*ROHO YAKE INADAI --- 23*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
.
.
“Nani?” Akauliza. Hakukuwa na majibu, akasita kwenda kufungua. Hodi ikapigwa tena. Akaamua kunyanyuka na kuusogelea mlango. “Nani?” akauliza tena. Hakukuwa na majibu. Brian akaamua kufungua mlango na kutazama nje.
.
.
Hamaki, kule sebuleni akauona mlango ukiwa wazi! Na kama haitoshi, akamwona Olivia akiwa anaishia, anaenda zake!
.
.
“Olivia!” Brian akapaza sauti. Haraka akatoka chumbani na kukimbilia nje.
.
.
ENDELEA
.
.
Alimuwahi Olivia na kumsimamisha. Binti hakuwa anajitambua. Brian alijaribu kumwamsha toka usingizini pasipo mafanikio. Bado Olivia alikuwa anataka kwenda, anataka kusonga mbele! Macho yake yalikuwa yamepandisha kiini cheusi juu kupotea!
.
.
“Olivia, amka! Oliviaa!” Brian aliita akimtikisa Olivia kwanguvu. Akaita pasipo kuchoka, hatimaye Olivia akarejewa na fahamu! Alikuwa anahema kana kwamba ametoka kukimbizwa. Alitazama kando na kando akaitaajabu kwanini yupo hapo.
.
.
“Olivia, upo sawa?” Brian akauliza. Olivia akatikisa kichwa. Uso wake ulikuwa umejawa na woga. “Nipo wapi hapa Brian?” akauliza.
.
.
“Upo nje! Ulikuwa umetoka, unaondoka!” Brian akamjibu akimtazama mtoto huyo kwa matumaini. Lakini ghafla, Olivia akatazama nyuma ya Brian na kuduwaza macho. Akaachama mdomo na kumuuliza Brian, “Ni nani yule?”
.
.
Brian akageuza shingo kutazama. Ajabu akamwona mwanaume mrefu mweusi aliyekuwa anaongozana na mtoto akija kwa kasi kuwafuata. Moyo wake ukaruka pigo. Haraka akamnyakua Olivia na kuanza kukimbia naye haraka!
.
.
Alitupa miguu kadiri alivyokuwa anaweza. Kila alipotazama nyuma akaona mwanaume yule akimjongea kwa kasi ya ajabu. Alikuwa anakimbia kana kwamba upepo!
.
.
“Wanatufikiaa!” Olivia akapiga kelele. “Brian, wanatufikiaa!” Olivia akalia. Lakini nini afanye Brian? Alikuwa anakazana kadiri ya uwezo wake wa mwisho. Alikimbia haswa. Alikuwa amebakiza hatua chache tu kufikia mlango wa nyumbani, ila ajabu napo, mlango huo ukaanza kujifunga wenyewe taratibu!
.
.
Kwa mahesabu ya wazi, Brian asingeweza kuufikia mlango huo kabla haujajifunga.
.
.
“Tafadhali, usifunge!” Brian akalia. Hakuwa anaweza kuongeza tena kasi kwani hapo alikuwa tayari kwenye kikomo. Alichokifanya, alipoukaribia kidogo mlango, wazi akiona unaelekea kufunga, akaruka hewani kuuparamia.
.
.
Akadondokea chini kama mzigo, Olivia akiangukia upande mwingine. Lakini kabla hajaugulia maumivu, akaukita mlango kwa mguu wake wa kuume, mlango ukafunga! Haraka akanyanyuka na kuutia komeo kisha akasimama hapo akiskiza nini kitaendelea.
.
.
Punde akasikia kishindo cha mtu mlangoni. Mlango ukagongwa mara mbili na sauti ikanong’ona, “Heeeeeyy! … wataka kucheza?” Brian hakusema kitu. Alikuwa amesimama hapo kuugandamizia mlango akiwa amejawa na woga.
.
.
“Najua unataka kucheza, sivyo hivyo Brian?” sauti iliendelea kunong’ona. “Najua unapenda kucheza … njoo basi, twende tukacheze … eti?”
.
.
Brian hakusema kitu, akaendelea kuwa kimya. Naye Olivia alikuwa ametulia akimtazama Brian.
