer, Anita na mwanaume mwingine ambaye hawakuwa wakimfahamu, alikuwa Tuchel.
Haraka sana Gideon akamfuata na kumkumbatia rafiki yake huyo na kumuuliza kilichokuwa kimetokea. Hakutakiwa kuzungumza kitu kwanza, hapakuwa na watu wengi waliokuwa wakijua kama alipatikana, ni polisi wachache na huyo Tuchel, nini kilitokea? Alitekwa na nani?
Hapakuwa na mtu aliyejua hilo, na kwa jicho la Angelina alipokuwa akimwangalia Amon na Jeniffer, kwa jinsi walivyokuwa wakishikana tu, akagundua hakuwa na chake, ilikuwa ni lazima wawili hao wawe wapenzi.
Moyo wake ukauma sana.
***
Konn alibaki akimwangalia Amon aliyekuwa ndani ya chumba kile huku akiwa hajui ni kwa sababu alikuwa humo. Alimwangalia kijana huyo, kwake hakuonekana kuwa mtu wa kawaida hata kidogo. Alikuwa na uwezo mkubwa mno uwanjani.
Kulikuwa na watu waliotajirishwa na kijana huyo, kila walipokuwa wakiweka pesa zao kuitaka Hertha Berlin ishinde, basi yeye alifanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanashinda.
Amon alipendwa na wacheza kamari wote, hakuwa akiwaangusha, wakati mwingine timu nzima ya Hertha Berlin uliiona ikikamatwa kabisa lakini bila kutarajia kijana huyo alikuwa akiibuka na kufanya maajabu makubwa.
Yeye mwenyewe Konn alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakinufaika na kijana huyo, leo eti alikuja mtu na kumpa ofa ya kumuua mwanaume huyo, hakutaka kufanya, badala yake akataka kumuua huyo kwani aliamini endapo angeondoka, angeweza kumpa dili hilo mtu mwingine na kumuua kitu ambacho hakutaka kabisa kuona kikitokea.
“Unajua kwa sababu gani upo hapa?” aliuliza Konn huku akimwangalia Amon.
“Hapana! Nilichukuliwa tu kutoka uwanjani!” alijibu.
“Ni kwa sababu kuna mtu anataka ufe.”
“Kwa sababu gani?”
“Sijui! Ila usiogope, huwezi kufa aisee. Leo umenifanya niingize kiasi cha euro laki moja na nusu,” alimwambia.
“Kivipi?”
“Kwa uliyoyafanya uwanjani! Wewe ni mtu muhimu sana. Pamoja ya kwamba sitoifanya kazi ya mwanaume huyo, ni lazima pia nikushikilie kwa siku kadhaa,” alimwambia.
Pamoja na kuambiwa hayo yote lakini hakutaka kumwamini mwanaume huyo hata kidogo, alikuwa muuaji tu, alikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya jambo lolote lile mbele yake, aliyapenda maisha yake hivyo hakuacha kusali moyoni mwake.
Alishikiliwa humo na baada ya siku mbili simu ikapigwa kwa Dawson na kuambiwa tayari Amon aliuawa. Walichokifanya ni kumchukua na kumlaza chini, wakachukua damu ya ng’ombe, wakammwagia usoni na pembeni kidogo kuonyesha alipigwa risasi. Kwa jinsi alivyoonekana usingejua kama mtu huyo hakuuawa.
Baada ya hapo simu ikapigwa mpaka kwa Dawson na kuambiwa kila kitu kilifanikiwa na ni yeye tu ndiye aliyekuwa akihitajika huko, kwenda kuuona mwili wa Amon lakini pia kumalizia kiasi cha pesa alichoahidi.
Haraka sana Dawson akatoka na kwenda huko, alipofika, akachukuliwa na kupelekwa ndani ya chumba kile na kuonyeshwa Amon aliyekuwa amekaa tu kwenye kiti akimwangalia.
Hakujua mwanaume huyo alikuwa nani, hakujua ni kwa sababu gani alitaka kummaliza, alimwangalia na kuishiwa maneno ya kusema. Dawson alishtuka, alibaki akimshangaa Amon.
Kwenye simu aliambiwa kijana huyo aliuawa, na picha akatumiwa lakini cha kushangza kabisa, alimkuta akiwa mzima wa afya, hakujua sababu ya kudanganywa na wakati tayari alifanya malipo.
“Mbona ham...” aliuliza lakini hata kabla ya kumalizia sentensi yake, mwanaume aliyekuwa nyuma yake akamtuliza kwa kumuwekea bastola mgongoni.
“Tulia!” alisema mwanaume huyo, baada ya sekunde chache, mlango ukafunguliwa na Konn kuingia.
Sura yake ilikuwa na tabasamu pana, alimwangalia Dawson, alimuona kama mtu fulani mjinga ambaye alimtaka kufanya kitu ambacho hakuwa radhi kabisa kukifanya.
Kumuua Amon ni kitu kisichowezekana, kummaliza kijana huyo kwa yeye mcheza kamari ya mpira ambaye alikuwa akipunwa mara kwa mara ilimaanisha angeendelea kupunwa endapo tu huyo Amon asingekuwa kwenye dunia hii.
Je, nini kitaendelea?