Sehemu ya 15.
Kadiri ziku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele ndivyo uzuri wa Angelina ulivyokuwa ukiongezeka, kila siku alionekana msichana mpya kama aliyeshushwa kutoka Mbinguni.
Hakuisha hamu, mwili wake ulikuwa ukizidi kujiboresha kila siku, hipsi zilikuwa zikionekana vyema, kifua chake kilizidi kujaa kuonyesha sasa alikuwa akienda kwenye urembo uliopitiliza.
Kila kona aliyokuwa akipita wanaume walibaki wakimwangalia, na alipopotea walikuwa wakimjadili ni kwa namna gani Mungu alimpendelea, hakuwa msichana wa kawaida hata kidogo, kama angesimama na wanawake ambao unawaamini ni warembo halafu ukaambiwa uchague mmoja, bila shaka ungemchagua Angelina.
Edmund hakutaka kumuacha Angelina, japokuwa alikuwa na mambo yake mengi lakini kwa msichana huyo alitulia kabisa.
Hakuacha kufuata wanawake mbalimbali, alijiambia baada ya kuwa na Angelina angebadilika, asingekuwa malaya tena lakini akashindwa kuvumilia kwa sababu moja tu, alimzoea.
Akawa anamuona msichana wa kawaida ila kwa sababu alisifiwa kila kona, akaona endapo angeachana naye basi kuna siku angekuja kujuta na kutamani sana kuwa naye. Alivumilia na kuvumilia, kutembea na wanawake wengine ilikuwa ni kwa siri kubwa, hapakuwa na mtu aliyekuwa akifahamu kama alikuwa wa aina hiyo.
Kitu kingine ambacho Edmund alimuweza Angelina ni kwa namna alivyokuwa mnyenyekevu mbele yake, alikuwa mtu aliyemuheshimu na alipokuwa akifanya kosa, haraka sana alimuomba msamaha na kuendelea na mambo mengine.
Kwa Angelina huyo alikuwa mwanaume wake wa ndoto, kulikuwa na wanaume wengi waliokuwa na kiburi ambao walimuona mwanamke kuwa takataka fulani lakini ilikuwa tofauti kwa huyo Edmund.
Kwa jinsi alivyokuwa akiishi na Angelina, kila mwanamke alitamani sana kuwa na mwanaume wa aina hiyo, alikuwa ni wa kipekee sana kiasi cha kuwafanya mpaka wanawake wengine kutamani hata siku moja wasimamishwe na mwanaume aliyekuwa na kariba kama ya Edmund.
“Ninakupenda kwa sababu unanielewa mpenzi,” alisema Edmund huku akimwangalia Angelina.
“Ninakupenda kwa sababu u mnyenyekevu na unajua kupenda,” alisema Angelina.
“Sidhani kama nisingekuwa na msichana kama wewe, nisingeweza kupata msichana sahihi kama wewe. Ninakupenda sana Angelina, nitakupenda maisha yangu yote,” alisema Edmund huku akimwangalia msichana huyo aliyekuwa akivaa nguo zake chumbani baada ya kazi nzito ya kukilazimisha kitanda kipige kelele.
Edmund akabaki kitandani akimwangalia Angelina pale alipokuwa amesimama, naye akasimama na kumsogelea, akiwa nyuma yake, akamshika kiuno na kusogeza mdomo wake shingoni mwa nyuma na kumbusu.
“Kila siku unazidi kuwa mzuri mpenzi,” alimwambia huku akiwa nyuma yake.
“Na wewe pia mpenzi! Kila siku moyo wangu unazidi kukupenda, nadhani wewe ni mwanaume sahihi kwangu,” alisema Angelina.
“Unadhani! Huna uhakika?”
“Simaanishi hivyo!”
“Unachokimaanisha wewe ni kipi?”
“Wanaume si wa kuwaamini sana!”
“Na wanawake?”