.
.
Wakasikia kishindo kile cha miguu kikisonga kwenda mbali na mlango na kisha kurudi karibu. Kwenda mbali na kisha kurudi karibu. Mara kikakoma. Alafu sauti ile ikauliza, “Brian, hutaki kumwona Silvia?”
.
.
Brian akakodoa kwa mshangao.
.
.
“Yupo wapi?” akaropoka kuuliza.
.
.
“Yupo kule, twende ukamwone!” sauti ikamjibu. “Twende upesi!”
.
.
“Anafanya nini huko?”
.
.
“Anatazama mazingaombwe! Hutaki na wewe kuona?”
.
.
“Sitaki!” Brian akafoka. “Sitaki kukuona maishani mwangu. Sitaki uje kwetu. Kaa mbali na sisi!” Brian alisema machozi yakiwa yanamtoka. Mara kukawa kimya kwa sekunde tano, hakuwa anasikia kitu. Alitega masikio yake vema akiwa anatazama madirishani.
.
.
Mara akasikia sauti ya kike, “Brian, niokoe! Niokoea tafadhali!”
.
.
Brian akagutuka. “Silvia!” akajikuta anaropoka. “Silviaa!”
.
.
“Ndio, Brian!” sauti ya kike ikamjibu. “Naomba uniokoe Brian!” sauti ikalia. “Naomba uniokoe, tafadhali!” ikaendelea kulia na kulia. Brian akatamani kufungua mlango. Alitazama kitasa akitaka kukiminya, Olivia akapaza sauti, “Hapana, Brian!”
.
.
Brian akamtazama Olivia.
.
.
“Usifungue, Brian. Usifungue! Sio Silvia huyo.”
.
.
Mara mlango ukaanza kupondwa kwanguvu! Nguvu ya kuponda ilikuwa kubwa sana. Ukuta ulikuwa unatikisika. Bawaba zilikuwa zinalegea. Olivia akaenda kumsaidia Brian kuminya mlango lakini haikusaidia chochote kwani mlango uliendelea kupondwa kwanguvu sana. Ukaanza kutia ufa kana kwamba gogo lililooza likikitwa na ncha ya shoka kali.
.
.
Mara,
.
.
“Briaaaan!” sauti ya kike ikaita. Brian alipotazama koridoni akamwona mama yake akiwa amesimama, anawatazama kwa mshangao mkuu. Ni ghafla pia mlango ukaacha kupondwa na kukawa kimya kabisa kana kwamba hakuna kilichotokea!
.
.
“Brian, kuna nini?” mama akauliza akijongea. Brian alikosa cha kusema akabaki kimya. Mama alisonga karibu akatazama mlango. Ulichora ufa haswa. Bawaba zilikuwa zimetema nati zake. Ukuta ulikuwa umechimba mistari!
.
.
**
.
.
Mama alifikicha macho yake kisha akamtazama Brian aliyekuwa ameketi kwenye kiti pamoja na Olivia. Akashusha pumzi ndefu na kukuna kichwa chake kilichojawa na nywele.
.
.
“Hili ni tatizo kubwa mno, kila siku linazidi kukua. Kama tusipochukua hatua za mapema, linaweza kutugharimu.”
.
.
Kukawa kimya Mama aliponyamaza. Vinywa vilikuwa vizito. Akili zilipoa. Ni kama vile walikuwa wamenyeshewa mvua.
.
.
“Nadhani inabidi turudi kule kwa mtaalamu demonolojia,” Mama akaendelea kuteta. “Bila shaka yule ndiye mtu pekee aliyebakia wa kutusaidia.”
.
.
“Tutaenda lini?” akauliza Brian.
.
.
“Jua litakapochomoza,” mama akajibu na kuongezea, “Jiandaeni kabisa maana umebaki muda mchache kwenda huko … nadhani tutalala hukohuko.”
.
.
Mama aliposema hayo akaenda zake. Kweli jua lilipochomoza wakajikwea kwenye gari wakiwa wamebebelea mahitaji kadhaa tayari kwa ajili ya safari. Brian aliona ni stara kubeba zile nyaraka tatu za Dkt Hamill, alizitia garini akilenga kuendelea kuzisoma safarini.