“Hahah! Kwa hiyo unataka kusemaje?” aliuliza Angelina na kugeuka, wakaanza kuangaliana, kila mmoja alikuwa akitabasamu.
“Kwamba sisi tuaminiane, tupendane na tuheshimiane,” alimwambia.
“Hilo lipo sawa. Unaahidi kufanya hayo yote?”
“Nakuahidi!”
“Nashukuru!”
Wakati huo Angelina alikuwa kidato cha tano, aliendelea kusoma kwa bidii huku akitamani sana kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari wa misuli, aliamini kwenye kusoma, japokuwa aliendekeza mapenzi lakini bado ndoto yake ilikuwa ni kuwa daktari mkubwa.
Huo mwaka ukaisha na kuingia mwaka mwingine. Wakati huo Edmund alimaliza shule na hatimaye kufaulu vizuri na kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya kusomea masomo yake ya biashara.
Aliendelea kuwasiliana na mpenzi wake, Angelina, kila siku ilikuwa ni lazima kuzungumza kwenye simu na wakati mwingine kuonana na kuongea mengi.
Chuoni hapo Edmund alikuwa msumali kwa wanawake wengi, kila mtu aliyekuwa akimwangalia, alimpenda, alikuwa na sura nzuri lakini kubwa zaidi alitoka kwenye familia iliyokuwa na pesa.
Alipenda sana wanawake lakini baada ya kuficha chuoni, akapunguza mambo ya wanawake kwa sababu alisikia tu kulikuwa na taasisi nyingi za UKIMWI zilizokuwa zikiwasomesha wanafunzi wao huko, wanafunzi walionona, waliovutia lakini waliathirika.
Hakutaka kuathirika, mawazo yake yalikuwa finyu kama ya watu wengine kwamba ukiathirika basi ndoto zako zote zimepotea, hivyo hakutaka kabisa kujihusisha na mwanamke yeyote yule.
Alikuwa mkimya lakini wanawake hawakuchoka kummendea, kila siku walijigongagonga, na mwanamke aliyekuwa tayari kwa lolote lile alikuwa Esta, msichana kutoka nchini Iringa aliyefika jijini Dar kwa mara ya kwanza, na alipomuona Edmund tu, moyo wake ukapiga paa.
Wakati Esta akitoka huko Iringa aliwaambia wazazi wake katika maisha yake ya chuo asingethubutu kabisa kuwa kwenye uhusiano na mwanaume yeyote yule, asingetaka kufanya mapenzi tena na mtu yeyote mpaka siku ambayo angeolewa na kuwekwa ndani.
Hakuwa bikira, tayari alitolewa na baada ya hapo alikutana kimwili na wanaume wengine wawili aliokuwa nao kwenye uhusiano kwa nyakati tofauti na alipoachana nao, akaamua kutulia, hakutaka tena mwanaume.
Esta alikuwa mwanamke fulani mweupe, mzuri aliyekuwa na lipsi pana, alikuwa na uzuri wa ajabu, kila alipokuwa akipita nao wanaume walikuwa wakimwangalia kwa matamanio, alivutia, alikuwa na ule mwili wa kuita ambao kwa rijali yeyote yule ilikuwa ni lazima kutokwa na udenda kwanza.
Esta hakugusika, alikuwa mkali, aliumizwa mapenzini na hakutaka kabisa kuwa na mpenzi mwingine, alijitahidi sana kujitunza kwa kila kitu kitu kilichomfanya kila siku kwenye maisha yake hapo chuoni kutamani kusoma sana.
Siku aliyomuona Edmund moyo wake ukapiga paa! Hakuamini kama angekutana na mwanaume mzuri kama alivyokuwa huyo, alitamani kuzungumza naye na kitu kizuri kwake ni kwamba wote walikuwa wakisomea Biashara.
Je, nini kitaendelea?
Kwa wanaotaka kusoma simulizi zangu BURE Whatsapp wabonyeze hiyo link, waingie moja kwa moja kundini

WhatsApp Group Invite
chat.whatsapp.com