.
.
Wakafunga nyumba, safari ikaanza.
.
.
Wakatembea kwa muda wa masaa mawili. Wakaacha mji wote nyuma na kuzama katikati ya misitu. Mwendo ulikuwa wa upesi maana safari ilikuwa ndefu. Basi Brian, ambaye alikuwa ameketi nyuma peke yake, akawa ameegamishia kichwa chake kwenye kiti akitazama miti irudiyo nyuma.
.
.
Alikuwa ametulia haswa. Alikuwa anawaza mambo yake kichwani. Lakini ukimya wake huo haukudumu kwa muda mrefu. Akiwa hana hili wala lile, mara akaanza kusikia sauti nyembamba ikimnong’oneza masikioni … “Brian, unataka kucheza?” akashtuka kidogo na kutumbua macho. Akatazama kila pande akiwa amekunja ndita.
.
.
Sauti ile masikioni ikacheka ikiishilia … “Wataka kuniona?” ikanong’ona. “Wataka kuniona Brian?” mara Brian alipotazama kushoto kwake akamwona mtu aliyevalia nguo nyeupe akikatiza ghafla kana kwamba radi! Akatoa macho kushangaa!
.
.
Akakunja uso wake kuangaza. Alitupa macho kwenye kioo cha nyuma cha gari lakini hakumwona mtu. Alishusha vioo vyote vya nyuma, akatazama pasipo mafanikio.
.
.
Basi punde, upepo mkali ukapuliza. Sijui ulikuwa umetokea wapi. Ulizama ndani ya gari kwakuwa vioo vvya nyuma vilikuwa wazi. Ajabu ukasomba zile nyaraka za Dkt Hamill na kuzimwagia nje!
ukazipeperusha huku na huko kutawanyika.
.
.
“Mama, simamisha gari! Simamisha garii!” Brian akawaka akimpigapiga mama yake begani. Mama akasimamisha gari upesi, na kumtazama Brian kwa taharuki. “Vipi?” Brian alitoka kwenye gari upesi kukimbilia nyaraka zake. Zilikuwa zinapeperushwa upesi na upepo kuzama msituni!
.
.
Aliikimbiza mojawapo lakini upepo ulizidi kuitokomeza. Mwishowe alisimama akadaka magoti yake akihema kwanguvu. Hakuamini macho yake, nyaraka zilikuwa zimepotea mbele ya macho yake!
.
.
Basi akiwa hapo, sura imemvurugika kwa kuchoka na mawazo, akaona mojawapo ya nyaraka yake ikiwa pembezoni mwa mti mkubwa umbali wa kama hatua kumi toka alipo kwa upande wa mkono wake wa kushoto.
.
.
Akasimama na kutazama vema. Ni kweli alichokuwa anakiona. Nyaraka ilikuwa imetuama hapo. Basi akakata shauri kuifuata. Alipopiga hatua tatu, akastaajabu kuona mkono ukitokea nyuma ya mti, ukaivuta ile nyaraka upesi!
.
.
Akakimbia kutazama, hakukuta kitu! Akabaki akiduwaa. Mara akasikia sauti ya makaratasi nyuma yake yakifunguliwa na upepo! Akageuka kutazama. Uso kwa uso akakutana na kiumbe ambacho hakuwahi kukiona wala kuja kukikumbuka. Asijue kinachoendelea, akadondoka chini na kupoteza fahamu!
.
.
.
.
“Briaaaaan!” mama aliita akiangaza huku na kule. Kandokando yake alikuwa pia Olivia naye akirusha macho kumtafuta Brian ndani ya msitu huu mkubwa.
.
.
“Briaaan!” mama aliendelea kuita. Macho yake yalishaanza kuwa mekundu akitaka kulia. Alipotembea kwa muda kidogo, akaona alama za miburuzo kwenye majani! Akajikuta analalama akiziba mdomo, “Mungu wangu, Brian!”
.
.
Alitazama kufuatilia alama hiyo ya miburuzo, kwa mbali akamwona mtu fulani akiishilia akiwa anavuta mwili wa Brian!
.
.
**